Muhidin Maalim Mohammed Gurumo enzi ya uhai wake akisalimiana na Rais Jakaya Kikwete.
Na Daniel
Mbega
HABARI za
kifo cha gwiji wa muziki nchini, Muhidini Maalim Mohammed Gurumo, zimeutikisa
ulimwengu wa muziki. Tunaambiwa amefariki leo Jumapili Aprili 13 saa 9.00
alasiri katika hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na kusumbuliwa na tatizo
la mapafu kwa muda mrefu.
Miaka takriban
minne iliyopita aliwahi kuzidiwa na kulazwa katika Hospitali ya taifa
Muhimbili, na walilazwa pamoja na nguli mwingine wa muziki, Ramazan Mtoro
Ongalla, maarufu Dk. Remmy Ongalla, ambaye jitihada za kupigania uhai
hazikuweza kuishinda nia na mipango ya Mwenyezi Mungu. Akatangulia mbele ya
haki.
Kifo ni
wajibu wetu, kwa maana ndiyo maagizo ya Mungu baada ya baba yetu Adam na mkewe
Hawa kutenda dhambi kule bustanini Aden.
Sote, ama
wengi wetu, tunautambua mchango mkubwa kabisa wa Gurumo katika maendeleo ya
muziki wa Tanzania. Kama Wazaire walivyokuwa wakimuenzi Verkys Kiamwangana Mateta,
ndivyo ambavyo nasi tunastahili kuuenzi mchango wa Mjomba Gurumo.
Wapo wanamuziki
wengi waliotangulia, wakatamba na bendi mbalimbali kama akina Salim Abdallah
Yazidu na Ahmed Kipande, au akina Mbaraka Mwinshehe Mwaruka, Marijani Rajabu
Marijani, Hemedi Maneti Ulaya, na wengineo wengi, lakini kwa uhalisia, mchango
wao hauwezi kufananishwa na huu wa Mjomba Gurumo.
Ndiyo. Wengine
watamtaja ‘Teacher’ King Michael Enock Chinkumba aliyeziongoza Dar Jazz, Dar
International na Sikinde, lakini bado tunaweza kusema mchango wa Gurumo ni
kipekee katika maendeleo ya muziki wa dansi Tanzania. Amefanya makubwa sana kwa
miaka 53 aliyodumu kwenye muziki.
Katika umri
wake wa miaka 74, hakuna kazi nyingine yoyote aliyoifanya kwa mapenzi makubwa
kama muziki. Sidhani na sina uhakika kama alikuwa mfanyabiashara ama mkulima.
Katika bendi
zote tatu maarufu alizopitia, NUTA Jazz (zamani ikijulikana kama Kilimanjaro
Chacha Band), Mlimani Park Orchestra na International Orchestra Safari Sound ya
Hugo Kisima, alikuwa kiongozi, mwalimu, mtunzi na mwimbaji mahiri sana.
Mitindo aliyoibuni
kwenye bendi hizo Msondo wa NUTA Jazz (baadaye ikaitwa JUWATA na OTTU), Sikinde
wa DDC Mlimani Park na ule wa Ndekule katika IOSS ambayo haipo kwenye ramani ya
muziki, ilishika hatamu nab ado inaendelea kutumika mpaka sasa huku Msondo
ukibeba jina la bendi. Mitindo yote hiyo mitatu ni ngoma za Kabila la Wazaramo
wanaopatikana mkoani Pwani.
Alizaliwa
mwaka 1940 katika Kijiji cha Masaki wilayani Kisarawe katika Mkoa wa Pwani. Kutoka
Masaki hadi Mzenga alikotokea Mbaraka Mwinshehe siyo umbali mrefu wa kutisha,
hiyo ikimaanisha kwamba Pwani inajivunia historia ya wanamuziki wengi kuwahi
kutokea huko wakiwemo Francis Lubua (Nassir Lubua) aliyekuwa anatokea Chalinze na
Athumani Momba ambaye alikuwa anatokea maeneo ya Msanga wilayani Kisarawe.
Wakati fulani
katika mahojiano enzi ya uhai wake aliweka bayana kwamba muziki ulikuwa kwenye
damu yake tangu akiwa mdogo. Alirithi kwa mama yake ambaye alikuwa mahiri katika
uimbaji wa ngoma ya Ndekule.
Alipopelekwa
Dar es Salaam kwa mjomba wake Suleiman Sultan Mikole ikabidi wampeleke madrasa
ili kupata elimu ya dini yake ya Kiislamu. Huku ndiko akaanza kujifunza kuimba
kaswida.
“Baada ya
kumaliza shule ya msingi pale Pugu Kajiungeni mwaka 1956, alikuja mjomba wangu,
baba mmoja mama mmoja na mama yangu , kunichukuwa na kunileta hapa jijini
ambapo alinisomesha elimu ya dini. Na wakati nipo hapo madrasa ndipo mwaka 1960
nilipoanza kushiriki kwa siri masuala haya ya muziki,” alipata kusema.
Alisema wakati
huo kwamba, yeye alianza na mshahara wa shilingi 5 kwa wiki wakati alipojiunga
na bendi ya Kilimanjaro Chacha mwaka 1961, bendi ambayo ilikuwa ikimilikiwa na
mfanyabiashara Samuel Machangu na ilikuwa na makao yake makuu sehemu ambayo
sasa ni Amana Club, yalipo makao makuu ya Msongo Music Band. Bendi hii ndiyo
ambayo Alfred Tandau, wakati huo akiwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi cha
TFL (Tanzania Federation of Labour) aliamua kuwashawishi viongozi wenzake
wainunue mwaka 1964 na ndipo ikazaliwa NUTA Jazz.
Kilimanjaro
Chacha ilimchukua baada ya kumuona akiimba vizuri katika bendi ya mtaani kwao
iliyokuwa ikiitwa African, ambayo mara nyingi ilikuwa ikifanya maonyesho yake
kwenye harusi.
Wakati huo
alikuwa akitoroka nyumbani akimdanganya mjomba wake kwamba anakwenda shughulini
na ustaadhi wake, huku akiwa amevalia kama vile kweli anaelekea kwenye shughuli.
Mjombe wake alikuwa akipenda dini na aliouona muziki kama ni uhuni.
“Haikuchukua
muda mrefu kukapatikana taarifa za kuanzishwa kwa bendi kubwa itakayokuwa
ikilipa watu mishahara hapa hapa maeneo ya Ilala,” alisimulia Gurumo
akimaanisha bendi hiyo kuwa ni Kilimanjaro Chacha.
Kwa kuwa
bendi hiyo kwa kiasi kikubwa iliundwa kwa kutegemea wanamuziki kutoka Afrikan
Band, mmiliki wa bendi hiyo mpya Machangu alielezwa bayana kuwa kati ya
wanamuziki waimbaji Gurumo awe wa kwanza kuorodheshwa.
Hata
hivyo, juhudi za kumsajili Gurumo kwenye kundi hilo zikakwaa kisiki baada ya
mjomba wake Mikole kutokuwa tayari mwanawe aache kusoma Qur’uan na kwenda
kujiunga na muziki.
Mmiliki wa
Kilimanjaro Chacha, Samuel Machangu, alielezwa na wapambe wake kuwa afanye kila
liwezekanalo hadi Gurumo apatikane, vinginevyo juhudi zake za kuanzisha bendi
kwa kipindi hicho zingeonekana ni kazi bure, aliamua kutumia nguvu ya fedha
kumlainisha mjomba wa nyota huyo wa muziki.
“Mjomba
alipoletewa kitita cha shilingi 300, mwaka huo wa 1961, wakati ambapo yeye
alikuwa akifanya kazi na mshahara wake ulikuwa shilingi 80, akaona isingekuwa
busara kwake kuendeleza msimamo wa kunizuia mwanawe kwenda kuimba kwenye bendi,
japo alinisisitiza sana nisiache kuswali na nisiguse pombe,” alibainisha.
Huo ukawa mwanzo
wa safari ndefu ya mwanamuziki huyo ambaye alisema kibao chake cha kwanza
kutunga na kushiriki kuimba kilikuwa kikiitwa ‘Mapenzi ya Kung’ang’aniana’
alichopiga mwaka 1963 akiwa na Rufiji Jazz Band ya jijini Dar es Salaam.
Kama
ilivyo kawaida ya wanamuziki wengi, suala la kuhamahama ni kitu cha kawaida
sana kwao, kama ambavyo Gurumo alivyohama kundi hilo na kujiunga na Kilwa Jazz,
bendi iliyokuwa na maskani yake Mtaa wa Kilwa Ilala ambapo alidumu kwa miezi nane
tu kabla ya kujiunga na NUTA Jazz mwaka 1964.
“Kilichonipeleka
hapo ilikuwa maslahi tu, kwani ingawa nilikuwa nikituzwa pesa jukwaani ambazo
wakati mwingine ni zaidi ya mshahara wangu, lakini ilikuwa haijafika shilingi
120, nilizoahidiwa kulipwa nilipojiunga na bendi hiyo iliyokuwa chini ya
Jumuiya ya Wafanyakazi,” alieleza Gurumo.
Akiwa na
bendi hiyo Gurumo alitunga na kurekodi nyimbo nyingi zilizokuwa zikipendwa sana
na mashabiki wa muziki zikiwemo Nidhamu ya Kazi, Mpenzi Zalina, Dada Fatuma,
Kilimo cha Kufa na Kupona, Heko Baba Nyerere na nyinginezo nyingi.
Alikaa
hapo mpaka mwaka 1978 alipotoka na kwenda kuanzisha bendi ya Mlimani Park
Orchestra na kuanzisha mtindo wa Sikinde Ngoma ya ukae unaotumiwa hadi leo na
bendi hiyo maarufu hapa nchini.
“Hii
ilikuwa ndiyo bendi yangu ya kwanza kuwa kiongozi wa bendi, na mtindo wa
sikinde mimi ndio niliuanzisha rasmi kutumika kwenye muziki wa dansi, ukiondoa
kwetu uzaramoni unakotumika kama aina mojawapo ya ngoma za asili,” alieleza.
Wakati alipokuwa
Sikinde, Gurumo alitunga nyimbo ambazo zilivuma sana, baadhi ya nyimbo hizo ni
kama vile Kassim Namba 1 na 2, Barua Kutoka kwa Mama utunzi wake Cosmas Thobias
Chidumule na yeye alishiriki kuweka sauti na kuimba.
Mwaka 1985
alihama Mlimani Park akiwa na wanamuziki watano - Hassan Bitchuka, Abel
Bartazal, Kassim Rashid Kizunga, Charles John ‘Ngosha’ - mwenyewe wa sita na
kwenda OSS kulisuka upya kundi hilo ambalo lilionekana kupoteza umaarufu na
kuanzisha mtindo wa Ndekule Ngoma ya Mababu.
Kundi hilo
ambalo liliwahi pia kutumia mitindo ya Masantula na Dukudukuku chini ya magwiji
Kikumbi Mwanzo Mpango ‘King Kiki na ‘Supreme’ Ndala Kasheba kwa nyakati
tofauti, lilikuwa moto wa kuotea mbali mara baada ya kutoka vibao kama Bwana
Kinyogoli na Usimchezee Chatu, ambao ulikuwa majibu ya ‘dongo’lililotupwa na
Mlimani Park alikokuwa kiongozi wa bendi.
Mwaka 1990
Gurumo alihama Ndekule na kurejea JUWATA Jazz. Amekuwa kiongozi wa bendi hiyo
tangu ikiwa chini ya Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi (OTTU, baadaye
TFTU na sasa TUCTA) hadi shirikisho hilo lilipojitoa kuihudumia na wanamuziki
wenyewe wakaamua kuiongoza. Amekaa nayo hadi mauti.
Huyu ndiye
Mjomba Gurumo, nguli wa muziki ambaye leo hii amefariki akiwa mwingi wa umri na
busara. MWENYEZI MUNGU AILAZE ROHO YAKE MAHALI PEMA, AMINA!
No comments:
Post a Comment