Pages

Pages

Pages

Sunday 7 August 2016

MAONYESHO YA SAYANSI YA WANAFUNZI YA YST 2016 KUFANYIKA AGOSTI 11 UKUMBI WA JNICC DAR


                                     TARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Young Scientists Tanzania (YST) - Shirika la Wanasayansi Chipukizi Tanzania- linapenda kuwafahamisha wanafunzi, walimu na wananchi kwa ujumla kuwa onesho la wanasayansi chipukizi la mwaka 2016 litafanyika katika ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC) jijini Dar es Salaam tarehe 10-11/08/2016. Tukio hili ni muhimu kwa kuonyesha kazi za ugunduzi wa kisayansi na teknolojia zilizotengenezwa na wanafunzi wa shule za sekondari kutoka mikoa yote ya Tanzania. Tunawashukuru Irish Aid na BG Tanzania kwa kuendelea kudhamini mashindano haya, sambamba na wadhamini wengine. Tunawakaribisha watu wote waje wajionee vipaji vya vijana wetu siku ya tarehe 11/08/2016 kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 6:30 mchana.

Mwaka huu wanafunzi 300 wataonyesha kazi zao za ugunduzi wakiwa na walimu/washauri wao 150. Hili ni ongezeko kubwa la washiriki ukilinganisha na mwaka jana. Kwa siku mbili, wanasayansi chipukizi wataonyesha ugunduzi wao katika sayansi ya kemia, fizikia na hisabati; biologia na ekolojia; sayansi ya jamii na tekinolojia. Ugunduzi huu umejikita hasa hasa kutafuta njia za kutatua matatizo yahayohusiana na masuala ya afya, kilimo na usalama wa chakula, mawasiliano na usafirishaji, nishati na mazingira, elimu, na matatizo ya kijamii.
Ili kutambua kazi nzuri zilizofanywa na wanasayansi chipukizi, zawadi zitatolewa kwa wanafunzi watakaoonyesha ugunduzi mzuri zaidi. Wanafunzi wapatao 50 watashinda zawadi za pesa, medali, vikombe, vifaa vya maabara, na kutengezewa maktaba kwa shule itakayoshinda zawadi ya maktaba. Wanafunzi wanne watashinda zawadi za udhamini wa kusomeshwa chuo kikuu katika fani za sayansi ili kuwawezesha kuwa wanasayansi mahili miaka ya badae. Washindi wa jumla wa mashindano ya mwaka huu watalipiwa gharama zote kwenda kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya BT Young Scientists huko Ulaya nchini Ireland mwezi Januari 2017 na pia watapewa udhamini wa kusomeshwa chuo kikuu.  
Mashindano ya mwaka huu ni ishara tosha kuwa namna ya ufundishaji sayansi katika nchi yetu umeanza kubadilika. Utamaduni wa sayansi umeanza kujengeka miongoni mwa wanafunzi kwani wameanza kusoma sayansi kwa wingi na kwa vitendo kwa kutumia sayansi kutafuta suluhisho la matatizo ya kiuchumi na kijamii yanayozikabili jamii zetu. Hii imefanya sayansi ifanyike kivitendo zaidi na kuwafanya wanafunzi wapende kujihusisha katika masula ya sayansi na tekinolojia.
Tunawakaribisha watu wote wa Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla kuwa kujionea ugunduzi huu wa sayansi na teknolojia uliofanywa na wanasayansi chipukizi.
Mawasiliano: Dr. Gosbert Kamugisha, Mkurugenzi & Mwanzilishi Mwenza - YST, +255767708579. 

No comments:

Post a Comment