Pages

Pages

Pages

Sunday, 13 April 2014

MAJANGA MAKUBWA DAR


Mvua kubwa ziliyonyesha mfululizo kuanzia juzi maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam zimesababisha vifo vya watu kumi na kuharibu miundombinu ya barabara ikiwamo madaraja sita kubomoka. 
 
Aidha, mradi wa mabasi yaendayo kasi (Dart) umelazimika kusimamisha shughuli zake, baada ya ofisi zake za Jangwani kukumbwa na mafuriko na kusababisha hasara ya zaidi ya Dola za Kimarekani 30,000.
 
NIPASHE ambayo ilizunguka katika maeneo mbalimbaliya Jiji la Dar es Salaam, ilishuhudia nyumba, barabara, madaraja na mali za watu zikiwa zimeathiriwa na mafuriko yaliyotokana na mvua hizo.
 
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,Suleiman Kova, alisema juma ya watu 10 wamepoteza maisha kutokana na mvua hizo. Alisema miongoni mwa watu hao watoto ni watano.      
 
MAGUFULI ASHUHUDIA DARAJA KUBOMOKA
Akizungumza katika eneo la tukio, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, alisema  Daraja la Mpiji lililounganisha mikoa wa Dar es Salaam na Pwani, limekatika na kupoteza mawasiliano ya mikoa hiyo.
 
Alisema mpaka jana saa 8:00 mchama ilikuwa limekatika mita 30 upana na kwenda chini mita saba.
 
Alisema, kutokana na athari hiyo, serikali imeamua kufunga  daraja hilo kwa muda wa siku mbili wakati juhudi za kurudisha mawasiliano zinafanyika.
 
Dk. Magufuli alisema kwamba serikali imeshafanya kazi ya kutafuta wakandarasi watakaofanya kazi ya kujanza mawe katika eneo lililoathirika.
 
"Tumepata magari zaidi ya arobaini ambayo yatafanya kazi ya kusomba mawe na kuja kujaza eneo la daraja lililobomoka, natumaini ndani ya siku mbili kazi hiyo itakamilika na huduma ya usafiri itarejea,' alisema Dk. Magufuli.
 
Alisema, amewasiliana na Mkuu wa Majeshi nchini, Jenerali Davis Mwamunyange, kuongeza nguvu zake kwa kutumia askari wake kusaidia ujenzi wa daraja la muda wakati kazi nyingine zikiendelea.
 
Aidha aliwataka wananchi wanaotaka kwenda Bagamoyo kwa siku hizo watumie barabara ya Kibaha hadi sekondari ya Baobab au kutokea Bunju B kuelekea Kibaha hadi sekondari ya Baobab.
 
WAKAZI WA BONDENI
Wakazi wa Jangwani wamelazimika kukimbia makazi yao na kwenda kuishi kwenye kambi maalum zilizoanzishwa na wasamaria wema pembeni ya eneo hilo kutokana na nyumba zao kujaa maji.
 
 Wengine wamelazimika kuzihamishia familia zao pamoja na baadhi ya mali walizoziokoa kwenye Kituo cha Mabasi yaendayo Kasi (DART) kilichopo Jangwani barabara Morogoro.
 
Hata hivyo,waandishi wa habari walipowafuata kwa ajili ya kuzungumzia athari walizopata, waligoma na kuwashambulia kwa maneno wakidai wamepewa rushwa ndiyo maana wanawageuza mradi wa kuuzia magazeti.
 
“Tumechoka jamani mtuache, serikali haitutambui, nyie mnataka nini tuacheni tufe na familia zetu tulizoamua kuzianzisha wenyewe, mmepewa rushwa, sasa tunasema hatutaki kuhojiwa,” alisikika mmoja wao akisema.
 
Wakati huo huo, wananchi hao walielekeza lawama nyingine kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, wakiilani kauli yake kuwa serikali haitawasaidia wakikumbwa na maafa. 
 
WATOTO WAATHIRIKA
Katika hali ya kusikitisha, gazeti hili lilishuhudia mtoto mwenye umri wa wiki tatu akiwa kwenye mazingira hatarishi huku nguo zilizotumika kumfunikiwa zikiwa zimelowa.
 
Mtoto huyo alikutwa akiwa amebebwa na mwanamke aliyejitambulisha kuwa ni jirani ya mama mzazi wa mtoto, ambaye wakati huyo alikuwa amejihifadhi kwenye kituo cha mabasi yaendayo kasi (DART) kilichopo Jangwani.
 
Wakati mtoto huyo akiwa amekumbatiwa na mama huyo, mvua iliyoambatana na upepo ilikuwa inaendelea kunyesha huku maji yenye kasi yakipita pembeni ya barabara ya Mororogo. 
 
MJUMBE ANENA
Mjumbe wa Jangwani B, kata ya Mtambani, Pilu Mahesh, aliliambia gazeti hili kuwa wakazi wa eneo hilo wapo tayari kuondoka wakati wowote ikiwa serikali itawafidia kwa sababu wapo hapo kisheria.
 
“Hatujavamia hapa, tunamiliki kihalali ardhi hii ambayo Mwalimu Nyerere aliwamilikisha wazee wetu mwaka 1974 ndiyo maana tulienda mahakamani kudai haki yetu tukashinda, na sasa tunadai fidia, serikali itekeleze hilo tutahama,” alisema na kuongeza:
 
“Eneo langu lina jumla ya nyumba 193 zote zimepata maafa ya mvua lakini hakuna aliyefariki zaidi ya uharibifu wa mali, mpaka sasa zipo kambi tatu za muda eneo la Yanga, Kongo Mwanzo na nyingine ipo kwenye makutano ya barabara ya Morogoro na Muhimbili,” alisema.
 
MRADI WA DART HALI TETE
Mvua hizo pia zimeleta maafa kwenye mradi wa DART na kusababisha hasara ya zaidi ya dola za kimarekani 30,000.
 
Meneja Mradi, Li Qiaojia, aliliambia NIPASHE kuwa, eneo ambalo lilitengwa kwa ajili ya mradi huo lililopo Jangwani limekumbwa na mafuriko ambapo hadi jana saa 6:00 mchana maji yalikuwa yanakaribia ghorofa ya kwanza ya ofisi hizo.
 
Qiaojia alisema wamepata hasara ya kiasi hicho na kwamba amelazimika kuja nchini kuja kuangalia hali ilivyo.
 
“Tumepoteza mali kama magari matatu aina ya Pick Up yameharibika, sementi mifuko 2,000 imeenda na maji, mashine na magari mengine ya kutengenezea barabara, hii ni hasara kubwa kwetu,” alisema.
 
 Aliongeza kuwa, wamelazimika kuwaacha baadhi ya watu kwenye jengo la ghorofa la ofisi hizo, ili walinde mali nyingine zilizopo kuanzia ghorofa ya kwanza kuendelea.
 
“Endapo maji yatajaa zaidi, itatubidi tuhamishe vitu vyote humo, ila kwa sasa wapo baadhi ya wafanyakazi wetu ndani ya jengo wanalinda mali, hii ni hatari,” alisema. Alieleza kusikitishwa na serikali kwa kitendo chake cha kukaa kimya licha ya kuwapo kwa tatizo hilo.
 
NIPASHE ilishuhudia magari maarufu kama ‘kijiko’ vikitumika kubeba wafanyakazi pamoja na baadhi ya mali za ofisi hizo na kuwaleta kwenye barabara kuu ya Morogoro ambayo kwa wakati huo maji yalikuwa yakipita pembeni.
 
Mmoja wa mshuhuda waliokutwa eneo la Mbezi kwa Msuguli, Samson Lazaro, alisema mwanamke mmoja amefariki baada ya kusombwa na maji wakati akijaribu kuvuka mto Mbezi.
 
 “Tulimsihi asivuke maji  ni mengi yatamzidi nguvu lakini hakusikia mara kidogo kaweka miguu huyooo akaondoka”, alisema Samsan.
 
Diwani wa Kata ya Mkongola Ilala, Anjelina Malembeka, alisema katika eneo lake wakazi wake wapo hatarini kukosa huduma za kijamii kutokana na daraja lililokuwa likiunganisha kata ya Mkongora na Chanika kusombwa na maji
Maeneo mengine yaliyokumbwa na kadhi hiyo ni Kibamba, Mbagala, Mbezi MalambaMawili, Gongolamboto, Kiluvya, Bagamoyo pamoja na Kigogo Mkwajuni.
 
RELI
Treni inayotoa huduma kwa wakazi wa Dar es Salaam, imeharibika kutokana na mvua hizo.
Msemaji wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Midladjy Maez, alisema  katika makutano ya reli eneo la Ilala,  kipande kimeharibika kutokana na mvua hizo.
 
“Matengenezo yataanza kufanyika leo (Jumapili) na haijajulika wataalamu hao watachukua siku ngapi kufanya marekebisho hayo,” alisema.
 
Mwenyekiti wa Kamati ya Mafuriko katika eneo la Basihaya, Renatus Mtakyawa, alisema zaidi ya nyumba 100 zimefurika maji.
 
Alisema licha ya mvua hizo kunyesha, maji mengi yamekuwa yakitokea kwenye mkondo wa maji unaotokea kiwanda cha Saruji. “Mvua zinaponyesha kiwanda hichi kimekuwa kikifungulia maji hali ambayo inachangia kutuongezea mafuriko na madhara kuendelea kuwa makubwa,” alisema.
 
Alisema tayari wameshapeleka malalamiko yao kwa serikali pamoja na kwa Waziri Mkuu lakini mpaka sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa hali ambayo inawafanya waendelee kuishi katika mazingira magumu.
 
Alisema kwa sasa wakazi wa eneo hilo wamekaa pembeni mwa barabara huku wengine wakiwa wanalinda nyumba zao.
                     
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki,  alisema miongoni mwa waliofariki, saba walikuwa wakijaribu kuvuka kwenye madaraja yaliyojaa maji.
 
“Miundombinu ya barabara na madaraja katika Manispaa tatu za Ilala, Kinondoni na Temeke mfano daraja la mto Kizinga linalounganisha watu wa Mbagala na Chanika imeharibiwa vibaya,” alisema.
 
Diwani kata wa Tuangoma, Rashid Mikuki, alisema daraja la mto Mkombozi linalounganisha watu wa Kongowe kwenda Tuangoma limekatika. Alisema katika eneo hilo lori la mafuta limetumbukia.
 
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alisema katika jimbo lake watu wawili akiwamo mtoto, wamefariki dunia baada ya kusombwa na mafurikio. Alisema mtoto huyo alisombwa na maji katika mtaa wa Usewe kata ya Ubungo na tayari wazazi wake wameshapatikana.
 
Alisema mtu mwingine amefariki katika kata ya Kimara baada ya kutumbukia kwenye mtaro uliopo pembeni ya barabara ya Morogoro inayoendelea na ujenzi.
 
Akitaja madaraja yaliyoharibika kwenye jimbo lake, Mnyika alisema linalotumiwa na watu wa kata ya Makuburi mtaa wa Makoka, lingine ni la kata ya Kimara ambalo linawaunganisha watu wa Kimara Mwisho na Bonyoka.
 
Aidha, daraja lingine la Kibamba mtaa wa Kiluvya na lililopo kata ya Saranga mtaa wa Golani ambalo Rais Jakaya Kikwete alilizindua mwaka huu ambalo kingo zake zimesombwa na maji. Alisema vivuko vilivyopo kata ya Ubungo na Goba mtaa Kulangwa navyo vimesombwa na maji.
 
Mnyika alisema tayari amewasiliana na malaka husika ili waweze kuchukua hatua sahihi na pia amekitaka kitendo cha maafa kilichopo ofisi ya waziri mkuu kutembelea maeneo hayo na kuona namna ya kuwasaidia wathirika.
Imeandikwa na Romana Mallya, Moshi Lusonzo, Beatrice Shayo na Efracia Massawe
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment