Katika vituo binafsi, wagonjwa wamekuwa wakipimwa kwa gharama inayofikia Sh50,000 hadi 60,000 kwa kila mtu.PICHA|MAKTABA.
Dar es
Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO),
limejiunga katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa ya dengue kwa kuagiza
vipimo 1,000 kwa ajili ya upimaji nchi nzima.
WHO imechukua hatua hiyo kusaidia juhudi
zinazoendelea za kupambana na homa hiyo na imeagiza utafiti zaidi ufanyike ili
kutambua aina halisi ya virusi vya dengue vilivyopo nchini kwa kulinganisha na
vile vinavyopatikana katika maeneo mengine duniani.
Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa
wa Taaluma na Udhibiti wa Magonjwa wa WHO, Dk Grace Saguti alisema tayari
chombo hicho kimeagiza vipimo hivyo vitakavyogharimu Sh17.7 milioni na kila
kimoja kinaweza kupima sampuli 25, hivyo kunufaisha watu 25,000.
Hatua hiyo imechukuliwa huku kukiwa na
taarifa kwamba baadhi ya hospitali za Serikali za wilaya na rufaa zinakabiliwa
na uhaba wa vipimo, hali iliyosababisha kutoza kati ya Sh25,000 hadi Sh30,000
kwa ajili ya kupima mgonjwa mmoja.
Katika vituo binafsi, wagonjwa wamekuwa
wakipimwa kwa gharama inayofikia Sh50,000 hadi 60,000 kwa kila mtu.
Juhudi hizo za WHO zimetangazwa siku
moja baada ya Serikali kupitia Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk
Steven Kebwe kulieleza Bunge kuwa kwa sasa vipo vipimo 350 na Serikali
inatarajia kuagiza vingine 750.
Dk Saguti alisema WHO imeshatengeneza miongozo,
mikakati na mafunzo pamoja na kutoa vitendea kazi ili kujua namna ya upimaji na
udhibiti.
“Sheria za afya za kimataifa za mwaka
2005 hadi 2007, zinaelekeza nchi kuhusu tatizo lolote lisilo la kawaida
liripotiwe WHO. Serikali ya Tanzania ilifanya hivyo na miongozo ya homa ya
dengue ikatolewa,” alisema.
Alisema miongozo iliyotolewa na WHO ni
pamoja na tatizo la dengue lisiachwe mikononi mwa Wizara ya Afya pekee, bali
sekta zote zihusishwe katika kuudhibiti.
Miongozo mingine ni uhamasishaji wa
upatikanaji wa vipimo ili kuhakikisha watu wenye dalili hizo na ambao wamepimwa
hawana malaria, wanapimwa na kutibiwa kama inavyotakiwa.
Alisema miongozo mingine ya WHO ni
kuwapo rasilimali fedha ili vituo vya afya viwe na dawa pamoja na vipimo.
Tayari Rais Jakaya Kikwete ameagiza
Wizara ya Fedha na ile ya Afya kushirikiana na Bohari Kuu ya Dawa (MSD)
kupambana na ugonjwa huo kwa dharura.
Takwimu
Jambo lingine ambalo WHO imeishauri
Serikali ni kutafuta takwimu sahihi ili kujua ukubwa wa tatizo na kulifanyia
kazi kulingana na uzito wake.
“Uhakiki wa takwimu, ushahidi na taarifa
sahihi za magonjwa ni suala muhimu katika kudhibiti. Ndiyo maana tunaitaka
wizara kuhakikisha inapata takwimu sahihi,” alisema.
Alisema wizara hiyo inatakiwa iwe na
mfumo mzuri wa takwimu kuanzia ngazi ya chini na ihusishe sekta za Serikali na
zile binafsi.
Wakati hadi jana takwimu za Serikali
zilionyesha kuwa idadi ya watu waliougua wamefikia 460, takwimu zilizopatikana
katika baadhi ya hospitali jijini Dar es Salaam zilionyesha kuwa walikuwa
wamefikia 677, achilia mbali waliokuwa wameugua kati ya Oktoba mwaka jana hadi
Machi.
Katika uchunguzi huo wa gazeti hili,
ilibainika kuwa Mwananyamala wamefikia wagonjwa 142, Amana (54), Maabara ya
Lancet (53), Hindul Mandal (26), Aga Khan (11), Kliniki ya IST (245), Regency
(63), Temeke (15), Dk Mvungi (3) Muhimbili (65).
MSD: Tuna vipimo vya kutosha
Wakati baadhi ya hospitali zikiripoti
uhaba wa vipimo, Kaimu Mkurugenzi wa MSD, Cosmas Mwaifani amesema inavyo vya
kutosheleza mahitaji.
“Sisi wakati wote tupo tayari kupambana
na dharura, si tu kwa sababu ya mlipuko, pia hatuhusiki kabisa na masuala ya kuongezeka
kwa bei za vifaatiba au dawa hospitalini kwa sababu ni taasisi ya Serikali,”
alisema.
Mmoja wa wasambazaji wa vipimo vya
upimaji wa dengue, Ally Hamimu alipiga simu chumba cha habari jana na kueleza
wasiwasi wake kuhusu gharama za vipimo kuwa akisema ni kubwa kuliko uhalisia.
??Tunaamini kuna vipimo mbalimbali vya
kupima homa ya dengue lakini hata kama hospitali zinatafuta faida, zinatakiwa
kutoza kati ya Sh13,000 na Sh15, 000 kwa kipimo,” alisema Hamimu na kutolea
mfano vitendanishi vya Dial Lab Dengue lgG/lgM ambavyo boksi la vipimo 30
huuzwa kati ya Sh175,000 na Sh190,000.
“Hii inamaanisha kuwa kipimo kimoja kwa
rejareja kinaweza kuuzwa kati ya Sh6,500 hadi Sh7,500 na huduma za kupima
zisizozidi Sh15,000.
“Sasa kutokana na mahitaji kuwa makubwa ya
vipimo hivi baada ya mlipuko wa dengue, baadhi ya wamiliki wa hospitali
wanapandisha bei, wananchi wasikubali,” aliongeza Hamim.
Dk Buberwa azikwa
Wakati huohuo, mamia ya wakazi wa Dar es
Salaam wakiwamo madaktari na watumishi wa hospitali mbalimbali, jana
walijitokeza katika Makaburi ya Tabata Kinyerezi, Dar es Salaam kumzika Dk
Gilbert Buberwa aliyefariki dunia Jumapili kutokana na homa ya dengue.
Dk Buberwa aliyekuwa daktari bingwa na
mkuu wa kitengo cha magonjwa ya akili katika Hospitali ya Temeke, ameacha mke
na watoto wawili.
Andrew Msechu, Florence Majani, Nuzulack
Dausen na Julius Mathias
CHANZO, MWANANCHI
No comments:
Post a Comment