Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Wednesday 9 March 2016

YANGA KUPAA KWENDA KIGALI KWA MKWARA, AZAM YAENDA SAUZI KWA KIAPO!


MABINGWA wa soka Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, wameondoka leo Jumatano Machi 9, 2016 kwenda Afrika Kusini huku mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga, nao wakitarajiwa kuondoka Alhamisi Machi 10, 2016 kwenda Kigali katika harakati za kuwania ushindi kwenye michuano ya klabu Afrika.
Yanga, ambayo imecheza mechi saba mfululizo bila kufungwa – zikiwemo tano za Ligi Kuu – inaondoka kwenda kuivaa APR Jumamosi Machi 12, katika mchezo wa kwanza wa mzunguko wa kwanza ikiwa na ushindi mnono wa mabao 5-0 ilioupata Jumanne, Machi 8, 2016 dhidi ya African Sports kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hali hiyo inawapa jeuri vijana wa Hans van der Pluijim, ambao wanaonekana kuimarika na kueleza kwamba wana uhakika mkubwa wa kuibuka na ushindi ugenini kwa APR, ambayo hivi karibuni ilimuajiri kimya kimya Nizar Khanfir, aliyewahi kuwa kocha wa timu ya Taifa ya Tunisia pamoja na klabu za Stade Gabasien, Club African, Esperance na Sfaxien.
Khanfir amechukua mikoba ya kocha wa muda, Emmanuel Rubona, ambaye ndiye ameiongoza vyema APR tangu Septemba 2015. Rubona sasa atarejea kwenye nafasi yake ya awali ya kocha msaidizi, wakati kipa mkongwe Jean Claude Ndoli ataendelea kuwa kocha wa makipa.
Yanga imecheza mechi tano za ligi bila kupoteza ambapo ilitoka sare ya 2-2 na Prisons, ikaifunga JKT Ruvu 4-0, ikaifunga Simba 2-0 kabla ya kubanwa mbavu na Azam kwa sare ya 2-2, lakini ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya ‘Wana Kimanumanu’ African Sports ni chachu ya kiwango cha juu kuweza kuchochea kufanya vizuri dhidi ya APR.
Mechi nyingine mbili za Yanga zilikuwa za raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa, ambapo kwanza iliifunga Cercle de Joachim 1-0 ugenini kabla ya kuichapa 2-0 jijini Dar es Salaam na kusonga mbele.
APR, ambayo inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Rwanda, imecheza mechi tisa mfululizo bila kupoteza, hii ni tangu ilipofungwa na Mukura Victory mabao 2-0 Septemba 22, 2015.
Baada ya hapo, ikiwa chini ya Rubona, imetoka sare mara mbili na imeshinda mechi saba, ikiwemo ya Machi 3, 2016 dhidi ya Amagaju ambayo Wajeda hao walishinda 2-1.
Japokuwa ilifungwa mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Mbabane Swallows ugenini, lakini ilizinduka nyumbani na kuishindilia timu hiyo ya Swaziland mabao 4-1.
Kwa upande wa Azam, wao wameondoka leo Jumatano kwenda kuvaana na Bitvest Wits ya Afrika Kusini katika mchezo wa kwanza wa mzunguko wa kwanza wa Kombe la Shirikisho, lakini wakiwaahidi Watanzania kwamba watawarejeshea furaha ya ushindi.
Mchezo ambao utafanyika kwenye Uwanja wa Bidvest jijini Johannesburg, Jumamosi Machi 12 kuanzia saa 1.00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, utachezeshwa na waamuzi kutoka Madagascar wakiongozwa na Andofetra Avombitana Rakotojaona atakayepuliza kipyenga, akisaidiwa na Pierre Jean Eric Andrivoavonjy na Lionel Hasinjarasoa Andrianantenaina.
Azam imeanzia moja kwa moja raundi ya kwanza, lakini Bidvest Wits imefika hatua hiyo baada ya kuiondoa Light Stars ya Seychelles kwenye raundi ya awali kwa ushindi wa jumla wa mabao 9-0, ikianza kwa kushinda ugenini 3-0 kabla ya kuichapa tena 6-0 nyumbani.
Bidvest, ambayo leo Jumatano iko ugenini kwa Polokwane, haijapoteza mechi tangu ilipofungwa 1-0 nyumbani na Kaizer Chief Fevruari 9, 2016. Baada ya hapo iliifunga Pretoria University 2-1 na ikatoa kipigi kama hicho kwa Maritzburg Februari 24.
Kwa sasa timu hiyo inashika nafasi ya pili nyuma ya Mamelodi Sundowns ikiwa na pointi 42 baada ya kushuka dimbani mara 21. Sundowns ina pointi 52.
Hata hivyo, kocha msaidizi wa Azam FC, Mario Marinica, alikaririwa wiki hii akisema wameiona Bidvest Wits kwenye mechi kadhaa na wanajua mbinu wanazotumia na kuahidi kwamba wanayo nafasi nzuri ya kuwatoa Wasauzi hao.
Marinica ndiye aliyekwenda kuipeleleza Bidvest Wits wakati ikiichapa Light Stars ya Seychelles mabao 3-0 kwenye raundi ya kwanza ya michuano hiyo, akiwa ameongozana na kocha mwingine msaidizi Dennis Kitambi.
“Tuna kikosi bora, lakini tatizo kubwa tulilonalo ni kushindwa kutumia vema nafasi tunazotengeneza za kufunga mabao, vinginevyo naamini tuna nafasi kubwa ya kufanya vizuri dhidi ya Bidvest kama tukicheza kwa staili yetu tunayocheza hivi sasa,” alisema kocha huyo raia wa Romania.
CREDIT: FIKRAPEVU

No comments:

Post a Comment