HOTUBA YA WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA MHESHIMIWA ASHA-ROSE
MTENGETI MIGIRO (MB) AKIWASILISHA BUNGENI MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA
MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2014/2015
A. UTANGULIZI
1. Mheshimiwa
Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo ndani ya Bunge lako
tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, naomba kutoa hoja
kwamba Bunge lako tukufu likubali kupokea, kujadili na kupitisha Mpango na
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa
mwaka 2014/2015.
2. Mheshimiwa
Spika, ninasimama mbele ya Bunge lako tukufu kwa mara ya kwanza
toka niteuliwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Mheshimiwa Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete, kuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Kwa hiyo kabla ya
kuwasilisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara
ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2014/2015, naomba nichukue fursa hii kumshukuru
sana Mheshimiwa Rais kwa kunipa heshima hii kubwa. Ninapenda kumhakikishia
Mheshimiwa Rais na Watanzania wenzangu wote kwamba nitafanya kazi kwa bidii,
uadilifu na kujituma kwa uwezo wangu wote.
3. Mheshimiwa
Spika, naomba sasa uniruhusu nitoe pole zangu za dhati kwako
kufuatia vifo vya wabunge mahiri, Mheshimiwa Dkt. William Augustao Mgimwa,
aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Kalenga na Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamhuri
ya Muungano ya Tanzania; na Mheshimiwa Saidi Ramadhani Bwanamdogo, aliyekuwa
Mbunge wa jimbo la Chalinze. Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi.
4. Mheshimiwa
Spika, ninayo furaha kuwapongeza wabunge wenzangu ambao ni
wapya, Mheshimiwa Yusuf Salim Hussein, kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa jimbo la
Chambani; Mheshimiwa Godfrey William Mgimwa kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa
jimbo la Kalenga; na Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Kikwete kwa kuchaguliwa kuwa
Mbunge wa jimbo la Chalinze. Ninawatakia kheri na mafanikio katika majukumu yao
mapya.
5. Mheshimiwa
Spika, kwa namna ya pekee natoa pongezi na shukurani zangu
za dhati kwa Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda, Mbunge wa jimbo la Mpanda
Mashariki, na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, kwa hotuba yake
ambayo imetoa mwelekeo wa ujumla wa shughuli za Serikali kwa mwaka wa fedha
2014/2015.
6. Mheshimiwa
Spika, naomba nitumie fursa hii pia kutoa shukurani zetu za dhati
kwa Waheshimiwa Wajumbe wote wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na
Utawala chini ya uongozi mahiri wa Mwenyekiti wake Mheshimiwa William Mganga
Ngeleja, Mbunge wa jimbo la Sengerema. Maoni, ushauri na maelekezo yao
yameiwezesha Wizara yangu kutekeleza majukumu yake kwa mafanikio. Tutaendelea
kuzingatia ushauri wa Kamati hii wakati tukitekeleza malengo yetu kwa mwaka
huu wa fedha na katika siku zijazo kwa ujumla.
7. Mheshimiwa
Spika, nichukue fursa hii kumpongeza sana Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba na Makamu wake
Mheshimiwa Jaji Augustino Ramadhani kwa kuiongoza vema Tume hiyo. Ninawapongeza
pia wajumbe wote kwa kazi kubwa waliyoifanya. Rasimu ya Katiba
waliyoiwasilisha imetuwekea msingi mzuri wa kujadili uandishi wa Katiba mpya,
jambo ambalo lina mchango wa pekee katika kujenga mustakabali wa taifa letu. Ni
matumaini yangu kwamba tutapata Katiba bora itakayotuongoza kwa miaka
mingi ijayo, itakayoimarisha umoja wetu na itakayoleta utangamano wa
kitaifa na ustawi wa nchi yetu.
B. MUUNDO NA
MAJUKUMU YA WIZARA
8. Mheshimiwa Spika, Wizara yaKatiba na Sheriainajumuisha Mahakama ya Tanzania, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Tume ya Kurekebisha Sheria,Tume ya Utumishi wa Mahakama, Wakala wa Usajili, Ufilisi, na Udhamini (RITA), Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo, na Chuo cha Uongozi wa
Mahakama. Kwa pamoja taasisi
hizi ndizo zinazotekeleza majukumu ya
Wizara kama yalivyoainishwa kwenye Tangazo la Serikali Namba 20 la mwaka 2010.
9. Mheshimiwa
Spika,Wizara ya
Katiba na Sheria kwa
kuzingatia dira yake ya upatikanaji haki kwa watu wote na kwa wakati,
inasimamia na kutekeleza majukumu yafuatayo: masuala
ya kikatiba na kisheria; shughuli za uendeshaji wa mashauri na utoaji
haki; utekelezaji wa haki za binadamu na utawala bora; shughuli za utafiti,
urekebu na uandishi wa sheria; kuishauri na kuiwakilisha Serikali katika
masuala ya kisheria ndani na nje ya nchi; shughuli za usajili, ufilisi na udhamini; kuratibu taasisi za mafunzo zilizo chini yake na
kusimamia maslahi na maendeleo ya watumishi.
C. MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA 2013/2014
10. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka wa fedha 2013/2014 Wizara yangu ilitekeleza malengo
iliyojiwekea ambayo ni yafuatayo: kuratibu
mchakato wa mabadiliko ya Katiba; kusikiliza
na kuendesha mashauri nchini;kusimamia masuala ya haki za binadamu na utawala bora; kutoa huduma za kisheria; kuhakiki
na kushiriki majadiliano ya mikataba mbalimbali; uandishi wa sheria na hati za Serikali; kufanya tafiti na tafsiri ya sheria;kuendesha shughuli za usajili, ufilisi na udhamini; na kuratibu mafunzo ya uanasheria kwa
vitendo na uongozi wa Mahakama. Pia, Wizara iliboresha miundombinu ya utoaji haki; ilitoa elimu na habari kuhusu upatikanajihaki kwa jamii;
iliratibu shughuli za maboresho
ya Sekta ya Sheria na kuimarisha usimamizi na uwajibikaji katika matumizi
ya rasilimali za
umma. Utekelezaji wa majukumu
hayo umefanyika kwa mafanikio na viwango mbalimbali vya utekelezaji.
Kuratibu
Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba
11. Mheshimiwa
Spika, katika kuhakikisha kwamba nchi yetu inakuwa na mfumo
imara wa sheria unaozingatia mahitaji ya wakati tulionao, Wizara ya Katiba na
Sheria ilisimamia na kuratibu mchakato wa kihistoria wa kuandika Katiba.
Tofauti na michakato miwili iliyopita (mwaka 1965 na mwaka 1977), safari hii
mchakato wa kuandika Katiba ulihusisha watu wengi zaidi. Wananchi wameshiriki
moja kwa moja kwa kutoa maoni yaombele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba au
kwa maandishi. Hali kadhalika watashiriki kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu
Katiba inayopendekezwa kupitia kura ya maoni. Aidha, wananchi walipata fursa ya
kupendekeza majina ambayo Mheshimiwa Rais aliyazingatia katika kufanya uteuzi
wa wajumbe wa Tume.
12. Mheshimiwa
Spika, Tume hii ilifanya kazi ya kukusanya maoni kutoka kwa
wananchi moja kwa moja na kupitia mabaraza ya Katiba ya wilaya na ya kitaasisi.
Baada ya zoezi hili Tume iliandaa Ripoti iliyojumuisha Rasimu ya Katiba. Ripoti
hiyo iliwasilishwa kwa Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri
ya Muungano ya Tanzania, na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi mnamo tarehe 30
Desemba, 2013.
13. Mheshimiwa
Spika, baada ya kupokea Ripoti ya Tume, Mheshimiwa Rais aliitisha
Bunge Maalum ambalo lilianza kazi rasmi kwa kupokea Rasimu ya Katiba
iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mheshimiwa Jaji
Joseph Sinde Warioba tarehe 18 Machi, 2014. Tume ilihitimisha kazi zake na kuvunjwa rasmi kwa Tangazo
la Serikali Namba 81 la tarehe 21 Machi, 2014.
14. Mheshimiwa
Spika,Bunge Maalum lilizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Rais tarehe 21
Machi 2014. Hadi sasa Bunge Maalum limefanya kazi ya kuandaa Kanuni za
kusimamia uendeshaji wa shughuli zake za kila siku. Aidha, Bunge Maalum
limejadili Sura ya Kwanza na Sura ya Sita ya Rasimu ya Katiba kama hatua za
awali za uchambuzi wa Rasimu hiyo.
Kuimarisha Haki za Binadamu na Utawala Bora
15. Mheshimiwa
Spika, katika kipindi cha mwaka 2013/2014 Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora imetoa elimu kwa umma katika masuala ya haki za
binadamu na utawala bora. Elimu iliyotolewa ilihusu sheria za ardhi na umiliki
wa mali, ambapo wananchi 8,529 kutoka katika kata 69 na Shehia 7
walifikiwa. Pamoja na kutoa elimu, Tume ilipokea malalamiko 923 ya aina mbalimbali
katika kipindi hicho yakiwemo yale yanayohusu migogoro ya ardhi. Kati ya
malalamiko hayo, malalamiko 324 yalishughulikiwa na kutolewa uamuzi.
16. Mheshimiwa
Spika, Tume iliandaa Mwongozo wa Utawala Bora wenye lengo la
kukuza uelewa katika eneo hili. Jumla ya nakala 25,000 za Mwongozo huo
zilisambazwa kwa watendaji wa ngazi za vijiji na kata ili waweze kuzingatia
misingi ya utawala bora na haki za binadamu wakati wanapotekeleza
majukumu yao.
17. Mheshimiwa Spika, hadhi ya Tanzania kuhusu haki za binadamu
imeendelea kuwa nzuri ndani na nje ya nchi yetu. Ni wajibu wa Wizara yangu
kukuza na kuendeleza mafanikio yaliyokwishapatikana. Wizara imekamilisha Rasimu
ya Taarifa ya utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu hapa nchini ambayo
itawasilishwa kwenye Kamisheni
ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu. Taarifa hiyo inaeleza namna ambavyo
Serikali yetu inatekeleza mikataba mbalimbali ya kitaifa, kikanda na kimataifa
katika kukuza na kulinda haki hizo.
18. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2013/2014, Wizara iliandaa Mpango
Kazi wa Kitaifa wa Haki za Binadamu (2013–2017) uliozinduliwa na Makamu wa Rais
Mheshimiwa, Dkt. Mohamed Gharib Bilal, tarehe 10 Desemba, 2013. Wizara yangu
ina wajibu wa kusimamia na kuratibu utekelezaji wa Mpango Kazi huu katika taasisi kadhaa za umma na za kijamii.
Kupitia Mpango huu wadau mbalimbali watapata fursa ya kujadili na kutekeleza
masuala ya haki za binadamu. Pia ni fursa kwa Wizara kuimarisha usimamizi na
ufuatiliaji wa masuala mbalimbali yanayohusu haki za binadamu na utawala bora.
19. Mheshimiwa Spika, uzinduzi
huo ulikwenda sambamba na uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Haki za
Watoto (2013-2017). Mpango huo uliandaliwa kutokana na tafiti mbili
zilizofanywa juu ya upatikanaji haki kwa watoto wanaokutana na mkono wa sheria
na hali ya watoto wanaokinzana na sheria. Matokeo ya tafiti hizo yaliwezesha
kubaini vipaumbele vya kimkakati ndani ya mkakati wenyewe na hatua madhubuti
zinazopaswa kuchukuliwa katika kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa
Mpango huo.
20. Mheshimiwa
Spika, Wizara yangu inaratibu shughuli za Kamati ya Kitaifa ya
Kuzuia Mauaji ya Kimbari iliyoundwa chini ya Itifaki ya nchi za Maziwa Makuu ya
kuzuia mauaji ya kimbari. Kamati hii ina jukumu la kujenga uelewa na kuishauri
Serikali juu ya viashiria vinavyoweza kuathiri amani na kusababisha vitendo vya
ukatili kwa binadamu. Katika kipindi cha mwaka 2013/2014, pamoja na kutoa elimu
kwa umma juu ya masuala ya amani kupitia redio na luninga, Wizara imewajengea
uwezo viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali katika kulinda amani katika
mikoa ya Arusha, Mbeya, Mwanza, Mjini Magharibi, Morogoro na Tanga. Katika
mikoa hii, viongozi wa dini waliunda Kamati za amani zenye wajumbe kutoka dini
na madhehebu mbalimbali. Kamati hizi zina jukumu la kuhakikisha amani
inadumishwa katika mikoa hiyo.
21. Mheshimiwa
Spika, katika uendeshaji wa shughuli zake, azma ya Serikali ni
kuongeza uwazi katika ngazi zote za utendaji. Ili kufikia lengo hilo Serikali
ilijiunga na Mpango wa Kimataifa wa uendeshaji wa Serikali kwa Uwazi (Open
Government Partnership) mwaka 2011. Tamko la Tanzania katika kutelekeza matakwa
ya ubia huu ni kuweka mazingira ya upatikanaji wa taarifa kuhusu shughuli
zinazofanywa na Serikali. Wizara yangu iliandaa Rasimu ya Waraka wa Baraza la
Mawaziri wa mapendekezo ya kutunga sheria ya haki ya kupata taarifa
kutoka katika taasisi za umma kwa lengo la kuongeza uwazi na uwajibikaji wa
Serikali.
22. Mheshimiwa Spika, pamoja na hali nzuri ya utawala bora na kuzingatiwa
kwa haki za binadamu katika nchi yetu, hivi karibuni kumekuwa na tuhuma nzito
kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu. Tuhuma hizo zilitokana na utekelezaji wa
“Operesheni Tokomeza” ambayo ililenga kuwasaka na kuwafikisha kwenye vyombo vya
Sheria watu wote waliokuwa wanajihusisha na vitendo vya ujangili katika hifadhi
za taifa na mapori tengefu. Kwa kuzingatia uzito wa tuhuma hizo Mheshimiwa Rais
ameunda Tume ya Uchunguzi chini ya Sheria inayohusu uundwaji wa Tume za
Uchunguzi (Commissions of Inquiry Act, Cap. 32). Kuundwa kwa Tume hiyo kulitangazwa katika Gazeti la
Serikali na. 131 la tarehe 2 Mei, 2014. Tume hiyo yenye makamishna watatu (3)
imepewa hadidu za rejea ambazo ni:
(i) Kuchunguza
namna Operesheni Tokomeza ilivyofanyika;
(ii) Kuchunguza
kama maofisa walioendesha Operesheni hiyo walifuata sheria, taratibu na hadidu
za rejea walizopewa;
(iii) Kuchunguza
endapo maofisa walioendesha Operesheni hiyo walivunja sheria, taratibu na
hadidu za rejea zilizotolewa;
(iv) Kuchunguza
kama kuna watu waliovunja sheria wakati wa Operesheni hiyo na kuona kama hatua
walizochukuliwa wenyewe au mali zao zilikuwa sahihi;
(v) Kushauri
hatua zinazopaswa kuchukuliwa kwa mtu yeyote aliyevunja sheria, taratibu na
kwenda kinyume na hadidu za rejea zilizokuwepo katika kutekeleza Operesheni
hiyo;
(vi) Kushauri
mambo yanayopaswa kuzingatiwa wakati wa kuandaa Operesheni nyingine kama hiyo
ili mambo yaliyojitokeza katika Operesheni hii yasijirudie.
Kusikiliza
na kuendesha mashauri
nchini
23. Mheshimiwa
Spika, kwa kuzingatia Dira ya upatikanaji haki kwa watu wote
na kwa wakati, Wizara yangu imeongeza
kasi ya kuendesha na kusikiliza mashauri yaliyosajiliwa Mahakamani. Kasi hiyo imetokana na mikakati mbalimbali na malengo
mahsusi ambayo Mahakama ya Tanzania imejiwekea ya kusikiliza mashauri
kwa ngazi zote za Mahakama. Utaratibu huu unaweka wastani wa idadi ya mashauri yatakayosikilizwa na kila
ngazi ya Mahakama kwa kila mwaka. Katika Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu
lengo ni kumaliza mashauri mapya ndani ya miezi 24, Mahakama ya Hakimu Mkazi
katika muda usiozidi miezi 18 na Mahakama ya Mwanzo kumaliza mashauri
mapya ndani ya miezi 12.
24. Mheshimiwa Spika, mkakati huu umesaidia kupunguza mlundikano wa mashauri
kwa kiasi kikubwa ambapo hadi kufikia Desemba, 2012 Mahakama ya Tanzania
ilikuwa na jumla ya mashauri 114,278 yaliyohusu masuala ya madai, jinai na
ardhi. Katika mwaka 2013 Mahakama ilisajili mashauri mapya ya aina hiyo 168,068
na kufanya idadi ya mashauri yaliyokuwepo kufikia 282,346. Hadi mwezi Desemba
2013 jumla ya mashauri 182,237 yalisikilizwa na kutolewa uamuzi, sawa na
asilimia 65 ya mashauri yote yaliyosajiliwa mahakamani. Mashauri yaliyobaki Mahakamani ni
100,109. (Kiambatisho “A”).
25. Mheshimiwa Spika, mkakati huu umeanza kwa mafanikio ambapo hivi sasa
mashauri mengi yanayosajiliwa Mahakamani yamekuwa yakimalizika katika kipindi
kisichozidi miaka miwili. Wizara yangu itaendelea kubuni njia mbalimbali
zitakazosaidia kuondokana na tatizo la mlundikano wa mashauri na ambalo
linaathiri utoaji haki.
26. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inaratibu na kusimamia
utekelezaji wa mpango wa kutenganisha kazi ya upelelezi wa jinai na uendeshaji
wa mashtaka. Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana hadi sasa ni pamoja na kupungua
kwa tuhuma za wananchi za kubambikiziwa kesi katika Mahakama ambazo Mawakili wa
Serikali wanaendesha mashauri ya jinai na kupungua kwa idadi ya wafungwa na
mahabusu magerezani. Kabla ya kuanza kwa mpango huu, mwaka 2007 kulikuwa na
wafungwa 22,622 na mahabusu 20,210. Tangu wakati huo idadi ya wafungwa na
mahabusu imekuwa ikipungua kadri Wizara inavyoendelea kueneza utekelezaji wa
mpango huu katika mikoa na wilaya mbalimbali. Katika mwaka wa fedha wa
2013/2014 idadi ya wafungwa ilipungua kutoka 16,869 mwezi Juni 2013 hadi
wafungwa 15,659 mwezi Machi 2014 na idadi ya mahabusu ilipungua kutoka 17,046
mwezi Juni 2013 na kufikia mahabusu 16,647 mwezi Machi 2014.
27. Mheshimiwa
Spika, Kurugenzi ya Mashtaka pamoja na Mahakama
ya Tanzania zimeanza kutekeleza utaratibu maalum wa kukamilisha usikilizaji wa
mashauri 28 ya dawa za kulevya yaliyosajiliwa Mahakama Kuu. Mashauri haya
yamepangwa kusikilizwa katika kikao maalumu cha Mahakama Kuu kitakachofanyika
kuanzia mwezi Juni 2014. Mashauri 110 yapo Mahakama za wilaya na mikoa kwa
hatua za awali za kuyaandaa ili yahamishiwe Mahakama Kuu kwa ajili ya
kusikilizwa. Mashauri haya ni yale yenye thamani inayoanzia shilingi milioni
kumi na kuendelea.
28. Mheshimiwa Spika, Wizara
inaendelea na utekelezaji wa mkakati maalumu wa kusikiliza mashauri 9 yajinai ya wizi wa shilingi bilioni 29.8 zilizokuwa katika akaunti ya madeni ya nje
(external payments arrears account - EPA) iliyokuwa Benki Kuu. Hivi
sasa Kurugenzi ya Mashtaka inaendesha jumla ya mashauri 14 yanayotokana na makosa ya
utakatishaji wa fedha kiasi cha shilingi bilioni 56zilizopatikana kwa njia
ya uhalifu,na mashauri mengine 70 ya kukutwa na nyara za Serikali, zenye
thamani ya shilingi bilioni 45
kinyume cha sheria.
29. Mheshimiwa
Spika, kufikia mwezi Aprili 2014 kulikuwa na jumla ya majalada 404
ya uchunguzi wa makosa mbalimbali ya rushwa yaliyowasilishwa katika Kurugenzi
ya Mashtaka kutoka TAKUKURU. Kati ya hayo, majalada 202 yaliandaliwa hati
za mashtaka, 103 yalirudishwa TAKUKURU kwa ajili ya uchunguzi zaidi, na
majalada 98 yanaendelea kufanyiwa uchambuzi.
30. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014 Wizara ikishirikiana na
taasisi mbalimbali iliongeza jitihada zake za kukabiliana na vitendo viovu
wanavyofanyiwa watu wenye ulemavu wa ngozi. Jitihada hizi zimechangia kiasi
kikubwa kupungua kwa idadi ya matukio ya aina hii katika kipindi cha Julai 2013
hadi Mei 2014, ambapo hakuna tukio lolote lililoripotiwa Polisi. Hali hii ni
tofauti na mwaka wa fedha 2012/2013 ambapo matukio matatu yaliripotiwa Polisi.
Hivi sasa Wizara yangu inaendelea na mashauri 9 ya aina hiyo yanayotokana na
matukio ya miaka ya nyuma.
31. Mheshimiwa
Spika, kuhusu mashauri ya ukiukwaji wa Haki za Binadamu,
Wizara yangu iliendesha mashauri 6 kwenye Mahakama ya Afrika ya Haki za
Binadamu na Watu iliyopo Arusha. Mashauri haya yanajumuisha mashauri 4 mapya
ambayo bado yanaendelea na mashauri 2 ambayo yametupiliwa mbali na Mahakama
hiyo kutokana na waombaji kutotimiza matakwa ya sheria.
32. Mheshimiwa
Spika, jumla ya mashauri ya madai ambayo Serikali ilishitaki au
kushitakiwa, na yale yanayohusu Katiba yaliyokuwa Mahakama Kuu, Mahakama ya
Rufani na katika mabaraza ya usuluhishi (mediation and arbitration) katika
kipindi cha Julai 2013 hadi Aprili 2014 ni 750. Kati ya hayo mashauri
yaliyosikilizwa na kutolewa uamuzi ni 89. Serikali ilishinda mashauri 77 yenye
thamani ya Shilingi 2,216,502,356,629 na kuokoa kiasi hicho cha fedha. Serikali ilishindwa mashauri 12 yenye
thamani ya Shilingi 25,986,416,661.
33. Mheshimiwa
Spika, pamoja na jitihada za Serikali za kupambana na vitendo vya
uhalifu, bado kumekuwepo na matukio ambayo baadhi ya watu wamejipatia mali
kinyume cha sheria. Kwa kutambua hilo, Wizara yangu imekuwa ikitenga fedha
kwenye mipango yake ya mwaka kwa ajili ya kujenga uwezo wa Kitengo cha
utaifishaji na urejeshaji wa mali zilizopatikana kwa njia ya uhalifu (Assets
Recovery and Forfeiture Section).Kati ya Julai 2013 na Machi 2014, Mahakama
iliamuru kurejeshwa Serikalini jumla ya mali na fedha zinazofikia thamani
ya zaidi ya shilingi milioni 233 baada ya watuhumiwa kutiwa hatiani.
Kuimarisha
utoaji wa huduma za kisheria
34. Mheshimiwa
Spika, Wizara imeboresha mazingira ya upatikanaji haki kwa
wananchi ikitambua kuwa uwakilishi mbele ya vyombo vya sheria ni haki ya
msingi. Katika kipindi cha Julai 2013 hadi Machi 2014 Wizara iliandaa Rasimu ya
Waraka wa Kutunga Sheria ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ili kuwapa fursa
wananchi kupata msaada wa kisheria. Rasimu ya Waraka huo imewasilishwa
Serikalini. Sheria hii itakapotungwa itawawezesha wananchi wengi wasio na uwezo
kupata ushauri na kuwakilishwa katika vyombo vya sheria.
35. Mheshimiwa
Spika, wakati utaratibu wa kutunga sheria hii ukiwa
unaendelea, Wizara imeanzisha chombo cha mpito kijulikanacho kama
Sekretarieti ya Msaada wa Kisheria, ili kuratibu utoaji wa msaada wa kisheria
kwa wananchi. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014 jumla ya wananchi
12,809 walipata huduma ya msaada wa kisheria kupitia Sekretarieti hii.
Kuhakiki na kushiriki
majadiliano ya mikataba mbalimbali
36. Mheshimiwa
Spika, kwa upande wa mikataba, Wizara yangu imetoa
ushauri wa kisheria kwa Serikali unaozingatia ubora na weledi, na pia
imeendelea kushiriki katika majadiliano mbalimbali ya mikataba ya kibiashara,
mikutano ya kitaifa, kikanda na kimataifa kwa manufaa ya nchi. Katika kipindi
cha Julai 2013 hadi Machi 2014, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilitekeleza
jukumu hili kwa kushiriki katika mikutano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,
Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika, Nchi za Umoja wa Afrika,
Jumuiya ya Ulaya na Umoja wa Mataifa.
37. Mheshimiwa
Spika, ili kulinda maslahi ya nchi katika mikataba kati ya
Serikali na wadau mbalimbali, Serikali imefanya mabadiliko ya Sheria ya Ununuzi
(Public Procurement Act, 2011). Pamoja na mambo mengine, Sheria hii
inazitaka wizara, taasisi na idara za Serikali kupata ushauri wa kisheria kutoka
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kabla ya kufunga mkataba wowote wenye
thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 50. Mabadiliko haya yamechangia kuongezeka
kwa mikataba inayowasilishwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili
ya kuhakikiwa, kutoka mikataba 120 mwaka 2013 hadi mikataba 375 kufikia
Machi 2014. Hali hii imeiepusha Serikali na mikataba isiyo na maslahi kwa
taifa.
Uandishi
wa sheria
na hati
za Serikali
38. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu iliandaa jumla
ya miswada 11 iliyojadiliwa na kupitishwa na Bunge lako tukufu kuwa sheria.
Miswada hiyo ilihusu: Sheria ya Fedha na Sheria ya Matumizi ya Fedha
inayopitishwa wakati wa Bunge la Bajeti; Sheria ya Taifa ya Umwagiliaji; Sheria
ya Vyama vya Ushirika; Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Sheria
ya Kura ya Maoni. Miswada mingine ni Sheria ya Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi
Serikalini, Sheria ya Takwimu, Sheria ya Marekebisho ya Ushuru na Bidhaa na
Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 1) na (Na. 2).
Aidha, Sheria Ndogo 136 zilitayarishwa na kuchapishwa katika Gazeti la
Serikali tayari kuanza kutumika.
Kufanya
utafiti na tafsiri ya sheria
39. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014, Tume ya
Kurekebisha Sheria ilifanya mapitio na utafiti wa mifumo ya sheria mbalimbali.
Utafiti wa kwanza ulihusu mfumo wa sheria wa utatuzi wa migogoro ya ardhi.
Utafiti huu umekamilika na Ripoti yake imekabidhiwa kwa Waziri wa Katiba na
Sheria. Ni azma ya Wizara yangu kuipitia Ripoti hii kwa kushirikiana na Wizara
nyingine zinazoshughulika na utatuzi wa migogoro ya ardhi. Utafiti wa pili
ulihusu mfumo wa sheria inayosimamia huduma ya hifadhi ya jamii kwa wazee.
Mwisho, Tume ilifanya utafiti kuhusu sheria zinazolinda watumiaji wa bidhaa na
huduma ili kubaini upungufu uliopo.
40. Mheshimiwa Spika, ufanisi katika
utekelezaji wa sheria unategemea sana uelewa wa wananchi kuhusu sheria hizo.
Kwa kutambua hiloWizara imetafsiri Sheria 7 kutoka Kiingereza kwenda lugha
ya Kiswahili.Wizara itaendelea kutafsiri Sheria
nyingi zaidi kwa kuzingatia mahitaji ya jamii na uwezo uliopo. Wizara inapenda
kutoa mwito kwa wadau mbalimbali ndani na nje ya Serikali
kuchangia katika kuhamasisha wananchi kuwa na mwamko wa kupenda kusoma na
kuzifahamu sheria za nchi. (Kiambatisho
“B”).
41. Mheshimiwa
Spika, katika kuimarisha ustawi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,
Wizara yangu kwa kushirikiana na nchi wanachama imeendelea kufanya mapitio ya
Sheria zinazosimamia haki za ubunifu na haki miliki (Intellectual
property laws). Lengo ni kuhakikisha kuwa sheria za nchi wanachama
zinawiana na sheria za Jumuiya hiyo kama ambavyo nchi hizo zimekubaliana
katika kutekeleza Itifaki ya Soko la Pamoja.
Kuimarisha
shughuli za Usajili, Ufilisi na Udhamini
42. Mheshimiwa
Spika, usajili wa matukio muhimu ya binadamu (vizazi, vifo, ndoa,
talaka na watoto wa kuasili) unalenga kulinda na kuhifadhi haki za binadamu na
za uraia. Aidha, usajili huu unaiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi kwa
ajili ya mipango mbalimbali ya maendeleo. Katika kipindi cha kuanzia Julai 2013
hadi Machi 2014 Wizara imeboresha mfumo wa usajili wa vizazi kwa kusogeza huduma
hii hadi ngazi za chini kama vile kata na vituo vya tiba. Maboresho haya
yamefanyika kupitia Mpango wa usajili wa vizazi kwa watoto wenye umri wa chini
ya miaka mitano uliozinduliwa rasmi mkoani Mbeya mwezi Julai 2013.
43. Mheshimiwa
Spika, utekelezaji wa mpango huu umeongeza idadi ya watoto wa umri
chini ya miaka mitano waliopatiwa vyeti vya kuzaliwa kutoka watoto 37,090 kabla
ya mpango huu kuanza, hadi 169,477 Machi 2014. Hii ni sawa na ongezeko
la asilimia 31.4 la watoto wote wa umri wa chini ya miaka mitano mkoani
humo. Mbali na usajili huu mkoani Mbeya, Wizara imefanya usajili wa kawaida
katika sehemu nyingine za Tanzania bara wa jumla ya vizazi 493,887, ndoa
14,031, talaka 53, vifo 34,460, na watoto wa kuasili 30. Hali kadhalika jumla ya
hati 182 za wadhamini wa vyama vya siasa, makanisa, misikiti na
mali za vikundi vya kijamii zilisajiliwa.(Kiambatisho
“C”)
Kuimarisha
Taasisi za Mafunzo ya Sheria
44. Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014 Wizara
imeimarisha taasisi ya mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo na Chuo cha
Uongozi wa Mahakama. Hadi kufikia Machi 2014, jumla ya wanafunzi 293 walihitimu
mafunzo ya uanasheria kwa vitendo na kustahili kusajiliwa kuwa mawakili,
ikilinganishwa na mwaka 2012/2013 ambapo wahitimu walikuwa 272. Jumla ya
wanafunzi 896 walihitimu mafunzo kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama, kati ya
hao wahitimu 267 walitunukiwa Stashahada ya Sheria na 629 Cheti cha Sheria.
Vile vile, Wizara imeanzisha Tawi la Chuo cha Uongozi wa Mahakama katika jiji
la Mwanza na kudahili wanafunzi 95 kwa mara ya kwanza mwaka 2013/2014. Jitihada
hizi zitaongeza idadi ya watalaam wenye sifa za kuajiriwa katika fani
mbalimbali za sheria.
Kuboresha
miundombinu ya utoaji haki
45. Mheshimiwa
Spika, ubora wa huduma unaotolewa na taasisi za sheria unategemea
ubora wa mazingira na miundombinu ya utoaji haki. Kwa kuzingatia umuhimu huo,
katika kipindi cha Julai 2013 hadi Machi 2014, Wizara imefanya yafuatayo:-
· Imekarabati
masijala kwenye Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu Kanda za Dar es Salaam na
Mtwara;
· Imepata
washauri elekezi kwa ajili ya kukarabati Mahakama za Mwanzo 10, na
kujenga Mahakama za Mwanzo 25. Utaratibu wa kupata wakandarasi
umetangazwa kwenye magazeti ya tarehe 11 na 12 Mei 2014;
· Imejenga
uzio wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba; kutenga vyumba vya ofisi za majaji na
makatibu muhtasi; na kuziba sehemu ya wazi ya paa;
· Imeboresha
masijala 71 za Mahakama za Mwanzo kwa kuziwekea mfumo wa kielektroniki wa
kutunza kumbukumbu za majalada;
· Imekamilisha
ukarabati wa Mahakama za Mwanzo za Mgandu na Mwamagembe katika mkoa wa Singida;
· Inakamilisha
ujenzi wa bweni la wanafunzi katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama;
· Imefungua
ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika mkoa wa Geita; na
inakamilisha taratibu za kuanza ukarabati wa Ofisi katika mikoa ya Simiyu na
Katavi;
· Imekamilisha
ujenzi wa jengo la Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini;
· Imekamilisha
upembuzi yakinifu wa mradi wa mfumo mpana wa mawasiliano (Wide Area
Network) utakaounganisha Makao Makuu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Kurugenzi ya Mashtaka na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali mkoa ya Dar es
Salaam.
46. Mheshimiwa
Spika, upembuzi yakinifu kuhusu mradi wa e-justiceutakaorahisisha
uendeshaji wa mashauri ya jinai umekamilika. Mradi huu utaunganisha
Mahakama, Magereza na Ofisi za mikoa za Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa njia
ya mtandao. Ripoti ya zoezi hili imewasilishwa Ofisi ya Rais -Tume ya Mipango
na Wizara ya Fedha kwa hatua za maamuzi.
47. Mheshimiwa
Spika, Wizara imetumia fursa za maendeleo zinazotokana na
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kuboresha huduma
zinazotolewa. Mahakama ya Tanzania imejiimarisha katika matumizi ya TEHAMA kwa
kuanzisha mfumo endelevu wa upatikanaji wa takwimu mbalimbali za Mahakama.
Mfumo huo umeanza kufanya kazi katika Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu katika
Divisheni za Biashara, Kazi na Ardhi, na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Itakapofika Desemba 2014 Mahakama Kuu zote nchini, mahakama za mikoa na
mahakama zote za wilaya zitatumia TEHAMA katika ukusanyaji na utunzaji wa
takwimu.
48. Mheshimiwa
Spika, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini umeanzisha utaratibu
wa kupokea taarifa za usajili wa vizazi kupitia simu za mkononi mara tu mtoto
anaposajiliwa kwenye kata au kituo cha tiba. Hivi sasa utaratibu huu unafanyika
mkoani Mbeya kupitia mpango wa kusajili watoto walio na umri wa chini ya miaka
mitano (U5BRI). Sambamba na hilo mwananchi yeyote nchini anaweza akapata
taarifa za huduma za RITA kupitia simu za mkononi kwa kutuma neno RITA kwenda
namba 15584 na Tovuti ya Wakala (www.rita.go.tz).
Elimu kwa Umma
49. Mheshimiwa Spika, Wizara inatambua kuwa wananchi wana nafasi
muhimu katika kuimarisha utawala wa sheria, misingi ya haki za binadamu na
utawala bora. Kwa kuzingatia hilo, Wizara imetoa elimu kwa umma kwa njia
mbalimbali zikiwemo redio na luninga. Katika kipindi cha mwaka wa fedha
2013/2014 Wizara ilirusha vipindi 35 vya redio na vipindi 9 vya luninga
vilivyotoa elimu kuhusu mapambano na rushwa; haki za watoto na misingi ya haki
za binadamu na utawala bora. Vile vile, Wizara iliandaa mikutano ya wadau
katika mikoa ya Rukwa na Tanga kwa lengo la kuwajengea uelewa wa sheria. Pia
Wizara ilishiriki maonesho ambapo jumla ya vitabu 25,000 na vipeperushi 2,800
kuhusu haki za binadamu na misingi ya utawala bora vilisambazwa. Katika
mikutano hiyo, vitabu 500 na vipeperushi 1000 kuhusu historia ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na majukumu ya Wizara vilisambazwa.
Uratibu
na Utekelezaji wa Maboresho ya Sekta ya Sheria
50. Mheshimiwa
Spika, Wizara yangu imetekeleza na kuratibu programu na miradi
mbalimbali ya kuboresha Sekta ya Sheria. Utekelezaji wa Programu ya Maboresho
ya Sekta ya Sheria unalenga kuimarisha mifumo ya utoaji haki na kukuza uwezo wa
taasisi za sheria katika kutoa huduma bora. Hadi sasa Programu hii imewezesha,
pamoja na mambo mengine, kutenganishwa kwa shughuli za upelelezi na mashtaka,
kufanya mapitio ya sheria mbalimbali na kuanzishwa kwa Taasisi ya Mafunzo ya
Uanasheria kwa Vitendo.
51. Mheshimiwa
Spika, katika kipindi cha Julai 2013 hadi Machi 2014, shughuli
nyingine muhimu za kuboresha sekta ya sheria zilizotekelezwa ni pamoja na:-
kufanya tathmini ya hali ilivyo sasa na kuishauri Serikali namna ya kuendeleza
maboresho katika sekta ya sheria; kuimarisha utendaji wa Sekretarieti ya Huduma
ya Msaada wa Kisheria; kuratibu uanzishwaji wa maeneo ya kuhifadhi watoto
waliokinzana na sheria ili kulinda haki zao, na kuimarisha madawati ya jinsia
na watoto katika vituo vya Polisi na Magereza.
52. Mheshimiwa
Spika, maboresho ya sekta ya sheria ni pamoja na mapambano na
rushwa. Wizara yangu ni moja ya taasisi zinazotekeleza mradi wa Uimarishaji wa
Mapambano na Rushwa Tanzania (Strengthening Tanzania Anti-Corruption Action
- STACA) unaolenga kuziba mianya ya rushwa katika taasisi zake. Mradi
huu ulianza kutekelezwa mwaka wa fedha 2011/2012 na unatarajia kukamilika mwaka
2014/2015. Kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014 jumla ya pikipiki 214
zilinunuliwa kwa ajili ya Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo kwa nia ya kuondoa
kero ya usafiri na kuongeza kasi ya usikilizaji wa mashauri. Pia jumla ya
masijala 68 za Mahakama za Mwanzo ziliboreshwa kwa kuwekewa mfumo wa
kielektroniki wa kutunza kumbukumbu za majalada. Mfumo huo umerahisisha
upatikanaji wa taarifa za kimahakama na hivyo kuondoa mianya ya rushwa.
53. Mheshimiwa
Spika, kupitia mradi huu kitengo cha utaifishaji na urejeshaji wa
mali zilizopatikana kwa njia ya uhalifu (Assets Recovery and Forfeiture
Section) kimeimarishwa kwa kupatiwa vitendea kazi ambavyo vimesambazwa katika
ofisi za Mikoa na Wilaya za Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Vifaa hivyo ni
kompyuta 35, mashine za uchapishaji, vitabu vya rejea na samani za ofisi. Hali
kadhalika mawakili 64 wa Serikali wamepatiwa mafunzo kuhusu stadi
za kuendesha mashauri ya rushwa na namna ya kushughulikia mali zinazopatikana
kwa njia ya rushwa. Kwa kuwa Kurugenzi ya Mashtaka ni kiungo muhimu katika
uendeshaji wa kesi na upelelezi, Kurugenzi iliandaa mikutano ya kikazi na
kiutendaji na wadau mbalimbali chini ya Jukwaa la Haki Jinai. Vikao hivyo
vilikuwa kati ya Mawakili wa Serikali Wafawidhi, Wakuu wa Upelelezi wa Mikoa na
Vikosi Tanzania Bara, TAKUKURU, Mkemia Mkuu wa Serikali, Idara ya Uhamiaji,
Idara ya Wanyamapori na Tume ya Uratibu wa Dawa za Kulevya. Lengo la mikutano
hiyo lilikuwa ni kuboresha uchunguzi na uendeshaji wa mashtaka. Ubia huu
unasaidia kukusanya nguvu pamoja ili kuleta ufanisi zaidi katika
utendaji.
54. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014, Wizara yangu ilichukua
hatua za kuziimarisha Kamati za Maadili za Mahakama za mikoa na wilaya. Tume ya
Utumishi wa Mahakama ilifanya ukaguzi wa Kamati za Maadili za Mahakama kwenye
ngazi ya mkoa na wilaya katika mikoa ya Iringa, Njombe na Ruvuma. Katika
ukaguzi huo, Tume ya Utumishi wa Mahakama ilibaini changamoto mbalimbali ikiwa
ni pamoja na ukosefu wa fedha. Wizara imeanza kukabiliana na changamoto hiyo
kwa kuzipatia fedha Kamati za Maadili za Mahakama ngazi za mikoa na wilaya.
Katika mwaka wa 2013/14 jumla ya shilingi 36,000,000 zilitolewa kwa mikoa 18 na
shilingi 136,500,000 kwa wilaya 91.
Kwa
upande wa mawakili, Kamati ya Maadili ya Mawakili wa Kujitegemea (Advocates’
Committee) ilishughulikia malalamiko 18 katika kipindi cha Julai 2013 hadi
Aprili 2014. Kati ya hayo, malalamiko 6 yamekwishatolewa uamuzi.
55. Mheshimiwa
Spika, Wizara yangu imewajengea uwezo watumishi waliopo na kuajiri
watumishi wapya ili kuleta tija na ufanisi katika kutekeleza majukumu yake.
Katika kipindi cha Julai 2013 hadi Machi, 2014 Wizara iliajiri watumishi wapya
541; ilipandisha vyeo watumishi 487; na kuwezesha watumishi 1,081 wa kada
mbalimbali kupata mafunzo ya muda mrefu na mfupi ndani na nje ya nchi.
Utekelezaji
wa masuala mtambuka
56. Mheshimiwa
Spika, Wizara ya Katiba na Sheria inazingatia masuala mtambuka
katika utekelezaji wa majukumu yake. Haya ni kama vile kuingiza masuala ya
jinsia katika sera, mipango na uendeshaji; kuzingatia mahitaji ya watu
wanaoishi na virusi vya UKIMWI; na masuala yanayohusu maadili. Kwa upande wa
kuzingatia jinsia katika ajira jumla ya watumishi 541 waliajiriwa. Kati yao
wanawake ni 241 (44.5%) na wanaume ni 300 (55.5%). Vile vile, jumla ya
watumishi 487 walipandishwa vyeo ambapo wanawake walikuwa 217 (44.56%) na
wanaume walikuwa 270 (55.44%). Aidha, jumla ya watumishi waliopata
mafunzo ni 1,081 kati yao wanawake ni 588 (54%) na wanaume 493(46%) (Kiambatisho
”G”). Aidha, Wizara imeendelea kujenga mazingira mazuri ya kuwawezesha
watumishi wake wa kike na wa kiume kuweka uwiano muafaka wa kutekeleza kazi zao
na vilevile kumudu majukumu ya uzazi na ulezi.
57. Mheshimiwa
Spika, kuhusu masuala ya UKIMWI, watumishi wa Wizara walipata
mafunzo ya jinsi ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya UKIMWI kupitia Kamati
za UKIMWI zilizopo katika Wizara na taasisi zake. Wizara inawahudumia watumishi
wanaoishi na virusi vya UKIMWI kwa matibabu na lishe.
58. Mheshimiwa
Spika, kuhusu masuala ya maadili, mafunzo yametolewa kwa
watumishi 100 wa kada mbalimbali kutoka Kurugenzi ya Mashtaka kwa nia ya kutoa
uelewa wa masuala ya rushwa, kujenga maadili na uhusiano wenye staha
kazini.
MAPATO NA MATUMIZI YA
FEDHA KWA MWAKA 2013/14
Ukusanyaji
wa Maduhuli ya Serikali
59. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014, Wizara yangu ilipanga
kukusanya jumla ya Shilingi 5,250,454,700 kama maduhuli ya Serikali kutoka
vyanzo mbalimbali vya mapato. Hadi kufikia mwezi Machi 2014 Wizara ilikusanya
jumla ya Shilingi 6,007,714,285, sawa na asilimia 114 ya lengo. Tofauti
hii inatokana na ongezeko la makusanyo ya ada za wanafunzi wa Taasisi ya
Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo na maduhuli ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na
Udhamini (RITA).
Mapato na Matumizi ya Fedha 2013/2014
60. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014 Wizara iliidhinishiwa jumla
ya Shilingi 260,656,733,000 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya
maendeleo. Kati ya fedha hizo Shilingi 205,397,547,000 ni matumizi ya kawaida
na Shilingi 55,259,186,000 ni fedha za miradi ya maendeleo. Kati ya fedha za
matumizi ya kawaida, Shilingi 42,537,099,000 ni kwa ajili ya mishahara na
Shilingi 162,860,448,000 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo. Kati ya fedha za
matumizi ya maendeleo Shilingi 44,000,000,000 ni fedha za ndani na Shilingi 11,259,186,000
ni fedha za nje.
61. Mheshimiwa
Spika, kufikia Machi 2014, Wizara imepokea kiasi cha Shilingi
120,363,046,912 sawa na asilimia 46 ya fedha zilizoidhinishwa. Kati ya fedha
hizo Shilingi 110,763,667,097 ni fedha za matumizi ya kawaida, sawa na asilimia
54. Kati ya fedha hizi za matumizi ya kawaida, shilingi 36,312,510,030 ni
mishahara ya watumishi; na Shilingi 74,451,157,067 ni kwa ajili ya matumizi
mengineyo. Fedha za maendeleo zilizopokelewa ni Shilingi 9,599,379,815, sawa na
asilimia 17 ya fedha zote za Maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi
5,157,500,000 ni fedha za ndani na Shilingi 4,441,879,815 ni fedha za nje.
Ufafanuzi wa taarifa hizi unapatikana katika (Kiambatisho ”D”).
D. CHANGAMOTO
ZILIZOPO
62. Mheshimiwa
Spika, pamoja na mafanikio ambayo Wizara yangu imeyapata, zipo
changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati wa kutekeleza majukumu yake.
Changamoto hizi ni pamoja na:
· Bajeti
ndogo inayotengwa ikilinganishwa na mahitaji halisi ya Wizara na taasisi zake;
· Mapokezi
ya fedha kidogo zilizoidhinishwa hayatabiriki na hivyo kuifanya Wizara na
taasisi zake kushindwa kutekeleza Mipango Kazi yao kwa namna endelevu;
· Wizara
kutotengewa fedha za maendeleo za ndani kwa ajili ya ujenzi wa ofisi na
makaazi. Hali hii inazilazimu baadhi ya taasisi za Wizara kutumia pesa nyingi
kwa ajili ya kulipia kodi ya pango, na hivyo kuathiri utekelezaji wa
majukumu ya utoaji haki na mazingira ya kazi;
· Wanafunzi
wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo kutopatiwa mikopo kutoka Bodi
ya Mikopo ya Elimu ya Juu kunachangia kuwepo kwa malalamiko ya mara kwa mara
kutoka kwa wanafunzi na kuathiri utulivu masomoni;
· Uhaba
wa vitendea kazi na rasilimali watu;
· Ongezeko
la matukio ya makosa ya jinai pamoja na mbinu mpya za kutenda uhalifu;
· Kuwepo
kwa mazingira yanayoweza kuhatarisha usalama wa majaji, mahakimu na mawakili wa
Serikali na hivyo kuathiri utendaji kazi wao; na
· Kuongezeka
kwa mmonyoko wa maadili miongoni mwa baadhi ya watendaji wanaoshughulika
na utoaji haki katika sekta ya sheria.
E. MPANGO NA
BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA 2014/2015
63. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015, Wizara yangu imepanga
kuimarisha utekelezaji wa malengo mkakati iliyojiwekea ili kutoa haki kwa watu
wote na kwa wakati. Ili kufikia azma hiyo, Wizara itasimamia na kufuatilia
utekelezaji wa majukumu yake katika maeneo ya kipaumbele yafuatayo:
i. Utekelezaji
wa Katiba ya nchi na Sheria
a) Kufuatilia
mchakato wa kutunga Katiba;
b) Kufanya
maandalizi ya mapitio na marekebisho ya sheria zitakazoguswa na mabadiliko ya
Katiba;
c) Kutoa
elimu ya Katiba kwa wananchi kuhusu taratibu za kimahakama zinazopaswa kuzingatiwa
katika kudai haki;
d) Kushughulikia
maswala ya urekebu wa Sheria;
e) Kushughulikia
uandishi wa Miswada ya Sheria, Sera na Hati za Serikali;
f) Kuhakiki
rasimu za mikataba ya Serikali na kushiriki katika majadiliano yanayohusu
mikataba hiyo.
ii. Kusimamia
na kufuatilia utoaji haki
a) Kusimamia
shughuli za uendeshaji na usikilizaji wa mashauri;
b) Kuziimarisha
Kamati za Maadili za Mahakama katika ngazi ya mikoa na wilaya kwa kuzipa
mafunzo na kuzifanyia ukaguzi. Kazi hii itaanzia katika mikoa ya Dodoma,
Katavi, Mara, Mwanza, Rukwa, Shinyanga, Singida, Tabora;
c) Kuimarisha
utekelezaji wa mpango wa kutenganisha shughuli za upelelezi na mashtaka.
iii. Kulinda
na kuhifadhi haki za binadamu na utawala wa sheria
a) Kuhakikisha
haki za binadamu zinalindwa na kuendelezwa;
b) Kuwasilisha
Bungeni miswada mbalimbali inayohusu upatikanaji wa msaada wa kisheria; kulinda
mashahidi na waathirika wa vitendo vya jinai (witness and victims of crime
protection law); kulinda watu wanaotoa taarifa kwa siri (whistle blowers)
kuhusu vitendo vya uhalifu au vya ukiukwaji wa maadili; marekebisho ya sheria
ya usajili wa vizazi na vifo; sheria ya ufilisi;
c) Kueneza
mfumo wa usajili wa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano katika mikoa
ya Simiyu na Shinyanga;
d) Kuimarisha
usimamizi na uendeshaji wa taasisi
za mafunzo za Wizara.
iv. Kuimarisha
miundombinu ya utoaji haki
a) Kujenga
nyumba za majaji, majengo ya Mahakama na majengo ya Ofisi;
b) Kuimarisha
huduma za masjala;
c) Kufunga
mfumo wa kielektroniki wa e-justice kwa ajili ya usikilizaji
wa mashauri;
d) Kuimarisha
usimamizi na uendeshaji wa Taasisi
za mafunzo za Wizara.
v. Kuboresha
mazingira ya uwekezaji na biashara nchini kupitia Mpango wa Matokeo
Makubwa Sasa
a) Kupunguza
mlundikano wa mashauri katika Mahakama zote;
b) Kuharakisha
ufunguaji na uendeshaji wa mashauri;
c) Kufanya
mapitio na utafiti wa sheria zinazohusu uwekezaji na biashara;
d) Kuhakiki
mikataba mapema na kwa weledi.
vi. Utekelezaji
wa Masuala Mtambuka
a) Kuimarisha
Kamati za Amani za Mikoa kupitia Kamati ya Kitaifa ya kuzuia mauaji ya kimbari
katika mikoa na wilaya. Vilevile, kutoa elimu na hamasa kwa Wabunge, Wanahabari
na wanafunzi wa vyuo vikuu ili kujenga utamaduni wa amani na utangamano kwa
kila Mtanzania;
b) Kuandaa
na kuratibu awamu ya pili ya shughuli za maboresho ya Sekta ya Sheria;
c) Kuimarisha
usimamizi wa maadili na uwajibikaji wa watumishi kazini.
64. Mheshimiwa
Spika, Pamoja na changamoto zilizopo, Wizara yangu imejizatiti
kufanikisha malengo iliyojiwekea katika kutekeleza mpango na bajeti kwa kipindi
cha mwaka 2014/2015.
