Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeandaa semina elekezi kwa klabu za Ligi Kuu za wanawake inayotarajiwa kuanza baadaye mwaka huu.
Semina hiyo kwa ajili ya maandalizi ya michuano hiyo, itafanyika Jumamosi Septemba 3, 2016 kwenye Ukumbi wa Hosteli za TFF zilizopo ofisi za Makao Makuu ya shirikisho hilo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, makutano ya barabara za Shaurimoyo na Uhuru jijini Dar es Salaam.
Ligi hiyo ya wanawake ni ya kwanza kufanyika nchini chini ya uongozi wa Rais Jamal Malinzi kwani kabla ya hapo hapakuwa na ligi inayohusisha mikoa mbalimbali. Shukrani za pekee ziende kwa Kituo cha Televisheni cha Azam, kilichoamua kudhamini ligi hiyo pamoja na ile ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 20.
TFF imeandaa semina hiyo kwa ajili ya kuwapa maelekezo kuhusu kanuni za ligi, usajili wa timu na taratibu nyingine za ligi hiyo ikiwa ni pamoja na sheria za mpira wa miguu ambazo zimekuwa na marekebisho kwa msimu wa 2016/2017 kama zilivyotolewa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Timu shiriki katika ligi ni Viva Queens ya Mtwara, Fair Play FC ya Tanga, Panama FC ya Iringa, Mlandizi Queens ya Pwani, Marsh Academy ya Mwanza, Baobao Queens ya Dodoma, Majengo Queens ya Singida, Kigoma Sisters FC ya Kigoma, Kagera Queen pamoja na JKT Queens, Mburahati Queens na Evergreen Queens za Dar s Salaam.
No comments:
Post a Comment