Pages

Pages

Pages

Friday 24 June 2016

TOVUTI YA WANANCHI INAVYOTATUA KERO ZA WANANCHI


Na Immaculate Makilika -MAELEZO

Ni ukweli usiopingika kwamba dunia imeingia katika maendeleo ya teknolojia yanayopelekea matumizi ya vifaa vya kisasa na vyenye utaalamu wa hali ya juu katika kufanya shughuli mbalimbali, ambazo hapo awali zilifanywa kwa kutumia nguvu kubwa na idadi kubwa ya watu na kwa muda mrefu.

Maendeleo hayo ya teknolojia yamejidhihirisha katika nyanja nyingi mojawapo ni hii ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano umerahisisha mawasiliano na unatoa fursa kwa jamii kwa ujumla kuwa huru zaidi katika kutekeleza majukumu yake. 
Serikali inatoa fursa kwa wananchi kutoa hoja na kero zao popote pale walipo kwa kuanzisha tovuti katika wizara, taasisi na ofisi zake ambazo zinawezesha wananchi kupata tarifa muhimu na kwa urahisi kuhusu wizara, ofisi ama taasisi husika na serikali kwa ujumla.

Katika kuzingatia maendeleo hayo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, mwaka 2006 Rais wa awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, aliitaka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wakati huo chini ya Idara ya Habari  -MAELEZO kuanzisha, kuratibu na kusimamia Tovuti ya Wananchi.

Dhamira kubwa ya kuanzishwa kwa tovuti hii ni kutokana na matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 Ibara ya 18 toleo la mwaka 2005, maagizo ya Sera ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003; na dhana ya Serikali inayozingatia Haki za Binadamu na Utawala Bora kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 19 ya Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu na Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Aidha, tovuti hii inatoa fursa kwa wananchi kuwasiliana moja kwa moja na Serikali yao, kuwawezesha watanzania popote walipo duniani kuweza kuwasilisha hoja zao, maoni na malalamiko serikalini kwa kutumia mtandao wa intaneti .

Vile vile, Tovuti ya Wananchi inarahishisha upelekaji wa hoja za wananchi kwenda kwa maafisa husika wa serikali ili zifanyiwe kazi na kujibiwa na kuiwezesha serikali kurudisha majibu na kutoa maelezo ya kina kuhusu hoja zinazopokelewa kutoka kwa wananchi kupitia njia za intaneti na ujumbe mfupi (SMS).

Malengo hasa ya kuanzishwa kwa tovuti ya wananchi ni:
Kuimarisha na kupanua dhana ya uwazi na uwajibikaji Serikalini dhana ambayo ni nguzo muhimu ya utawala bora. Kusaidia mapambano dhidi ya rushwa, uonevu, unyanyasaji na maovu mengine katika jamii kwa kusaidia mawasiliano ya haraka na vyombo husika vya dola.

Malengo mengine ni pamoja na kuiwezesha Serikali kupata maoni ya wananchi juu ya vipaumbele vyao vya maendeleo na kuhusu ubora wa huduma mbalimbli wanazopatiwa na watumishi wa umma kwa lengo la kuziboresha pamoja na kuiwezesha Serikali kupata hoja na takwimu zitakazoiwezesha kubuni mbinu mikakati mipya ya mageuzi ya kiuchumi na kijamii ili nchi yetu ipige hatua kubwa zaidi ya maendeleo na kuifanya ifikie uchumi wa kati ifikapo 2020.

Katika hotuba ya bajeti ya mwaka 2016/2017 iliyowasilisha Bungeni na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Nape Nnauye, alisema kuwa Wizara imeratibu utoaji wa ufafanuzi kuhusu hoja na kero mbalimbali za wananchi kwa serikali zilizowasilishwa kupitia Tovuti ya Wananchi. katika kipindi cha mwezi Julai, 2015 hadi Machi, 2016. Jumla ya hoja 93 zilipokelewa. kati ya hizo, hoja 70 zimepatiwa ufafanuzi na hoja 23 zimeendelea kufanyiwa kazi.

