Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Tuesday 13 May 2014

KIGWANGALLAH ALIUTOA WAPI UZUSHI HUU KUHUSU MZEE WARIOBA?

Mjadala wa Rasimu ya Katiba Mpya katika Bunge Maalum uliingiliwa na chunusi pale 'Wabunge Walio Wengi', wengi wao kutoka CCM, walipoamua kuliteka bunge hilo na kuanza kupigania maslahi yao kupinga ujio wa Serikali ya Tanganyika.
Wengi mpaka sasa wanaamini kwamba ikiwa muundo wa Serikali Tatu utapita, basi watakuwa hawana chao tena majimboni kutokana na mfumo ulivyo.
Lakini wengine wanahofia mengi - ikija Serikali ya Tanganyika wale waliozowea vya kunyonga kama kukwapua mali za umma, kuingia mikataba na serikali wakitumia makampuni yao binafsi katika idara wanazoziongoza, kusafirisha nyara zetu na kadhalika - kamwe watakuwa hawana nafasi.
Ndiyo maana wengi wao walitamka maneno yenye kukera na kuikashfu Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba wakimtuhumu mze huyo kwamba hana nia njema na Muungano, tena takwimu alizozitoa ni za kutunga na haziwawakilishi Watanzania wote, na mambo kama hayo.
Kapteni John Komba yeye aliapa Bungeni kwamba zikipita serikali tatu ataingia msituni. Sijui kufanya nini, lakini kwa kuwa yeye ni mjeshi, basi huenda atakuwa anajiandaa kufanya mapinduzi ili kudhihirisha kauli ya Waziri William Lukuvi aliyoitoa kanisani pale Dodoma kwamba Jeshi ndilo litaongoza nchi.
'Walio Wengi' kila mmoja wake, kwa kutaka kukifurahisha chama chake cha CCM, aliibuka na kuponda kila hoja inayoelekea kuunga mkono serikali tatu, wakatoa uzushi mkubwa kwa mambo ambayo wengine hata hawayajui.
Dk. Hamis Kigwangallah akawa mmoja wao, yeye akaandika mpaka kwenye ukurasa wake wa facebook akimtuhumu Mzee Warioba kwamba amependekeza serikali tatu kwa vile tu yeye alikuwemo kwenye Tume ya Jaji Robert Kisanga na ile Jaji Francis Nyalali, ambayo ilizaa 'White Paper'. Tume hizo zilibaini kero za Muungano na kupendekeza mabadiliko ya muundo wake ambayo leo hii tumeyaona kwenye Rasimu ya Katiba Mpya.
Lakini wakati Mbunge huyo wa Nzega akieleza uongo wake huo, nadhani hakupitia vizuri kuona majina ya wajumbe wa tume hizo, pengine kwa vile alikuwa bado yuko shuleni wakati huo!
Warioba mwenyewe akafafanua vizuri wakati akihojiwa na kituo cha luninga cha ITV katika kipindi cha Dakika 45 na kukanusha madai hayo ya Kigwangallah, kama anavyosikika na kuonekana kwenye kipande hiki cha video.
Sasa Kigwangallah aliyatoa wapi hayo majungu? Kama alielezwa, basi nadhani waliomweleza nao hawana hata kumbukumbu nzuri.
Tunapotafuta Katiba Mpya, ni kwa manufaa ya Watanzania wa sasa na hasa wa kizazi kijacho, tusiangalie matumbo yetu, maana wengi wanapiga kelele na kuunga mkono mambo ambayo nafsi zao zinafahamu kwamba siyo sahihi, lakini kwa sababu 'wanachumia tumbo', wanaendelea kuipotosha jamii.

Ndugu yenu,
Daniel Mbega
Iringa, Tanzania
0656-331974

No comments:

Post a Comment