Mkuu wa kituo cha Polisi Mirerani Wilayani Simanjiro, SP Ally Mohamed Mkalipa (kushoto) akimwelezea Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Manyara, Deusdedit Nsimeki, kuhusiana na maendeleo ya polisi jamii, kwenye mji mdogo wa Mirerani juzi.
Na Mwandishi wa brotherdanny5.blogspot, Manyara
Askari polisi jamii wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wameuomba uongozi wa mkoa huo kuwapa sare, vitambulisho, pingu na filimbi ili wawezekufanya shughuli za ulinzi kikamilifu.
Askari hao walitoa maombi hayo juzi mji mdogo wa Mirerani wakati wakizungumza na Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara, SACP Deusdedit Nsimeki alipoitembelea wilaya hiyo.
Walisema wanafanya kazi zao za kuimarisha ulinzi katika mji huo kwenye mazingira magumu kutokana na kukosa vifaa hivyo ambavyo vitawasaidia na kuwatambulisha kwa wananchi kuwa wao ni polisi jamii.
Hata hivyo, Kamanda Nsimeki alisema suala la sare, vitambulisho na filimbi, linaweza kushughulikiwa kwani polisi jamii ni suala la kitaifa na baadhi ya sehemu kama Hanang’ na Mbulu wamepatiwa vifaa hivyo.
“Hivyo vifaa mtavipata kwani vitawawezesha kufanya kazi zenu kwa kujiamini ila suala la pingu litakuwa gumu, kwani hiyo ni silaha hamuwezi mkapewa mtumie ninyi labda filimbi, sare na vitambulisho,” alisema Kamanda Nsimeki.
Kwa upande wake, mkuu wa kituo cha polisi Mirerani, SP Ally Mohamed Mkalipa alisema askari polisi jamii hao wanatumika kufanya doria na ulinzi kwenye mji huo wakishirikiana na askari polisi wa kituo hicho.
“Kwa kweli Kamanda hawa polisi jamii wanatusaidia sana katika ulinzi wa mji wetu, kwani huwa ni chanzo chetu cha kutueleza uhalifu unafanyika wapi na pia huwa tunashirikiana nao katika mambo mengi ya usalama,” alisema Mkalipa.
No comments:
Post a Comment