Na Eleuteri Mangi- MAELEZO
03/03/2016
Serikali imeongeza wigo wa utoaji wa kibali cha
uchangiaji wa elimu msingi bila malipo hadi kwa Wakuu wa Mikoa baada ya
kujiridhisha kuwa taratibu zilizowekwa zimefuatwa kikamilifu.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo
jijini Dar es salaam Msemaji wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI) Rebecca Kwandu amesema kuwa awali vibali hivyo vilitolewa na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
pekee ikiwa na lengo la kudhibiti michango holela.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa azma ya Serikali ya kutoa
elimumsingi bila malipo haizuii wadau mbalimbali wa elimu kuchangia maendeleo ya
elimu kwa hiari ambapo wadau wakiamua kuchangia kwa nia ya kushughulikia kero
fulani iliyopo katika shule yao au shule zao baada ya kupata kibali
wanaruhusiwa kufanya hivyo.
Katika kutekeleza dhana ya utoaji wa elimumsingi bila
malipo, hadi kufika mwishoni mwa mwezi Januari, 2016 Serikali inatoa elimu hiyo kwa jumla ya
wanafunzi 9,771,902.
Kati ya wanafunzi hao, 8,301,759 ni wa elimu ya msingi na
1,470,143 ni wa sekondari ambao wanapatiwa elimumsingi bila malipo kuanzia
kidato cha kwanza hadi cha nne.
Serikali inasisistiza kuwa viongozi wanahusika katika
kusimamia utekelezaji wake ambapo kwa upande wa wazazi au walezi, kamati na
Bodi ya shule pamoja na jamii wao nao wanajukumu la kuelewa majukumu yao
ipasavyo.
Aidha, juhudi za makusudi zinapaswa kufanywa na viongozi
na watendaji wa elimu ili kuwezesha jamii kufahamu wajibu wao katika
utekelezaji wa elimumsingi bila malipo na hatimaye kufikiwa kwa malengo
yaliyokusudiwa.
Katika kutekeleza wajibu wake, Serikali ya Awamu ya Tano
(SAT) kuanzia mwezi Januari, mwaka huu imeanza kutoa elimumsingi bila malipo
imetoa waraka wa Elimu Namba 6 wa Mwaka 2015 ambao unaofafanua na kubainisha
majukumu ya serikali na wadau mbalimbali katika utekelezaji wa elimu msingi
bila malipo.
No comments:
Post a Comment