Tunakuomba kwa mara nyingine kuhamasisha mamlaka zako kutokomeza vitendo hivi vya kikatili kwa kuhakikisha havijirudii tena na kufanya uchunguzi makini na kuwafungulia mashtaka wale wote waliohusika,”.PICHA|MAKTABA
Dar es
Salaam. Mabalozi 12 wa Umoja wa Ulaya (EU),
nchini wamemtumia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda barua ya wazi wakimtaka kuchukua
hatua stahiki kwa watu waliofanya mauaji ya albino wilayani Bariadi, mkoani
Simiyu.
“Tumesikitishwa na mauaji ya kikatili ya
albino Munghu Lugata yaliyotokea Mei 12, 2014 wilayani Bariadi,” ilieleza
sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na mabalozi 12 wa nchi wanachama wa EU
Tanzania, wakiongozwa na Balozi wa Umoja huo nchini, Filiberto Sebregondi.
Mabalozi wengine waliosaini barua hiyo
ni Dianna Melrose wa Uingereza, Koenraad Adam wa Ubeligiji, Johnny Flento wa
Denmark, Sinikka Antila wa Finland, Marcel Escure wa Ufaransa, Fionnuala
Gilsenan wa Ireland, Luigi Scotto wa Italia, Jaap Frederiks wa Uholanzi, Luis
Manuel Cuesta Civis wa Uhispania, Lennarth Hjelmaker wa Sweden na Kaimu Balozi
wa Ujerumani, Hans Koeppel.
Katika tukio hilo linalohusishwa na
ushirikina, watu wasiofahamika walimuua Lugata na mwili wake ulikutwa nje ya
nyumba yake ukiwa umejeruhiwa vibaya.
Barua hiyo ilisema kuwa Pinda amekuwa
mstari wa mbele kupambana na vitendo hivyo, bila shaka atahamasisha mamlaka za
chini yake kuchukua hatua za kisheria.
“Tunakuomba kwa mara nyingine
kuhamasisha mamlaka zako kutokomeza vitendo hivi vya kikatili kwa kuhakikisha
havijirudii tena na kufanya uchunguzi makini na kuwafungulia mashtaka wale wote
waliohusika,” ilisema.
Kwa mujibu wa barua hiyo, Lugata ni
albino wa 73 kuuawa nchini tangu mwaka 2000 na wa kwanza kwa mwaka 2014.
Katika barua hiyo ambayo pia
ilithibitishwa na Mkuu wa Idara ya Siasa, Habari na Mawasiliano ya EU, Tom
Vens, mabalozi hao 12 wanafahamu fika kuwa waganga wawili wa jadi wanahusika
katika mauaji hayo.
Wakati huohuo; Ubalozi wa Uingereza
nchini umezungumzia suala la uchunguzi wa uchotaji wa zaidi ya Sh200 bilioni
katika Akaunti ya Escrow ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ukisisitiza kuwa
suala hilo lishughulikiwe ipasavyo na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria.
Pia ubalozi huo umekanusha madai ya
balozi wake nchini kuhusika katika mkakati wa kujaribu kukwamisha Bajeti ya
Wizara ya Nishati na Madini.
Taarifa ya ubalozi huo iliyotolewa jana,
ilieleza kwamba unafuatilia kwa karibu kuhusu taarifa za ubadhirifu uliofanywa
kupitia Kampuni ya IPTL, ikihusisha Akaunti ya Escrow na BoT, lakini hauna
sababu ya kuingilia kukwamisha bajeti ya Wizara ya Madini kama ilivyotajwa na
baadhi ya vyombo vya habari.
CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment