HOTUBA YA KAMBI YA UPINZANI MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA MAMBO
YA NDANI YA NCHI KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015 NA MHE.GODBLESS JONATHAN
LEMA (MB).
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa ‘Instrument’ ya Serikali inayoainisha
majukumu kila Wizara, Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi imepewa majukumu
ya kushughulikia masuala ya Usalama wa Raia, Uhamiaji na utekelezaji wa
Sera za zima moto na uokoaji. Aidha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
inashugulikia pia masuala ya huduma za Jeshi la Polisi, Magereza,
Uhamiaji, Uraia, Vitambulisho vya Taifa, Huduma za Wakimbizi, Usajili wa
Vikundi au Vyama vya Kijamii, Huduma za Zima Moto na Uokoaji na mambo
mengine yanayohusu maendeleo ya rasilimali watu katika Wizara hiyo.
Mheshimiwa Spika,
Ukitazama
majukumu ya Wizara hii, utaona kwamba ina majukumu mazito sana
yanayohusu usalama wetu sote kama raia wa nchi hii. Ni majukumu
yanayohusu maisha yetu. Hivyo wizara hii inatakiwa
iwezeshwe sana kibajeti ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo
ili wananchi na hata wageni waliopo katika nchi yetu waweze kuishi kwa
usalama na amani. Kwa kuwa Wizara hii ina taasisi chini yake
zinazohusika na ulinzi wa maisha ya watu na mali zao, hivyo ni Wizara
inayotakiwa kufuatiliwa na kusimamiwa kwa karibu sana.
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA 2013/2014
Mheshimiwa Spika,
Katika
bajeti ya Wizara hii kwa mwaka wa fedha unaomalizika wa 2013/2014
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliitaka Serikali kufanya mambo kadhaa
ili kuboresha mapungufu tuliyoyaona katika katika kipindi hicho. Mambo
hayo ni:
i. Kuchukua hatua kali na
madhubuti ya kukabiliana na matukio yenye sura ya ugaidi kwa mfano
kulipuliwa kwa bomu Kanisa Katoliki katika Parokia ya Olasiti huko
Arusha, kuchomwa moto kwa makanisa huko Zanzibar na Dar es Salaam,
Mapadre kuuwawa na Mashehe kumwagiwa tindikali Arusha na Zanzibar na
matukio yanayofanana na hayo.
ii. Kuongeza posho ya chakula
(Ration allowance) kwa askari wa Jeshi la Polisi ili walau posho hiyo
ishabihiane na posho ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ili
waweze kukabiliana na ugumu wa maisha. Kwa mujibu wa kumbukumbu rasmi za
bunge (hansard) Waziri wa Fedha wa wakati huo Marehemu William Mgimwa
alikubali posho ya chakula ya shilingi 225,000/= kwa mwezi kwa kila
askari. Taarifa tulizo nazo ni kwamba posho hiyo haijalipwa mpaka leo.
Je, askari waandike deni au wahesabu kwamba wamedhulimiwa?
iii. Kutoa mwongozo kwa maafisa
wa Jeshil la Polisi na Magereza juu ya marekebisho ya sheria kuhusu umri
wao wa kustaafu ambapo marekebisho ya sheria yaliongeza umri wa
kustaafu kutoka miaka 50 kwenda miaka 55 kwa maafisa wa Polisi na kutoka
miaka 55 kwenda miaka 60 kwa akari wa Magereza.
iv. Kuondoa urasimu na utaratibu
kandamizi katika Jeshi la Magereza kuhusu Mpango wa kujiendeleza kielimu
kwa maafisa wa Magereza. Tuliitaka Serikali kufanya hivyo kwa kuwa, kwa
mujibu wa General Service Order (GSO) na sheria nyingine za kazi, mtu
akiajiriwa kwa mara ya kwanza (first appointment) na akataka
kujiendeleza kimasomo nje ya kituo chake cha kazi anatakiwa kukaa
kazini kwa muda wa miaka miwili au mitatu ndipo aweze kuomba ruhusa ya
kwenda masomoni. Lakinini tulipokea malalamiko kutoka kwa maafisa wa
Magereza kwamba sheria hiyo haifuatwi na badala yake maafisa hao
wanatakiwa wakae miaka sita kazini ndipo wapewe kibali cha kujiendeleza
kimasomo.
v. Kujenga nyumba za Askari wa
Magereza ili kuboresha mazingira yao ya kazi na kuwafanya wasijisikie
kama vile na wao ni wafungwa.
vi. Kuchukua hatua ya kupunguza msongamano wa wafungwa na mahabusu Magerezaji
vii. Kuboresha lishe na huduma za afya kwa Wafungwa na Mahabusu Magerezani
viii. Kuongeza fedha kwa ajili ya ununuzi
wa vifaa vya zima moto na uokoaji kwa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji
ix. Kuwachukulia hatua askari wa
Jeshi la Polisi wenye vyeo vya juu wanaowanyanyasa askari wa vyeo vya
chini.
x. Kuacha kulitumia Jeshi la Polisi vibaya kwa ajili ya kulinda maslahi ya kisiasa ya CCM
xi. Kuwachulia hatua kali za
kisheria viongozi wa Jeshi la Polisi na viongozi wa Serikali waliotoa
kauli za vitisho kwa waandishi wa habari walioandika habari za
unyanyasaji unaofanywa na Jeshi la Polisi
xii. Kutoa ukomo wa muda ambapo
kila raia wa Tanzania atapatiwa Kitambulisho chake cha Taifa na
kuainisha ghrama zilizotumika katika mchakato wa kutengeneza
vitambulisho vya Taifa.
xiii. ,Kudhibiti kuzagaa kwa silaha za moto ambazo hutumika katika matukio mengi ya kijambazi.
xiv. Kuchukua hatua kali kwa watu wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya hapa nchini
xv. Kuchukua hatua madhubuti za
kupunguza matukio ya ajali barabarani ambayo yamepoteza maisha ya
wananchi wengi sana wakiwemo polisi pia.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa taarifa ya
utekelezaji wa masuala niliyoyataja hivi punde wakati wa majumuisho ya
bajeti ya Wizara hii.
Mheshimiwa Spika,
Kwa
mujibu wa Randama ya Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi fungu 51 na
randama za taasisi zilizoko chini yake yaani Fungu 93(Idara ya
Uhamiaji); fungu 28(Jesh la Polisi); fungu 29 (Magereza) na fungu 14
(Idara ya Zima Moto) hadi kufikia mwezi Machi, 2014 Wizara na taasisi
zilipata mgawo wake wa kibajeti kwa wastani wa asilimia 70 isipokuwa
idara ya zima moto na uokoaji ambayo ilipata asilimia 46.3 tu ya fedha
zilizoidhinishwa. Aidha kwa Mujibu wa Randama ya Jeshi la Zimamoto,
fungu 14 (uk. 2) katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/14 hakuna fedha
yoyote iliyotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa Jeshi la Zima
Moto.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa Randama
hiyo, huu ni mwaka wa tatu mfululizo kwa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji
kutotengewa fedha kwa ajili ya miradi ya Maendeleo. Kutokana na hali
hiyo, Jeshi hilo limeshindwa kuendeleza ujenzi wa jengo la Ofisi ya
Makao Makuu – TAZARA, Dar es Salaam, kushindwa kukarabati na kujenga
vituo vipya vya zimamoto, kushindwa kununua vitendea kazi mbalimbali
ikiwemo vifaa vya maokozi na vifaa vya kuzimia moto.
Mheshimiwa Spika,
Sote ni mashahidi wa
majanga ya moto, maghorofa kuporomoka, meli kuzama, mafuriko na kila
aina ya majanga ambapo idara ya zima moto imekuwa ikishindwa kufanya
chochote na hivyo kuwaacha wananchi wakiangamia katika majanga hayo.
Kambi Rasmi ya Upinzani inashawishika kuamini kwamba Serikali haina nia
njema na usalama wa raia na ndio maana haitengi fedha hata senti moja
katika miradi ya maendeleo ya Jeshi la Zima Moto. Kama Serikali haioni
umuhimu wa Jeshi la Zima Moto ni bora kulifuta kuliko kuliacha wakati
hailiwezeshi kufanya kazi yake.
Endelea........
HALI YA USALAMA NCHINI .
Mheshimiwa Spika ,
Hali
ya Usalama Nchini imeendelea kuwa tete kutokana na sababu mbalimbali.
Utafiti wa kiufuatiliaji uliofanywa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
ni kwamba; sababu zifuatazo zinazorotesha hali ya usalama na amani hapa
nchini.
i. Ukosefu wa Ajira na Kazi zenye Kipato kwa Jamii.
Mheshimiwa Spika,
Ukosefu
wa kazi na ajira kwa Jamii umekuwa ni sababu moja ya msingi kabisa ya
kuendelea kuhatarisha hali ya usalama na amani Nchini. Wananchi wengi
hususan Vijana wamekuwa hawana uhakika wa ajira. Mbali na hofu na
wasiwasi mkubwa walio nao, vijana hawa kutokana na kutojua hatima ya
maisha yao, bado Serikali imeendelea kuwasakama katika shughuli zao
ndogo ndogo. Kitendo cha Serikali kuwafukuza mijini vijana wajasiriamali
wanaofanya biashara ndogondogo kumesababisha vijana hawa kushindwa
kabisa kuweza kumudu hata mlo mmoja kwa siku. Jambo hili limewakatisha
tamaa vijana wengi na matokeo yake ni kwamba baadhi yao wanajiingiza
katika matukio ya kihalifu ili waweze kumudu maisha yao.
Mheshimiwa Spika,
Ili kujenga mazingira
ya usalama, amani na utulivu katika nchi yetu, ni lazima sasa Serikali
itambue wajibu wake wa kukuza uchumi na biashara kwa kasi ili kuongeza
ajira na kazi zenye tija kwa jamii kwani kuachia Jeshi la Polisi
kudhibiti hali ya ulinzi na usalama katika Taifa ambalo asilimia 80% ya
Vijana wake wanarandaranda mitaani bila kuwa na kazi zenye uwezo wa
kukidhi mahitaji yao muhimu ni hatari kubwa sio tu kwa walinzi hawa wa
amani bali pia kwa taifa zima.
Mheshimiwa Spika,
Hivyo ni muhimu tukafahamu kwamba
propaganda na tathimini feki kuhusu ukuaji wa uchumi zinazotelewa kila
mwaka na Serikali wakati Watu wengi wanaendelea kuishi maisha yasiyo na
matumaini na wengine wakishindwa kufurahia ajira na kazi kwa sababu ya
masilahi duni na mfumuko wa bei za bidhaa unaosababishwa na uchumi
kushuka kila mwaka, bila shaka sasa ni kweli kabisa kuwa hali ya usalama
Tanzania ni tete na Jeshi Polisi haliwezi kujipanga kushindana na
kundi kubwa la jamii iliyojaa hasira na kupoteza matumaini na maisha .
ii.
Maslahi ya Askari wetu katika Muktadha wa Hali ya Usalama
Nchini.
Mheshimiwa Spika,
Maisha ya Askari wa Jeshi
la Polisi, Magereza, Zimamoto ni miongoni mwa kundi katika jamii ambalo
linaishi maisha ya umasikini wa kupindukia sana. Nyumba zao, mishahara
yao na masilahi yao mengine mbali mbali bado ni duni kiasi kwamba Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inaona kuwa ni kebehi na dharau kubwa sana
kwa vikosi vya ulinzi na usalama .
Mheshimiwa Spika,
Kazi ya Jeshi ni wito.
Ni hatari kubwa sana kuwa na Askari ambao wanafanya kazi bila wito kwa
sababu walikosa matumaini kwingineko, hivyo wakachagua kujiunga na Jeshi
kama sehemu ya biashara.
Mheshimiwa Spika,
Ni ukweli usiopingika
kuwa Askari wengi wanafanya kazi kwa moyo uliovunjika na kupondeka.
Aidha, wana msongo mkubwa wa mawazo sababu ya ugumu wa maisha. Hali hii
inaondoa uimara wa majeshi yetu haya kwani Jeshi imara sio tu kuwa na
silaha za kisasa peke yake bali ni muhimu pia kuwa na askari wanaoona
fahari kulinda raia na mali zao kama wajibu uliotukuka. Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutambua na kuthamini kazi
inayofanywa na askari wetu ambao ni sehemu ndogo ya jamii iliyojitoa
mhanga kufanya kazi za hatari hata kwa maisha yao ili kuwalinda raia na
mali zao
iii. Rushwa na Uadilifu kwa Jeshi la Polisi
Mheshimiwa Spika,
Jeshi
la Polisi limekuwa likitajwa kuwa kinara wa rushwa na chanzo cha
biashara nyingi haramu. Jambo hili zio zuri hata kidogo kwa chombo
kilichokabidhiwa jukumu la kuwalinda raia na mali zao. Hata hivyo,
tafiti nyingi zinaonesha kwamba mazingira mabaya ya maisha yao
yaliyojengwa katika maslahi duni ni miongoni mwa sababu
zinazowasababisha kuingia katika tabia hii mbaya ambayo ni hatari kwa
usalama wa Nchi .
Mheshimiwa Spika
Rushwa ndani ya Majeshi
yetu ya ulinzi na usalama ni majaribu yanayo sababishwa na Serikali
yetu. Hii ni kwa sababu mishahara na makazi ya askari wetu ni duni,
vitendea kazi vichache na duni jambo linalochangia kwa kiasi kikubwa
kuwa na askari wasio na
ari na shauku ya kazi ya ulinzi na usalama. Matokeo yake wanakosa
nidhamu ya kazi na hivyo kujiingiza kwenye vitendo viovu ikiwemo rushwa
na unyanyasaji wa raia. Ili kuwa na askari wenye nidhamu ya kazi, ni
lazima kuwa na Serikali inayojua na kuthamini wajibu mkubwa wa vikosi
vya ulinzi na usalama katika taifa. Kama vile Serikali inavyotoa
mishahara mikubwa kwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)na
Benki kuu ili kuwapa motisha wasiibe, vivyo hivyo Serikali ingeona
umuhimu wa kuwalipa na kuwatunza vyema askari wa vikosi vya ulinzi na
usalama kwa kuwa na askari wanaofanya kazi kwa moyo uliopondeka ni
hatari kwa ukuaji wa uchumi na usitawi wa wananchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika,
Kitendo cha Serikali
kupuuza maslahi mbalimbali ya askari wetu ni kuwaingiza katika majaribu
mbalimbali ikiwemo rushwa, ukandamizaji na unyasaji dhidi ya raia
wanaopaswa kuwalinda. Ifahamike kwamba kuwaingiza watu majaribuni ni
dhambi. Aidha majaribu ya kumfanya mtu atende jambo baya yanahesabika
kuwa ni dhambi. Ni katika muktadha huu, hata Bwana Yesu alipokuwa
akiwafundisha wanafunzi wake kusali, aliwaambia wamwombe Mungu
wakisema“….Usitutie Majaribuni bali utuokoe na Yule mwovu” Kwa hiyo
Mheshimiwa Spika, Dhamira isiyokuwa na utu ya Serikali hii CCM juu ya
usitawi wa nchi hii na watu wake ndio chanzo kikubwa cha askari wetu na
wananchi wengine kuingia katika majaribu ya rushwa na aina mbalimbali za
uhalifu.
Mheshimiwa Spika,
Ni kweli inawezekana
kabisa binadamu akawa muadilifu bila kuwa na masilahi bora katika jamii,
lakini vile ni ukweli usiopingika kwamba umasikini na hali duni ya
maisha ndio unachangia kwa kiasi kikubwa kuondoa uadilifu na uimara wa
nidhamu katika kukabiliana vishawishi vya rushwa na mambo mengine
machafu yenye sura hizi.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na Serikali
kuwa ndio mlezi wa rushwa, imekosa mamlaka ya kiuadilifu (moral
authority) wa kukemea vitendo vya rushwa vinavyofanywa na taasisi
mbalimbali zilizo chini yake. Kwa mfano kwa mujibu wa vyombo vya habari
na kwa mujibu wa mjadala wa bajeti ya Serikali unaoendelea bungeni
imeibuliwa kashfa ya wizi wa fedha zaidi ya shilingi bilioni 200 ambapo
Viongozi Wakuu wa Serikali wamehusishwa. Katika jambo kama hili,
Serikali inatoa wapi nguvu na sauti ya kukemea rushwa katika taasisi
inazoziongoza kama vile jeshi la Polisi .
Mheshimiwa Spika,
Kama wanaopaswa kukemea
na kuzuia rushwa ni wala rushwa, ni wazi moja kwa moja kuwa, utamaduni
wa kupokea rushwa na kula rushwa katika taasisi zote za Serikali ni
jambo la Kawaida, na linaoipendeza Serikali ya CCM. Kwa hiyo, hakuna
hata Kiongozi mmoja mwenye mamalaka ya kiuadilifu kukemea jambo hili,
kwa kuwa familia zao zinaishi, zinasoma na kufurahia maisha kwa ajili
ya ufisadi, wizi wa mali za Umma na rushwa .
Mheshimiwa Spika,
Kwa dhati kabisa, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaikemea Serikali kujenga mazingira ya rushwa kwa
askari wetu. Kwa mfano kitendo cha Serikali hii ya CCM kukigeuza kitengo
cha Askari wa Usalama Barabarani kuwa kitengo cha ukusanyaji mapato kwa
makosa ya kutafutiwa na kulazimishiwa barabarani ni rushwa iliyowekewa
mfumo rasmi. Jambo hili ni hatari sana kwa sababu rushwa ya aina hii
haiwezi kumalizika kwa kuwa ina baraka za Serikali. Hali ni mbaya zaidi
kwa kuwa katika kutekeleza jukumu hilo la askari kukusanya mapato,
utaratibu umewekwa ambapo kila askari anatakiwa kutafuta kwa bidi,
kulazimisha na kukamata makosa yasiyopungua sita mpaka tisa na kuyatoza
faini. Mfumo huu mpya wa Serikali wa ukusanyaji wa mapato umeifanya
rushwa barabarani kuwa rasmi.
Kambi Rasmi ya Upinzani inafahamu kwamba Serikali imeishiwa fedha,
lakini tunaisihi sana isitumie njia za ukandamizaji na uonevu
kujikusanyia mapato.
Mheshimiwa Spika,
Baada
ya kuacha jukumu lao la msingi la kusimamia sheria za barabarani na
kuanza kukusanya mapato, ajali za barabarani zimeongezeka sana. Kwa
mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka 2013, jumla ya ajali za
barabarani zilizohusisha magari katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza,
Mbeya, Pwani, Kilimanjaro, Arusha na Morogoro zilikuwa ni 459,931, na
ajali hizi zilisababisha vifo vya watu 2,408 na majeruhi 16,040. Kwa
upande wa bodaboda watu waliofariki kutokana na ajali ni 1,106 na
majeruhi 6,581.
Mheshimiwa Spika,
Ripoti ya Haki za
Binadamu ya 2013, inasema kwamba nchi inapata hasara ya kati ya asilimia
1 hadi 2 ya Pato la Taifa (GDP) kutokana na ajali za barabarani. Kwa
hiyo, uamuzi wa Serikali wa kukifanya kikosi cha usalama barabarani
kuwa kitengo cha ukusanyaji mapato umekuwa ni hatari kubwa kwa maisha ya
raia na uchumi wa nchi.
iv. Ukandamizaji, Ukatili na Uonevu Unaofanywa na Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Spika
Hivi
karibuni kumekuwa na matukio ya mahubusu kugoma kula , kuvua nguo
hadharani na mambo mengine yakusikitisha ili kuonyesha hisia zao juu
ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa dhidi yao. Madai makubwa ya
mahabusu hao ni kwamba wanapata mateso makubwa gerezani kwa makosa
ambayo wengi wao hawajayatenda. Hii maana yake ni kwamba Mahabusu wengi
katika magereza yetu wamebambikizwa kesi jambo ambalo ni kinyume kabisa
na utawala wa sheria na haki za binadamu.
Mheshimiwa Spika,
Ili kuondoa mwanya
uliopo hivi sasa wa Polisi kuwabambikiza raia kesi na kuwaweka mahabusu,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kufanyia marekebisho
sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ili kuondoa fursa kwa baadhi ya
askari wenye nia mbaya kutumia madaraka yao kuwabambikizia watu kesi
kutokana na chuki au sababu nyingine. Kwa mfano, kijana mmoja wa
Arusha, aliingia katika ugomvi wa mapenzi na askari polisi kwa sababu ya
kumgombania binti. Askari yule alitengeneza mazingira kwa kijana yule
kumbakiziwa kesi ya wizi wa kutumia silaha na mauaji na kuswekwa
rumande. Kijana huyo wakati alipokuwa anaendelea kuteseka mahabusu, yule
askari alimwoa mwoa yule binti. Baadaye askari huyo na binti huyo
ambaye sasa ni mke wa yule askari wakaenda Magereza kumtembelea yule
kijana aliyekuwa mahabusu kwa uonevu kama ishara ya kuonyesha
umwamba!!!!!
Mheshimiwa Spika,
Mambo kama haya hayana
idadi katika magereza zetu. Ni mengi. Uonevu na unyanyasaji unaofanywa
na askari wetu katika kila kona ya nchi yetu ulijidhihirisha pia bomu
lilipolipuliwa katika mkutano wa CHADEMA wakati wakuhitimisha kampeni
za marudio ya Udiwani mwaka jana ambapo watu wanne walifariki Dunia na
wengine wengi zaidi ya 100 kujeruhiwa vibaya wakiwemo watoto wadogo na
Wanawake.
Mheshimiwa Spika,
Tuna ushaidi wa kutosha
juu ya ni nani alihusika na mlipuko huo wa bomu. Licha ya kuwa baadhi
ya polisi walihusika na mlipuko huo; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
ilimtaka Rais mara nyingi aunde tume ya Kijaji kwa ajili ya uchunguzi wa
suala hili kubwa lakini hakufanya hivyo mpaka sasa. Badala yake
kumekuwa na kejeli nyingi na mizaha juu ya suala hili hatari kwani
waliokufa kwenye mkutano wa CHADEMA wanaonekana hawana tofauti na mbuzi
au Kondoo.
Mheshimiwa Spika,
Sisi walengwa tuliotaka
kuuwawa tunafahamu uchungu na mashaka tuliyo nayo dhidi ya maisha yetu.
Hata hivyo mnaweza kuendelea kudharau jambo hili kwa sababu bado
Utawala na Mamlaka yenu yanaendela kuelekeza, kupanga na kuendesha Nchi.
Lakini jambo dhahiri ni kwamba; mateso haya, damu hizi, uonevu huu
utafika mwisho na kama nyie hamtakuwepo basi watoto wenu watakuwepo na
ndugu zenu wengine watakuwepo kushuhudia ukomo wa ukandamizaji, utesaji,
uuaji na udhalimu huu dhidi ya raia wasio na hatia.
Mheshimiwa Spika,
Ni jambo la kusikitisha
sana kwamba waliotaka kutuua pia waliendelea kupanga mipango ya
kutubambikia kesi hiyo ya mauaji na ugaidi. Lakini Mungu akawa mwema,
walikamatwa vijana wengi, wamepigwa, wameteswa na wengine sina uhakika
kama wataweza kuwa na uwezo wa Nguvu za kuzaa tena tena kwa jinsi ya
simulizi zao walivyofanyiwa ukatili wa ajabu na wote walilazimishwa
kumtaja Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema viongozi waandamizi wa
CHADEMA kuwa ndio waliohusika na mlipuko wa mabomu Kanisani Olasiti na
kwenye Mkutano wa kufunga Kampeni za Udiwani za CHADEMA mwaka jana.
Mheshimiwa Spika ,
Katika vijana hawa
waliopatiwa mateso makali baadhi yao walitolewa gerezani wakiwa na kesi
nyingine na wakaelekezwa , wakapigwa , wakateswa na wengine kutishiwa
kuuwawa wakubali kuwa mipango ya milipuko ya mabomu kanisani Olasiti na
kwenye Mkutano wa CHADEMA yaliratibiwa na Mbunge wa Arusha Mjini na
viongozi wakuu wa CHADEMA. Kwa tafsiri hii, inaonekana kwamba;
waliolipua bomu katika Kanisa la Olasiti, ndio hao hao waliolipua bomu
katika mkutano wa CHADEMA. Hii ni kwa sababu badala ya polisi
kutawatafuta wahalifu hao na kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria,
wanahangaika kutafuta watu wa kuwabambikizia kesi kulipua bomu kanisani
ili wawaunganishe na tukio la mlipuko wa bomu katika mkutano wa CHADEMA.
Kwa sababu wanawatafuta watu wa kuwabambikiza kesi ni dhahiri kwamba
Serikali inajua undani wa tukio hilo.
Mheshimiwa Spika,
Uadilifu wa Jeshi la
Polisi umeendelea kuwa mashakani kwani baada ya Uchaguzi mdogo wa Jimbo
la Arumeru Mashariki , Kijana mmoja Kiongozi wa CHADEMA wa Kata ya Usa
river Msafiri Mbwambo aliuwawa kwa kuchinjwa shingo. Wauwaji wale
walikamatwa na Jeshi la Polisi lakini cha kusikitisha ni kwamba baada
ya muda mfupi wahalifu hawa waliweza kutoroka mbele ya Polisi kwenye
chumba cha mahakama wakiwa wamefungwa pingu eti nakufanikiwa kumpora
Askari Bunduki aina ya SMG na kukimbia nayo mpaka leo hawajaonekana
wakiwa na pingu zao . Mheshimiwa Spika, huu ni upumbavu usiofikirika.
Mheshimiwa Spika
Hata wewe unaweza pia
kuziba masikio yako kana kwamba hiki kinachosemwa ni “blues” na ngojera
lakini Mungu yule unayemfuata Kanisani kila asubuhi kumuomba amesikia
na yuko kazini . ‘Only Time will tell’.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa Ripoti ya
Haki za Binadamu ya mwaka 2013 (uk.22) watu 23 waliuwawa na vyombo vya
dola kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Juni, 2013. Kuna mateso
makubwa wanayopitia wananchi kutokana na uonevu wa askari wetu. Wanalia
machozi mazito lakini hakuna msaada kwani Serikali inayopaswa
kuwatazama na kuwalinda raia wake dhidi ya ukandamizaji huu , Serikali
hiyo imepoteza ladha ya utu kwa hiyo kelele na mateso wanayopata Watu
kwa kubambikiziwa kesi na kuwekwa mahabusu na kufungwa miaka mingi na
kuuwawa, mateso hayo sasa yamegeuka kuwa laana kwa Nchi yetu.
v. Polisi Jamii
Mheshimiwa Spika,
Kambi
Rasmi ya Upinzani ina mtazamo kwamba ni vema kuwajengea wananchi
utamaduni wa kuripoti matukio ya kihalifu kwa Jeshi la Polisi kuliko
kuanzisha taasisi nyingine isiyo rasmi ndani ya Jeshi la Polisi.
Tunatambua kwamba Jeshi la Polisi limeanzisha mfumo huu wa Ulinzi
shirikishi kwa sababu ya uchache wa askari iliyo nao. Katika Randama ya
Jeshi la Polisi, fungu 28, mojawapo ya changamoto zilizotajwa ni uchache
wa askari Polisi. Kwa mujibu wa randama hiyo, idadi ya askari
inayohitajika nchini kwa kiwango cha kimataifa ni 90,000 wakati waliopo
sasa hawafiki nusu ya idadi hiyo. Aidha, Jeshi la Polisi linapata ugumu
wa kupata taarifa za kihalifu kutoka kwa wananchi kwa sababu ya uadui
uliojengeka kati ya wananchi na Jeshi la Polisi .
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni Bungeni inaitaka Serikali kuongeza ufanisi katika matumizi yake
ya fedha, kuzuia ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma, kuwajengea
wananchi uwezo wa kiuchumi ili fedha zitakazopatikana zitumike kuajiri
askari ambao ni wataalamu wenye uwezo wa kuwalinda raia na mali zao
badala ya kurasimisha mfumo usio rasmi wa polisi jamii ambao wengi wao
ni green guards wa CCM.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, inalaani Jeshi la Polisi kupuuzwa huko Zanzibar kwa kuvipa
mamlaka zaidi dhidi ya Jeshi la Polisi vikosi vya KMKM, JKU na KVZ
katika kusimamia shughuli za Ulinzi na Usalama wa Zanzibar. Jambo hili
limeondoa mamlaka ya Jeshi la Polisi ambalo lina wajibu wa kulinda raia
na mali zao katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
vi. Uchochezi wa Kidini na Kikabila
Mheshimiwa Spika,
Tatizo
la udini na ukabila katika taifa hili linaonekana kuendelea kukomaa.
Lakini ni tatizo ambalo halitamwacha hata mmoja wetu salama. Ni tatizo
ambalo hakuna mshindi atakayepatikana. Ni tatizo ambalo hata kama
litaisambaratisha nchi, hata wale watakaofanikiwa kuikimbia nchi
hawatakuwa salama huko wanakokwenda kwa sababu watakuwa bado na imani
zao na chuki hiyo dhidi imani nyingine itaendelea popote watakapokuwa.
Mheshimiwa Spika,
Kwa vile jambo hili
linatishia usalama mpana wa taifa hili, ni vema sasa Serikali
ikatafakari upya na kuleta sheria mpya itakayokataza na kuwawajibisha
kwa nguvu zote wale wote watakaojaribu hata kwa maneno kueneza chuki au
ubaguzi dhidi ya dini, kabila au rangi. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inaitaka Serikali iombe radhi na kuwaondoa madarakani viongozi
wote wa Serikali walitotoa kauli za uchochezi wa kidini, kikabila na
rangi.
MAHUSIANO YA SERIKALI KATIKA BIASHARA HARAMU YA MADAWA YA KULEVYA NCHINI.
Mheshimiwa Spika,
Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, haina sababu ya kupoteza muda eneo hili
kwani ni ukweli usiopingika kuwa biashara hii inafanywa na viongozi
wakuu wa Serikali, hivyo basi waamue wao wenyewe kama wangependa
kuendelea kuwa sehemu ya mateso na mauaji ya vijana wetu katika jamii
ya watu inaowaongoza.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani
imelazimika kufikia uamuzi huu kwa kuwa viongozi wakuu wa nchi hii
walishakiri hadharani kuwa wanawafahamu kwa majina watu
wanaojishughulisha na biashara hii. Ni ajabu na ni kituko kama Rais wa
Nchi ambaye ndiye amiri jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama
anaogopa kuwataja wafanyabiashara haramu wa dawa za kulevya ambao
alisema kuwa anawafahamu kwa majina. Tunashawishika kuamini kwamba bila
shaka watu hao ambao mpaka Rais anagwaya kuwataja watakuwa ni malaika
kutoka mbinguni au Mungu.
Mheshimiwa Spika,
Ni vema kama taifa
tukatambua madhara ya madawa ya kulevya kwa vijana wetu ambao ndio nguvu
kazi ya taifa. Kupuuzia na kutochukua hatua kwa wahusika wa dawa za
kulevya ni kuangamiza nguvu kazi ya taifa. Nguvu kazi ya taifa
ikishaharibiwa na dawa za kulevya hatuna taifa tena. Hivyo Serikali
ifahamu kwamba kuendelea kulifumbia macho jambo hili ni kulihujumu taifa
na huo ni usaliti mkubwa.
MAUAJI YA RAIA NA POLISI
Mheshimiwa Spika,
Toka
mwaka 2011 katika hotuba zetu kuhusu Wizara hii tumeendelea kuonesha
mauaji ya raia yanayofanywa na vyombo vya dola likiwemo Jeshi la Polisi.
Wakati akihitimisha hoja yake hapa Bungeni Mhe. Waziri Mku Mizengo
Pinda aliahidi mbele ya Bunge lako tukufu kuwa serikali ingeunda
Mahakama ya Korona kwa ajili ya kuchunguza vifo hivyo kwa mujibu wa
Sheria ya Uchunguzi wa vifo vyenye utata (Inquest Act).
Mheshimiwa Spika,
Serikali ilirudia kutoa
ahadi ya kuanzisha Mahakama hiyo ya Korona kwa ajili ya kuchunguza vifo
vilivyosababishwa na Operesheni ya kuondoa Majangili “Tokomeza” miezi
michache iliyopita.
Mheshimiwa Spika,
Hadi leo ahadi hiyo ya
Waziri Mkuu haijatekelezwa na badala yake Rais ameamua kuunda tume
nyingine huku Bunge lako tukufu likiwa limewasilisha taarifa kuhusu
Tokomeza jambo ambalo linaonesha serikali kutoamini taarifa ya Kamati ya
Bunge lako tukufu.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mwaka wa 2013
taarifa zinaonesha kuwa watu 23 waliuwawa na vyombo vya dola. Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Waziri mwenye dhamana ya Wizara hii
kueleza Bunge lako tukufu juu ya kukithiri kwa tabia hii isiyokoma mwaka
hadi mwaka na ni hatua gani zilizochukuliwa dhidi ya askari wanaohusika
na mauaji haya.
Mheshimiwa Spika,
Aidha Kambi Rasmi ya
Upinzani inamtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi mpya kuchukulia hali kama
janga ndani ya Jeshi la Polisi na hivyo awe na mkakati wa kuzuia hali
hii.
Mheshimiwa Spika,
Katika hali ya kushangaza
hata wananchi wameanza kuchukua sheria mkononi kwa kuwadhuru na hata
kuwaua askari polisi. Kwa mwaka 2013 vituo vya polisi takribani vitano
vilivamiwa na wananchi na mali kadhaa za Jeshi hilo kuharibiwa, aidha
vifo kadhaa vya askari viliripotiwa kutokea katika maeneo mbalimbali
nchini.
Mheshimiwa Spika,
Kama matukio hayo
hayatoshi wananchi kwa makundi yao katika maeneo mbalimbali ya nchi
walizidi kujichukulia sheria mkononi kwa kuwaua watu mbalimbali ambao
wametuhumiwa kufanya makosa ya jinai kama vile wizi. Kwa mwaka jana
pekee watu 1669 waliuwawa[1].
Mheshimiwa Spika,
Upo uhalifu mwingine
ambao umejitokeza katika nchi yetu ambapo watu wamekuwa wakizikwa wakiwa
hai. Matukio kama ya hayo yametokea katika Wilaya Chunya na maeneo
mengine katika Mkoa Mbeya.
Mheshimiwa Spika,
Hali hii ya mauaji ya
raia yanayofanywa na vyombo vya dola na pia mauaji yanayofanywa na
wananchi kwa wahalifu na pia kuvamia na hata kuua Polisi sio jambo la
kulifanyia mzaha kabisa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka
serikali kuchukua hatua za dharura na kutoa taarifa Bungeni na bila
kufanya hivyo italazimika kuamini kuwa serikali iliyopo madarakani
imetoa Baraka kuhusu vitendo hivi vya kinyama kuendelea kutokea katika
nchi yetu.
UHAMIAJI HARAMU NA USALAMA KATIKA MIPAKA YA NCHI YETU
Mheshimiwa Spika,
Mipaka
ya Tanzania haipo salama kabisa kwa sababu imeendelea kuwa kichaka kwa
wahamiaji haramu. Hali hiyo pia inathibitika na kile kilichosemwa na
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi Bungeni katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa kuhusu kung’olewa kwa alama (beacons) za mipaka yetu
katika maeneo mbalimbali nchini. Hata hivyo, mahusiano mabaya ya
Tanzania na baadhi ya jirani zake yanafanya hali ya usalama mipakani
kuwa ya hatari zaidi. Kwa mfano, kumekuwa na mvutano kati ya Rais
Kikwete na Rais Kagame kwa mujibu wa vyombo vya habari. Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inahoji, kutofautiana kwa maneno kati ya Rais Kikwete
na Kagame kunatosha kuwa ugomvi kati ya nchi hizi mbili kwani hili
lisipotazamwa vizuri linaweza kufifisha matumani ya wananchi wa nchi
hizi mbili kuishi kama ndugu ndani na nje ya mipaka yetu.
Mheshimiwa Spika,
Tanzania imejaa wageni
wengi kutoka nchi mbalimbali kama vile Bangladesh, India, China,
Pakistan, na nchi nyingene za Afrika na Afrika Mashariki wanaofanya kazi
hapa nchini katika fani na taaluma ambazo watu wetu wanazo. Kambi
Rasmi ya Upinzani inahoji kama ni sera ya Serikali hii ya CCM kutoa
kipaumbele cha ajira kwa wageni katika fani, ujuzi na taaluma ambazo
watanzania wanazo. Aidha, tunaitaka serikali kupitia idara ya uhamiaji
na idara nyingine za serikali kupitia takwimu za wageni waliopo nchini
na shughuli wanazozifanya ili kuona kama wageni hao wana uhalali wa
kuendelea kuwepo na kufanya kazi nchini ikiwa hakuna kazi inayohitaji
taaluma maalumu (special skills) ambazo watu wetu hawana.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
Kila
aliyepata fursa ya kusikiliza kwa makini maoni haya ya Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni angetaka kuona tunatoa suluhisho gani juu ya nini
kifanyike kuhusu mambo haya. Hata sisi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
tunafikiri ni vyema kushauri na kusaidia kuonyesha njia muafaka ili
kuliokoa taifa letu na mateso haya, lakini tunapata wakati mgumu
kuishauri Serikali ambayo imepoteza thamani ya utu dhidi ya watu wake.
Hivyo basi, kama kuna mambo ya kushauri, basi tungeshauri yafuatayo:
Moja: Mungu asaidie Serikali hii ya CCM iondoke
madarakani mapema kabla haijaharibu mfumo wa kumpata kiongozi kwa njia
ya demokrasia kwani hali ikiendelea hivi; iko siku watu wataingia
barabarani. Hali hii tayari imeshaanza kujitokeza kwani mwaka Kwa
kipindi cha Januari hadi Desemba 2013 pekee watu 1669 waliuwawa kwa
sababu ya watu kujichukulia sheria mkononi. Tunajua watu
watakapojitokeza kudai haki zao na kupinga uonevu watapigwa mabomu ya
machozi, risasi, na vitisho na mateso mbali mbali lakini tunajua
hawatarudi nyuma; kwani watakuwa wamedhamiria kujitetea na kuwatetea
ndugu zao na nchi yao dhidi ya mateso, ukandamizaji, uonevu na dhiki
inayotokana na mambo hayo. Kinyume chake, yatakapotokea hayo, Serikali
itakuwa imetangaza ukomo wa utawala wa kidemokrasia na hilo linaweza
kuwa chimbuko la machafuko na umwagaji damu, hivyo ni vyema waumini wa
imani mbalimbali wafanye dua na sala ili Serikali hii ya CCM iondoshwe
madarakani katika uchaguzi mkuu ujao kwa amani.
Pili: Siku Serikali hii ya CCM ikijua kuwa nguvu ya
Mfalme ni watu na sio bunduki na mabomu ya machozi, siku hiyo ndipo
mtakapoanza kupata hekima ya kuheshimu utu wa binadamu na kile
kinachoonekana sasa kama mateso, udhalimu na ukandamizaji vinaweza
kurekebishwa.
Tatu: Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
kutambua kuwa heshima ya kiongozi haijengwi kwa uwezo wa mali wala
utawala bali katika kazi njema, heshima, utu, na upendo. Ikiwa Serikali
itaelewa hivyo; basi wajibu wake katika kutafuta na kupigania maisha ya
mtu mmoja mnyonge anayeteswa na kudhalilishwa itakuwa ndio hazina na
heshima kubwa kwa viongozi wa serikali na taifa kwa jumla.
Mwisho: Tunafahamu kwamba ndani ya Serikali kuna
watu wengi waadilifu na wenye dhamira njema na nchi yetu. Hata hivyo,
wanashindwa kuchukua uamuzi wa kukemea uovu kutokana na utamaduni wa
Serikili kuwatisha na kuwawekea vikwazo mbalimbali watu wa namna hiyo.
Kutokana na hali hiyo, jamii yetu imejengwa katika fikra za hofu na woga
kwa mambo ambayo yanahitaji uamuzi thabiti na kauli za kijasiri ili
kulinusuru taifa na maangamizi.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inataka Serikali ijue na wananchi wote wajue kwamba;“Dhambi
mbaya na kubwa kuliko zote Duniani ni woga”. Hivyo Basi Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inawaasa viongozi wachache wenye dhamira njema kwamba
waache woga wasimamie misingi ya haki na ukweli hata kama gharama zake
ni Maisha yao kwani msingi wa Taifa letu la kesho unajengwa na viongozi
na utawala ulioko madarakani leo.
Mheshimiwa Spika,
Baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, naomba kuwasilisha.
Godbless Jonathan Lema (Mb)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI NA
WAZIRI KIVULI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI
Imesomwa leo, tarehe 15 Mei, 2014
No comments:
Post a Comment