Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza
Na Daniel Mbega
HADI kufikia Juni 2020 thamani ya mali za Chama cha
Maoinduzi (CCM) ilikuwa imepanda huku mapato yake yakifikia Sh. 59.8 bilioni kwa
mwezi.
Ongezeko hilo yalikuwa ni matunda ya uhakiki wa mali za Chama, kwani kabla ya zoezi hilo chama hicho kilikuwa kikiingiza mapato ya Sh. 191 bilioni kwa mwaka huku mali nyingi zikiwa chini ya watu wachache, hali iliyokifanya chama kuwa maskini na hoi kiuchumi na kuwa ombaomba licha ya kuwa na rasilimali nyingi.
Mageuzi haya makubwa ya kimuundo, kiutendaji na kiuchumi,
pamoja na kuondolewa kwa wanachama waliokuwa wakijali zaidi maslahi yao na kujimilikisha
mali za chama, yalileta matokeo mazuri ambayo yanahitaji usimamizi makini, kuondoa
urasimu na kuongeza ufanisi na kukijenga chama kiuchumi,.
Kusema ukweli, huko nyuma hali ya chama hicho kiuchumi na
hata kimuundo, haikuwa inafurahisha. Chama tawala kikiwa hoi kiuchumi inakuwa vigumu
kuzungumzia mageuzi makubwa ndani ya serikali.
Hata baada ya kuanza kwa siasa ya vyama vingi mwaka 1992,
CCM ilibaki na rasilimali zake yakiwemo majengo, taasisi kama Shule za Jumuiya
ya Wazazi, pamoja na viwanja vya michezo.
CCM inamiliki vyombo vya habari kama magazeti ya Uhuru na
Mzalendo, Radio Uhuru, kituo cha runinga cha Channel 10, ambacho pamoja na kuwa
mali ya CCM lakini hakikuwa chini ya CCM lakini kikarejeshwa, majengo, vituo
vya mafuta, vitalu na rasilimali nyingine zikarejeshwa baada ya zoezi.
Pia CCM ilipitia upya mikataba ya uwekezaji ikiwemo Vodacom,
jengo la makao makuu ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Dar es Salaam na
kuanzisha mfumo wa eletroniki wa usimamizi wa mali na rasilimali za chama
hicho.
Baada ya kuthaminisha upya mali za chama, thamani yake
imeongezeka kutoka Sh. 41.033 bilioni mwaka 2016/17 hadi Sh. 974.66 bilioni sawa
na ongezeko la asilimia 2,275.2.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, chama hicho kilipokea
wanachama mbalimbali kutoka upinzani na hali hiyo ikaongeza ruzuku kutoka
serikalini kutoka Sh. 12.4 bilioni mwaka 2015/2016 hadi Sh. 13.5 bilioni kwa
mwaka hivi sasa.
Vyanzo vya mapato na rasilimali ni vingi mno lakini vilikosa
usimamizi imara na ufisadi ukatawala. Mali nyingi ziliwanufaisha wachache na
baadhi ya viongozi walijimilikisha mali hizo. Chama kilibaki kuwa ombaomba na
kutegemea fedha za matajiri wachache waliojiita wafadhili wa chama.
Ndiyo, kwa miaka mingi CCM ilikuwa ni shamba la bibi, kila
mtu alikuwa akitafuna mali za chama mahali alipo.
Kulikuwa na upotevu mkubwa wa mali za chama uliosababishwa
na mikataba mibaya, ubadhirifu, wizi, usimamizi mbaya wa mali, utapeli na
ukosefu wa maadili katika uendeshaji wa miradi ya chama.
Kufa kwa Shirika la Uchumi na Kilimo Tanzania (SUKITA) lililokuwa mali ya chama ni matokeo ya ufisadi huo.
Viwanja vya michezo
Viwanja vya michezo vinavyotumika katika Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania viko zaidi ya 30, lakini CCM inamiliki takriban 16 kati ya hivyo.
Viwanja hivi kwa nyakati kadhaa hutumika kwa mechi za mpira
wa miguu kwa ligi mbalimbali kuanzia Daraja la Tatu hadi Ligi Kuu na baadhi
vinatumika kwa mechi za kimataifa.
Pia viwanja hivi hutumika kwa michezo mingineyo kama riadha
pamoja na matukio mengine.
Kwa hakika, viwanja hivi ni chanzo kikubwa cha mapato hasa
kwa uzingatia kwamba, mechi za mpira wa miguu znachezwa ila kukicha, lakini
pengine usimamizi makini na ukosefu wa ‘msamiati’ wa ‘ukarabati’ unavifanya
viwanja vingi viwe katika hali mbaya.
Uwanja wa CCM Mkwakwani, Tanga
Kumbukumbu nilizo nazo zinaonyesha kwamba, kwa msimu huu wa
Ligi Kuu ya NBC 2021/2022 viwanja wa CCM vinavyotumika ni CCM Kirumba (Mwanza)
chenye uwezo wa kuingiza watazamaji 35,000 kikiwa kiwanja cha pili kwa ukubwa
baada ya Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa wa jijini Dar es Salaam.
Uwanja wa CCM Kirumba ulijengwa mwaka 1980 na umetumika kwa
mechi nyingi za ligi na za kimataifa. Ulichukua nafasi ya uwanja wa Nyamagana unaomilikiwa
na Halmashauri ya Jiji la Mwanza uliojengwa na wakoloni tangu mwaka 1945.
Timu ambazo zimeutumia uwanja huo kama uwanja wao wa
nyumbani ni Pamba FC wana T.P. Lindanda, Toto African wa Kishamapanda, RTC
Mwanza (Biashara Mwanza), Mbao FC, Alliance Schools FC.
Viwanja vingine na idadi ya watazamaji kwenye mabano ni Kambarage
wa Shinyanga (30,000), CCM Gombani wa Chake Chake, Pemba (30,000), Ali Hassan
Mwinyi –Tabora (20,000), Kumbukumbu wa Shekhe Amri Abeid Kaluta – Arusha (20,000),
ambao mwaka 2011 ulitumika kwa mashindano ya Global Kilimanjaro Bowl kati ya CONADEIP
Stars na Drake Bulldogs, mechi ya kwanza ya mchezo wa American Fotball kuchezwa
barani Afrika.
Uwanja wa Jamhuri, Dodoma
Viwanja vingine ni Lake Tanganyika – Kigoma (watazamaji 20,000),
CCM Mkwakwani – Tanga, zamani ukijulikana kama Manispaa (15,000), uwanja huu ulijengwa
mwaka 1973, Uwanja wa Nangwanda Sijaona = Mtwara (15,000), CCM Jamhuri – Morogoro
(10,000), CCM Jamhuri – Dodoma (10,000), Sokoine –Mbeya – zamani ukijulikana
kama Mapinduzi kabla ya kubadilishwa jina mwaka 1984 baada ya kifo cha Edward
Moringe Sokoine (10,000).
Aidha, viwanja vingine ni Maji Maji – Songea (10,000), CCM Kaitaba
– Bukoba (5,000), Kumbukumbu ya Karume – Musoma (5,000), CCM Namfua - Singida (10,000),
Samora Machel – Iringa (10,000), na Nelson Mandela – Sumbawanga (10,000).
Viwanja hivi baadhi vinamilikiwa na CCM Taifa na vingine
vinamilikiwa na CCM Mkoa.
Viwanja ambavyo haviko chini ya umiliki wa CCM ni Uwanja wa
Taifa (watazamaji 60,000) na Uwanja wa Uhuru (23,000) vya jijini Dar es Salaam
ambavyo vinamilikiwa na Serikali.
Uwanja wa Jamhuri, Morogoro
Uwanja Amaan Unguja (15,000) unaomilikiwa na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, Azam Complex - Dar es Salaam (10,000) unaomilikiwa na Azam
FC, Manungu – Turiani (5,000) unaomilikiwa na Mtibwa Sugar, Majaliwa Stadium –
Ruangwa (20,000) unamilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Ilulu Lindi
(10,000) unamilikiwa na Halmashauri ya Manispaa, Ushirika Moshi (10,000)
unamilikiwa na Chuo cha Ushirika, Mgambo Mpwapwa unamilikiwa na Halmashauri ya
Mji Mpwapwa, Nyamagana Mwanza (5,000) unamilikiwa na Halmashauri ya Jiji.
Mgodi wa dhahabu
Viwanja hivi vya michezo ni mgodi wa dhahabu kwa CCM endapo
itaamua kuwekeza kwa dhati, kwanza kwa kuvifania ukarabati wa kutosha ikiwa ni
pamoja na kuweka nyasi bandia na kujenga majukwaa na kiundombinu mingine,
pamoja na kuweka usimamizi makini.
Waumini wa soka ni wengi na mahali pengine hujaa hata kabla
ya ‘kengele’, hivyo kwa kuamua kuviboresha utakuwa ni uwekezaji wa uhakika kwa CCM
na chanzo muhimu cha mapato kitakachokifanya chama hiki, ambacho kimetimiza
miaka 45, kujitegemea kiuchumi.
0768-687007
No comments:
Post a Comment