MJUMBE wa Bunge Maalumu, Freeman Mbowe, amewaumbua wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwa wengi wao ni wanafiki katika kuchangia mijadala na hoja bungeni.
Mbowe alisema kutokana na unafiki huo, wajumbe wa CCM wamekuwa wakiwaomba wale wa upinzani kusimamia hoja ya uundwaji wa serikali tatu wanaouamini utakuwa mkombozi wa kero za muungano zilizodumu kwa miaka 50.
Kauli hiyo aliitoa jana bungeni alipokuwa akitoa ufafanuzi ya maoni ya walio wachache katika kamati namba saba, ambapo alisema woga wa aina hiyo hautakiwi kwenye Bunge la Katiba lenye kutoa kinga kwa wajumbe kuzungumza wanachokiamini.
Kutokana na kauli hiyo ya Mbowe, mjumbe mwingine Paul Makonda, aliomba mwongozo wa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta, akimtaka Mbowe kuwataja kwa majina wanafiki hao ndani ya Bunge hilo ili jamii iwatambue.
Makonda alisema kutajwa kwa watu hao kutaisaidia jamii kujua watu wenye tabia ya kuomba hoja zao ziwasilishwe kupitia upande mwingine ambao msimamo wao ni serikali tatu.
Mara baada ya Makonda kumaliza kuzungumza, Sitta alimpa nafasi Mbowe ya kuwataja au kutowataja wanafiki hao kadiri anavyoona inafaa.
Baada ya kupata nafasi hiyo Mbowe, alisema wanafiki wasiokubaliana na msimamo wa CCM lakini wanashindwa kuweka hadharani mmoja wao ni Paul Makonda, anayetokea katika kundi la wajumbe 201, ambaye licha ya kuwa ni kada wa CCM kwa nafasi ya Katibu wa Vijana Taifa (UVCCM), hakubaliani na chama chake.
Mbowe alisema anasikitishwa na vitendo vya baadhi ya wajumbe wa bunge hilo kushindwa kutoa maoni yao kwa kadiri wanavyoamini kutokana na kuogopa misimamo ya vyama vyao.
Mbowe alisema Makonda, ni miongoni mwa wajumbe hao wanaotamani kuunga mkono serikali tatu lakini wanaogopa msimamo wa chama chao unaotaka serikali mbili.
Mbowe alisema inasikitisha kuona baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo wakimshambulia Jaji Joseph Warioba kwamba amechakachua maoni ya wananchi.
Alisema Warioba aliandika vema maoni ya rasimu ya Katiba ambayo kimsingi imejitosheleza kwa takwimu.
Mbowe alisema kama wajumbe wengi ndani ya Bunge Maalumu, wanataka kujadili muundo wa serikali mbili ambao ni kinyume na rasimu ya pili ya Katiba ni vema Bunge livunjwe ili yakusanywe maoni upya kwa lengo la kutoa fursa ya kuwapa nafasi wananchi kutoa maoni yao .
“Inasikitisha kuona kuwa wapo watu ambao wanabeza Tume ya Jaji Warioba, bila kuangalia ni jinsi gani tume hiyo ilikuwa na watu wazito kutoka serikalini na serikali ambayo inaongozwa na CCM wakati tume hiyo ilikuwa na watu wanaotoka katika ofisi nyeti za serikali ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Rais Ikulu pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu.
“Kitendo cha kukataa rasimu ya Jaji Warioba ni sawa na kuwakataa watendaji wa serikali yao na kutokuwa na imani na serikali iliyopo madarakani iliyowachagua wajumbe hao,” alisema Mbowe.
Mbowe, alisema anawapongeza Wazanzibari kwa kuonesha moyo wa uzalendo kwa kudai nchi na serikali yao ambayo kimsingi wana haki ya kuilinda kwa gharama yoyote.
Alisema pamoja na juhudi nyingine za kuendelea kutetea serikali tatu watawala wanatakiwa kuacha kuwa na sera za vitisho kwa wananchi kuwa serikali tatu ni tatizo na zinaweza kusababisha kuwepo kwa gharama kubwa.
Alisema hakuna ukweli wowote kuwa wananchi watashindwa kuzihudumia serikali tatu, kwakuwa muundo huo utapunguza gharama za uendeshaji tofauti na ule wa serikali mbili..
Akizungumzia kuhusu kuwepo kwa Hati ya Muungano, mbowe alisema kupatikana kwa Hati ya Muungano ni jambo zuri ambalo linajenga roho ya utungaji wa Katiba mpya.
“Upatikanaji wa Hati ya Muungano ni jambo la msingi na bora, tena nataka niungane na mjumbe wa Bunge Maalumu mzee Stephen Wassira, kwa kueleza kuwa Hati ya Muungano itapatikana baada ya siku mbili, lakini nilikuwa nikiomba kama kweli kuna dhamira ya kweli ya upatikanaji wa katiba ni bora ikafanya juhudi ya kutafuta hati hiyo mapema bila kusubiri siku mbili…
“Serikali ina uwezo wa kupata hati hiyo mapema na ikumbukwe kuwa hiyo hati siyo kwamba inaenda kuandikwa upya ni vema ikawasilishwa bungeni mapema ili wajumbe waweze kuiona na mjadala uendelee bila kuwa na shaka ya Hati ya Muungano kama ilivyo sasa,” alisema Mbowe.
Mbowe alisema kuwa kwa sasa inaonekana watawala tayari wamepewa upofu na Mungu, wamekuwa wakitoa misimamo yao inayopinga walio wengi na kuendesha nchi kwa kutumia mabavu, jambo ambalo haliwezi kukubalika hata kidogo.
Alisema kuwa kwa sasa kinachotakiwa ni kuzungumza mambo ya ukweli na kuacha kufanya mambo kwa mashinikizo na ubabe wa viongozi waliopo madarakani.
TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment