HOTUBA YA WAZIRI MKUU, MHESHIMIWA
MIZENGO
PETER PINDA (MB), KUHUSU MAPITIO NA MWELEKEO WA KAZI ZA SERIKALI NA
MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE
KWA MWAKA 2014/2015
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba, kutokana na
Taarifa zilizowasilishwa katika Bunge lako Tukufu na Wenyeviti wa Kamati
za Katiba, Sheria na Utawala; Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa; Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara na Kamati ya Masuala ya
UKIMWI zilizochambua Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako sasa
lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za
Serikali kwa mwaka 2013/2014 na Mwelekeo kwa Mwaka 2014/2015. Aidha,
naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Matumizi ya
Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, Taasisi zilizo chini yake pamoja na Ofisi ya Bunge
kwa mwaka 2014/2015.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote na kwa masikitiko makubwa
naomba
nichukue fursa hii kutoa salamu za pole kwako na kwa Bunge lako
Tukufu kwa kuondokewa na wabunge wawili, Mheshimiwa William Augustao
Mgimwa, aliyekuwa Mbunge wa Kalenga, aliyefariki tarehe 01 Januari, 2014
na Mheshimiwa Saidi Ramadhani Bwanamdogo, aliyekuwa Mbunge wa Chalinze,
ambaye alifariki tarehe 22 Januari 2014. Aidha, niwape pole Wananchi wa
Mkoa wa Mara kwa kifo cha Mheshimiwa John Gabriel Tupa aliyekuwa Mkuu
wa Mkoa huo, kilichotokea tarehe 25 Machi 2014, na kwa Wananchi wa
Wilaya ya Urambo kwa kifo cha Mheshimiwa Anna Magowa aliyekuwa Mkuu wa
Wilaya hiyo, kilichotokea tarehe 24 Septemba 2013. Vilevile, natoa pole
kwa Wananchi wa Wilaya ya Kalambo kwa kifo cha Mheshimiwa Moshi Mussa
Chang’a aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, aliyefariki tarehe 21 Aprili
2014. Naomba pia niwape pole Waheshimiwa Wabunge na Wananchi wote
waliofiwa na ndugu na jamaa zao kutokana na majanga na matukio
mbalimbali tangu nilipowasilisha Bajeti yangu ya mwaka 2013/2014.
Tunamwomba
Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu wote mahali pema Peponi. Amina!
Nichukue fursa hii pia kuwapa pole Wahanga wote wa majanga mbalimbali
yakiwemo mafuriko na ajali za barabarani, na niwashukuru kwa dhati wote
waliotoa misaada ya hali na mali wakati wa ajali na maafa hayo.
3.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2013/2014, Bunge lako
Tukufu limepata Wabunge wapya watatu ambao ni Mheshimiwa Yusuf Salim
Hussein, Mbunge wa Chambani; Mheshimiwa Godfrey William Mgimwa, Mbunge
wa Kalenga; na Mheshimiwa Ridhiwan Jakaya Kikwete, Mbunge wa Chalinze.
Nawapongeza kwa kuchaguliwa kuwawakilisha Wananchi katika Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nawaomba watumie fursa waliyoipata kwa
manufaa ya Wananchi na Taifa kwa ujumla.
MAANDALIZI YA BAJETI
4.
Mheshimiwa Spika, huu ni mwaka wa pili tangu tuanze
utaratibu wa Mzunguko mpya wa Bajeti ambao unatuwezesha kukamilisha
Mjadala wa Bajeti ya Serikali ifikapo tarehe 30 Juni ya kila mwaka.
Taarifa za awali zinabaini kwamba utaratibu huu umeanza kuonesha
mafanikio ya haraka katika utekelezaji wa kazizilizopangwa. Bajeti hii
imeendelea kutayarishwa kwa kuzingatia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi
ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2010; Awamu ya Pili ya Mkakati
wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini Tanzania (MKUKUTA II); Mpango wa
Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Mwaka 2011/12 hadi 2015/16; Dira
ya Taifa ya Maendeleo 2025; Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015; na
Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa (Big Results Now – BRN).
Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya
kipaumbele iliyoainishwa kwenye mipango hiyo ya Kitaifa ili kuleta
maendeleo endelevu na ya haraka yatakayowanufaisha Wananchi wa
Tanzania.
5.
Mheshimiwa Spika, nawashukuru Wajumbe wa Kamati zote za
Kudumu za Bunge lako Tukufu kwa mchango wao mkubwa wakati wa uchambuzi
wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za
Serikali Zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kazi
waliyoifanya ni kubwa na ambayo imetuwezesha kukamilisha maandalizi ya
Bajeti ninayoiwasilisha leo. Maoni na Ushauri wao utazingatiwa wakati wa
kukamilisha mjadala wa Bajeti ya Serikali na utekelezaji wake.
HALI YA SIASA
6.
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla hali ya siasa Nchini ni tulivu
na Vyama vya Siasa vinaendelea kutekeleza majukumu yao. Nchi yetu
inapitia kwenye kipindi cha mpito ambapo tunaandika Katiba Mpya
itakayoweka mustakabali wa mwelekeo wa Taifa letu kwa miaka mingi
ijayo. Nawasihi Wanasiasa na Wananchi wote kwa ujumla kutoa ushirikiano
mkubwa wakati wa maandalizi ya Katiba hiyo ambayo baadaye wananchi wote
wataipigia kura ya maoni. Nawaomba tushindane kwa nguvu ya hoja na si
hoja ya nguvu katika kuandaa Katiba hii ambayo itatuongoza sasa na
vizazi vijavyo.
7.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kukuza na kuimarisha
demokrasia ya vyama vingi Nchini, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa
imeratibu shughuli za Vyama vya Siasa kwa kuhakikisha kunakuwepo na
fursa sawa katika shughuli za siasa Nchini. Hadi Aprili 2014, idadi ya
Vyama vya Siasa vyenye Usajili wa kudumu imefikia 21 baada ya Chama cha
Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kupata usajili wa kudumu mwezi Juni, 2013.
Aidha, Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-TANZANIA),
Chama cha Wananchi na Demokrasia (CHAWADE) na Chama cha Maridhiano na
Uwiano (CMU) vimepata usajili wa muda. Nirejee wito wangu kwa Viongozi
na Wanachama wa vyama vyote vya siasa kuendeleza utamaduni wa
kuvumiliana na kutohamasisha siasa za chuki na vurugu ambazo zinaweza
kutugawa na kuhatarisha amani, utulivu na umoja wa Taifa letu
tulioujenga kwa miaka mingi.
ULINZI NA USALAMA
Usalama wa Raia
8. Mheshimiwa Spika, Nchi yetu imeendelea kudumisha amani na
utulivu kama tunu ya Taifa iliyojengwa na kuimarishwa tangu tulipopata
uhuru. Katika mwaka 2013/2014, Jeshi la Polisi limeendelea kutekeleza
Programu ya Maboresho ya Jeshi na Mkakati wa Kupunguza Uhalifu ambavyo
vimeongeza ushirikiano na wananchi. Jeshi hilo limeongeza Vikundi 1,778
vya Ulinzi Shirikishi na kufikia vikundi 6,798 kwa mwaka 2013 kwa Nchi
nzima. Vikundi hivyo vimechangia kupunguza vitendo vya uhalifu Nchini
kutoka Asilimia 4.3 mwaka 2012 hadi Asilimia 2.8 mwaka 2013 na hivyo
kuchangia kupungua kwa makosa makubwa na madogo ya jinai kutoka makosa
566,702 mwaka 2012 hadi makosa 560,451 mwaka 2013.
Mauaji ya Wanawake
9.
Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali
kwa kushirikiana na Wananchi katika kuimarisha ulinzi na usalama wa
raia, hivi karibuni kumetokea wimbi la mauaji ya kikatili dhidi ya
wanawake. Katika kipindi cha Januari hadi Aprili 2014, wanawake wanane
(8) wameuawa kikatili katika Kata za Mugango, Etaro, Nyakatende na
Nyegina Wilayani Butiama. Uchunguzi uliofanyika umebaini kwamba, mauaji
hayo yamefanyika mchana na kwa mtindo unaofanana wa kunyongwa na kanga
au kamba na miili yao kufukiwa kwenye mashimo mafupi au kufichwa
vichakani. Mara zote walengwa ni wanawake wanapokuwa kwenye shughuli zao
za kilimo.
10.
Mheshimiwa Spika, Serikali inalaani vitendo hivyo
visivyokubalika katika jamii na itawachukulia hatua kali za kisheria
wale wote watakaobainika kuhusika kwa namna yoyote. Serikali imechukua
hatua kadhaa za kudhibiti vitendo hivyo vya mauaji ikiwa ni pamoja na
kuwakamata watuhumiwa 26 na kati yao 13 wamefikishwa mahakamani.
Vilevile, Jeshi la Polisi limeunda kikosi kazi kwa ajili ya kudhibiti
hali hiyo na kufanya mikutano ya kuhamasisha jamii kuhusu kuanzisha na
kuimarisha vikundi vya Polisi Jamii. Nitoe wito kwa wananchi wema, wenye
upendo na Nchi yetu kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwenye vyombo
vya usalama ili Sheria ichukue mkondo wake.
Ajali za Barabarani
11.
Mheshimiwa Spika, ajali za barabarani zimeendelea kuwa tishio
kwa maisha ya watu na mali zao. Takwimu za Jeshi la Polisi zinaonesha
kuwa katika mwaka 2013, kulitokea ajali za barabarani 24,480
zilizosababisha vifo vya watu 4,091 na majeruhi 21,536 ikilinganishwa na
ajali 23,604 zilizosababisha vifo vya watu 4,062 na majeruhi 20,037
mwaka 2012. Kwa upande wa pikipiki pekee, mwaka 2012 zilitokea jumla ya
ajali 5,763 na kusababisha vifo 930 na majeruhi 5,532. Mwaka 2013,
zilitokea ajali 6,831 na kusababisha vifo 1,098 na majeruhi 6,578.
Aidha, katika kipindi cha Januari hadi Machi, 2014 zimetokea ajali 1,449
na kusababisha vifo 218 na majeruhi 1,304. Ajali hizi ni nyingi na
zinasababisha vifo vingi na majeruhi ambao wengi wao ni nguvukazi ya
Taifa. Ni vyema ikumbukwe kwamba, Serikali iliruhusu matumizi ya
pikipiki kwa nia njema ya kupunguza matatizo ya usafiri hususan maeneo
ya Vijijini. Hata hivyo, fursa hiyo imeambatana na changamoto ya ajali
nyingi barabarani. Hivyo ni wajibu wa madereva wote kuzingatia sheria za
barabarani na kukidhi vigezo vyote vya kuwa na vibali halali vya
kufanya biashara hizo pamoja na leseni za udereva. SUMATRA, Jeshi la
Polisi, Mamlaka za Serikali za Mitaa, na Mamlaka nyingine zinazohusika
zinatakiwa kukaa pamoja ili kuweka mkakati wa kukabiliana na ajali hizo
ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba Kanuni za Leseni za Usafirishaji
wa Pikipiki na Bajaji za mwaka 2010zinatekelezwa ipasavyo.
Hali ya Mipaka ya Nchi
12.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuliwezesha Jeshi la
Wananchi wa Tanzania kutimiza majukumu yake ya kulinda mipaka ya nchi
yetu na raia wake. Katika mwaka 2013/2014, Serikali imewezesha Wanajeshi
wetu kupata mafunzo mbalimbali katika vyuo vya ndani na nje ya Nchi
pamoja na kushiriki katika mazoezi ya ushirikiano kikanda. Aidha, Jeshi
limeshiriki katika operesheni mbalimbali za kulinda amani zinazoongozwa
na Umoja wa Mataifa huko Darfur (Sudan), Lebanon, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo na Sudan Kusini. Nafurahi kulieleza Bunge lako
Tukufu kuwa Jeshi limefanya kazi kubwa, nzuri na kwa weledi mkubwa,
nidhamu na kujituma hivyo kuendelea kuipatia heshima kubwa Nchi yetu.
Katika jitihada za kuwapatia Askari mazingira mazuri ya kuishi, Serikali
imeanza kutekeleza Awamu ya Kwanza ya mradi wa ujenzi wa nyumba za
Askari ambapo ujenzi wa majengo 191 kati ya 6,064 unaendelea katika
vikosi mbalimbali vya Jeshi Nchini.
Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa
13.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2013/2014 ni wa tatu tangu Serikali
iliporejesha utaratibu wa kuwachukua Vijana wanaohitimu kidato cha sita
kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa Mujibu wa
Sheria. Hadi kufikia mwezi Desemba 2013, jumla ya Vijana 15,167
wamehitimu mafunzo ya JKT wakiwemo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wa
Bunge hili Tukufu. Mafunzo hayo yamewapatia vijana hao fursa ya
kujifunza juu ya Ulinzi, Usalama na Ukakamavu, Uzalishaji mali, Uzalendo
na Umoja wa Kitaifa. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itachukua vijana
zaidi kujiunga na JKT kwa Mujibu wa Sheria.
SHUGHULI ZA UCHAGUZI, BUNGE, MUUNGANO, MABADILIKO YA KATIBA NA VITAMBULISHO VYA TAIFA
Tume ya Taifa ya Uchaguzi
14.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Tume ya Taifa ya
Uchaguzi ilisimamia na kuendesha chaguzi ndogo za Wabunge katika Majimbo
matatu na Udiwani katika Kata 53 nchini. Chaguzi hizo zimefanyika
kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo vifo na baadhi ya Waheshimiwa
Madiwani kukosa sifa za kuendelea na nyadhifa hizo. Katika Uchaguzi wa
Ubunge uliofanyika katika Jimbo la Chambani - Zanzibar, CUF ilishinda
kwa kupata Asilimia 84 ya kura zote. CCM ilipata kura Asilimia 12.4, ADC
ilipata kura Asilimia 3.5 na CHADEMA ilipata Asilimia 0.4 ya kura zote.
Katika Jimbo la Kalenga – Iringa, CCM ilishinda kwa kupata Asilimia
79.3 ya kura, CHADEMA ilipata kura Asilimia 20.2 na CHAUSTA ilipata kura
Asilimia 0.5. Katika Jimbo la Chalinze – Pwani, CCM ilishinda kwa
kupata Asilimia 86.61, CHADEMA ilipata kura Asilimia 10.58, CUF ilipata
kura Asilimia 1.98, AFP ilipata kura Asilimia 0.59 na NRA ilipata
Asilimia 0.25 ya kura zote. Aidha, katika Chaguzi za Madiwani
zilizofanyika katika Kata 53, CCM ilishinda viti 40, CHADEMA viti 12 na
NCCR – Mageuzi kiti kimoja (1).
15.
Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea na
maandalizi ya kupata vifaa vya kisasa kwa ajili ya zoezi la kuboresha
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Katika awamu hii ya uboreshaji wa
Daftari, Mfumo wa Biometric Voter Registration utatumika tofauti na
Mfumo wa awali wa Optical Mark Recognition ambao ulikabiliwa na
changamoto nyingi za utendaji. Mfumo huu wa kisasa unawezesha
uandikishaji na uchukuaji wa alama za vidole kwa haraka zaidi na
hatimaye mwananchi kupatiwa kitambulisho cha kupiga kura kwa muda mfupi.
Hii itasaidia sana kuokoa muda na kupata takwimu sahihi za wapiga kura
watakaoshiriki kwenye chaguzi.
16.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwaomba Viongozi wa Vyama
vya Siasa kuhamasisha Wanachama na Watanzania wote wenye sifa
kujiandikisha kwenye Daftari hilo na kupata kitambulisho halali cha
mpiga kura pale zoezi hilo litakapoanza rasmi. Aidha, ninatoa wito kwa
Wananchi wote wenye sifa kujitokeza kujiandikisha. Ni imani yangu kwamba
tukitumia fursa hii kikamilifu tutaondoa malalamiko ya majina ya baadhi
ya wapiga kura kutokuwepo kwenye orodha wakati wa chaguzi. Ni muhimu
tukumbuke kwamba ni wananchi wenye sifa tu ndiyo watakaoandikishwa.
Katika mwaka 2014/2015, Tume itakamilisha zoezi la kuboresha Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura, kusimamia Kura ya maoni kwa ajili ya Katiba Mpya,
na kuendelea kutoa elimu ya Mpiga Kura kwa Wananchi.
Bunge
17.
Mheshimiwa Spika, kuanzia mwezi Julai, 2013 hadi Aprili 2014,
Ofisi ya Bunge imeendesha Mikutano Mitatu ya Bunge na Mikutano mitatu ya
Kamati za Bunge. Maswali ya Msingi 410 pamoja na maswali 73 ya papo kwa
papo kwa Waziri Mkuu yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa.
Aidha, Miswada minane (8) ya Sheria ilipitishwa na Bunge. Pia, Bunge
limekamilisha ukarabati wa Ukumbi wa Bunge na Miundombinu yake kuwezesha
Mkutano wa Bunge la Katiba kufanyika na ujenzi wa Ofisi za Wabunge
Majimboni umeendelea kufanyika. Vilevile, Ofisi ya Bunge imewajengea
uwezo Wabunge na Watumishi wake kupitia semina mbalimbali katika masuala
ya Utawala Bora. Katika mwaka 2014/2015, Ofisi ya Bunge itaendelea
kuratibu Mikutano ya Bunge, Vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge pamoja
na kuimarisha miundombinu na majengo ya Bunge.
Muungano
18.
Mheshimiwa Spika, tarehe 26 Aprili 2014, tumeadhimisha Miaka 50
ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Miaka 50 kwa lugha yoyote ile
siyo kipindi kifupi. Tumeweza kufika hapa tulipo kutokana na misingi
imara ya Muungano iliyowekwa na Waasisi wetu na kuendelezwa na Viongozi
walioongoza Taifa letu katika awamu zilizofuatia. Tunajivunia kwamba
Muungano wa Tanzania umejengeka kwenye historia ya muda mrefu ya
ushirikiano wa watu wa pande hizi mbili. Jamii hizi zina uhusiano wa
damu, kifikra na mapambano ya pamoja dhidi ya wakoloni waliotawala kwa
vipindi tofauti. Walichofanya waasisi wetu mwaka 1964 ni kurasimisha
ushirikiano wetu wa muda mrefu. Nichukue fursa hii kuwashukuru na
kuwapongeza Watanzania wote kwa kuadhimisha Miaka 50 ya Muungano. Aidha,
ninawashukuru kwa dhati Viongozi wote walioongoza Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na Zanzibar tangu kuasisiwa kwa Muungano. Kwa namna ya pekee
namshukuru Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein, Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa Uongozi wao ambao
umezifanya pande mbili za Muungano kuwa karibu zaidi.
19.
Mheshimiwa Spika, tumeadhimisha Miaka 50 ya Muungano tukiwa na
takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012. Takwimu hizo zinaweka
jambo moja wazi kwa Muungano wetu; kwamba zaidi ya asilimia 90 ya
Watanzania wote wamezaliwa baada ya Muungano. Hivyo, tuliozaliwa kabla
ya Muungano ni chini ya asilimia kumi. Kwa mujibu wa takwimu hizo,
Tanzania nzima ina watu 44,926,923. Kati yao, watu 40,640,425, sawa na
Asilimia 90.6 ni wa umri wa siku moja hadi miaka 50. Kwa upande wa
Tanzania Bara, idadi ya watu ilikuwa 43,625,354, kati ya hao,
watu 39,456,065 sawa na asilimia 90.5 wamezaliwa baada ya Muungano. Kwa
upande wa Zanzibar kulikuwa na watu 1,303,569, ambapo watu 1,184,360
sawa na asilimia 90.9 wamezaliwa baada ya Muungano. Takwimu hizo zina
maana kwamba, asilimia 90.6 ya watu wote wamezaliwa ndani ya Muungano na
nchi wanayoifahamu ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sote
tunawajibika kuwatendea haki watu hawa kwa kuulinda, kuuimarisha na
kuudumisha Muungano wetu.
20.
Mheshimiwa Spika, tuna kila sababu ya kuadhimisha Miaka hii 50
ya Muungano kwa furaha. Katika maadhimisho ya mwaka huu, tuliandaa
maonesho maalum, makongamano na shughuli nyingine ambazo zilisaidia
wananchi kuelimishwa kuhusu masuala ya Muungano. Aidha, kimeandaliwa
kitabu maalum kinachoelezea historia, utekelezaji wa mambo ya Muungano,
mafanikio, changamoto, fursa na matarajio ya Muungano kwa miaka ijayo.
Kitabu hicho kitatumika kama rejea kwa kizazi chetu na vizazi vijavyo.
21.
Mheshimiwa Spika, tutaendelea kuulinda Muungano wetu kwa nguvu
zote tukiwa na uelewa kwamba, katika kipindi cha miaka 50 iliyopita
Watanzania wameishi kwa amani na kufanya kazi zao za kujiletea maendeleo
wakiwa upande wowote wa Muungano. Tunatambua changamoto zilizopo na
tumeweka utaratibu mzuri wa vikao ili kuzitafutia ufumbuzi changamoto
hizo. Vikao hivyo vitaendelea kufanyika katika ngazi ya wataalam,
Watendaji Wakuu na Viongozi wa Kitaifa. Ni imani yangu kwamba, Muungano
huu utaendelea kudumu na watu watapata maendeleo makubwa kwani Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ina fursa nyingi zinazoweza kutumika kwa manufaa
ya wote. Sote tukumbuke kuwa, UTANZANIA WETU NI MUUNGANO WETU,
TUULINDE, TUUIMARISHE NA KUUDUMISHA!
Mabadiliko ya Katiba
22.
Mheshimiwa Spika, tarehe 30 Desemba 2013, Tume ya Mabadiliko ya
Katiba ilikamilisha Rasimu ya Pili ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na kuikabidhi kwa Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein,
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Napenda
kuishukuru Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na
Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba kwa kuandaa Rasimu ya Katiba Mpya
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rasimu hiyo imeliwezesha Bunge
Maalum la Katiba kuanza mjadala. Nitumie fursa hii kuwashukuru
Watanzania wote kwa kutoa maoni yaliyowezesha Tume kuandaa Rasimu hiyo
ya Katiba.
23. Mheshimiwa Spika, Bunge Maalum la Katiba linaundwa na
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge wa Baraza
la Wawakilishi na Wajumbe 201 walioteuliwa kwa mujibu wa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011. Naomba nitumie fursa hii kuwapongeza
Wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba kwa kupata fursa hii ya
kuwawakilisha Watanzania katika kuandaa Katiba mpya ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Ni dhahiri kuwa dhamana hii ni kubwa sana!
24.
Mheshimiwa Spika, Bunge Maalum la Katiba lilianza kazi rasmi
tarehe 18 Februari, 2014 kwa kumchagua Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho
kuwa Mwenyekiti wa muda wa Bunge hilo. Nichukue fursa hii kumpongeza
Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kulisimamia
Bunge Maalum hadi kuwezesha kupatikana kwa Kanuni za kuliongoza Bunge
hilo. Aidha, niwapongeze Mheshimiwa Samwel John Sitta kwa kuchaguliwa
kuwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Makamu Mwenyekiti
wa Bunge Maalum la Katiba. Nampongeza Katibu wa Bunge la Katiba Bwana
Yahaya Hamadi Khamis na Naibu wake Dkt. Thomas Kashililah pamoja na
Wajumbe wote waliochaguliwa kuwa Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati
12 za Bunge Maalum. Baada ya kukutana kwa muda wa siku 67, Bunge Maalum
limeahirisha Mkutano wake tarehe 25 Aprili, 2014 ili kupisha
majadiliano ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2014/2015. Ni
matumaini yangu kwamba, Bunge Maalum la Katiba litakaporejea
litakamilisha kazi hiyo kwa umakini na kupata Rasimu ambayo hatimaye
itapelekwa kwa wananchi kwa ajili ya kura ya maoni.
Vitambulisho vya Taifa
25.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu ya Bajeti ya mwaka
2013/2014 nilielezea dhamira ya Serikali ya kutoa Vitambulisho vya Taifa
kwa Wananchi wake. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali
imekamilisha usajili na utambuzi wa watu kwa upande wa Zanzibar,
Watumishi wa Umma na vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na wakazi wa
Mkoa wa Dar es Salaam. Serikali pia, imekamilisha ujenzi wa vituo vya
kuingiza na kuhakiki taarifa, kituo cha kutengeneza Vitambulisho na
kuhifadhi kumbukumbu pamoja na kituo cha uokozi na majanga ya taarifa na
takwimu. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea na zoezi la
Utambuzi na Usajili wa Watanzania katika Mikoa mingine ili kwa pamoja
tuweze kunufaika na Vitambulisho vya Taifa katika nyanja za kijamii,
kiuchumi na kiusalama.
Sensa ya Watu na Makazi
26.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali
imeendelea kutoa machapisho mbalimbali ya matokeo ya Sensa ya Watu na
Makazi ya mwaka 2012. Machapisho hayo yanajumuisha Taarifa ya Mgawanyo
wa Watu kwa Maeneo ya Utawala; Mgawanyo wa Watu kwa Umri na Jinsia na
Taarifa za Msingi za Kidemografia, Kijamii na Kiuchumi. Taarifa hizo
zimebaini kuwa, katika miaka kumi iliyopita kumetokea mabadiliko makubwa
ya kiuchumi na kijamii katika nchi yetu. Kiwango cha watu wanaojua
kusoma na kuandika kimeongezeka kutoka asilimia 69 mwaka 2002 hadi
asilimia 78 mwaka 2012. Aidha, uandikishaji halisi katika shule za
msingi umeongezeka kutoka asilimia 69 mwaka 2002 hadi 77 mwaka 2012.
Idadi ya watu wanaoishi kwenye nyumba zenye kuta imara ni asilimia 74 na
asilimia 65.4 wanaishi kwenye nyumba zilizoezekwa kwa bati. Hata hivyo,
pamoja na mafanikio hayo,
hali ya utegemezi nchini ni kubwa kutokana na ukweli kuwa kati ya
Watanzania Milioni 44.9, Asilimia 50.1 ni watoto wenye umri chini ya
miaka 18. Aidha, takwimu zimebainisha kuwa Asilimia 7.7 ya Watanzania ni
watoto yatima. Kutokana na hali hiyo, ni jukumu letu kama Taifa kuweka
mipango madhubuti ya kukabiliana na changamoto hizo katika sekta za
huduma za jamii ili hatimaye kila mwenye uwezo wa kufanya kazi achangie
ipasavyo katika kukuza uchumi na maendeleo ya nchi yetu.
MASUALA YA UCHUMI
Hali ya Uchumi
27. Mheshimiwa Spika, Pato la Taifa katika mwaka 2013 lilikua
kwa Asilimia 7.0 ikilinganishwa na ukuaji wa Asilimia 6.9 mwaka 2012.
Ongezeko hilo limetokana na ukuaji mzuri wa shughuli za huduma za
mawasiliano, viwanda, ujenzi na huduma za fedha. Kutokana na ongezeko
hilo, wastani wa Pato la Mtanzania limeongezeka kutoka Shilingi
1,025,038 mwaka 2012 hadi Shilingi 1,186,424 mwaka 2013, sawa na
ongezeko la Asilimia 15.7. Mfumuko wa Bei umepungua kutoka Asilimia 9.8
Machi 2013 hadi Asilimia 6.1 Machi 2014. Kupungua kwa mfumuko wa bei
kumechangiwa na kupungua kwa kasi ya kupanda bei za bidhaa na vyakula
hasa mahindi, mchele na aina nyingine ya nafaka.
28.
Mheshimiwa Spika, pamoja na uchumi wetu kukua kwa kasi ya
asilimia 7.0 kwa mwaka 2013 na Pato la Mtanzania kuongezeka, kiwango
hicho siyo kikubwa sana kuwezesha umaskini wa wananchi kupungua kwa
kasi. Utafiti wa kitaalam unaonesha kwamba, ili umaskini upungue kwa
kasi kubwa, uchumi unatakiwa kukua kwa zaidi ya Asilimia 8 kwa kipindi
cha miaka 10 mfululizo. Ukuaji huo pia unatakiwa kulenga Sekta ambazo
zinagusa maisha ya watu wengi, hususan kilimo, mifugo na uvuvi. Mwelekeo
wa Serikali ni kuweka mazingira wezeshi kwa Sekta za kipaumbele kukua
kwa kushirikisha Sekta Binafsi.
Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano
29.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mpango wa Maendeleo wa
Miaka Mitano 2011/2012 – 2015/2016 ambao unatekelezwa katika kipindi cha
mwaka mmoja mmoja. Katika mwaka 2013/2014, Serikali ilitekeleza Mpango
huo kupitia Kauli mbiu ya Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa. Msingi wa
kauli mbiu hii ni kuainisha maeneo machache ya kimkakati na
kuyatengea rasilimali za kutosha, kusimamia na kufuatilia utekelezaji
kwa karibu zaidi. Chombo maalum cha Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa
Miradi ya kimkakati chini ya Ofisi ya Rais kinachojulikana kama
President’s Delivery Bureau – (PDB) kimeanzishwa na Watendaji Wakuu
wameteuliwa. Ninapenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, matunda ya
utekelezaji wa Mfumo huo yameanza kuonekana katika maeneo makuu sita ya
kipaumbele kitaifa ambayo ni Nishati ya Umeme, Uchukuzi, Kilimo, Elimu,
Maji na Ukusanyaji wa Mapato. Utekelezaji wa miradi hiyo na mafanikio
yaliyoanza kupatikana yatatolewa maelezo na Mawaziri katika Sekta
husika.
Maendeleo ya Sekta Binafsi na Uwekezaji
30.
Mheshimiwa Spika, njia ya uhakika ya kuliwezesha Taifa kuwa na
uchumi imara na wa kisasa utakaohimili ushindani katika masoko ya
Kikanda na Kimataifa ni kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji. Katika
kufikia azma hiyo, tarehe 31 Januari, 2014 nilizindua rasmi Taarifa ya
Tathmini ya Sera, Sheria na Kanuni mbalimbali zinazosimamia Uwekezaji
Tanzania. Mapendekezo ya Taarifa hiyo yatatumika kuihuisha Sera ya Taifa
ya Uwekezaji ya mwaka 1996 pamoja na Sheria ya Uwekezaji Tanzania ya
mwaka 1997. Aidha, ili kuwawezesha Wawekezaji na Wafanyabiashara kupata
huduma na taarifa zote muhimu kama vile Sheria, Kanuni na Taratibu
mbalimbali kuhusu biashara na uwekezaji kwa njia ya mtandao, Serikali
imezindua upya Tovuti ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania. Kupitia Tovuti
hii, Wawekezaji popote duniani wanaweza kupata taarifa kuhusu
usajili wa Kampuni na viwango vya kodi kwa njia ya mtandao.
Dhamira
ya Serikali ni kuboresha mazingira ya uwekezaji na kupunguza gharama za
kufanya biashara nchini ili kukabiliana na ushindani mkubwa kutoka nchi
nyingine zilizotekeleza maboresho ya mifumo yao ya udhibiti wa
biashara.
31.
Mheshimiwa Spika, Sekta Binafsi inaendelea kupewa nafasi kubwa
katika kukuza uchumi Nchini. Takwimu zinaonesha kwamba, Miradi
iliyosajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania imeongezeka kutoka 869
yenye thamani ya Shilingi Bilioni 31.5 mwaka 2012 hadi miradi 885
yenye thamani ya Shilingi Bilioni 141.2 mwaka 2013.
Napenda
pia kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Nchi nyingi duniani zinaendelea
kuiamini Tanzania kama Kituo maarufu cha uwekezaji Duniani. Mwezi
Novemba, 2011 nilizindua Mpango wa Ushirikiano kati ya Tanzania na
Uingereza unaojulikana kama Partnership in Prosperity. Mpango huo
umelenga kuongeza uwekezaji kutoka Sekta Binafsi ya Uingereza kwenye
mafuta na gesi, kilimo na Nishati jadidifu. Lengo ni kuongeza uwekezaji
kutoka Nchi hiyo kwa zaidi ya maradufu ya kiwango cha sasa. Aidha,
tumekubaliana kushirikiana kuimarisha mazingira ya biashara ili
kurahisisha uwekezaji katika sekta hizo.
32.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya Kampuni za Uingereza tayari
zimeanza kutekeleza makubaliano hayo kwenye Sekta ya kilimo. Kampuni ya
Unilever kwa mfano, itawekeza zaidi ya Shilingi Bilioni 275 kwenye
kilimo cha chai kwa kushirikiana na wakulima wadogo. Tayari Kampuni hiyo
imeanza kupanua Kiwanda cha Chai Kibwele, Mufindi na kufungua zaidi ya
Hekta 300 za mashamba ya chai katika Wilaya ya Mufindi. Aidha, Kampuni
hiyo imeingiza nchini vipando 250,000 vya miche bora ya chai. Pia,
Kampuni inaandaa zaidi ya miche milioni 2 kwa ajili ya kuwagawia
wakulima wadogo Wilayani Njombe ili waongeze uzalishaji wa chai Nchini.
33.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Kituo cha Uwekezaji
kimeshirikiana na Uongozi wa Mikoa mbalimbali Nchini kuratibu maandalizi
ya Makongamano ya Uwekezaji yenye lengo la kuhamasisha, kukuza na
kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo kwenye Mikoa hiyo.
Jumla ya Mikoa 11 imeshiriki kikamilifu kuandaa na kufanikisha
Makongamano ya Uwekezaji katika maeneo yao. Mikoa hiyo ni Mwanza,
Mara, Kagera, Geita, Simiyu, Shinyanga, Tabora, Manyara, Tanga,
Kilimanjaro na Arusha. Makongamano hayo yamechangia kwa kiasi kikubwa
kuzitangaza fursa za uwekezaji zilizopo kwenye Mikoa hiyo, pamoja na
kuihamasisha Mikoa na Halmashauri za Wilaya ndani ya Mikoa hiyo
kuainisha na kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji. Aidha, Wawekezaji
wengi walioshiriki kwenye Makongamano hayo wameonesha nia na utayari wa
kuwekeza kwenye Mikoa husika. Jitihada hizi zitaendelezwa katika kipindi
kijacho.
Majadiliano na Sekta Binafsi
34.
Mheshimiwa Spika, kwenye hotuba yangu ya Bajeti mwaka 2013/2014,
nilieleza kuhusu Mkutano wa Kimataifa wa Majadiliano ya Ushirikiano kwa
Manufaa ya Wote. Mkutano huo ulifanyika kuanzia tarehe 28 Juni hadi
tarehe 1 Julai 2013, Jijini Dar es Salaam chini ya Uenyekiti wa
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Mkutano huo ulitoa fursa ya kipekee kwa Viongozi wa Serikali
kujadiliana na kupata maoni ya makundi mbalimbali ya Wananchi kuhusu
mbinu za kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Serikali
imedhamiria kufanya Majadiliano ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote kila
mwaka kuanzia ngazi ya Wilaya, Mkoa hadi Taifa kwa kuzingatia fursa
kubwa za maendeleo shirikishi zilizopo kwenye maeneo husika.
35.
Mheshimiwa Spika, Baraza la Taifa la Biashara lilifanya Mkutano wake wa
Saba tarehe 16 Desemba 2013 chini ya Kauli Mbiu ya “Ukuaji Shirikishi
wa Uchumi”. Maazimio ya Mkutano huo ni pamoja na kuunda Kamati Tatu
ambazo zitashughulikia Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Mazingira Wezeshi
ya Biashara na Matumizi Endelevu ya Maliasili za nchi. Kamati ya
Mazingira Wezeshi ya Biashara imeanza kuishauri Serikali kuhusu mikakati
ya kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje na kuongeza ushindani wa
bidhaa za Tanzania. Kazi hiyo imefanyika kwa utaratibu wa Maabara chini
ya Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa. Utaratibu huo ulianzisha
maeneo sita muhimu ambayo yakishughulikiwa yataboresha mazingira ya
biashara nchini. Maeneo hayo ni kuboresha Kanuni na Taasisi
zinazosimamia biashara; upatikanaji wa ardhi na haki za umiliki wake na
kuimarisha ukusanyaji wa kodi na kupunguza wingi wa kodi na tozo
mbalimbali. Maeneo mengine ni kuzuia na kupambana na rushwa; kuboresha
Sheria za Kazi na kuimarisha mafunzo na stadi za kazi pamoja na
kusimamia utekelezaji wa mikataba na utawala wa sheria. Katika mwaka
2014/2015, Baraza la Taifa la Biashara litaendelea kuratibu utekelezaji
wa maazimio hayo ya Mkutano wa Saba sanjari na kusimamia mikutano ya
Mabaraza ya Wilaya na Mikoa.
UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI
36.
Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali ya kubuni na kutekeleza
Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 ni kuhakikisha kwamba
Watanzania wananufaika na rasilimali za nchi yao badala ya kubaki kuwa
watazamaji. Kwa kutambua umuhimu wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi,
katika Mwaka 2013/2014 Serikali imeanzisha Taasisi ya Ujasiriamali na
Ushindani wa Kibiashara (Tanzania Entrepreneurship Competitiveness
Centre). Taasisi hiyo itatekeleza jukumu la kutoa miongozo ya uandaaji
wa mitaala ya ujasiriamali katika ngazi tofauti na kuhamasisha
uzalishaji wa bidhaa bora zitakazohimili ushindani. Aidha, Serikali
imeendelea kusimamia Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na kuongeza
ufanisi wake. Hadi kufikia mwezi Februari 2013, Mfuko wa Uwezeshaji wa
Mwananchi ulikuwa umepokea Shilingi Bilioni 2.1 zilizotumika kudhamini
mikopo ya wajasiriamali kupitia Benki ya CRDB kwa makubaliano ya
kukopesha mara tatu ya dhamana ya Serikali. Kutokana na makubaliano
hayo, hadi kufikia mwezi Desemba 2013, mikopo yenye thamani ya zaidi ya
Shillingi Bilioni 9.5 ilikuwa imetolewa kwa Wajasiriamali 9,790
waliojiunga kwenye Vikundi 283 na Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) 51
katika Mikoa 12 na Wilaya 27.
37.
Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa Mfuko wa Kuendeleza
Wajasiriamali Wadogo na wa Kati, hadi kufikia Desemba 2013, ulikuwa
umetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 36.39 kwa
Wajasiriamali 62,720. Aidha, Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ulikuwa
umetoa mikopo kwa Vijana yenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.22
kupitia SACCOS 244; na Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake ulikuwa
umetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 5.44 kwa
Wanawake 500,000 Nchini. Vilevile, Mradi wa Mikopo kwa Wajasiriamali
Wadogo (SELF) ulikuwa umetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni
57.1 kupitia Asasi 375 za Kifedha ambapo Wajasiriamali 95,034
walinufaika.
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii – TASAF
38.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Awamu ya Tatu ya Mfuko wa Maendeleo
ya Jamii (TASAF III) inatekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini zilizo
katika Mazingira Hatarishi Tanzania Bara na Zanzibar. Katika kutekeleza
Mpango huo, utaratibu wa uhawilishaji fedha kwa kaya maskini ulifanyika
katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 22 ambapo kaya 138,032 katika
Vijiji na Shehia 1,179 zilitambuliwa na kuandikishwa katika Mfumo wa
Masijala wenye walengwa 464,552. Hadi sasa, Shilingi Bilioni 5.5
zimehawilishwa katika kaya hizo. Lengo ni kuziwezesha kaya hizo kupata
chakula na kujiongezea fursa ya kipato.
39.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imejenga uwezo kwa Viongozi na
Wataalam kutoka maeneo ya utekelezaji wa Mpango huo. Uwezo umejengwa kwa
kutoa mafunzo katika masuala ya utambuzi, uandikishaji na ukusanyaji
taarifa za kaya maskini. Aidha, mafunzo ya usanifu wa miradi ya ujenzi
yalitolewa kwa wataalam kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa. Pia,
Wajumbe 17 wa Baraza la Wawakilishi na Wakuu wa Mikoa na Wilaya kutoka
Zanzibar walitembelea Vijiji vya Pongwe-Kiona na Malivundo (Bagamoyo) na
Gwata (Kibaha) ili kujifunza kuhusu utekelezaji bora wa Mpango huo.
Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kufanya utambuzi na
uandikishaji wa kaya maskini kufikia maeneo yote 161 ya utekelezaji wa
Mpango Tanzania Bara na Zanzibar. Lengo ni kutambua na kuandikisha Kaya
920,000 kutoka Vijiji, Mitaa na Shehia 9,000.
UZALISHAJI MALI
Uzalishaji wa Mazao
40. Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa chakula ni ya
kuridhisha katika maeneo mengi nchini kufuatia mavuno mazuri ya msimu wa
2012/2013. Uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu huo ulikuwa Tani
Milioni 14.38 ikilinganishwa na mahitaji ya chakula ya Tani 12.15 kwa
mwaka 2013/2014 ikiwa ni ziada ya Tani Milioni 2.3 za chakula. Ongezeko
hilo limefanya Taifa kujitosheleza kwa chakula kwa Asilimia 118 na
hivyo, kufanya wastani wa bei za mazao ya chakula katika masoko Nchini
kuwa za chini katika kipindi chote cha mwaka 2013/2014.
Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo
41.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na juhudi za kuongeza
tija katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara kulingana na
Mipango inayotekelezwa chini ya Kaulimbiu ya KILIMO KWANZA, na Mpango wa
Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa. Katika mwaka 2013/2014, Serikali
imesambaza jumla ya vocha za ruzuku 2,796,300 zenye thamani ya Shilingi
Bilioni 83 kwa ajili ya mbolea na mbegu bora za mpunga na mahindi kwa
Kaya 932,100. Pia, Serikali ilitoa ruzuku ya dawa za korosho kiasi cha
lita 158,845 na Tani 620 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.5.
Vilevile, ruzuku ilitolewa kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu bora za
pamba Tani 4,000 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 4.8, miche ya kahawa
350,000 yenye thamani ya Shilingi Milioni 100 na miche ya chai 1,850,000
yenye thamani ya Shilingi Milioni 300.
42.
Mheshimiwa Spika, ongezeko la tija katika uzalishaji wa mazao
unategemea sana huduma bora za ugani kwa wakulima. Serikali katika mwaka
2013/2014, ilitoa kibali cha kuajiri Maafisa Ugani 1,452 ili
kufanikisha kufikiwa kwa malengo ya kuwa na Afisa Ugani wa Kilimo mmoja
kwa kila kijiji. Vilevile, Serikali imeongezaMashamba Darasa kutoka
16,330 yenye wakulima 344,986 mwaka 2012/13 hadi 16,543 yenye wakulima
345,106 mwaka 2013/2014 ili kuimarisha utoaji wa mafunzo kwa wakulima.
43.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kushirikisha Washirika wa
Maendeleo kuchangia Programu ya Kuendeleza Kilimo katika Ukanda wa
Kusini mwa Tanzania (SAGCOT). Miongoni mwa malengo ya Programu hiyo ni
kuwaunganisha wakulima wadogo na mnyororo wa thamani wa kibiashara wa
Makampuni makubwa ya ndani na nje ya nchi. Ili kufikia lengo hilo,
Serikali imeanzisha Mfuko Chochezi wa Uendelezaji wa Kilimo katika
Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT Catalytic Trust Fund). Mfuko huo
utatoa mitaji itakayogharamia hatua za awali za miradi inayotoa tija ya
haraka ambayo imebainishwa kwenye Mpango Mkakati wa Uwekezaji. Vilevile,
Mfuko huo utahamasisha biashara inayolenga kumuinua Mkulima mdogo kwa
kumuunganisha na mnyororo wa thamani na kampuni kubwa kupitia madirisha
makuu mawili. Dirisha la kwanza ni Matching Grant Fund linalolenga
kuwezesha kampuni kubwa zilizoanzisha biashara ya Kilimo Nchini,
kuimarisha minyororo ya thamani inayowahusisha wakulima wadogo zaidi au
kuanzisha kilimo cha Mkataba kati ya wakulima wakubwa na wakulima
wadogo. Dirisha la pili ni Social Venture Capital Fund, linalolenga
kuziwezesha biashara changa na za kati kwenye Sekta ya Kilimo au
kuwezesha Kilimo cha mkataba kati ya wakulima wakubwa na wakulima
wadogo. Tayari Bodi ya Mfuko imeteuliwa na Mtendaji Mkuu wa Mfuko
ameajiriwa.
44.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali kupitia
Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa, inategemea kuvutia uwekezaji
na kuanzisha Kilimo cha mashamba makubwa 25 ya Kilimo cha kibiashara
kwa mazao ya mpunga na miwa kwa utaratibu wa kuwaunganisha wakulima
wakubwa na wadogo wanaozunguka mashamba hayo. Aidha, itaanzisha,
itaboresha na kuendesha kitaalamu maghala 275 ya kuhifadhi mahindi kwa
kuwaunganisha wakulima katika umoja wa kibiashara kwa ajili ya kupata
masoko ya pamoja.
Umwagiliaji
45.
Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kuendeleza Kilimo cha
umwagiliaji Nchini, Sheria ya Umwagiliaji Namba 5 ya mwaka 2013 imeanza
kutumika Mwezi Januari, 2014. Sheria hiyo itaiwezesha Serikali kuanzisha
Tume ya Umwagiliaji ambayo ni chombo cha kitaifa chenye dhamana ya
kusimamia, kuendeleza na kudhibiti shughuli za Umwagiliaji Nchini.
Sheria hiyo pia itaanzisha Mfuko wa Taifa wa Umwagiliaji utakaosaidia
kutekeleza mipango ya umwagiliaji kwa kulipia gharama za umwagiliaji
zinazofanywa na mkulima mmoja mmoja na wawekezaji kupitia mikopo na
dhamana. Serikali pia iliendelea na ujenzi na ukabarati wa skimu 24 za
umwagiliaji zilizopo katika wilaya 15 Nchini. Katika mwaka 2014/2015,
Serikali itaendeleza Skimu za Umwagiliaji 39 kwa ajili ya Kilimo cha
mpunga.
Miundombinu ya Masoko ya Mazao
46.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali kupitia
Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za
Kifedha Vijijini imekarabati kilometa 352 za barabara za vijijini kwa
kiwango cha changarawe katika Halmashauri za Iringa Vijijini, Njombe
Vijijini, Singida Vijijini, Mbarali, Lushoto, Same, Mbulu, Msalala na
Mpanda. Halmashauri nyingine ni Maswa, Songea Vijijini, Rufiji, Karatu
na Kwimba. Vilevile, imejenga maghala matano yenye uwezo wa kuhifadhi
tani 1,000 za mazao kila moja katika halmashauri za Iringa Vijijini,
Njombe Vijijini, Same, Songea na Mbarali na kukarabati maghala matatu
katika Halmashauri za Sumbawanga, Mbulu na Kahama. Aidha, Programu hiyo
imezijengea uwezo benki tisa za wananchi/ushirika ili kuimarisha mfumo
wa kifedha Vijijini.
47.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali kupitia
Programu hiyo imepanga kukarabati kilometa 434 za barabara kwa kiwango
cha changarawe, kujenga maghala 14 na masoko saba katika Halmashauri 64
za Tanzania Bara na Wilaya 10 za Zanzibar. Aidha, wazalishaji wadogo
kutoka Mikoa 24 ya Tanzania Bara na Mikoa mitano ya Zanzibar
watajengewa uwezo wa kuhifadhi mazao na mbinu za kufikia masoko ambapo
zaidi ya wananchi 100,000 watanufaika na mafunzo hayo.
Maendeleo ya Ushirika
48.
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Ushirika Namba 6 ya mwaka 2013
imetungwa na imeanza kutumika Mwezi Januari, 2014. Sheria hiyo
itawezesha kuanzishwakwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika ambayo itakuwa na
majukumu ya kusimamia moja kwa moja Vyama vyote vya Ushirika. Aidha,
kupitia Sheria hiyo, Serikali imetoa Waraka Namba 1 wa mwaka 2014
unaotoa ufafanuzi kuhusu Chaguzi katika Vyama vya Ushirika. Ili kuondoa
migogoro ya kimaslahi, Waraka huo umewaondoaViongozi wa Siasa na
Serikali katika uongozi wa Vyama vya Ushirika katika ngazi zote. Katika
mwaka 2014/2015, Serikali itaimarisha uratibu wa Vyama vya Ushirika
kulingana na mahitaji ya Wananchi na kuunganisha Vyama vya Ushirika na
Taasisi za fedha ili kuboresha utoaji wa huduma za kifedha kwa Vyama vya
Ushirika.
Maendeleo ya Sekta ya Mifugo
49.
Mheshimiwa Spika, kupitia Mpango wa Ruzuku ya dawa ya kuogeshea
mifugo, Serikali ilitoa jumla ya lita 11,020 zenye thamani ya Shilingi
Milioni 181.8 na kusambazwa nchini. Vilevile, ilitoa chanjo kwa ajili ya
kudhibiti magonjwa ya mifugo ambapo dozi 150,000 za chanjo ya Ugonjwa
wa Homa ya Bonde la Ufa zenye thamani ya Shilingi milioni 119 ilitolewa
katika Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga na Dodoma. Vilevile,
Serikali imeimarisha Kituo cha Uhamilishaji kilichopo katika eneo la
Usa River, Arusha pamoja na Vituo vingine vitano vya Kanda kwa kusimika
mitambo ya kuzalisha kimiminika cha naitrojeni na kujenga Vituo vitano
vya madume bora. Vilevile, ng’ombe walionenepeshwa wameongezeka kutoka
132,246 mwaka 2011/2012 hadi kufikia 175,000 mwaka 2013/2014. Ili
kuboresha upatikanaji wa maziwa Nchini, Serikali imeongeza uzalishaji
mitamba katika mashamba yake kutoka mitamba 943 kwa mwaka 2012/2013 hadi
mitamba 1,046 mwaka 2013/2014 na kusambaza Mbuzi wa maziwa 9,530
kupitia Mpango wa Kopa Mbuzi lipa Mbuzi. Jitihada hizi, zimesaidia
wafugaji kuongeza tija na hivyo kuchangia ongezeko la uzalishaji wa
maziwa kutoka lita Bilioni 1.9 mwaka 2012/2013 hadi lita Bilioni 2 mwaka
2013/2014.
50.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itatoa
ruzuku ya dawa za kuogesha mifugo na kununua dozi milioni moja kwa ajili
ya chanjo ya ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa kwa Mikoa ya Arusha,
Tanga, Tabora na baadhi ya mikoa katika Kanda ya Ziwa. Vilevile,
Serikali itaimarisha Vituo vya uhamilishaji, mashamba ya kuzalisha
mifugo bora na yale yanayozalisha mbegu bora za mifugo pamoja na kununua
mifugo wazazi.
Maendeleo ya Sekta ya Uvuvi
51.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali kwa
kushirikiana na wadau ilihuisha Sera ya Taifa ya Uvuvi ya mwaka 1997 na
Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya mwaka 2003 ili ziendane na mabadiliko ya
kiuchumi, kisayansi na kiteknolojia. Katika kuimarisha ufugaji wa
samaki, wakulima 2,604 walipewa mafunzo ya ufugaji bora wa samaki na
mabwawa 64 yalichimbwa. Hatua hiyo imeongeza idadi ya mabwawa ya Samaki
kufikia 20,198 yenye uwezo wa kuzalisha Tani 3,029.7 za samaki
ikilinganishwa na mabwawa 20,134 yaliyokuwepo mwaka 2012/2013. Vituo
vya kuzalisha vifaranga wa samaki kwa wingi kwa kutumia teknolojia ya
ndani viliongezeka kutoka kituo kimoja mwaka 2012/2013 hadi kufikia
vituo vitano mwaka 2013/2014 vyenye uwezo wa kuzalisha vifaranga bora
vya samaki Milioni 10 kwa mwaka. Serikali pia, ilijenga matanki sita
yenye lita za ujazo 8,000 kila kimoja kwa ajili ya kuzalisha vifaranga
vya samaki.
52.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itaanzisha
Vituo vya kuzalishia vifaranga vya samaki katika maeneo ya Bacho Dareda -
Manyara, Hombolo – Dodoma, na Kigoma. Vilevile, itajenga bwawa la
kufuga samaki katika Kituo cha Mafunzo ya Kilimo cha Kilimanjaro – KATC;
na kutoa ruzuku kwa ajili ya kuchimba mabwawa na kuzalisha vifaranga wa
samaki.
Ufugaji Nyuki
53.
Mheshimiwa Spika, Sekta ya ufugaji nyuki imeendelea kuimarika
na kuchangia kuongeza ajira na kupunguza umaskini. Mwaka 2013, thamani
ya mauzo ya asali nje yalifikia Shilingi Milioni 287.3 ikilinganishwa na
mauzo ya Shilingi Milioni 262 mwaka 2012. Katika kipindi hicho, jumla
ya Tani 384 za nta zenye thamani ya Shilingi Milioni 4,660 ziliuzwa nje
ikilinganishwa na Tani 277 zenye thamani ya Shilingi Milioni 2,583
zilizouzwa mwaka 2012. Nchi zilizoongoza katika ununuzi wa Asali na Nta
ya Tanzania ni Ujerumani, Oman, China, Japan, Yemen, India, Ubelgiji,
Botswana, Kenya na Marekani. Kutokana na maendeleo haya mazuri katika
mwaka 2013/2014, Serikali imetenga maeneo 20 yenye ukubwa wa Hekta
58,445 sehemu mbalimbali Nchini kwa ajili ya hifadhi za nyuki. Aidha,
imetoa mafunzo kwawafugaji nyuki 924 na vikundi 49 kutoka Wilaya 12
pamoja na kutoa elimu ya miongozo na sheria za ubora wa mazao ya nyuki
kwa wafanyabiashara wa mazao ya nyuki.
54.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Tanzania ilishiriki
kwenye Kongamano la Ufugaji nyuki lililofanyika Kiev, Ukraine. Katika
Kongamano hilo, mazao ya nyuki kutoka Tanzania yalikuwa kivutio kikubwa
na yaliwezesha kupata medali ya Banda Bora la Asali kutokana na asali
yake kuwa na viwango vya ubora na usalama vinavyokubalika Kimataifa.
Aidha, kampuni mbalimbali zilionesha nia ya kuwekeza kwenye Sekta ya
ufugaji nyuki Nchini. Kama ambavyo nimesisitiza mara kwa mara, sekta ya
nyuki ina fursa kubwa ya kibiashara hapa nchini na nje ya nchi. Ni
sekta inayoweza kuleta mapinduzi makubwa katika maeneo mengi kwani
yanahitajika mafunzo kidogo na vifaa vichache ambavyo vinaweza kutumika
kikamilifu kupata asali na mazao yake. Niendelee kusisitiza
kwamba, tuwahimize wananchi katika Majimbo yetu watumie fursa za ufugaji
nyuki zinazopatikana katika maeneo yao ili kujiongezea kipato.
Maendeleo ya Viwanda
55.
Mheshimiwa Spika, Sekta ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo
imeendelea kutoa mchango muhimu katika upatikanaji wa ajira, ongezeko la
kipato na ukuaji wa uchumi. Katika mwaka 2013/2014, Serikali imefungua
Vituo vya Teknolojia Mikoani kwa ajili kuhudumia Wajasiriamali
wanaotengeneza mashine za kusindika mazao na kutengeneza bidhaa
mbalimbali za uzalishaji mali. Vituo hivyo vimewezesha kuanzishwa kwa
miradi mipya 4,127 ya uzalishaji mali kwenye mikoa ya Lindi, Mbeya,
Iringa, Arusha, Kigoma na Kilimanjaro. Aidha, Wajasiriamali 23,546
walipatiwa mafunzo ya ujasiriamali na ujuzi maalum wa ufundi na utumiaji
wa mashine za uzalishaji mali. Vilevile, huduma za ushauri na ugani
zilitolewa kwa Wajasiriamali 20,769 kwenye Vikundi na Vyama vyao vya
Biashara kwa kuviimarisha na kuviwezesha kujenga misingi ya kujitegemea.
56.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mkakati wa “Wilaya
Moja, Bidhaa Moja” kwa kujenga uwezo wa kuzalisha bidhaa kutokana na
malighafi zilizopo kwenye Wilaya husika. Kupitia Mkakati huo, Serikali
imejenga uwezo wa kuongeza thamani ya mazao na bidhaa mbalimbali,
kuzalisha mitambo na vipuri pamoja na zana za kilimo ambapo viwanda
vidogo 198 vilianzishwa na kuwezesha upatikaji wa ajira 1,809. Aidha,
Serikali inatekeleza Mradi wa Kuendeleza Ujasiriamali Vijijini (MUVI)
kwa kutumia dhana ya kuimarisha mlolongo wa thamani kimikoa kwa mazao
mbalimbali. Mradi umewezesha uanzishwaji wa miradi midogo 15,580
Vijijini; urasimishaji wa Vikundi 65,308 vya uzalishaji na upatikanaji
wa ajira 39,574.
57.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia iliendelea na juhudi za
kuhamasisha uwekezaji kwenye miradi mipya katika Maeneo Maalum ya
Uzalishaji (Export Processing Zones) na Maeneo Maalum ya Kiuchumi
(Special Economic Zones). Hadi kufikia mwezi Desemba 2013, kampuni 32
zilikuwa zimesajiliwa na Mamlaka ya EPZ kwa ajili ya kuanzisha viwanda
vipya kwenye maeneo hayo. Aidha, Serikali imekamilisha utafiti kwenye
Mradi wa Makaa ya Mawe Mchuchuma na kuthibitisha uwepo wa tani Milioni
370 za makaa ya mawe katika eneo la kilomita za mraba 30 kati ya
kilomita za mraba 140 zilizotengwa kwa ajili ya Mradi huo. Aidha,
utafiti huo ulithibitisha uwepo wa tani Milioni 219 za madini ya chuma
katika eneo la kilomita za mraba 10 kati ya kilomita za mraba 166
zilizotengwa kwa ajili ya mradi huo. Ujenzi wa mradi wa makaa ya mawe
Mchuchuma na madini ya chuma Liganga unatarajiwa kuanza mwaka 2014 na
kukamilika mwaka 2018. Katika mwaka 2014/2015,
Serikali
itajielekeza katika kuendeleza viwanda vya kuongeza thamani ya mazao na
bidhaa za kilimo. Aidha, itaendelea kujenga Mradi wa Makaa ya Mawe ya
Mchuchuma na Ngaka na Mradi wa Chuma Liganga.
Sekta ya Utalii
58.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutangaza fursa za
utalii zilizopo nchini kwa kutumia mbinu mbalimbali kama vile
vipeperushi, majarida, matangazo ya Televisheni na kutumia Balozi za
Tanzania zilizoko nje ya nchi. Mbinu nyingine zilizotumika ni kutumia
maonesho ya Kimataifa na kuweka matangazo kwenye viwanja sita vya Ligi
Kuu ya Mpira wa Miguu ya Uingereza. Pamoja na matangazo hayo, huduma za
kitalii hususan hoteli, miundombinu ya barabara na mawasiliano
zimeimarishwa na hivyo kuwashawishi watalii wengi kutembelea nchini.
Kutokana na hatua hizo, idadi ya watalii walioingia nchini imeongezeka
kutoka Watalii 1,077,058 mwaka 2012 hadi 1,135,884 mwaka 2013, sawa na
ongezeko la Asilimia 5.46. Watalii hao wameliingizia Taifa Dola za
Marekani Bilioni 1.8 ikilinganishwa na Dola za Marekani Bilioni 1.7
zilizopatikana mwaka 2012. Vilevile, Serikali imeanzisha utalii wa usiku
katika Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara; utalii wa kuangalia wadudu
katika Hifadhi ya Taifa ya Kitulo na Hifadhi ya Amani; utalii wa makasia
katika Hifadhi ya Arusha – Ziwa Momela na Utalii wa kutembea katika
Hifadhi za Mahale na Gombe.
59.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Sekta binafsi
kupitia Baraza la Taifa la Biashara, imeandaa mkakati maalum wa kukuza
sekta ya utalii hasa kuondoa vikwazo vinavyokwamisha kasi ya ukuaji wa
sekta hii. Aidha, katika kukuza utalii wa ndani, Serikali inatumia fursa
za maonesho na matamasha mbalimbali ya ndani kuelezea vivutio vya
utalii na imeandaa kijitabu cha utalii wa Utamaduni kwa lengo la
kutangaza vivutio vya utalii. Katika mwaka 2014/2015, Serikali
itatafsiri tovuti ya Bodi ya Utalii pamoja na vielelezo mbalimbali kwa
lugha za Kifaransa, Kijerumani, Kichina na Kihispaniola ili zitumike
kutangaza utalii kwa nchi zinazotumia lugha hizo. Hatua hiyo itasaidia
kupanua wigo wa utalii katika masoko hayo yenye fursa kubwa.
Wanyamapori
60.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na juhudi za kuhifadhi
wanyamapori katika Hifadhi na Mapori ya Akiba Nchini kwa nia ya
kuwalinda na kuendeleza utalii. Katika mwaka 2013/2014, Serikali
imeendesha doria mbalimbali ndani na nje ya hifadhi zilizowezesha
kukamatwa watuhumiwa 391 pamoja na silaha 73 zikiwemo bunduki 22 za
kivita. Jumla ya kesi 277 zilifunguliwa ambapo kesi 123 zimemalizika na
kesi 154 zinaendelea. Vilevile, katika kuhamasisha wananchi wanaoishi
kando kando ya hifadhi hizo kuzilinda, Halmashauri 38 zenye vitalu vya
uwindaji zilipatiwa Shilingi Bilioni 8.7 kama mgawo wa Asilimia 25 ya
fedha zinazotokana na uwindaji wa kitalii kwa ajili ya shughuli za
maendeleo ya wananchi.
61.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itaanza
utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Ujangili. Mkakati huo
umeainisha uwezo tulionao, upungufu uliopo na mahitaji muhimu ambayo
yataimarisha uhifadhi Nchini na kupunguza migongano iliyopo ya matumizi
ya ardhi. Vilevile, itaanzisha Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania
itakayosimamia shughuli zote zinazohusu uhifadhi wa wanyamapori ikiwa ni
pamoja na kukusanya mapato, kuendeleza hifadhi na kuimarisha ulinzi wa
wanyamapori.
Sekta ya Madini
62.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali imeimarisha
ukaguzi kwenye uzalishaji na biashara ya madini. Hatua zilizochukuliwa
ni pamoja na kuweka Wakaguzi katika migodi yote mikubwa na baadhi ya
mitambo ya uchenjuaji madini. Aidha, imeanzisha dawati maalum la kukagua
madini yanayosafirishwa nje ya Nchi kupitia viwanja vya ndege ili
kudhibiti utoroshaji wa madini. Kutokana na jitihada hizo, madini ya
dhahabu na vito yenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.9 yalikamatwa na
kuwasilishwa kwenye vyombo husika kwa hatua za kisheria.
63.
Mheshimiwa Spika, Serikali inathamini mchango wa Wachimbaji
Wadogo wa Madini katika kukuza uchumi wa Nchi yetu. Katika mwaka
2013/2014, Serikali imewajengea uwezo wachimbaji wadogo kwa kuwapatia
mafunzo na mikopo ili kuongeza uzalishaji. Kutokana na juhudi hizo,
jumla ya kilo 237 za dhahabu zenye thamani ya Shilingi Bilioni 14.5
zilizalishwa na kuingiza mrabaha wa Shilingi Milioni 519. Aidha,
Serikali imetenga maeneo mapya ya uchimbaji ya Isamilo na lwenge
(Geita); Rwabasi (Butiama) na Saza na Itumbi “B” (Chunya). Jitihada hizo
zimefanya shughuli za wachimbaji wadogo hasa katika uchenjuaji wa
madini ya dhahabu kukua.
64.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itakamilisha
Mkakati wa utekelezaji wa Sera ya Madini ya mwaka 2009, Sheria ya
Uongezaji Thamani Madini na Sheria ya Baruti pamoja na Kanuni zake.
Serikali pia itahamasisha uwekezaji kwenye sekta ya Madini na
kuziwezesha taasisi zake kama vile Tanzania Extractive Industrials
Transporency Initiatives (TEITI) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO)
ili ziweze kufanya kazi kwa ufanisi. Vilevile, itatenga maeneo zaidi
kwa ajili ya wachimbaji wadogo na kuwawezesha kupata mitaji na
teknolojia. Pia, itaboresha Mfumo wa utoaji na usimamizi wa leseni za
madini kwa kuanzisha huduma za kuomba leseni kwa njia ya mtandao.
HUDUMA ZA KIUCHUMI
Ardhi
65. Mheshimiwa Spika, ardhi ni msingi na kichocheo muhimu cha
maendeleo ikiwa itapangiwa matumizi bora, itapimwa na kusimamiwa
ipasavyo. Ili kufanikisha azma hiyo, Serikali inachukua hatua
madhubuti kuhakikisha kuwa kila kipande cha ardhi Nchini kinapangwa,
kupimwa, kumilikishwa na kutumiwa kwa mujibu wa Sheria. Katika mwaka
2013/2014, Serikali imekamilisha sehemu ya kwanza ya ujenzi wa Mfumo
Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Ardhi (Integrated Land Management
Information System) na kurahisisha upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya
uwekezaji na matumizi mengine. Sambamba na hatua hiyo, Serikali
inaboresha utunzaji wa kumbukumbu za upimaji Ardhi kwa kuzibadili
zilizopo kuwa katika mfumo wa Kanzidata za Kielektroniki ili ziweze
kuunganishwa na Mfumo Unganishi wa Kutunza Kumbukumbu za Ardhi. Hatua
hiyo inalenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa za upimaji ardhi na
kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Hadi mwezi Februari 2014,
kumbukumbu za ramani 5,000 za Jiji la Dar es Salaam zimebadilishwa na
kuwekwa katika ramani unganishi. Katika mwaka 2014/2015, Serikali
itaandaa Kanzidata ya viwanja 300,000 katika Miji mbalimbali Nchini.
66.
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu Sekta ya Ardhi imekumbwa na
tatizo la migogoro ya mara kwa mara inayotokana na matumizi mbalimbali
ya ardhi hususan baina ya wakulima na wafugaji. Aidha, migogoro hiyo
imekuwa ikihusisha wananchi na maeneo ya hifadhi, Vijiji kuwepo ndani ya
maeneo ya hifadhi, wananchi dhidi ya wawekezaji na baina ya wananchi
wenyewe kwa wenyewe. Migogoro hii imekuwa ikiongezeka zaidi katika siku
za hivi karibuni kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu, mifugo na
shughuli za kiuchumi zinazotegemea ardhi kama vile madini, utalii,
viwanda, kilimo na makazi. Migogoro ya ardhi ina athari kubwa kwa
wananchi ikiwemo uvunjifu wa amani, uharibifu wa mali na hata vifo.
Serikali imekuwa ikichukua hatua kudhibiti migogoro hiyo kila
inapotokea. Ili kupata suluhisho la kudumu la kushughulikia
migogoro ya ardhi, Serikali imeanza kusimika mifumo ya kisasa kwa ajili
ya upimaji, umilikishaji na usimamizi wa sekta ya ardhi. Hii ni kwa
sababu uzoefu umeonesha kwamba ukosefu wa ramani, mipaka rasmi na miliki
kamilifu ndicho chanzo kikuu cha migogoro inayojitokeza mara kwa mara.
Katika mwaka 2014/2015, Serikali itatoa kipaumbele katika Sekta ya
Ardhi hasa kushughulikia maeneo yanayolenga kutatua migogoro ya ardhi
kama vile upimaji wa mipaka ya vijiji, kutoa hati miliki na kuandaa
mipango ya matumizi bora ya ardhi ya Vijiji. Aidha, Serikali itajenga
Mfumo Unganishi wa Kutunza Kumbukumbu za Ardhi, kukamilisha usimikaji wa
alama za msingi za upimaji, kurasimisha hati milki na kupima mipaka ya
Kimataifa.
Nishati
67.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeimarisha huduma za upatikanaji
wa umeme Nchini kwa kutekeleza miradi mbalimbali ili kuongeza idadi ya
Watanzania wanaopata umeme. Mwaka 2013/2014, Serikali imekamilisha kwa
Asilimia 90 Awamu ya Kwanza ya Mradi Kabambe wa Usambazaji wa Umeme
unaotekelezwa katika Mikoa 16 Nchini. Pia, Mradi huo unajumuisha
usambazaji wa umeme Vijijini ambapo wateja 15,305 kati ya wateja 22,000
waliolengwa wameunganishiwa umeme. Vilevile, Wakala wa Nishati Vijijini
imesaini Mikataba 35 na Wakandarasi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya
usambazaji wa umeme Vijijini kupitia Mradi Kabambe wa Usambazaji wa
Umeme Vijijini. Aidha, tarehe 8 Septemba 2013, Mheshimiwa Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua mtambo
wa kufua umeme wa Megawati 60 unaotumia mafuta mazito katika eneo la
Nyakato, Mwanza. Mtambo huo umeongeza uwezo wa kufua umeme kwenye gridi
ya Taifa na kufikia Megawati 1,583. Mtambo huo umeimarisha upatikanaji
wa umeme katika Mikoa ya Mwanza, Geita na Mara. Kutokana na juhudi za
kusambaza umeme Mijini na Vijijini hadi mwezi Machi 2014, zaidi ya
Asilimia 30 ya Watanzania wamepatiwa huduma hiyo, na hivyo kuvuka lengo
la Asilimia 30 lililotarajiwa kufikiwa mwaka 2015.
68.
Mheshimiwa Spika, kutokana na kukua kwa kasi kwa Sekta ya gesi,
Serikali katika mwaka 2013/2014, imeandaa Sera ya Gesi Asilia ambayo
inatoa miongozo ya kusimamia rasilimali hiyo. Serikali pia inatekeleza
miradi mbalimbali chini ya sekta ndogo ya gesi ikiwa ni pamoja na
kuendelea na Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Gesi Asilia kutoka
Mtwara na Lindi hadi Dar es Salaam. Hadi sasa, mabomba yote kwa ajili ya
kutekeleza mradi huo wenye urefu wa Kilomita 542 yamewasili na kazi ya
kuunganisha inaendelea. Ujenzi wa Bomba la Kusafirishia Gesi pamoja na
mitambo miwili ya kuchakata gesi hiyo inatarajiwa kukamilika mwishoni
mwa mwaka 2014. Aidha, Awamu ya Kwanza ya Mradi wa Kinyerezi
utakaozalisha Megawati 150 kwa kutumia Gesi Asilia umeanza
kutekelezwa. Katika hatua nyingine, Serikali imepitia upya miundo ya
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania na Shirika la Umeme Tanzania
kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi wa utendaji wa Mashirika hayo.
69.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itakamilisha
mchakato wa Maboresho ya sera mbalimbali za Nishati ikiwemo Sera ya
Nishati ya Mwaka 2003; Sera Mpya ya Mafuta na Sera Mpya ya Uwezeshaji
Wazawa. Kukamilika kwa sera hizo kutaimarisha usimamizi wa Sekta ya
Nishati kwa maendeleo ya Nchi yetu.
Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano
70.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha Awamu ya Kwanza na ya
Pili ya ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wenye urefu wa
kilomita 7,560 ambao pia unatoa maunganisho ya mawasiliano kwa Nchi
jirani. Awamu ya Tatu ya ujenzi itakayoziunganisha Unguja na Pemba na
Mkongo wa Taifa imeanza mwezi Desemba, 2013 na inatarajiwa kukamilika
katika miezi 18. Mkongo umesaidia watoa huduma kufikisha huduma za
mawasiliano kwa Wananchi kwa uharaka zaidi, uhakika na kwa gharama
nafuu. Hatua hiyo inaharakisha maendeleo ya Taifa kwa Wananchi
kupata fursa ya kutumia TEHAMA katika kupambana na umaskini na kujiletea
maendeleo kwa kasi zaidi. Pia, Serikali kwa kutumia ruzuku imeendelea
kupeleka huduma za mawasiliano katika maeneo yasiyokuwa na mvuto wa
kibiashara kwa kushirikiana na Sekta binafsi. Katika mwaka 2013/2014
jumla ya Kata 52 zenye Vijiji 316 vimefikishiwa huduma za mawasiliano
kupitia Mpango huo. Aidha, Serikali imetia saini makubaliano na watoa
huduma za mawasiliano kufikisha huduma hizo katika Kata nyingine163
zenye Vijiji 922. Watu 1,211,841 watanufaika na juhudi hizo. Katika
mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea na ujenzi wa Mkongo maeneo ya
mijini katika Miji ya Morogoro, Arusha, Mwanza na Dodoma na kuendelea
kuunganisha Unguja na Pemba na Mkongo huo.
Simu za Mkononi na Intaneti
71.
Mheshimiwa Spika, mazingira mazuri yaliyowekwa na Serikali
kwenye Sekta ya Mawasiliano yameonesha matokeo chanya na ya kuridhisha
sana. Idadi ya watumiaji wa huduma za mawasiliano Nchini imeongezeka
kutoka laini za simu za mkononi Milioni 2.96 mwaka 2005 hadi Milioni
27.45 mwaka 2013. Watumaji wa mfumo wa intaneti nao wameongezeka kutoka
Milioni 3.56 mwaka 2008 hadi Milioni 9.3 mwaka 2013. Pia, kuna ongezeko
kubwa la huduma kupitia mawasiliano ya simu za mkononi. Huduma hizo ni
pamoja na miamala ya kifedha na ununuzi wa huduma na bidhaa kwa
kutumia miamala ya kibenki. Hivi sasa wananchi wanaweza kufanya
malipo ya huduma mbalimbali wanazozitumia kupitia simu za kiganjani.
Hatua hiyo imesaidia kuokoa muda na kupunguza msongamano sehemu za
kulipia na kupata huduma hizo.
Mfumo wa Kuhakiki na Kusimamia Huduma za Mawasiliano
72.
Mheshimiwa Spika, Serikali ililiahidi Bunge lako Tukufu kwamba
ingesimika Mfumo wa Kusimamia Mawasiliano ya Simu Nchini. Lengo la
kujenga Mfumo huo ni kubaini takwimu zinazopita katika mitandao ya
mawasiliano. Mfumo huo unaweza kutoa takwimu za mawasiliano
yanayofanyika ndani na nje ya Nchi; kutambua mapato na miamala ya
fedha; kufuatilia na kugundua mawasiliano ya ulaghai; na kutambua
taarifa za laini ya simu na za kifaa cha mawasiliano. Napenda kuliarifu
Bunge lako Tukufu kuwa, tayari Mtambo wa kuwezesha Mfumo wa Kusimamia
Mawasiliano Tanzania umejengwa kwa gharama ya Dola za Marekani Milioni
25 kwa kutumia utaratibu wa Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi
(Build, Operate and Transfer). Ili kuweza kutumia Mfumo huo ipasavyo,
Serikali imekamilisha Kanuni za Uhakiki na Mgawanyo wa Mapato yatokanayo
na simu zinazoingia Nchini kutoka nje ya Nchi. Mfumo huo umeanza rasmi
kutumika mwezi Oktoba, 2013 na kwa kipindi cha miezi mitatu ya Oktoba
hadi Desemba, 2013 umeingizia Serikali Shilingi Bilioni 5. Katika
mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kuboresha taarifa za kiutendaji
zitakazowezesha kupunguza kasi ya udanganyifu wa simu zinazoingia nchini
kwa lengo la kuongeza mapato. Vilevile, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
itasimamia miamala ya malipo ya fedha kupitia simu za mkononi
yanayofanywa na kampuni za simu.
Mfumo wa Utangazaji wa Digiti
73.
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwamba, Serikali ilianza
kutekeleza awamu ya kwanza ya zoezi la kuhama kutoka mfumo wa utangazaji
wa Analojia kwenda Digiti tarehe 31 Desemba, 2012. Awamu hiyo
ilihusisha Miji Saba ya Dar es Salaam, Mbeya, Tanga, Mwanza, Arusha,
Dodoma na Moshi. Uhamaji huo ulifanyika kwa mafanikio makubwa na
tathmini ilifanywa ili kuweka mazingira bora zaidi ya kuendelea na zoezi
hilo. Kufuatia tathmini hiyo, Awamu ya Pili ilianza kutekelezwa kuanzia
tarehe 31 Machi, 2014 na inatarajiwa kukamilika tarehe 30 Septemba,
2014. Miji kumi itakayohusika na zoezi hilo ni Singida na Tabora,
ikifuatiwa na Miji ya Musoma, Bukoba, Kigoma, Kahama, Iringa, Songea,
Morogoro na Lindi. Uzimaji wa mitambo ya utangazaji ya Analojia
unahusisha maeneo yote yanayopata huduma za matangazo kupitia mitambo ya
kusimikwa ardhini tu, ambayo ni Asilimia 24 ya eneo lote la Nchi yetu.
Maeneo yanayopata huduma za matangazo kupitia mitambo ya Satellite
na Cable hayahusiki na zoezi hilo.
Serikali
imelenga ifikapo mwezi Oktoba, 2014 mitambo yote ya Analojia iwe
imezimwa Nchini. Napenda kurudia wito wangu kwamba, zoezi hili ni la
muhimu na lina lengo la kuifanya Nchi yetu iendane na mabadiliko
yanayotokea duniani ambayo hayakwepeki. Wadau wote watoe ushirikiano
kwa vyombo vinavyohusika.
Barabara na Madaraja
74.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali imekamilisha
ujenzi wa kilometa 505.7 za Barabara Kuu na kukarabati kilometa 146.6.
Aidha, imejenga kwa kiwango cha lami kilometa 22.3 za Barabara za Mikoa
na kukarabati kilometa 145.1 kwa kiwango cha changarawe. Serikali
inaendelea kukamilisha ujenzi wa madaraja ya Kigamboni – Dar es Salaam
na Mto Malagarasi - Kigoma. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itajenga
Barabara mpya zenye urefu wa kilometa 633 za Barabara kuu na Barabara za
Mikoa kwa kiwango cha lami. Vilevile, itakarabati kilometa 165 za
barabara za lami na kilometa 1,150 za barabara za changarawe katika
Barabara Kuu na Barabara za Mikoa. Aidha, itaendelea na ujenzi wa
madaraja 57 ya barabara hizo.
Msongamano wa Magari Jijini Dar es Salaam
75.
Mheshimiwa Spika, msongamano wa magari katika Jiji la Dar es
Salaam umekuwa kikwazo katika utekelezaji wa shughuli za kila siku za
kiuchumi na kijamii. Katika kukabiliana na tatizo hilo, mwaka
2013/2014, Serikali imekamilisha ujenzi wa barabara za lami za Ubungo
Bus Terminal - Kigogo - Kawawa yenye urefu wa kilometa 6.4; barabara ya
Jet Corner –Vituka - Davis Corner yenye urefu wa kilometa 10.3 na
barabara ya Ubungo Maziwa - Mabibo External yenye urefu wa kilometa 2.25
pamoja na daraja la External. Ujenzi wa barabara ya Mzunguko wa Kigogo
- Jangwani yenye kilometa 2.72 na zile zitakazotumika kwa Mabasi
yaendayo haraka unaendelea.
76.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itajenga
barabara sita Jijini Dar es Salaam kwa kiwango cha lami. Barabara hizo
ni Tabata Dampo - Kigogo (km 1.6); Kifuru - Kinyerezi (km 4); Goba -
Mbezi Mwisho (km 7); Tangi bovu (Samaki) - Goba (km 9); Kimara Baruti -
Msewe (km 2.6) na Kimara - daraja la Maji Chumvi External (km 3). Tayari
Serikali imesaini mikataba na wakandarasi kwa ajili ya ujenzi wa
barabara hizo ambazo zinatarajiwa kukamilika kati ya miezi 8 hadi 18.
HALI YA UCHUKUZI
Reli ya Kati na TAZARA
77. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali imefanya
upembuzi yakinifu na usanifu wa awali wa ujenzi wa reli ya Arusha –
Musoma yenye urefu wa Kilomita 600. Lengo ni kuimarisha usafiri na
usafirishaji wa mizigo kwa Mikoa ya Kaskazini na Nchi jirani ya Uganda
kupitia Bandari ya Tanga. Vilevile, Serikali imekamilisha usanifu wa
kina wa mradi wa ujenzi wa reli kwa kiwango cha kimataifa yenye urefu wa
Kilometa 1,464 kutoka Dar es Salaam - Isaka - Keza - Kigali na Kilometa
197 kutoka Keza hadi Msongati.
78.
Mheshimiwa Spika, Mkataba wa Maelewano kati ya Tanzania na
Burundi kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya Uvinza hadi Msongati umesainiwa.
Kuhusu Reli ya TAZARA, Serikali inatekeleza Makubaliano ya Itifaki ya
15 iliyosainiwa mwezi Machi, 2012 kati ya Serikali ya Watu wa China na
Serikali za Tanzania na Zambia ambapo ununuzi wa vichwa vinne vya treni,
vichwa vinne vya Sogeza umefanyika pamoja na ununuzi wa mabehewa 18 ya
abiria ya Reli ya TAZARA. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaboresha
Kilometa 308 za miundombinu ya Reli ya Kati na vituo vya Bandari kavu
vya kuhifadhi Makasha vya Ilala na Isaka. Aidha, Kampuni ya Reli (TRL)
itakarabati vichwa nane vya treni na kununua vichwa vipya 12 na
mabehewa 204 ya mizigo na kukarabati majengo ya Stesheni.
Bandari
79.
Mheshimiwa Spika, kijiografia nchi yetu imejaliwa kuwa na eneo
kubwa la maziwa na bahari ambalo limetuwezesha kuwa na bandari
zinazohudumia pia Nchi jirani zisizopakana na bahari. Ili kutumia fursa
hii kikamilifu, Serikali katika mwaka 2013/2014, imekamilisha upembuzi
yakinifu kwa ajili ya kuboresha Gati namba 1 hadi 7 katika Bandari ya
Dar es Salaam. Vilevile, inatekeleza miradi ya ujenzi wa magati kwenye
Bandari za Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa. Aidha, kupitia Mfumo wa
Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa, Mamlaka ya Bandari imevuka malengo
kwa kuhudumia zaidi ya tani Milioni 13 za mizigo hadi Desemba 2013,
ikilinganishwa na tani Milioni 12 kwa mwaka 2012. Vilevile, Serikali
imeanza kutekeleza utaratibu wa kufanya kazi bandarini kwa saa 24 kwa
siku zote za juma ili kuongeza kasi ya uondoshaji wa mizigo inayotoka.
Hatua hiyo imesaidia kupunguza msongamano wa mizigo katika Bandari
ya Dar es Salaam na kupunguza malalamiko kutoka kwa watumiaji wa
bandari hiyo. Aidha, kumekuwa na ongezeko la ufanisi katika kuhudumia
wasafirishaji wa mizigo katika maeneo ya mipakani, hususan Rusumo,
Tunduma, Namanga, Kasumulo na Mtukula. Wasafirishaji wanatumia muda
mfupi hivi sasa ikilinganishwa na hapo awali. Kwa mfano, muda wa huduma
katika mpaka wa Rusumo, umepungua kutoka siku tatu hadi nusu saa.
80.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itaanza
kuboresha Gati namba 1 hadi 7 ili kuwezesha Bandari ya Dar es Salaam
kuhudumia mizigo tani Milioni 18 kutoka tani Milioni 13.5 za sasa.
Aidha, itakamilisha ujenzi wa magati katika Bandari ya Mtwara,
kukamilisha majadiliano na kuanza ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo na
kuendelea na miradi ya ujenzi wa magati kwenye Bandari za Ziwa Victoria,
Tanganyika na Nyasa. Vilevile, itakarabati meli za MV Umoja, MV
Victoria, MV Butiama, MV Serengeti, MV Liemba, MT Sangara, MT Ukerewe na
meli ya MV Songea ili kuboresha usafiri na usafirishaji katika maziwa.
Usafiri wa Anga
81.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeboresha miundombinu ya viwanja
vya ndege Nchini na kuviwezesha kutoa huduma kwa kuzingatia Sheria na
Kanuni za uendeshaji za kimataifa. Katika mwaka 2013/2014, jumla ya
viwanja vya ndege 13 ikiwemo Viwanja vya Mwanza, Musoma, Bukoba, Kigoma,
Tabora, Arusha, Tanga, Lindi, Mtwara, Iringa, Songea, Nachingwea na
Kilwa Masoko vilifanyiwa ukaguzi na kupata leseni ya uendeshaji. Aidha,
Serikali imeanza mradi wa ujenzi wa jengo jipya la tatu la abiria katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere utakaogharimu Shilingi
Bilioni 518. Mradi huo ambao umewekwa jiwe la msingi na Mheshimiwa Dkt
Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 24 Aprili, 2014 unatarajiwa kukamilika
mwezi Oktoba, 2015. Jengo hilo litakuwa na ukubwa wa meta za mraba
70,000 ambao ni zaidi ya mara nne ya ukubwa wa jengo lililopo sasa lenye
ukubwa wa meta za mraba 15,000. Baada ya kukamilika kwa jengo hilo na
miundombinu yake, Uwanja huo utakuwa na uwezo wa kuegesha ndege kubwa za
abiria. Aidha, utahudumia abiria milioni sita kwa mwaka ikilinganishwa
na abiria milioni 2.5 kwa sasa. Vilevile, Uwanja huo utatoafursa
mbalimbali za kiuchumi, kibiashara na kukuza utalii nchini. Aidha,
utazalisha ajira mpya zaidi ya 7,000 kwa Watanzania.
82.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha
miundombinu ya usafiri wa anga ili kuimarisha huduma za usafiri nchini
pamoja na kuvutia uwekezaji na utalii. Kwa kuzingatia azma hiyo, mwezi
Oktoba 2013, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete alizindua rasmi Uwanja wa Ndege wa Mafia baada ya
ujenzi wake kukamilika kwa kiwango cha lami. Kuzinduliwa kwa uwanja
huo kumefungua fursa za kibiashara, hususan ya utalii katika kisiwa
hicho. Vilevile, mwezi Julai 2013, Mheshimiwa Rais, aliweka jiwe la
msingi la ujenzi wa njia ya kuruka na kutua ndege kwa kiwango cha lami
katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba. Katika mwaka 2014/2015, Serikali
itaendelea na ujenzi wa jengo jipya la abiria katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere na kukamilisha ujenzi wa Uwanja mpya wa
Kimataifa wa Ndege wa Songwe, Mbeya. Serikali pia itakamilisha ukarabati
wa Viwanja vya ndege vya Mwanza, Bukoba, Kigoma na Tabora na kuanza
kukarabati viwanja vya ndege vya Shinyanga, Mtwara na Sumbawanga.
MAENDELEO YA SEKTA YA ELIMU
Elimu ya Msingi
83. Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kuwa utoaji wa elimu
unafuata Sera, Miongozo na Mitaala, Serikali imeendelea kupitia Sera ya
Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995. Aidha, kupitia Mfumo wa Tekeleza Sasa
kwa Matokeo Makubwa katika elimu ya msingi, utaratibu wa kupima stadi za
Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (K3) kwa wanafunzi wa darasa la Kwanza na
la Pili umeanzishwa kwa lengo la kupima na kuweka msingi wa kuboresha
stadi husika kabla ya kuingia darasa linalofuata. Katika mwaka huu wa
fedha, Serikali imeajiri jumla ya walimu 17,928 wa shule za msingi na
kupangiwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kuajiriwa kwa walimu hao
kutapunguza pengo la walimu lililopo.
84.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali kupitia
Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa, itaimarisha elimu ya msingi
kwa kuongeza uwazi wa kiutendaji, kuwajengea walimu uwezo wa kutoa
msaada wa kimasomo kwa wanafunzi wenye uhitaji maalum, kuinua ubora wa
mazingira ya kufundishia na kujifunzia, kuongeza upatikanaji wa vifaa
vya kufundishia na kujifunzia na kuongeza uwajibikaji wa watendaji
katika utoaji wa elimu.
Elimu ya Sekondari
85.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali imeweka
juhudi kubwa katika kuimarisha Elimu ya Sekondari hasa ujenzi wa
madarasa, nyumba za walimu, maabara, ununuzi wa madawati na vitabu
pamoja na kuboresha miundombinu na mazingira ya kujifunzia na
kufundishia. Aidha, Serikali imeajiri Walimu wapya wa Sekondari 18,410
na kutoa mafunzo kazini kwa Walimu 12,476. Kati ya hao, Walimu 8,400 ni
wa masomo ya Sayansi na Hisabati. Hatua hizo zimechangia kuongeza ufaulu
wa Wanafunzi waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2013 kufikia
Asilimia 58.25 ikilinganishwa na Asilimia 43.08 mwaka 2012. Katika mwaka
2014/2015, Serikali itatoa kipaumbele cha uwekezaji kwenye miundombinu
ya Shule za Sekondari, Walimu, Ukaguzi na Vitendea kazi.
Mafunzo ya Ufundi Stadi
86.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kutekeleza Mpango wa
Maendeleo ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi wa mwaka
2013/2014 hadi 2017/2018. Mpango huo unalenga kuongeza udahili katika
ngazi mbalimbali za Elimu na Mafunzo ya Ufundi ili kujenga uwiano wa
nguvukazi katika ngazi mbalimbali kwa kila fani. Vilevile, unalenga
kujenga nguvukazi yenye kuhimili ushindani wa soko la ajira kwa kuinua
ubora wa elimu na mafunzo ya ufundi ili kukidhi mahitaji ya soko la
ndani na nje ya Nchi. Ili kutekeleza mpango huo, katika mwaka 2013/2014,
Serikali ilianza kutumia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 25 kutoa
mafunzo ya masomo ya ufundi stadi ili kuongeza udahili wa wanafunzi.
Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaanza ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi
katika Mikoa ya Rukwa, Geita, Simiyu na Njombe.
Elimu ya Juu
87.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeboresha mazingira ya kujifunzia
na kufundishia masomo ya sayansi na teknolojia kwenye Vyuo Vikuu nchini.
Katika mwaka 2013/2014, kupitia Mradi wa Sayansi, Teknolojia na Elimu
ya Juu, Serikali imekamilisha ujenzi wa vyumba 48 vya Mihadhara, Maabara
93 za sayansi na Ofisi 302 za wafanyakazi katika Vyuo Vikuu mbalimbali
vya Umma nchini. Aidha, vifaa vya kufundishia na kujifunzia na vya
TEHAMA vilinunuliwa katika Vyuo hivyo na kuziunganisha Taasisi 28 za
elimu ya juu katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
88.
Mheshimiwa Spika, kutokana na kuwepo kwa malalamiko mengi
kuhusu Vyuo Vikuu nchini kutoza ada tofauti kwa mafunzo ya aina moja,
Serikaliimekamilisha Mwongozo wa Gharama Halisi ya Kumsomesha Mwanafunzi
wa Elimu ya Juu. Mwongozo huo unatoa ukomo wa ada inayotakiwa kutozwa
na chuo kwa kila programu au kozi kwa mwanafunzi. Lengo ni kuondoa
upangaji na upandishaji wa ada kiholela kwa wanafunzi wanaosoma elimu ya
juu pasipo kuzingatia gharama halisi ya kumsomesha mwanafunzi husika
kulingana na kozi anayosoma. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itasimamia
utekelezaji wa Mwongozo huo.
MAENDELEO YA SEKTA YA AFYA
Huduma ya mama na mtoto
89. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuimarisha huduma ya
afya ya Mama na Mtoto kwa kutekeleza Mpango Mkakati wa Kuongeza Kasi ya
Kupunguza Vifo vitokanavyo na Matatizo ya Uzazi na Vifo vya Watoto wa
mwaka 2008 hadi 2015. Katika kutekeleza Mkakati huo, Serikali imeandaa
Mpango Kazi wa Uzazi wa Mpango Uliothaminiwa. Mpango Kazi huo unalenga
kununua na kusambaza dawa na vifaa vya uzazi wa mpango nchini. Aidha,
Serikali imeimarisha mfumo wa rufaa kwa mama wajawazito kwa kununua
vyombo vya usafiri kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii na kuvisambaza
katika mikoa yenye kiwango cha juu cha vifo vya mama vitokanavyo na
matatizo ya uzazi. Vilevile, Serikali inatekeleza Mpango Mkakati wa
Kutokomeza Maambukizi Mapya ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto
ambao ulizinduliwa tarehe Mosi, Desemba, 2012 na Mheshimiwa Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Awamu ya kwanza
ya Mpango huo ilianza mwezi Oktoba, 2013 na kuhusisha Mikoa tisa yenye
uambukizo mkubwa wa VVU kwa wajawazito. Mikoa hiyo ni Iringa, Njombe,
Mbeya, Tabora, Simiyu, Shinyanga, Mwanza, Geita na Kagera. Awamu ya
pili imeanza mwezi Januari, 2014 kwa Mikoa 16 iliyobakia.
90.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itakamilisha
mapitio ya Mpango Mkakati wa Kuongeza Kasi ya Kupunguza Vifo vya Mama
vitokanavyo na Uzazi na Vifo vya Watoto na kutekeleza afua nyingine za
kipaumbele. Aidha, kupitia Mpango wa Kitaifa wa Uzazi wa Mpango dawa na
vifaa vyote vya uzazi wa mpango vitanunuliwa na kusambazwa ili viweze
kuwafikia wananchi wanaovihitaji. Lengo ni kufikia Asilimia 60 ya
kiwango cha utumiaji huduma za uzazi wa mpango kama ilivyoanishwa kwenye
Malengo ya Maendeleo ya Milenia.
Udhibiti wa Maambukizi ya Malaria
91. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na maambukizi ya
ugonjwa wa malaria, Serikali imeendelea kugawa vyandarua shuleni na
kuhimiza matumizi endelevu. Katika mwaka 2013/2014, Serikali iligawa
vyandarua 510,000 katika shule 2,302 za msingi na Sekondari za Mikoa ya
Lindi, Mtwara na Ruvuma kupitia Programu ya Wanafunzi Shuleni. Aidha,
kupitia mikakati na afua nyingine Serikali ilisambaza vyandarua 879,856
vyenye viuatilifu vya muda mrefu kupitia Mpango wa Hati Punguzo kwa
wajawazito na watoto wenye umri chini ya mwaka mmoja.
92.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya
Cuba, inatekeleza Mpango wa kuangamiza Viluwiluwi vya Mbu kwa kutumia
njia za Kibaiolojia katika Jiji la Dar es Salaam. Mpango huo pia,
utatekelezwa katika Mikoa mingine mitano. Aidha, Serikali kwa
kushirikiana na wadau iliendelea na zoezi la kupulizia dawa ya ukoko
katika kaya 838,000 zilizopo kwenye Mikoa ya Kagera, Mara na Mwanza
ambapo zaidi ya Wananchi 4,505,752 wamekingwa dhidi ya maambukizi ya
ugonjwa wa malaria. Pia, Serikali imekamilisha kusambaza kipimo cha
malaria kinachotoa majibu ya haraka katika vituo vyote vya
kutolea huduma Nchini. Vilevile, jumla ya dozi 14,655,000 za Dawa
Mseto na Vitendanishi 9,853,710 vimenunuliwa na kusambazwa katika vituo
vya huduma na hivyo kuimarisha upatikanaji wa dawa na vitendanishi
Nchini.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kugawa vyandarua
Milioni 7.2 vyenye viuatilifu vya muda mrefu kupitia Mpango wa Hati
Punguzo, na kuendeleza kampeni maalum ya kugawa vyandarua kwa jamii
katika ngazi ya kaya. Aidha, zoezi la kugawa vyandarua kwa wanafunzi
shuleni litaendelezwa kwa Mikoa ya Kusini. Sambamba na hatua hizo, mradi
wa kuangamiza viluwiluwi vya mbu katika mazalia utapelekwa katika Mikoa
mingine mitano kwa kutumia viuatilifu (Biolarvicides) vitakazozalishwa
katika kiwanda kinachojengwa Kibaha, Mkoa wa Pwani ambacho kinatarajiwa
kuanza kazi mwaka huu wa 2014.
Huduma kwa Wazee na Watu Wenye Ulemavu
93.
Mheshimiwa Spika, Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003 na Sera
ya Taifa ya Huduma na Maendeleo kwa Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004
zinasisitiza kuwa makundi hayo yana haki ya kupata matunzo katika jamii.
Katika mwaka 2013/2014, Serikali ilitoa huduma za msingi kwa wazee na
watu wenye ulemavu wasiojiweza wanaotunzwa na kulelewa katika Makazi 17
ya Serikali. Jumla ya wahudumiwa 1,235 walipatiwa huduma za msingi
ikiwemo chakula, malazi, mavazi pamoja na kuwapatia vifaa yakiwemo
magodoro, mashuka, vitanda na nyenzo za kujimudu. Vilevile, Serikali
iliratibu huduma za matunzo katika Makazi 24 yanayoendeshwa na Mashirika
Yasiyo ya Kiserikali ili kupunguza malalamiko kuhusu upungufu wa huduma
zinazotolewa.
94.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kusisitiza kuwa, wazee na
watu wenye ulemavu na wasiojiweza wanahitaji kupatiwa matunzo katika
jamii zao. Huduma zinazotolewa kwenye vituo na taasisi za Serikali na
zisizo za Serikali ni hatua ya mwisho pale ambapo itathibitika kuwa mzee
au mlemavu huyo hana mtu kabisa wa kumtunza katika familia na jamii.
Natoa rai kwa wananchi kuendeleza utamaduni wa kuwatunza wazee wetu na
watu wenye ulemavu. Huu ni utamaduni mzuri sana. Aidha, nazikumbusha
Halmashauri kutenga fedha za kuyahudumia makundi hayo. Katika mwaka
2014/2015, Serikali itazindua Baraza na Mfuko wa Taifa wa Huduma kwa
Watu wenye Ulemavu ili kuwajengea na kuongeza uwezo wao katika kuzifikia
fursa za maendeleo na kuimarisha utawala bora.
Lishe
95.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali imeendelea
kusimamia Kanuni za Uongezaji wa Virutubishi katika vyakula ambapo
viwanda vikubwa sita vya kusindika unga wa ngano na viwanda vitatu vya
kusindika mafuta ya kula vinaweka virutubishi katika vyakula
vinavyotengenezwa. Takwimu zinaonesha kuwa, takribani watu milioni 10
wanatumia unga wa ngano uliorutubishwa na Milioni 4 wanatumia mafuta ya
kupikia yaliyorutubishwa na vitamin A. Vilevile, Serikali imeandaa
Mpango wa Uongezaji wa Virutubishi kwenye vyakula Ngazi ya jamii ambapo
utekelezaji wake ulishaanza katika Mikoa ya Iringa, Njombe, Arusha na
Dar es Salaam. Mpango huo unalenga uwekaji virutubishi kwenye unga wa
mahindi unaozalishwa na wajasiriamali wadogo na kusagwa kwenye viwanda
vya kati na vidogo.
96.
Mheshimiwa Spika, Sekta binafsi inashirikishwa kikamilifu
katika mapambano dhidi ya utapiamlo nchini. Mwezi Mei 2013, Serikali
ilikabidhi tani nane za Madini joto kwa Muungano wa Wasindikaji wa
Chumvi katika maeneo mbalimbali Nchini kama sehemu ya mchango wa
Serikali wa kuimarisha Sekta Binafsi katika mapambano dhidi ya
utapiamlo. Serikali pia imeimarisha Maabara za uwekaji madini joto
katika chumvi kwa kununua na kugawa vitendanishi katika Maabara 13 za
Mikoa. Lengo ni kupanua wigo wa Wananchi wanaopata vyakula vyenye
virutubishi. Natoa wito kwa Viongozi katika ngazi zote. Kusimamia juhudi
hizo za Serikali na kuhakikisha zinaendelezwa katika maeneo yao. Aidha,
ninawasihi Wafanyabiashara wote wenye viwanda vya chakula kutekeleza
jukumu hilo kikamilifu. Kwa wale ambao hawajakamilisha taratibu za
ufungaji wa mashine za kuongeza virutubishi wafanye hivyo mapema
iwezekanavyo.
HALI YA UPATIKANAJI WA MAJI NCHINI
Huduma ya Maji Vijijini
97.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka
2002 inayolenga kuboresha huduma ya maji Mijini na Vijijini kwa
kushirikisha Wananchi na Sekta Binafsi. Katika kutekeleza azma hiyo,
Serikali iliweka lengo la kutoa huduma za maji kwa Asilimia 65 Vijijini
katika umbali usiozidi mita 400. Ili kuongeza kasi ya kufikia lengo
hilo, katika mwaka 2013/2014, Serikali iliongeza bajeti ya maji kwa
Shilingi Bilioni 184 kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya maji.
98.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mradi wa Maji kwa Vijiji Kumi
kwa kila Halmashauri upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ambapo
ujenzi na ukarabati wa miradi ya maji 248 katika Vijiji 270 umekamilika.
Pia, jumla ya vituo 10,393 vya kuchotea maji vinavyohudumia Watu
2,598,250 vimejengwa. Ujenzi wa miundombinu ya maji kwenye Vijiji 613
upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na miradi katika Vijiji 374
inafanyiwa tathmini ya zabuni. Aidha, katika kipindi hicho, vyombo vya
watumia maji 373 vimeundwa. Vilevile, katika kipindi cha miezi sita ya
utekelezaji wa miradi ya maji chini ya BRN! kinachoishia Desemba 2013,
Wanavijiji 2,390,000 wamefikishiwa huduma za maji safi na salama,
ikilinganishwa na Wanavijiji 300,000 hadi 500,000 waliokuwa wakipatiwa
huduma za maji safi Vijijini kabla ya mpango huo kuanza.
99.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia inatekeleza Awamu ya Pili ya
mradi wa maji wa Chalinze ambao utatoa huduma ya maji kwa Vijiji 47
vyenye Watu 197,684 katika Wilaya za Bagamoyo, Pwani. Hadi kufikia
Desemba 2013, utekelezaji wa mradi ulikuwa umefikia Asilimia 88.
Vilevile, Serikali inaendelea na ujenzi wa mabwawa katika maeneo
mbalimbali hususan maeneo kame kwa lengo la kuwapatia wananchi huduma ya
maji kwa matumizi ya nyumbani na mifugo. Ujenzi wa mabwawa ya Iguluba
(Iringa Vijijini) na Wegero (Butiama, Mara) na ukarabati wa Bwawa la
Ingodini –Longido Arusha umekamilika. Ujenzi wa mabwawa ya Kawa (Nkasi,
Rukwa), Sasajila (Chamwino, Dodoma), Mwanjoro (Meatu, Shinyanga) na
Kidete (Kilosa, Morogoro) umekamilika kwa zaidi Asilimia 75. Mabwawa
yaliyokamilika kwa wastani wa Asilimia 50 ni Habiya (Itilima, Simiyu),
Sekeididi (Kishapu, Shinyanga) na Matwiga (Chunya, Mbeya). Natoa wito
kwa Wananchi kulinda vyanzo na miundombinu ya maji. Vilevile, natoa wito
kwa Viongozi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kusimamia vyema Vyombo
vya watumia maji ili miradi hii iwe endelevu.
Huduma ya Maji Mijini
100.
Mheshimiwa Spika, Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira
katika miji mikuu ya mikoa zinatoa huduma ya maji kwa wakazi wake kwa
wastani wa Asilimia 80. Katika Jiji la Dar es Salaam, upatikanaji wa
huduma ya maji utaongezeka zaidi mara baada ya upanuzi na ujenzi wa
bomba kuu la maji kutoka Ruvu Juu na Ruvu Chini kukamilika. Kazi ya
kulaza bomba la maji kutoka mtambo wa Ruvu Chini hadi Dar es Salaam
lenye urefu wa kilometa 55.5 umekamilika kwa Asilimia 60.5 na kazi ya
kupanua mtambo wa Ruvu Juu na kulaza bomba hadi Dar es Salaam imeanza
mwezi Februari, 2014. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaanza
kutekeleza Mpango Maalum wa Kuhifadhi na Kutunza Vyanzo vya Maji wa
Miaka Mitano (2014/2015 – 2018/2019) ili kuimarisha ushirikishwaji wa
wadau katika shughuli za uhifadhi, utunzaji na ulinzi wa rasilimali za
maji. Aidha, Serikali itaendelea kutekeleza Mradi wa Maji kwa Vijiji
Kumi kwa kila Halmashauri.
UTAMADUNI NA MICHEZO
Utamaduni
101. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali imeendelea
na urasimishaji wa tasnia za filamu na bidhaa zake kwa kushirikiana na
taasisi zinazohusika ili kuiongezea Serikali mapato na kulinda kazi za
wasanii. Moja ya hatua zilizochukuliwa ni kufanyika kwa operesheni ya
kufuatilia matumizi ya stempu za kodi za Mamlaka ya Mapato Tanzania
ambapo zaidi ya stempu milioni moja za bidhaa za filamu zimetolewa.
Jumla ya operesheni nane za kufuatilia filamu zilizoingia sokoni kinyume
na taratibu zimefanyika na jumla ya filamu 301 zilibainika kuingia
sokoni kinyume na taratibu na wahusika kuchukuliwa hatua. Natoa wito kwa
mamlaka husika kuhakikisha kuwa zoezi hili linafanyika Nchi nzima na
linakuwa endelevu. Vilevile, natoa rai kwa wananchi kununua bidhaa za
filamu zenye viwango zinazothibitishwa na uwepo wa stika maalumu.
Michezo
102.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali kwa
kushirikiana na Wadau wa maendeleo ya michezo imetekeleza Mradi wa
Kimataifa wa Kukuza Ari ya Michezo wenye lengo la kuimarisha ushiriki
wa vijana na watoto katika michezo bila kujali jinsia ama uwezo.
Kutokana na juhudi hizo, katika mashindano ya Kombe la Dunia kwa Watoto
wa Mitaani yaliyofanyika Nchini Brazil mwezi Aprili 2014, Timu yetu ya
Watoto wa Mitaani ya Mkoani Mwanza imetwaa Kombe la Dunia la Watoto wa
Mitaani. Napenda kuwapongeza Vijana hao kwa kuiletea Nchi yetu heshima
kubwa. Vijana hao wanapaswa kuendelezwa ili waweze kutuwakilisha vyema
katika mashindano mengine ya Kimataifa. Aidha, mafanikio hayo yawe
chachu ya kuendeleza michezo mingine Nchini. Ni muhimu tukakumbuka
kwamba vipaji vya michezo viko vingi na vimejificha. Kinachotakiwa ni
kufanyika jitihada za dhati kuviibua na kuvitumia. Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo ishirikiane kwa karibu na Maafisa Utamaduni
wa Halmashauri zote nchini kubuni mkakati maalum wa kuibua vipaji vya
michezo kuanzia ngazi ya kitongoji.
USHIRIKIANO WA KIMATAIFA NA KIKANDA
103.
Mheshimiwa Spika, Nchi yetu imeendelea kufanya vyema katika medani
za Kimataifa kufuatia kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Napenda
kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kutunukiwa Tuzo tarehe 9 Aprili, 2014 kwa
kuwa Kiongozi Mwenye Mchango Mkubwa Zaidi katika Maendeleo Barani
Afrika kwa mwaka 2013, huko Jijini Washington, Marekani. Tuzo hiyo ya
heshima kubwa inayotolewa kwa Viongozi wa Afrika ambao hutoa mchango
mkubwa zaidi wa kiuchumi na kijamii kila mwaka kwa watu wao, hutolewa na
jarida maarufu la kimataifa la African Leadership Magazine Group. Tuzo
hiyo imetolewa kutokana na mwelekeo wake thabiti na wenye mafanikio
makubwa kwa masuala ya utawala bora. Vilevile, napenda kumpongeza Dkt.
Stergomena Lawrence Tax kwa kushinda kinyang’anyiro cha nafasi ya Katibu
Mtendaji wa Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) mwezi Agosti,
2013. Namtakia kila la kheri katika kutekeleza majukumu yake na
kuendelea kupeperusha vyema bendera ya Nchi yetu.
104.
Mheshimiwa Spika, tarehe 1 hadi 2 Julai, 2013 Watanzania walipokea
ugeni mkubwa wa Kiongozi wa Taifa la Marekani, Rais Barack Obama
aliyeambatana na mamia ya Wafanyabiashara. Kupitia ziara hiyo, Marekani
ilizindua Mpango wa Umeme Afrika (Power Africa), ambao utaongeza kwa
mara mbili upatikanaji wa umeme katika Bara la Afrika. Tanzania ni
miongoni mwa Nchi zitakazonufaika na Mpango huo unaolenga kuzalisha
zaidi ya Megawati 8,000 za umeme katika Nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa
la Sahara. Serikali ya Marekani imeahidi kutoa zaidi ya Dola za
Marekani Bilioni 7. Kampuni za Marekani, Ulaya, Asia na Afrika
ziliahidi kutoa zaidi ya Dola za Marekani Bilioni 9 kwa ajili ya Mradi
huo kwa miaka mitano ijayo. Nchi yetu pia kupitia ziara hiyo ilipata
fursa ya kujitangaza na kujiweka katika nafasi nzuri ya kukuza Uchumi,
Biashara, Utalii na Uwekezaji.
105.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji mzuri wa Malengo ya Maendeleo ya
Milenia ambayo yatafikia ukomo wake mwaka 2015 umeifanya Nchi yetu
izidi kung’ara Kimataifa na hivyo kuwa kati ya Nchi 30 zitakazounda
kikundi kazi kitakachoandaa Malengo ya Maendeleo Endelevu
yatakayotekelezwa baada ya mwaka 2015. Aidha, katika Mkutano wa
Jukwaa la Uchumi (WEF) uliofanyika mjini Davos, Uswisi mwezi Februari
2014, Mpango wa WEF wa kuvutia uwekezaji katika miundombinu muhimu
ulijadiliwa ambapo Bandari ya Dar es Salaam ilichaguliwa kuwa miongoni
mwa Bandari zitakazonufaika na Mpango huo. Tayari Timu ya Wataalam
imefika Nchini kufanya tathmini ya awali ya mradi huo. Aidha, Kongamano
maalum lililohusisha Nchi kadhaa zinazohusika na Mpango wa Uchukuzi wa
Ukanda wa Kati lilifanyika tarehe 15 Aprili, 2014. Kongamano hilo
lilizinduliwa na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
MASUALA MTAMBUKA
Vita Dhidi ya Rushwa
106. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali
imeendelea na mapambano dhidi ya rushwa kwa kutoa elimu kuhusu rushwa,
athari zake na wajibu wa wananchi katika mapambano dhidi ya rushwa
kupitia semina, midahalo, maonesho ya kitaifa, vipindi vya Radio na
Televisheni pamoja na machapisho. Aidha, tuhuma 3,872 zikiwemo tuhuma
mpya 679 zilichunguzwa, ambapo hadi sasa uchunguzi wa tuhuma 589
umekamilika. Majalada 4 ya tuhuma za rushwa kubwa yalifikishwa kwa
Mkurugenzi wa Mashtaka kwa hatua za kisheria. Katika mwaka 2014/15,
TAKUKURU itaendelea kuchunguza tuhuma 3,193 zilizopo na mpya
zitakazojitokeza na kuendesha kesi 635 zilizopo Mahakamani hivi sasa na
zitakazoendelea kufunguliwa. Vilevile, itaendelea na uchunguzi wa
tuhuma zitokanazo na taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali za mwaka 2011/2012.
Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi
107.
Mheshimiwa Spika, Serikali imetekeleza Awamu ya Kwanza ya Mpango
wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi. Lengo ni kuendesha
shughuli zake kwa uwazi zaidi ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa
Wananchi, kusikiliza Wananchi, kupambana na rushwa na kujenga dhana ya
kuaminika kwa Wananchi. Katika mwaka 2013/2014 Serikali imechapisha,
Bajeti yake kwa lugha rahisi za Kiswahili na Kingereza na kuiweka katika
Tovuti ya Wizara ya Fedha ili iweze kusomwa na Wananchi wote. Aidha,
imeanzisha Tovuti ya Serikali (Government Portal) yenye anuani ya http://www.egov.go.tz/ na
Kituo Maalum cha Mawasiliano kwa masuala ya OGP Nchini pamoja na
kuimarisha Tovuti ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaanza kutekeleza Awamu ya
Pili ya Mpango huo kwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na
kutunga Sheria ya Uhuru wa Habari; kukamilisha na kuimarisha Mfumo wa
Kuweka Wazi Taarifa na Takwimu kwenye Tovuti.
Maafa
108.
Mheshimiwa Spika, Nchi yetu imeendelea kukumbwa na Maafa ambayo
yameleta athari kwa Wananchi na mali zao. Katika mwaka 2013/2014, ukame
umesababisha upungufu wa Chakula kwa Watu 828,063 katika Wilaya 54 za
Mikoa 14 Nchini. Serikali ilitoa tani 26,663 za chakula cha msaada
chenye thamani ya Shilingi Bilioni 15.2 pamoja na Shilingi Bilioni 2.2
kwa ajili ya kukisafirisha hadi kwa walengwa. Mafuriko makubwa pia
yametokea katika maeneo mengi hususan, Mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam,
Pwani, Mbeya, Tanga, Kilimanjaro, Lindi, Dodoma, Iringa, Kagera na Mara
na kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali na miundombinu.
Katika kukabiliana na athari zilizojitokeza, Serikali na wadau
mbalimbali imetoa misaada ya dharura ya kibinadamu kwa waathirika na
imechukua hatua za kurejesha miundombinu ya maji, elimu, afya, barabara
na madaraja na umeme. Nitumie fursa hii kulipongeza Jeshi la Wananchi wa
Tanzania, TANROADS, Wakandarasi, Wadau mbalimbali pamoja na Wananchi
wote kwa kazi kubwa waliyoifanya na misaada waliyoitoa kwa Waathirika
wa Maafa yaliyojitokeza. Napenda kurudia wito wangu kwa Wananchi
wote wanaoishi katika maeneo hatarishi hasa mabondeni, kutii maagizo
ya Serikali kuondoka katika maeneo hayo na kuhamia maeneo
yaliyoainishwa ambayo ni salama kwa maisha yao.
Aidha,
ninatoa wito kwa Wananchi wote kufuata Sheria ili kuepuka uvunjifu wa
amani na kusababisha maafa kutokana na mapigano, hasa ya kugombea ardhi
na malisho.
Mafunzo ya Kukabili Maafa
109.
Mheshimiwa Spika, mafunzo ya kuijengea jamiii uwezo wa kukabiliana
na maafa ikiwemo kupokea na kugawa misaada wakati wa maafa yametolewa
katika ngazi za Mkoa na Wilaya kwa Mikoa ya Mara, Geita, Singida,
Simiyu, Shinyanga, Manyara, Kilimanjaro, Dodoma, Tabora na Arusha. Pia,
Mipango ya Kujiandaa Kukabili Maafa katika Halmashauri za Wilaya za
Maswa, Bariadi, Meatu, Mwanga na Same imeandaliwa. Katika mwaka
2014/2015, Serikali itafanya Tathmini ya Maafa yanayoweza kutokea na
uwezo wa kuyakabili pamoja na mipango ya kujiandaa na kukabiliana na
maafa katika Halmashauri za Wilaya za Mtwara Mjini, Mtwara Vijijini,
Masasi, Mvomero na Kilosa. Vilevile, itaanza Ujenzi wa Kituo cha Dharura
cha Utendaji na Mawasiliano (Emergency Operation and Communication
Centre) katika eneo la Mabwepande Wilayani Kinondoni
...
No comments:
Post a Comment