F. SHUKRANI
65. Mheshimiwa
Spika, naomba nitumie nafasi hii kuwashukuru sana wadau
wetu wa maendeleo kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha Sekta
yetu ya Sheria. Kwa namna ya pekee napenda kushukuru nchi za Canada, Denmark,
Sweden, Uswisi na Uingereza kupitia Mashirika yao ya Maendeleo yaCIDA,
DANIDA, SIDA na DFID. Vilevile, nayashukuru Mashirika na Taasisisi za
Kimataifa zifuatazo: Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia
Watoto (UNICEF), Shirika la Umoja wa Mataifa la
Maendeleo (UNDP) na Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki
(EADB) katika kuchangia maendeleo ya Sekta ya Sheria.
66. Mheshimiwa
Spika, napenda kutoa shukrani za pekee kwa wadau mbalimbali wa
Sekta ya Sheria kwa ushirikiano na ushauri wao uliowezesha kutekelezwa kwa
majukumu ya Wizara kwa mwaka 2013/2014 kama yalivyobainishwa katika hotuba hii.
Ninapenda kumshukuru Mheshimiwa Angellah Jasmine Kairuki (Mb), Naibu Waziri wa
Katiba na Sheria, Mheshimiwa Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu, Mheshimiwa Jaji
Frederick Mwita Werema, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mheshimiwa Fakih A.R
Jundu, Jaji Kiongozi, Ndugu Fanuel E. Mbonde, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba
na Sheria, Ndugu Hussein Kattanga, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, na
Ndugu George Masaju, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
67. Mheshimiwa
Spika, naomba niwashukuru Mheshimiwa Ignas Paul Kitusi,
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. Eliezer M. Feleshi, Mkurugenzi wa Mashtaka,
Bi. Winifrida Korosso, Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria, Bibi.
Mary Massay, Katibu Mtendaji Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora,
Mheshimiwa Jaji Dkt. Gerald Ndika, Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa
Vitendo, Mheshimiwa Jaji Ferdinand Wambali, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa
Mahakama, Ndugu Phillip Saliboko, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa RITA, Bibi Enzel
William Mtei, Katibu Msaidizi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Wakurugenzi wa
Idara na Taasisi zilizo chini ya Wizara yangu na Watumishi wote kwa ushirikiano
na kazi kubwa waliyoifanya katika kuandaa Mpango na Bajeti hii. Mwisho nitoe
shukurani kwa Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kwa kufanikisha uchapishaji wa
hotuba hii.
G. MAJUMUISHO
68. Mheshimiwa
Spika, Sekta ya Sheria ina umuhimu wa pekee katika kuchangia
maendeleo ya nchi kiuchumi, kisiasa na kijamii. Wizara yangu ina wajibu mkubwa
wa kuhakikisha kuwa inakuza na kuimarisha amani, utawala wa sheria na haki za
raia. Kwa kuzingatia dhana hii, napenda kutoa mwito kwa
wananchi wote pamoja na Waheshimiwa Wabunge kuhakikisha kuwa dhamira ya
Serikali ya kulinda amani, utulivu na haki za binadamu inazingatiwa na kupewa
kipaumbele kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
H. MAOMBI
YA FEDHA KWA MWAKA 2014/2015
69. Mheshimiwa
Spika, ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu yaliyopangwa katika
mwaka wa fedha 2014/2015, Wizara yangu inaomba kuidhinishiwa kiasi cha Shilingi
231,372,948,000 kwa ajili ya Taasisi, Idara na vitengo vyake. Kati ya
fedha hizo, Shilingi 134,006,144,000 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na
Shilingi 48,804,234,000 ni Mishahara. Fedha za Maendeleo ni
Shilingi 48,562,570,000, kati ya hizo Shilingi 44,000,000,000 ni fedha za ndani
na Shilingi 4,562,570,000 ni fedha za nje.
Fedha za Matumizi
70. Mheshimiwa
Spika, mchanganuo wa matumizi ya bajeti kwa Mafungu saba ya Wizara
ni kama ifuatavyo:-
Fungu 12: Tume ya
Utumishi wa Mahakama
Matumizi ya
Mishahara Sh. 208,764,000
Matumizi Mengineyo Sh. 2,871,716,000
Matumizi ya Maendeleo
(ndani)
-
Sh. 0.0
Matumizi ya Maendeleo
(nje) Sh.
0.0
Jumla
Sh. 3,080,480,000
Fungu 16: Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Matumizi ya Mishahara Sh.
2,426,898,000
Matumizi Mengineyo Sh. 8,332,865,000
Matumizi ya
Maendeleo
(Ndani)
Sh.
0.0
Matumizi ya Maendeleo
(nje)
Sh.
457,149,000
Jumla Sh. 11,216,912,000
Fungu 35: Kurugenzi ya
Mashtaka
Matumizi ya
Mishahara- Sh. 5,215,201,000
Matumizi
Mengineyo Sh. 16,460,826,000
Matumizi ya Maendeleo
(ndani)
Sh.
0.0
Matumizi ya Maendeleo
(nje)
Sh. 468,299,000
Jumla Sh. 22,144,326,000
Fungu 40: Mfuko wa
Mahakama
Matumizi ya
Mishahara Sh. 35,040,061,000
Matumizi Mengineyo
Sh. 89,660,284,000
Matumizi ya Maendeleo
(ndani)
Sh. 40,000,000,000
Matumizi ya Maendeleo
(nje)
Sh. 1,687,748,000
Jumla Sh. 166,388,093,000
Fungu 41: Wizara ya
Katiba na Sheria
Matumizi ya Mishahara
Sh. 3,154,642,000
Matumizi
Mengineyo Sh.
8,028,651,000
Matumizi ya Maendeleo
(ndani)
-
Sh. 4,000,000,000
Matumizi ya
Maendeleo
(nje)
-
Sh.
1,048,621,000
Jumla - Sh. 16,231,914,000
Fungu 55:Tume ya
Haki za Binadamu na Utawala Bora
Matumizi ya
Mishahara Sh. 2,041,593,000
Matumizi
Mengineyo Sh.
4,795,802,000
Matumizi ya Maendeleo
(ndani)
-
Sh.
0.0
Matumizi ya Maendeleo
(nje)
-
Sh.
900,753,000
Jumla
- Sh. 7,738,148,000
Fungu 59: Tume ya
Kurekebisha Sheria
Matumizi ya
Mishahara Sh.
717,075,000
Matumizi
Mengineyo Sh.
3,856,000,000
Matumizi ya Maendeleo
(ndani)
-
Sh.
0.0
Matumizi ya Maendeleo
(nje)
-
Sh.
0.0
Jumla - Sh. 4,573,075,000
Makusanyo ya Maduhuli ya
Serikali
71. Mheshimwa
Spika, kwa mwaka 2014/2015 Wizara yangu inatarajia kukusanya kiasi
cha Shilingi 8,577,362,121 kama maduhuli ya Serikali, kama
ifuatavyo:-
Fungu 12: Tume ya
Utumishi wa Mahakama
|
Sh.
|
0.0
|
|||
Fungu 16: Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali
|
Sh.
|
4,502,000
|
|||
Fungu35: Kurugenzi
ya Mashitaka
|
Sh.
|
17,103,000
|
|||
Fungu 40: Mfuko wa
Mahakama
|
Sh.
|
4,115,843,000
|
|||
Fungu 41: Wizara ya
Katiba na Sheria
|
Sh.
|
4,434,270,121
|
|||
Fungu 55: Tume ya
Haki za Binadamu na Utawala Bora
|
Sh.
|
5,644,000
|
|||
Fungu 59:Tume ya
Kurekebisha Sheria
|
Sh.
|
0.0
|
|||
JUMLA
|
Sh.
|
8,577,362,121
|
|||
72. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment