Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadick
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, alithibitisha kuongezeka kwa watu waliofariki kutokana na mvua hizo, alipozungumza na NIPASHE jana.
Alisema katika Wilaya ya Ilala watu waliofariki kutokana na mvua hizo wamefikia 11, huku watu wawili wakiwa hawajulikani waliko hadi kufikia jana.
Sadiki alisema katika Wilaya ya Temeke watu walioripotiwa kufariki dunia kutokana na mvua hizo wamefikia saba wakiwa idadi na sawa na wale walioripotiwa kupoteza maisha katika Wilaya ya Kinondoni.
Hata hivyo, alisema kuna taarifa za watu wengine 14 kuwa walizikwa kimyakimya katika mitaa yao, ambao wanasaidikiwa kufa kwa mafuriko hayo.
“Juzi kuliripotiwa vifo 13. Hadi kufikia leo (jana) nimepokea taarifa ya vifo 25 vya watu waliokufa maji kwa mjumlisho wa idadi katika wilaya zote tatu,” alisema Sadiki.
Aliongeza: “Bado kuna utata wa taarifa za vifo vya watu wawili katika Wilaya ya Ilala, wanaosadikiwa kufa maji. Kinondoni pia inasemekana watu 14 waliofariki kwa mafuriko. Wamezikwa bila sisi kujua. Nimeagiza Jeshi la Polisi kufuatilia suala hili ili kujua ukweli.”
Alisema watu wanaosadikiwa kuzikwa kimyakimya kwa Wilaya ya Ilala ni wawili wakati Kinondoni wakiwa 14.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alimtaja mmoja kati ya watu waliofariki kuwa ni Frank Bwashee, mkazi wa Jagwani baada ya kusombwa na mafuriko wakati alipotaka kutaka kuokoa mali za watu eneo hilo, karibu na Kanisa la Miito ya Baraka, juzi majira ya saa 1:30 asubuhi.
Alisema mali alizotaka kuokoa zilikuwa zinaelea kwenye maji wakati wa mvua zikiendelea kunyesha na kwamba, mwili wake umehifadhiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Alimtaja mwingine kuwa ni Elfaza Mbasha (65), ambaye alifariki dunia majira ya saa 6:55 mchana baada ya mafuko kuingia nyumbani kwake, eneo la Mabibo, Kata ya Ubungo, wakati akijaribu kuokoa vitu katika nyumba yake na kuzidiwa nguvu na maji.
Pia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo, aliwataja Dunia Matandi (25), aliyekuwa kondakta wa daladala na Hassan Juma (34) kuwa walikufa kwa kusombwa na mafuriko katika daraja la mto Mzinga na miili yao kuhifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Temeke.
Alisema watu hao walikumbwa na mkasa huo juzi, majira ya saa 1:45 jioni, katika daraja hilo linalounganisha Kivule na Kitunda.
OFISI YATEMBELEA MAENEO YA MAFURIKO
Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ubungo inafanya ziara ya kukagua uharibifu uliosababishwa na mafuriko jimboni humo kwa ajili ya kuangalia namna ya kutatua athari zilizosababishwa na mafuriko.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa katika vyombo vya habari jana, mbali na kuangalia athari mbalimbali, jana timu iliyokuwa katika ziara hiyo ilishiriki katika mazishi ya baadhi ya watu waliokufa kutokana na mafuriko jimboni humo.
Baadhi ya maeneo ambayo timu hiyo ilitembelea ni pamoja na Kata ya Msigani, eneo la Msingwa, ambako kivuko kilikatika na kukata mawasiliano.
Sehemu nyingine, ambayo timu hiyo inatarajia kutembelea ni Kata ya Makuburi, iliyoko Mtaa wa Makoka, ambako daraja limekatika na kusababisha kukatika kwa mawasiliano kati ya Tabata na Makoka.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, ambaye yuko mjini Dodoma kushiriki Bunge Maalumu la Katiba, alisema anakusudia kurejea jimboni kwake kushirikiana na wananchi kwa karibu zaidi ili kuona namna ya kutatua matatizo yaliyojitokeza.
MAFURIKO YAPANDISHA BEI ZA VYAKULA
Wateja kwenye wa Soko Kuu la Kariakoo, jijini Dar es Salaam wamelalamikia upandaji wa bei za bidhaa katika soko hilo, kutokana na magari ya mizigo kushindwa kuingia kutokana mafuriko yaliyotokea wiki iliyopita.
Mmoja wa wateja, Halima Ally, mkazi wa Mbezi Kimala, alisema bidhaa zilizopanda bei, ni za viungo vya mboga, kama vile karoti, ambazo awali zilikuwa zikiuzwa kwa Sh. 1,000, lakini sasa zinauzwa Sh. 2,500.
Alisema pia nyanya zinauzwa, kuanzia Sh. 2,500 hadi Sh. 3,000 na njegere zinauzwa Sh. 2,000 hadi 2,500, hali ambayo imewaongezea makali ya maisha.
“Juzi bei ya vyakula ilikuwa juu kutokana na magari ya mizigo kushindwa kuingia Dar es Salaam. Kitendo hicho kimetupelekea sisi wafanyabiashara kupandisha bei ya baadhi ya vyakula,” alisema mmoja wa wafanyabiashara wa soko hilo, Selestine Mroso.
Mroso alisema kuna baadhi ya bidhaa, kama vile mchele, unga na maharagwe, zinauzwa bei za kawaida kwa kuwa mizigo hiyo huhifadhiwa kwenye maghala tofauti na vyakula, ambavyo vinaoza.
HALI YA MADARAJA
Magari yaliruhusiwa kuendelea na safari zake za mikoani na katikati ya jiji la dare s Salaam baada ya miundombinu, ikiwamo madaraja kukarabatiwa.
Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Martin Ntemo, alisema katika daraja la Mbagala-Kongowe, magari yalianza kupitia tangu juzi, majira saa 4.00 usiku, wakati katika daraja la mto Ruvu magari madogo yanaruhusiwa kupita na katika daraja la Bagamoyo, yalitarajiwa kuanza kupita jana.
Alisema daraja la Kongowe-Kigamboni litawekwa la muda, huku matengenezo yakiendelea.
USAFIRI WA MABASI UBT WAREJEA
Usafiri katika Kituo cha Mabasi Ubungo (UBT) umerejea katika hali ya kawaida kutokana na kupungua kwa maji katika mito ya Ruvu, Kizinga na Kozi.
NIPASHE, ambayo ilitembelea UBT jana ilishuhudia baadhi ya mabasi, ambayo yalilala njiani, yakiingia na mengine yakiendelea na safari kuelekea mikoani.
Hata hivyo, baadhi ya abiria walilazimika kulala kwenye magari kutokana kuishiwa fedha za kujikimu katika safari na kuna baadhi ya abiria waliachwa na magari kwa kutopewa taarifa za kuanza safari.
“Abiria kwa leo wamepungua tofauti na siku mbili za nyuma. Kuna baadhi ya abiria walitapeliwa kwa kukatiwa tiketi, huku magari yakiwa yamezuiliwa kufanya safari zao za kila siku kutokana na uelewa wao mdogo,” alisema Katibu wa Chama cha Kutetea Abiria (Chakua), Gervas Rutabuzinda.
MABONDENI WAENDELEA KUISHI
Wakazi wa mabondeni wameendelea kufanya usafi katika nyumba zao, huku wakisema hawaondoki na kwamba, wataendelea kuvizia mvua, zikinyesha watakimbia na ikiacha wataendelea na makazi yao.
“Mimi ni miongoni mwa wakazi, ambao tulipelekwa Mabwepande na serikali. Lakini tulishindwa kukaa kule kutokana na serikali kutotuboreshea miundombinu na kututelekeza,” alisema Irene Mathias, ambaye ni mkazi wa Mkwajuni.
Alisema inakuwa ngumu kulala na watoto kwenye hema moja na kwamba, wanaona bora warudi kwenye makazi yao.
KAYA ZILIZOATHIRIKA NA MAFURIKO ZAONGEZEKA MORO
Idadi ya kaya zilizoathirika na mafuriko na kukosa makazi zimendelea kuongezeka katika Manispaa ya Morogoro kutoka 1,000 hadi kufikia 2,120, huku Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, akiagiza taasisi za umma, likiwamo Shirika la Umeme Tanzania ( Tanesco) Mkoa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Moruwasa) kusitisha kupeleka wa huduma hizo kwenye makazi yaliyojengwa mabondeni.
Mbali na kutoa agizo kwa taasisi hizo, Bendera pia amewataka watu wote waliojenga na kuishi mabondeni kuondoka mara moja.
Pia amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri za wilaya zote kuorodhesha maeneo, ambayo ni hatarishi ili kuwaelimisha wananchi juu ya madhara ya kuishi mabondeni.
Dk. Bendera alitoa maagizo hayo mara baada ya kuhitimisha ziara ya ghafla ya ukaguzi wa maeneo yaliyokumbwa na mafuriko katika maeneo ya manispaa akiongozana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na za wilaya ya Morogoro.
Alisema zipo sheria zinazozuia wananchi kuendesha shughuli za kibinadamu na ujenzi maeneo ya mabondeni na mikondo ya maji, wengi wameshindwa kufuta sheria na kuwataka watendaji wa halmashauri kufuatilia usimamizi wake wa karibu ili kuzuia ujenzi kwenye maeneo hayo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Javis Simbeye, akiwasilisha taarifa ya athari za mafuriko hayo mbele ya Dk. Bendera alisema mvua zilizonyesha, kuanzia Aprili 12, mwaka huu ziliathiri kaya 424 zenye watu 2,120 katika maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo.
Alisema kutokana na athari za mafuriko hayo, wananchi kutoka katika maeneo mbalimbali wamekosa makazi na kupewa hifadhi na majirani, huku wengi wakiishi katika baadhi ya shule na hivyo kuhitaji misaada, ikiwamo chakula, malazi na nguo.
Diwani wa Kata ya Mazimbu, ambayo ni moja ya kata zilizoathirika, Richard Massawe, aliiomba serikali kufanya jitihada za kurejesha katika uasili wake mto Ngerengere ili kuepusha maafa ya aina hiyo.
Alisema mto huo umeingiliwa baada ya baadhi ya wanachi kuchimba visima vidogo kando kando kwa ajili ya shughuli za kilimo cha bustani za mboga na kusababisha mvua zinazoendelea kunyesha kusomba mchanga na kujaza mtoni.
Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) Mkoa wa Morogoro, Dorothy Mtenga, alisema mvua hizo zimetishia kuharibu daraja la mto Ngerengere katika barabara kuu ya Moro-Dodoma, eneo la Kihonda Mbuyuni.
Hata hivyo, alisema wanasubiri kupungua kwa maji ya mvua ili matengenezo yafanyike na kwamba, kwa sasa magari yanaruhusiwa kupita upande mmoja ili kunusuru kumomonyoka zaidi.
Imeandikwa na Hussein Ndubikile, Enles Mbegalo, Kamili Mmbando, Elizabeth Zaya (Dar) na Ashton Balaigwa (Morogoro).
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment