Pages

Pages

Pages

Thursday 3 November 2016

MWAKA MMOJA WA JPM SEKTA YA UTALII YATOA MCHANGO MKUBWA KWENYE UCHUMI NCHINI

Na Beatrice Lyimo - MAELEZO

Mnamo Novemba Tano mwaka huu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli atatimiza mwaka mmoja tangu alipoapishwa kuongoza Nchi hii katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Katika uongozi wake wa mwaka mmoja, Sekta ya Utalii nchini imeendelea kutoa mchango mkubwa katika kuongeza mapato ya serikali kupitia mikakati mbalimbali ambayo imeifanya kuwa sekta kuwa yenye manufaa zaidi ya kiuchumi.

Hatua hii inatokana takwimu zilizotolewa na  Wizara ya Maliasili na Utalii ambazo zinaoonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2015 idadi ya watalii waliongia nchini ilikuwa 1,376,182 na kuingizia mapato kiasi cha Dola za Marekani 1.9 bilioni.

Aidha ,idadi ya watalii walioingia nchini katika kipindi cha Julai mpaka Agosti imeongezeka asilimia 11, na hivyo kuifanya ni eneo linaloiingizia Serikali takribani asilimia 25 ya fedha za kigeni.
Kwa mujibu wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Profesa Jumanne Mghembe anasema kwa kuzingatia dhamira ya Serikali ya kujitegemea kiuchumi Wizara yake imeanzishakodi ya ongezeko la thamani (VAT) katika sekta ya utalii, hatua iliyolenga kuiongezea Serikali mapato yatakayoweza kuchangia katika kutoa huduma za jamii.
“Uanzishaji wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) katika sekta ya utalii, kumesaidia kuongeza watalii nchini na mapato yamekuwa kwa asilimia 22 zaidi,” anasema Waziri Maghembe.
Waziri Maghembe anasema uanzishaji wa VAT haujaathiri ongezeko la idadi ya watalii nchini, na badala yake Tanzania inaendelea kuwa kimbilio la watalii duniani
Kwa mujibu taarifa iliyotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii, idadi ya watalii wanaoingia katika Hifadhi za Taifa (TANAPA) katika kipindi cha Juni-Julai 2016 imeongezeka kwa wastani wa asilimia 2.2 na mapato yatokananyo na viingilio hifadhini yameongezeka kwa wastani wa asilimia 19.7
Huduma za malazi pia zimekuwa zikitozwa kodi na Serikali hivyo kuondoa msamaha wa miaka 10 uliokuwepo awali na sasa vinachangia zaidi katika mapato ya nchi moja kwa moja kwa kuondoa msamaha huo.
 Taarifa hiyo imeongeza kuwa pamoja na huduma za utalii zimeanza kutozwa VAT kwa asilimia 18, lakini safari kwa ujumla zimeongezeka kwa asilimia chini ya hiyo kwa sababu huduma za malazi zimekuwa zikitozwa kodi hiyo tangu miaka ya nyuma.
Katika hatua hiyo Watalii mbalimbali waliohojiwa nchini wameonyesha kuunga mkono hatua hiyo ya Serikali za kuwatoza kodi kwani fedha zitakazokuwa zikilipwa na wataliii zitasaidia katika shughuli nyingine za uchumi.

Pia katika kuendeleza kutangaza Sekta ya Utalii nchini, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imetenga kiasi cha Tsh Milioni 648 kwa ajili ya shughuli za utangazaji wa Utalii nje ya nchi na Tsh.Milioni 300 kwa ajili ya utangazaji wa vivutio vya utalii wa ndani ya nchi.
Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kutekeleza majukumu yake licha ya mabadiliko na changamoto mbalimbali na inatarajiwa kuwa rasilimali za maliasili, malikale na utalii zitaendelea kuchangia kwa kiwango kikubwa juhudi za kukuza uchumi wa Taifa.
Kwa upande wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) katika kipindi cha mwaka mmoja imeimarisha utangazaji wa vivutio vya utalii kupitia mtandao wa kompyuta yaani Tourism Destination Portal pamoja na mitandao ya kijamii kwa kuweka taarifa zaidi za vivutio vya utalii katika tovuti hiyo maalumu ya utalii zikiwemo ramani (digital map), picha za video na picha za mgando kwa kila kivutio cha utalii katika tovuti hiyo.

Aidha, TTB imeendelea kushirikiana na watu maarufu katika kutangaza utalii wetu. Miongoni mwa watu hao ni wasanii wa ndani wakiwemo mchezaji maarufu wa Tanzania anayecheza mpira wa miguu nchini Ubelgiji Mbwana Samatta na mwanamuziki Vanessa Mdee.

Mpaka kufikia mwezi Juni 2016 idadi ya watalii wa Kimataifa waliongia nchini ilikuwa ni 519,582ikilinganishwa na watalii 504,711 waliongia nchini mpaka kufikia         mwezi Juni 2015.
Idadi hii ni sawa na ongezeko la asilimia 2.86. Kwa kipindi cha miezi ya Julai na Agosti 2016 inaonyesha kuwa idadi ya watalii waliongia kwenye hifadhi za Taifa imeongezeka kwa wastani wa asilimia 11.16. 

Akiongea wakati wa uzinduzi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Magufuli aliwataka mabalozi wanaowakilisha Tanzania nchi za nje kutumia fursa zilizopo katika kutangaza utalii wa nchi ili kuweza kuongeza pato la Taifa.

No comments:

Post a Comment