Pages

Pages

Pages

Thursday 2 January 2014

TFF YAHAMIA MKOA WA KAGERA

NI kwa utuki au kwa mikakati maalum, nafasi kadhaa za juu katika Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) zinashikiliwa na viongozi wenye asili ya mkoa wa Kagera.Wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa TFF, Oktoba 27, 2013 kwenye ukumbi wa NSSF Waterfront, walimchagua kwa kura nyingi Jamal Emil Malinzi kuwa Rais mpya kurithi kiti kilichoachwa na Leodegar Tenga aliyeachia ngazi. Malinzi ana asili ya Kagera.


Baada ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji, kupangwa katika kamati ndogondogo, wiki hii Malinzi amemtangaza aliyekuwa Katibu Mkuu wa klabu ya Yanga, Mwesigwa Selestine kuwa Katibu Mkuu wa TFF akichukuwa nafasi ya Angetile Osiah aliyesitishiwa mkataba wake kwa kupewa likizo ya malipo hadi mwezi huu. Mwesigwa ana asili ya Kagera.

Aidha, Malinzi alimtangaza Katibu Mkuu wa klabu ya Simba, Evodius Mtawala kuwa Mkurugenzi wa Vyama, Wanachama na Masuala ya Sheria. Mtawala ambaye kitaaluma ni mwanasheria, pia anatoka Kagera.

Tofauti na Malinzi na katika kujali misingi ya utawala bora uongozi uliopita wa Tenga uliiteua kampuni moja ya kimataifa kufanya usaili wa watu walioomba nafasi mbalimbali za uongozi. Lakini Malinzi ‘aliunda’ kamati ya kufikirika iliyopokea maombi na kufanya mchujo kwa kuzingatia sifa mbalimbali ikiwemo ya elimu. 

Baadaye majina yaliyopitishwa yalipigiwa kura na Kamati ya Utendaji. Lakini habari kutoka ndani ya TFF zinasema Rais ndiye alikuwa anapokea maombi hayo.

Vilevile, Malinzi amemteua Pelegrinius Rutayuga kuwa mshauri wake wa masuala ya Ufundi. Mshauri huyu ni mwakilishi wa mkutano mkuu kutoka mkoa wa Kagera.

Mwenyekiti wa Kamati ndogo ya Kamati ya Mashindano itakayoshughulikia mpira wa ufukweni ni Ahmed Mgoyi, mjumbe wa TFF kutoka Kigoma, lakini makamu mwenyekiti ni Shaffih Dauda ambaye pia anatoka mkoani Kagera.

Akihisi kwamba watu wanaweza kumpigia kelele kuhusu uteuzi wa viongozi watokao eneo moja, Malinzi aliwaambia waandishi wa habari Jumanne, “Mimi sijali kwamba waombaji ni dini gani na wanatoka wapi bali najali sifa na utendaji kazi.”

Kauli hiyo ya utetezi imeanza kukosolewa na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji ambao wameidokeza MAWIO kuwa hiyo ni dosari kubwa kwa uongozi wa Malinzi.

Malinzi alisema kuwa mchakato wa upatikanaji wa ajira hizo ulipitia taratibu walizoziweka na hao ndio wameonekana kuwa wanafaa kuendana na malengo na sera za TFF.

Alisema mchakato huo ulianza kwa watu mbalimbali kuomba nafasi hizo na baada ya kamati ya ajira, ambayo hakutaka kuiweka wazi kwa madai kuwa ni kamati ya ndani ya TFF, kupitia majina ya waombaji yalipelekwa katika Kamati ya Utendaji ya TFF ambayo ilipata washindi.

Akifafanua, Malinzi alisema TFF ina malengo yake na Mtawala na Mwesigwa ndio walioonekana kuendana na matakwa na hakuna kitu kingine zaidi ya uwezo wao na uzoefu wao uliowashawishi wajumbe kuwapa ajira hizo.

Uteuzi mwingine wenye harufu ya asili ya Kagera ni wa wakili Julius Lugaziya ambaye anakuwa mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa ya TFF. Malinzi amemteua Melchesedeck Lutema aliyekuwa wakili wa Malinzi katika kesi mbalimbali wakati anafanya kazi kwenye kampuni ya mwanasheria maarufu marehemu Julius Ndyanabo kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi.

Halafu Malinzi ameondoa masalia yote ya uongozi wa Tenga isipokuwa Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura. Nafasi ya Mkurugenzi wa Mashindano iliyokuwa chini ya Sadi Kawemba kwa sasa inakaimiwa na Idd Mshangama ambaye ni ofisa wa itifaki.

Sunday Kayuni, aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi, ameondolewa na nafasi yake inakaimiwa na Salum Madadi, huku Danny Msangi akishikilia kwa muda nafasi ya Mkurugenzi wa Fedha.

Nafasi zinazokaimiwa ni kutokana na walioomba kutokuwa na sifa zinazohitajika na Malinzi amesema zitajazwa baadaye isipokuwa wote walioomba awali wasijisumbue kuomba tena.

Rais huyo wa TFF amesema waajiriwa wote mikataba yao itaanza rasmi Januari Mosi 2014 na itakoma baada ya miaka miwili.

Chanzo gazeti la Mawio toleo la wiki iliyopita

No comments:

Post a Comment