IDARA YA HABARI - MAELEZO
P.O. Box
8031, Dar es Salaam, Tel: 2110585,
2122771/3, Fax: 2113814, e-mail: maelezo@habari.go.tz
Tarehe: 01/03/2016
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Gazeti la Dira ya Mtanzania, Toleo Na.404 la Februari, 29 – Machi 6, 2016 liliandika
taarifa yenye kichwa cha habari kisemacho “Uchafu
wa Ombeni Sefue Ikulu”. Taarifa hiyo, ambayo ni muendelezo wa makala nyingine kwenye toleo la
gazeti hilo la wiki iliyopita, ilimtuhumu Katibu Mkuu Kiongozi kushawishi juu
ya uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa MSD pamoja na Kampuni za “CRJE” na “UGG” kupewa tenda
ya kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma, Daraja la Kigamboni na Reli ya Dar es Salaam
- Kigali. Taarifa zote hizi ni za uongo na za kupotosha wananchi.
Kuhusu uteuzi wa nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa MSD,
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, hakuhusika kwa
namna yoyote kushawishi uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa MSD. Uteuzi huo ulitekelezwa
kwa kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa. Nafasi hiyo ilitangazwa na Bodi
tarehe 20 Novemba, 2013. Usaili ulifanywa na kampuni huru iliyopewa jukumu hilo
na Bodi. Mapendekezo ya majina matatu yalipelekwa kwa Mhe. Rais na Waziri wa
Afya, kwa ajili ya uteuzi. Balozi Sefue
alikuwa hamjui aliyeteuliwa na wala hakuwahi kuwa na uhusiano naye. Alichofanya
Balozi Sefue ni kutangaza tu uteuzi
baada ya Rais kuteua.
Gazeti hilo pia limeandika uwongo kuwa MSD haijawahi
kuongozwa na Mkurugenzi Mkuu asiye Mfamasia.
Tangu MSD ianzishwe mwaka 1993 hadi sasa, ni Mkurugenzi Mkuu mmoja tu,
Rino Meyers (1996-1999), ndiye alikuwa Mfamasia.
Wakurugenzi wengine kama Peter Mellon
(1993-1995), Jay Drosin (2001-2004) na Joseph Mgaya (2004-2013) hawakuwa
Wafamasia.
Kuhusu Kampuni ya CRJE kuhusishwa na Balozi Ombeni Y. Sefue
Suala la kumhusisha Katibu
Mkuu Kiongozi na kampuni hii nalo ni uzushi na uongo wa kupindukia. Wakati kampuni
hii ikipewa tenda ya kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma mwezi Oktoba 2007, Balozi Ombeni Y. Sefue hakuwa Katibu
Mkuu Kiongozi; alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani. Kadhalika mchakato
wa kumpata mkandarasi wa daraja la Kigamboni, ulipoanza mwezi Machi, 2011, Balozi Sefue hakuwa Katibu Mkuu
Kiongozi; alikuwa Balozi wa Tanzania, Umoja wa Mataifa, New York. Hata mkataba
wa ujenzi wa Daraja hilo uliposainiwa tarehe 9 Januari, 2012, Balozi Sefue
alikuwa na wiki moja tu ya kuwa Katibu Mkuu Kiongozi kufuatia kuteuliwa tarehe 30
Disemba, 2011. Aidha, Kampuni iliyoshinda tenda hiyo wala siyo CRJE
kama ilivyoandikwa na gazeti hilo bali ni China Major Bridges Engineering Company
(BCEC) kwa kushirikiana na Kampuni ya China Railway Construction
(CRCEG).
Kuhusu tuhuma kuwa Katibu Mkuu Kiongozi Chapuo Kampuni ya UGG:
Katibu Mkuu Kiongozi
hajawahi kuipigia chapuo kampuni yoyote ile pahala popote. Isitoshe, hakuna
kampuni yenye jina la “UGG” iliyowahi kuonesha nia ya kujenga reli ya kati. Hii
ni moja ya uthibitisho kwamba gazeti
hili linatoa taarifa za kuokoteza zisizo na ukweli kama vile walivyopotosha
kuhusu jina la Katibu Mkuu Kiongozi kwenye makala yao ya pili kwenye ukurasa wa
tisa wa gazeti hilo yenye kichwa cha habari “Magufuli anaishi na jipu Ikulu” ambapo walimpachika Katibu Mkuu
Kiongozi jina la Sifuni, jina ambalo hajawahi kuwa nalo. Balozi
Sefue hajahusika, hahusiki na wala hatahusika katika kuchagua wa kupewa
tenda hiyo kwa sababu yeye si sehemu ya wenye mamlaka ya kutoa tenda.
Kuhusu Eliachim Maswi:
Gazeti
la Dira ya Mtanzania limeandika kuwa moja ya “madudu” aliyofanya Balozi Sefue ni walichoita kumsafisha Bwana
Eliachim Maswi. Wanadai hivyo
wakati wamekiri kuwa alichofanya Balozi
Sefue ni kusoma matokeo ya uchunguzi, ambao hakuufanya yeye. Waliomsafisha Maswi ni Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Serikali; Sekretarieti ya Maadili ya Umma; na hatimaye kamati
ya uchunguzi iliyoongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu. Kwa hiyo, kwa maoni ya gazeti hili, Balozi Sefue asingepaswa kusoma matokeo
ya uchunguzi uliofanywa na vyombo hivyo huru.
Kwa maoni yao kusoma taarifa ya uchunguzi ni “madudu”.
Habari hizo hazina chembe
yoyote ya ukweli, na wao wenyewe ndani ya gazeti wamekiri hawana ushahidi, ni wazi kuwa habari hizo ni za kubuni na
zimetungwa.
Kwa sababu hiyo, Serikali
inalitaka Gazeti la Dira ya Mtanzania kukanusha uongo na uzushi wao na kumuomba
radhi Balozi Ombeni Sefue, kuiomba
radhi Serikali na kuwaomba radhi wote walioumizwa na uzushi huo kwa uzito ule
ule uliotumika kuchapisha taarifa hiyo.
Vinginevyo iwapo gazeti la
Dira ya Mtanzania lina ushahidi wa huo “uchafu” wa Katibu Mkuu Kiongozi, waupeleke
mara moja kwenye vyombo vinavyohusika ikiwamo Sekretarieti ya Maadili na
TAKUKURU. Vinginevyo,
hatua zikichukuliwa dhidi yao wasiseme Serikali inavibana vyombo vya habari.
Aidha
Serikali inashauri wenye vyombo vya habari, wachapishaji, wahariri na waandishi
wa habari wajikite kwenye weledi na ukweli, wafanye utafiti na kuandika mambo
waliyo na uhakika nayo, na kamwe wasikubali kutumiwa kuendeleza agenda za watu
wengine.
No comments:
Post a Comment