Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Monday 14 October 2013

NYERERE ALISEMA, UJAMAA HAUKUSHINDIKA BALI HAUKUJARIBIWA

Mwalimu Nyerere akiwa na Waziri Mkuu wake, Edward Moringe Sokoine


Na Daniel Mbega

KAMA kuna kitu ambacho Mwalimu Nyerere alikiabudu – mbali ya Mungu kupitia katika imani yake ya Kikatoliki – ni Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea iliyozaliwa ndani ya Azimio la Arusha, ambayo aliendelea kuihubiri na kuitetea kwa nguvu zake zote hadi kikomo cha uhai wake.
Kila alikokwenda daima alitembea na Biblia pamoja na Azimio la Arusha, akiamini kwamba misingi ambayo TANU iliiweka kwenye azimio hilo Februari 5, 1965 pale Arusha ilikuwa mizuri na ingeendelea kuwa mizuri ikiwa tu Watanzania wangemwelewa dhamira yake.
Azimio la Arusha lililohimiza Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea bado liko katika maandiko, ikiwemo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ingawa kwa sasa ni nadharia tu na si vitendo.
Hii inatokana na azimio hilo ‘kuuawa’ na Azimio la Zanzibar la mwaka 1991, ambalo lilileta ‘Soko Huria’ enzi za Awamu ya Pili ya uongozi chini ya Alhaj Ali Hassan Mwinyi, ambaye alitoa ruksa kwa kila kitu, zikiwemo nguo za mitumba (maarufu wakati huo kama ‘kafa Ulaya mazishi Bongo’).
Soko huria hili likatafsiriwa vibaya na watu wengi, wakiwemo watumishi wa umma ambao enzi zile za Mwalimu na siasa yake ya ujamaa na kujitegemea walijiona wameminywa, sasa wakaachana hata na misingi ya utawala bora na maadili ya uongozi wa umma, pamoja na miiko ya viongozi, na kuamua kujilimbikizia mali kadiri walivyotaka kwa kutumia nyadhifa zao, jambo ambalo TANU, na baadaye CCM, ililikemea kwa nguvu zote.
Kwa zaidi ya miaka 24 chini ya utawala wa Mwalimu Nyerere, Tanzania iliishi chini ya mfumo wa Ujamaa, siasa ambayo iliweka njia zote kuu za uchumi chini ya umiliki wa umma, ambapo wengi wanasema hali hiyo ndiyo ilichelewesha maendeleo kwa Tanzania.
Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, alikaririwa Julai 2008 akisema kwamba ujamaa ulikuwa hautekelezeki.
Ujamaa ni siasa nzuri lakini unapingana na uasili wa binadamu. Watu, wakati wote wanapenda kuwa matajiri. Hawataki kuwa maskini kwa maisha yao yote. Msingi mmoja wa ujamaa ni kwamba kusiwepo na pengo kubwa kati ya matajiri na maskini, pengo ambalo sasa tunalishuhudia huku wachache wakiwa wamejilimbikizia mali kinyume cha utaratibu na wakitamani kuendelea kuchota mali za umma na hata kununua uongozi au madaraka ili waendelee kuifaidi keki ya fursa za kiuchumi huko walio wengi wakiendelea kuogelea katika ufukara wa kutisha.
Alhaji Mwinyi, au maarufu kama ‘Mzee Ruksa’, alisema wakati anashika uongozi wa juu katika miaka ya 1980 bidhaa mbalimbali muhimu zikiwemo sukari, dawa za meno na hata sabuni zilikuwa adimu.
“Tungeweza kuendelea na sera ile au kufanya mabadiliko? Ujamaa kweli ulikuwa unafanya kazi 1980? Lakini ukiniuliza kama ujamaa ulikuwa mbaya? Nitakwambia, ni siasa nzuri duniani. Tatizo lake ni kama ndoto,” alikaririwa akisema siku hiyo ya uzinduzi wa kitabu chenye maoni ya wakuu 13 wa nchi za Afrika akiwemo yeye mwenyewe na Rais aliyemfuata Benjamin Mkapa ambapo wanaeleza uzoefu wao.
Ndani ya kitabu hicho, Mwinyi anasema alikuwa mkuu wa nchi ambaye alitaka kufanya mabadiliko lakini wakati huo makamu mwenyekiti wa CCM ambacho wakati huo mwenyekiti wake alikuwa ndiye muasisi wa Azimio la Arusha, Mwlaimu Nyerere.
Itakumbukwa kwamba, sera na mipango aliyoianzisha Mwinyi ikafuatiwa kwa kasi kubwa na Rais Mkapa asliyemfuatia, hali ambayo ilidhihirisha kuuzika kabisa ujamaa.
Ingawa hili lilikuwa dhahiri, lakini hakuna aliyewahi kuthubutu kutoa kauli kwamba ujamaa umeshindikana wakati Mwalimu Nyerere akiwa hai, hadi baada ya kifo chake mwaka 1999 ndipo tunazisikia kauli hizi kwa uwazi zaidi. Wengi enzi hizo walipenda kusema chini chini.
Lakini nakumbuka vyema Mwlimu Nyerere aliwahi kukaririwa na jarida la New Internationalist, toleo namba 309 la Januari-Februari 1999 (wakati huo akiwa msuluhishi mkuu wa mgogoro wa Burundi) akisema kwamba ujamaa haukushindwa duniani, bali haukuwahi kujaribiwa!
Ndiyo! Alikuwa na kila sababu ya kusema hivyo, kwa sababu hadi wakati huo mataifa makubwa yaliyoasisi ujamaa yalikuwa yamegeukia ubepari. Sera za ujamaa katika Poland zilikuwa zimeshindikana, Cuba iliendelea kukabiliwa na upinzani mkubwa na vikwazo vingi kutoka Mataifa ya Magharibi, Urusi (USSR) ilikuwa imesambaratishwa mwaka 1991 chini ya Rais Mikhail Gorbachev, Ujerumani Mashariki nayo ilikuwa imeungana na Magharibi mwaka 1990 na ‘kuuvunja ukuta wa Berlin’ uliodumu kwa miaka mingi, huku Czechoslovakia ikigawanyika na kuzaliwa kwa mataifa mawili – Jamhuri ya Czech na Slovakia, kama ilivyokuwa kwa Yugoslavia ya zamani iliyozaa Yugoslavia na Serbia!
Mwalimu Nyerere alikuwa na lengo zuri tu (kwa maoni yangu) katika kuanzisha Azimio la Arusha, kama alivyokaririwa akisema; “Bado naendelea kulibeba (azimio) kila niendako. Kila wakati nasoma tena na tena kuona nini ambacho naweza kukibadili. Labda nitaboresha katika Kiswahili kilichotumiwa lakini Azimio hili bado linafaa: Siwezi kubadili chochote. Tanzania ilikuwa imepata uhuru muda mfupi tu lakini tayari tulikuwa tumeshuhudia pengo kubwa kati ya wenye-nacho na wasio-nacho. Matajiri walikuwa wameibuka kutoka katika kundi la wanasiasa na maofisa ambao walikuwa maskini wakati ule wa utawala wa wakoloni, lakini sasa walikuwa wanatumia madaraka yao ndani ya chama na serikali kujinufaisha. Maendeleo ya aina hii yangewanyang’anya wananchi madaraka (kama ilivyo sasa). Kwa hiyo tukaanzisha chombo kipya: tukasema maendeleo ni kwa watu wote na si kikundi kidogo cha watu,” alisema.
“Azimio la Arusha ndicho kitu kilichoifanya leo Tanzania iwe Tanzania. Tulisema kile tulichokisimamia, tukaweka miiko ya uongozi kwa viongozi wetu na tukafanya juhudi kufikia malengo yetu. Hili lilikuwa dhahiri kwa kila mmoja, hata kama tulifanya makosa – na mtu anapojaribu kitu fulani kipya na kigeni lazima kuwepo na makosa.
“Azimio la Arusha na mfumo wetu wa demokrasia ya chama kimoja, pamoja na lugha yetu ya taifa, Kiswahili, na jeshi la taifa lililonolewa kisiasa na lenye nidhamu, liliweza kuyaunganisha makabila zaidi ya 126 katika taifa imara.
“Hata hivyo, pamoja na mafanikio yote haya, bado wanasema tulishindwa katika Tanzania, kwamba ‘tulichemka’. Lakini ni kweli tulishindwa? Lazima tuseme hapana. Hatuwezi kukanusha kila jambo tulilofanikiwa. Kuna rafiki zangu ambao hatukuwaruhusu wawe matajiri; sasa wametajirika na wanasema “Unaona, tunatajirika sasa, kwa hiyo hukuwa sahihi’. Lakini hilo ni jibu la aina gani? Kusuasua kwa ujamaa kumekuwa ni kwa dunia nzima. Hili ndilo linalopaswa kutolewa maelezo, siyo tu upande wa Tanzania. George Bernard Shaw, ambaye alikuwa anapinga kuwepo kwa Mungu, alipata kusema: “Huwezi kusema Ukristo umeshindikana kwa sababu haujajaribiwa.’ Hivyo ndivyo ilivyo hata kwa ujamaa: huwezi kusema ujamaa umeshindwa eti kwa sababu haukujaribiwa,” alifafanua.
Lakini leo hii tunapokumbuka miaka 10 ya kifo chake tunapaswa kujiuliza: Hivi ni kweli ujamaa ulishindwa au haukujaribiwa? Inavyoonekana ni kwamba viongozi wetu ndio wanaotufanya tuamini kwamba ujamaa kweli ulishindwa, wakati wananchi wa kawaida wanaelewa tofauti.
Itakumbukwa kwamba, enzi zile wakati siasa ya ujamaa na kujitegemea ikiimbwa kila kona, hata wanafunzi walijifunza kujitegemea, kwa kuzingatia Azimio la Musoma lililopitishwa Halmashauri Kuu ya TANU Novemba 1974 mjini Musoma likisisitiza kwamba ‘Elimu ni Kazi’.
Enzi zile kila shule, hasa za vijijini, zilikuwa na mashamba zikijishughulisha na kilimo, ikiwa ni elimu mojawapo ya kumwandaa mtoto aje ajitegemee baada ya kumaliza elimu yake ya msingi. Kilimo bora kilionekana hata katika Mashamba ya Ujamaa ya Vijiji ambapo kila kaya ilitakiwa kuwa na walau ekari moja na mazao yaliyovunwa humo yaliwekwa katika akiba ya kijiji ili kupambana na baa la njaa endapo lingetokea.
Wananchi walikuwa tayari kushiriki, lakini ukweli ni kwamba, viongozi wetu – wengi wao – hawakuwa tayari kuijaribu siasa ya ujamaa na kujitegemea kwa sababu iliwanyima fursa za kuchuma mali na kujilimbikizia.
Leo hii watoto hawajui hata mche wa mhindi ukoje, hawajui hata jembe linashikwaje, wakimaliza elimu ya msingi wanaambiwa ni wadogo, watafanya kazi gani. Lakini watu hawajiulizi kuhusu wale watoto waliokosa fursa za elimu ambao wengi ni wadogo kuliko hata hawa wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari, ambao wanachunga na kulima. Hawasemi kama ni wadogo, badala yake wanapiga kelele kwamba serikali imeshindwa kazi. Hivi ni kweli?
Tutafakari katika kipindi hiki na tuone tunawezaje kuinusuru nchi yetu na kongwa hili. <Mwisho>.





No comments:

Post a Comment