Wizari wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu
Na
Eleuteri Mangi-MAELEZO, Dodoma
Serikali imewasilisha Miswada miwili inayohusu
Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa mwaka 2016 na ule wa
Sheria ya Usimamizi wa Wanataaluma wa Kemia wa mwaka 2016 ambayo imesomwa kwa
mara ya pili Bungeni ili ijadiliwe na wabunge.
Awali akisoma Muswada wa Sheria ya Mamlaka
ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa mwaka 2016, Wizari wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalim amesema kuwa madhumuni ya Muswada
huo ni kuanzisha Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kuweka
kisheria majukumu yake.
Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa Muswada huo
umezingatia masuala mbalimbali ikiwemo kuanzishwa kwa Mamlaka ya Maabara ya
Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na kuainisha majukumu yake na kuanzisha Bodi ya
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Mambo mengine yaliyozingatiwa katika
Muswada huo ni kubainisha utaratibu wa uteuzi wa Mkemia Mkuu wa Serikali,
majukumu yake na mamlaka yake, kuifanya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa
Serikali kuwa maabara ya rufaa na msemaji wa mwisho wa Serikali katika shughuli
za uchunguzi wa kimaabara wa kikemia, sayansi jinai na vinasaba na Muswada huo
utawwzesha kuwekwa utaratibu wa kusajili, kuratibu na kusimamia maabara na
shughuli zote za maabara za kikemia, sayansi jinai na vinasaba.
Zaidi ya hayo, Waziri Ummy amesema kuwa
kupitia Muswada huo kitawekwa kifungu maalum chini ya Mamlaka ya Maabara ya
Mkemia Mkuu wa Serikali kitakachogharimiwa na Serikali kwa ajili ya uchunguzi
wa vielelezo vya makosa ya jinai, majanga na masuala mengine yenye maslahi ya
taifa ili kuwezesha utekelezaji wa jukumu hilo kwa ufanisi hali itakayosaidia
utoaji wa haki katika vyombo vya maamuzi na kuleta utengamano katika jamii.
Aidha, Muswada wa pili uliowasilishwa
unahusu Sheria ya Usimamizi wa Wanataaluma wa Kemia wa mwaka 2016 ambapo maoni
na ushauri yaliyotolewa na Kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma ya Maendeleo ya
Jamii yaliyosawilishwa na Jasmin Tisekwa (Mb) kwa niaba ya Mwenyekiti wakamati
hiyo Peter Serukamba amesema kuwa Muswada huo utasaidia kutungwa kwa sheria ambayo italeta tija kwa maendeleo ya
jamii na taifa kwa ujumla.
Zaidi ya hayo, Jasmini amesema kuwa Muswada
huo utasaidia wanataaluma ya Kemia kukabiliana na maendeleo ya sayansi na
teknolojia pamoja kwa kuzingatia taaluma hiyo kwani ina mchango mkubwa katika
maendeleo ya sekta za elimu, kilimo, viwanda, sheria, afya, mazingira na jamii
kwa ujumla wake.
Akisoma maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, Waziri Kivuli wa Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ester Mtiko amepongeza jitihada zinazofanywa na wataalamu
wa kemia katika sekta mbalimbali kwa kuwa wana wajibu mkubwa kwa maslahi ya
taifa kwa ajili ya usalama na kuendeleza maarifa ya kisayansi.
No comments:
Post a Comment