Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba
Na Beatrice Lyimo-MAELEZO,
Dodoma.
09/09/2016
Serikali
imetoa kauli kuhusu hali ya chakula nchini na kusema kuna chakula cha kutosha
pamoja na ziada ya asilimia 123.
Ziada
hiyo ya chakula inatokana na uzalishaji wa msimu wa mazao mwaka 2015/2016 ambao
unapelekea upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2016/2017.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba leo mjini
Dodoma alipokuwa akitoa kauli ya Serikali kuhusu hali ya chakula nchini.
“Takwimu
zinaonesha upatikanaji na mahitaji ya chakula nchini ni wa kuridhisha kwa kiwango
cha utoshelevu wa ziada kwa asilimia 123,” Dkt. Tizeba.
Katika
kufafanua hali hiyo, Dkt. Tizeba amesema kuwa kulingana na takwimu zilizopo
hali ya upatikanaji na mahitaji ya chakula nchini inautoshelevu wa ziada kwa
asilimia 123 ambapo nafaka ni asilimia 113 na mazao yasio ya nafaka ni asilimia
140 ambapo viwango vya ziada kwa mazao
yote ya chakula ni tani 3,013,515.
Dkt.
Tizeba ameongeza kuwa Wakala wa Hifadhi ya Chakula ya Taifa (NFRA) inauwezo wa
kuhifadhi jumla ya tani 246,000 ambapo kufikia Septemba 6, ilikuwa na akiba ya
tani 67,506.920 za chakula kinachojumuisha mahindi, mpunga na mtama.
Pia
amesema kuwa Serikali inaendelea na
mpango wake wa kuiongezea NFRA uwezo wa kuhifadhi chakula katika kanda sita
baada ya kupata mkopo wa dola za Kimarekani million 55 kutoka Serikali ya
Poland ambazo zitatumika kujenga vihenge vyenye uwezo wa kihifadhi tani 190,00
na maghala yenye uwezo wa kuhifadhi tani 60,000.
Kuhusu
muda wa Serikali wa kutoa vibali vya kuuza chakula nje ya nchi, Dkt Tizeba
amesema kuwa lengo ni kutoa nafasi kwa Serikali kukamilisha taarifa ya
tathimini ya awali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa mwaka 2015/2016 na
hali ya upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2016/2017.
Mbali
na hayo, Dkt Tizeba amesema kuwa katika
kuboresha hali ya usalama wa chakula
nchini, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi inapitia upya
mfumo wa utoaji wa vibali vya kusafirisha chakula nje ya nchi ili kuwezesha
ufuatiliaji wa karibu kuliko ilivyo sasa.
Aidha,
Dkt. Tizeba amesema kuwa utoaji wa vibali vya kusafirisha mazao nje umejitokeza
baada ya kuona chakula kinasafirishwa nje bila kufuata utaratibu maalumu ambapo
wafanyabiashara wa nchi jirani walijihusisha kununua vyakula vikiwa bado mashambani
kabla ya kuvunwa.
Aidha,
ametoa wito kwa wananchi kuhifadhi chakula cha kutosha kwa matumizi katika kaya
ambapo ameitaka sekta binafsi kuendelea kushiriki katika kutoa masoko ya
kununua na kuuza mazao katika maeneo yenye uhaba.
Kuhusu
hali ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi inayoikabili dunia ikiwamo
upungufu wa mvua , Dkt Tizeba amesema kuwa Serikali itaendelea na juhudi za
kuhimiza na kupanua kilimo cha umwagiliaji mashambani kwa kuimarisha
miundombinu iliyopo na uvunaji wa maji ya mvua ili kuongeza uzalishaji wa mazao
wenye tija.
Hata
hivyo, Serikali inaendelea kuhamasisha na kuelimisha wafanya biashara kuuza unga
nje ya nchi badala ya mahindi au mchele badala ya mpunga ili kuendana na Sera
ya kuendeleza Viwanda nchini na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo.

No comments:
Post a Comment