Lakini pia Tovuti ya Wananchi imepokea jumla ya hoja 117,336 tangu ilipoanza kazi mwaka 2007 hadi kufikia Machi mwaka 2016, kati ya hizo hoja 78,328 zimeshughulikiwa, huku wananchi 48 walitembelea Idara ya Habari- MAELEZO na kuwasilisha hoja zao. Hoja hizo zimeshughulikiwa.

Wananchi hao ni pamoja na wananchi wa mtaa wa Zavara katika kata ya Chanika ambao eneo lao lilivamiwa. Hoja yao iliwasilishwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala na kushughulikiwa. Mtoto mwenye saratani aliwasilisha hoja yake na kupelekwa Wizara ya Afya na kufanikiwa kupata matibabu nchini India.

Aidha, wananchi wengi waliowasilisha hoja zao zilizohusu kucheleweshwa kwa kusikilizwa kwa kesi zao mahakamani, hoja zao zilishughulikiwa na kesi zao zilisikilizwa na kutolewa maamuzi.

Tovuti hii inamwezesha Mtanzania yeyote aliyeko mahali popote duniani penye mtandao wa intaneti au mwenye simu ya mkononi kuwasiliana na Maafisa Wakuu wa Wizara yoyote ili kutoa maoni, ushauri, pongezi au malalamiko au kuiuliza swali serikali moja kwa moja.

Hoja huwasilishwa Serikalini kwa kutumia intaneti kwa kufungua anwani ya tovuti – www.wananchi.go.tz – bonyeza sehemu iliyoandikwa weka hoja. Njia nyingine ya kuwasilisha hoja ni kwa kuandika ujumbe mfupi kwa kutumia simu ya mkononi. Hii itatumika mara baada ya namba ya kutuma na kupokea ujumbe huo itakapokuwa tayari, kwa kuandika barua kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari –MAELEZO S.L.P 8031 au tembelea ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO zilizopo mtaa wa Samora jijini Dar es Salaam karibu na Makao Makuu ya Shirika la Bima la Taifa (NIC).

Hoja zinapotumwa huingia moja kwa moja katika Wizara, Idara zinazojitegemea na Wakala wa Serikali. Iwapo mtumaji hana uhakika na sehemu ambapo anataka hoja yake aielekeze, hoja hiyo huingia moja kwa moja makao makuu ya Tovuti ya Wananchi, Idara ya Habari – MAELEZO, waratibu wa Tovuti huiwasilisha hoja hiyo Wizara au taasisi inayohusika.

Hoja hizo hutafutiwa majibu na Maafisa wa Wizara husika ambao nao huyatuma majibu hayo kwa mtuma hoja ndani ya siku tano za kazi, kwa kupitia njia aliyoitumia mtuma hoja.

Baadhi ya Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi wameweza kuwasilisha kero zao kupitia na Tovuti hii ya Wananchi, ambapo walipatiwa majibu ya hoja zao, kama vile Bibi Valeria Luzebigo aliweza kupata majibu ya vipimo kutoka kwa mkemia Mkuu wa Serikali kufuatia kifo cha baba yake mzazi.

Aidha Bwana Saidi Bundela, mkazi wa Dar es Salaam mwenye ulemavu wa miguu alipatiwa msaada wa magongo ya kutembelea na Rais Msaaafu Dkt. Jakaya Kikwete. Naye BwanaGeofrey Bwananali, mkazi wa Dar es Salaam ameendelea kupatiwa msaada wa matibabu ya ngozi baada ya kuwasilisha matatizo yake kupitia tovuti hii.

Ni wakati sasa kwa watanzania walioko ndani na nje ya nchi kutumia fursa hii ya maendeleo ya teknolojia hasa matumizi ya Tovuti ya Wananchi katika kuwasilisha hoja na kero mbalimbali, ambazo zinalenga kuboresha hali ya wananchi pamoja na utendaji wa Serikali kwa maendeleo ya Taifa.

Tovuti ya Wananchi imekuwa msaada mkubwa kwa watumiaji. Ni wito kwa kila Mtanzania kutumia haki yake ya kikatiba ya kutoa maoni yake kwa uhuru kupitia Tovuti hii. Ikumbukwe kwamba mawasiliano hai katika maisha ni kama mishipa ya damu mwilini.

MWISHO


No comments:

Post a Comment