Picha ya Mtandaoni
Zaidi ya wasusi 200 kutoka katika mkoa wa Arusha na Manyara wamefanikiwa kupatiwa elimu na mbinu bora za kuboresha biashara zao huku lengo likiwa ni kuongeza kipato kutokana na kazi zao
Aidha elimu hiyo pia ilienda sanjari na mbinu bora za ususi wa kimataifa ambao unafanywa na nchi ambazo zimeendelea duniani na hivyo kufanya kazi ya ususi kuwa bora zaidi
Elimu hiyo ilitolewa mjini hapa na kampuni ya Hair Tanzania Indusry mapema jana ambapo pia iliweza kuwakutanisha wasusi wote wa mji wa Arusha lakini pia mji wa Manyara.
Akiongea mara baada ya kumalizika kutolewa kwa elimu pamoja na mbinu bora za ususi Meneja wa kampuni hiyo kwa kanda ya kaskazini Bw Noah Mfinanga alisema kuwa kuna sababu kubwa ambazo zimesababisha waweze kuwakutanisha wasusi hao.
Alitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na kuwafanya waweze kukubali kazi zao za ususi kwani wanaweza kufanya kazi hiyo kwa kiwango cha hali ya juu sana na hivyo wanaweza kuongeza uchumi wa familia zao lakini pia hata nchi kwa ujumla.
Pia aliongeza kuwa sababu nyingine ni pamoja na kuwapa mbinu za kimataifa za ususi lakini pia namna ya kuendelea kutunza na kuimarisha ususi wao ambao utaweza kulinda utamaduni wa mwanamke wa kitanzania.
"Ususi ni moja ya kazi lakini pia ni moja ya kazi ambayo kila mara inadharaulika sana kwa jamii wakati ni kazi ambayo inaweza kuwajenga watu katika uchumi wa hali ya juu ila kwa sasa tumeweka mpango maalumu wa kuhakikisha kuwa hawa wasusi wa mikoa hii wanajijua na kutambua kazi zao"aliongeza Bw Mfinanga
Wakati huo huo aliwataka hata watanzania kuhakikisha kuwa wanajijengea utaratibu wa kupenda kununua bidhaa za Tanzania kwani kwa kufanya hivyo kutaweza kuruhusu nchi kujijenga kiuchumi zaidi.
Hata hivyo wasusi hao ambao wengi wao ni wanawake walisema kuwa wanashukuru kuweza kupewa mbinu mbalimbali za kuongeza ufanisi wa kazi zao lakini ni changamoto kwa makampuni mingine kuhakikisha kuwa wanajiwekea tabia ya kutoa elimu kwani uwepo wa bidhaa nyingine bado haziwanufaishi watanzania ingawaje ni bidhaa za Tanzania.
No comments:
Post a Comment