Pages

Pages

Pages

Sunday 12 January 2014

YANGA YAMUAJIRI BABU MHOLANZI, ANAKWENDA UTURUKI KESHOKUTWA KUUNGANA NA TIMU

Amekula maisha Jangwani; Hans van der Pluijm ndiye kocha mpya Yanga na Jumanne anakwenda Uturuki kuungana na timu

Na Prince Akbar, Dar es Salaam

KOCHA Mholanzi, Johannes Franciscus ‘Hans’ van der Pluijm, ametua leo Dar es Salaam na kufikia makubaliano ya kuifundisha Yanga kwa kumalizia msimu na Jumanne atapanda ndege kwenda Uturuki kuungana na timu kambini.
Pluijm alikuwa na kikao na uongozi wa Yanga leo baada ya kuwasili na kimsingi wamekubaliana kufunga ndoa fupi kwa majaribio, iwapo atafanya vizuri basi ataongezewa Mkataba mwishoni mwa msimu.

Yanga itampima mwalimu huyo kwa ushiriki wa timu katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika kuanzia mwezi ujao.
Franciscus Johannes ‘Hans’ van der Pluijm alizaliwa Januari 3 mwaka 1949 na alianzia kwenye kucheza soka akiwa kipa.
Enzi zake aliidakia kwa miaka 28 klabu ya FC Den Bosch akicheza mechi 338 ndani ya misimu 18 na alipostaafu baada ya kuumia goti akawa kocha wa timu hiyo.
Alianza vyema ukocha akiiwezesha FC Den Bosch kutwaa ubingwa wa Daraja la Kwanza na kupanda Ligi Kuu na ndiye aliyempa nafasi ya kwanza mshambuliaji Ruud van Nistelrooy akiwa kinda wa miaka 17 tu kucheza kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Aprili mwaka 1995, alisaini Mkataba wa miaka miwili na SBV Excelsior kabla ya kutimuliwa Januari 1997 na nafasi yake ikachukuliwa na Msaidizi wake, John Metgod.
Hiyo ilifuatia timu hiyo ya Rotterdam kushinda mechi mbili tu na sare tatu katika mechi 17 za msimu mzima.
Baada ya kuboronga Ulaya, ndipo akahamia Afrika mwaka 1999, alipokwenda kufundisha Ashanti Gold SC ya Ghana, akianza na Mkataba wa mwaka mmoja.
Ajax ya Uholanzi ikanunua hisa katika klabu hiyo Ijumaa ya Juni 18, mwaka 1999 asilimia 51 naye akatupiwa virago na kuhamia Saint-George SA ya Ethiopia kabla ya mwaka 2010 kujiunga na B-juniors Feyenoord ya Ghana, ambayo ni tawi la timu hiyo ya Rotterdam.
Mwaka 2012 alijiunga na Berekum Chelsea ambako pia alifukuzwa mwaka jana na kuhamia Medeama ya Ghana pia ambako nako alifukuzwa baada ya mechi saba tu, kufuatia matokeo mabaya mwanzo mwa msimu, akivuna pointi nane kati ya 21.

Chanzo: Bin Zubeiry

No comments:

Post a Comment