Pages

Pages

Pages

Thursday 2 January 2014

MCHUNGAJI MSIGWA AMBEZA JK KUHUSU UJANGILI

Mizoga ya tembo

Na Geofrey Nyang’oro, Mwananchi

Iringa. Mbunge wa Iringa Mjini,  Mchungaji Peter Msigwa (Chadema)  amesema kama Rais Jakaya Kikwete anadhamira ya kweli kutokomeza ujangili nchini ni vyema akasafisha kwanza Serikali na chama chake.
Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Mwembetogwa mjini hapa juzi,  Mchungaji Msigwa alisema kasi ya ujangili ni kubwa na baadhi ya wahusika  ni vigogo ndani ya CCM.
Alisema wengine wanatoka serikalini hususan jeshini; Idara ya Usalama wa  Taifa na Polisi jambo linalosababisha operesheni hiyo kuwa ngumu kwa utekelezaji.
Alisema hali hiyo ndiyo chanzo hata cha Operesheni Tokomeza Ujangili iliyositishwa kwa muda kupoteza mwelekeo.
“Tulipoanza kupiga kelele juu ya vitendo vya ujangili tuliambiwa tunataka umaarufu kisiasa, lakini hali ilipofikia wao wenyewe wamekubali na kuanzisha hata Operesheni Tukomeza Ujangili, lakini niliwaambia mtandao wa ujangili ni mkubwa,” alisema Mchungaji Msigwa na kuongeza:
“Unahusisha vigogo ndani ya CCM, si mnakumbuka niliwahi kuwatajia majina na kuwaambia wawekwe mbali na Tembo... baadhi yao ni polisi wengine ni wanajeshi, kama kweli Rais Kikwete ana nia ya dhati kupambana na ujangili ni vyema akasafisha nyumba yake kwanza.”
Mchungaji Msigwa alisema Serikali ilianzisha Operesheni Tokomeza Ujangili kwa nia njema, lakini kwa sababu majangili wanatoka ndani ya Serikali  hivyo imekuwa vigumu kufanikisha kazi hiyo. Alisema ndiyo sababu hata malengo yake yalipotoshwa, huku walengwa wakiachwa na kuanza kuua raia wasio na hatia.
Mbunge huyo alisema hivi sasa kasi ya ujangili  inatisha na kuongeza  kuwa, kwa siku zaidi ya Tembo 60 wamekuwa wakiuawa jambo linalowafanya wanyama hao muhimu kuwa hatarini  kutoweka.
Alisema hatua ya mawaziri wanne kujiuzulu inaonyesha dhahiri wabunge wa upinzani na Bunge kwa jumla limetekeleza wajibu wake na kwamba, hiyo inatosha kujiaminisha kwa wapigakura wao.
Hata hivyo, Msigwa alisema msimamo wake ni kwamba Serikali ina viongozi mzigo, huku akimtaja Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwa ni kiongozi mzigo.

CHANZO: Mwananchi

No comments:

Post a Comment