Pages

Pages

Pages

Sunday, 13 April 2014

AKINAMAMA 6 WALALA KITANDA KIMOJA HOSPITALI

Hospitali ya mkoa ya Ligula mkoani hapa inakabiliwa na wimbi kubwa la wagonjwa na kusababisha akina mama wanaokwenda kujifungua kulala watu sita kitanda kimoja.

Afisa kiongozi wodi ya wazazi, Lucy Mkolea, alisema kwa siku wodi hiyo imekuwa ikipokea akina mama 70 huku ikiwa na uwezo wa kulaza  akina mama 30 tu.

Alisema wodi ya wazazi ina vitanda 31 na leba ina vitanda sita na kufanya jumla ya vitanda katika wodi  ya wazazi kuwa 38 hali ambayo alisema inawafanya kulala kitanda kimoja watu sita (yaani akina mama watatu na watoto wao).

Alisema wanalazimika kuwaruhusu wazazi  kabla ya saa 24 kupita kama ambayo inatakiwa na badala yake huwaruhusu saa 12 kutokana na msongamano mkubwa wa akina mama.

Kwa upande wake,  Dk. Frank Sudei wa kitengo cha afya ya uzazi, alisema wodi ya kujifungulia inakabiliwa na changamoto nyingi  ikiwemo kuelemewa na akina mama wanaofika kujifungua.

NIPASHE ilifika katika hospitali hiyo na kujionea msongamano mkubwa katika wodi hiyo huku sehemu kubwa ya akina mama waliojifungua wakiwa wamelala chini na wakiwa wamewalaza kwenye vitanda.

Akizungumzia hali hiyo, Zamda Athumani, ambaye ni mzazi alisema katika kitanda chake wamelalala akina mama wanne hivyo kuwafanya walale chini na watoto wao wakiwa kitandani.

Hospitali hiyo pia inakabiliwa na upungufu wa wafanyakazi, vitendea kazi na majengo vikiwa kikwazo kikubwa katika kutoa huduma bora kwa wananchi wa mkoa huo.

Akizungumza na NIPASHE,  Daktari  Mfawidhi wa hospitali hiyo,  Mohamed Gwao,  alisema kuwa hosptali hiyo kwa sasa imeelemewa kutokana na kuhudumia wagonjwa wasiopungua milioni 1.3 kwa mwaka, huku wagonjwa wanaofika katika hospitali hiyo kupata matibabu kwa siku ni 100.

Alisema ongezeko hilo haliendani na wafanyakazi waliopo kwa sasa ambao ni 268  na kuutaja muongozo wa  hospitali hiyo kwa sasa unaitaji wafanyakazi wasiopungua 680 ili kwenda na idadi ya wagonjwa wanaofika hospitalini hapo.

Akizungumzia udogo wa hospitali na uchakavu wa baadhi ya majengo, alisema ilijengwa mwaka 1964  na wakati huo ikihudumia wagonjwa  wachache hivyo inaitaji kuboreshwa zaidi ili iendane na wingi wa wagonjwa.

Dk Gwao alisema yapo baadhi ya majengo yameanza kujengwa likiwemo la dharura ambalo wameamua kubadilisha matumizi na kulikarabati kuwa  wodi ya wazazi ili liweze kukidhi mahitaji makubwa yaliyopo sasa.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment