MKUTANO wa Bunge Maalumu la Katiba unaondelea hivi sasa, unatarajiwa kuahirishwa Mei 25, kupisha vikao vya kamati za Bunge la Bajeti vilivyopaswa kuanza mapema mwezi huu.
Mwenyekiti Bunge Maalumu, Samuel Sitta, alitangaza uamuzi huo jana bungeni ambapo alisema ulifikiwa juzi kwenye kikao cha Kamati yaUongozi kilichokutana juzi.
Sitta, alisema Bunge hilo litaahirishwa Aprili 17 kupisha Sikukuu ya Pasaka na litaendelea na shughuli zake Aprili 22.
Alisema Bunge hilo litaahirishwa tena Aprili 25 kupisha Sikukuu ya Muungano pamoja na Bunge la Bajeti.
Sitta, alibainisha kuwa hivi sasa wajumbe wanajadili sura ya kwanza na sita ambazo majadiliano yake yatachukua muda usiopungua siku saba.
“Kwa mujibu wa kanuni zetu, sura hizi zilipaswa kujadiliwa kwa siku tatu, lakini kutokana na wachangiaji 350 kuomba itatubidi kesho tutengue kanuni na kuongeza siku za majadiliano ili kufikia idadi hiyo ya wajumbe.
“Tunalazimika kuongeza siku za kujadili jambo hilo kwakuwa ni nyeti na linabeba masilahi ya umma na mustakabali wa taifa,” alisema.
Uamuzi huo umekuja siku chache baada ya Sitta kuutangazia umma kuwa Bunge hilo litaahirishwa Mei 28 kupisha vikao vya Bunge la Bajeti ambavyo ndivyo huidhinisha bajeti ya serikali.
Sitta, alitoa kauli hiyo alipokwenda kuwatembelea viongozi wa dini, Mhadhamu Kardinali Polycap Pengo na Sheikh Mkuu, Mufti Isa bin Shaaban Simba.
Tanzania Daima ilidokezwa kuwa wajumbe wa Bunge Maalumu, wanaweza kurejea kwenye vikao vyao Agosti au Septemba kulingana na ratiba zitakavyopangwa.
Hata hivyo, jitihada za kumpata Mwenyekiti wa Bunge, Sitta, kuelezea jambo hilo hazikufanikiwa kwakuwa simu yake ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila majibu.
Ndugai anena
Akizungumza na Tanzania Daima, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri, alikiri Bunge la Bajeti kuathiriwa na Bunge la Katiba ingawa alisema linaweza kumaliza kazi zake ndani ya siku 70.
Alisema kuwa kama Bunge hilo litaongezewa siku 20, viongozi wa Bunge la Jamhuri watakutana kuangalia namna bora ya kupanga ratiba za vikao vyao.
Tanzania Daima lilitaka kujua iwapo kama muda wa siku 90 walizopewa wajumbe wa Bunge la Katiba zitamalizika bila kukamilisha kazi zao ni taratibu gani zitatumika.
Akijibu swali hilo, Ndugai alisema Bunge Maalumu linakutanisha wabunge wote wa Bunge la Jamhuri, hivyo chochote kinachowahitaji wanaweza kukutana kwa jambo maalumu huku lile la katiba likiahirishwa kwa muda fulani.
“Kuna hati ya dharura inaweza kuletwa na rais ili Bunge la Jamhuri ya Muungano likutane na kujadiliana, iwe kuongeza muda au chochote kinachoonekana kinafaa.
“Nadhani si tatizo kwa Bunge la Katiba kuongezewa siku nje ya zile zilizosemwa na sheria… mimi naona tatizo litakalokuwepo ni Bunge la Bajeti kuathirika,” alisema.
CHANZO: TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment