Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Saidi Mecki Sadiki akizungumza na wajumbe wa Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Dar es salaam kwenye kikao cha kwanza cha Bodi hiyo kwa mwaka 2016. Kulia ni Zungu Azzan na Kushoto ni Bw. Edward Otieno Kaimu Katibu Tawala wa mkoa huo.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Bw.Isaya Mngurumi akichangia jambo kuhusu uboreshaji wa miundombinu ya barabara katika Manispaa yake wakati wa Kikao cha kwanza cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Dar es salaam.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Sophia Mjema akichangia jambo wakati wa wakati wa Kikao cha kwanza cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Dar es salaam kwa mwaka 2016.
Baadhi ya Wabunge wa jiji Dar es salaam wakifuatilia kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Dar es salaam. Kutoka kulia ni Mhe. Bonnah Kalua - Mbunge wa Segerea, Mhe. Faustine Ndugulile - Mbunge wa Kigamboni, Mhe. Zungu Azzan – Mbunge wa Ilala na Mhe. Abdallah Mtolea – Mbunge wa Temeke.
Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Dar es salaam Muhandisi Julius Ndyamkama akitoa ufafanuzi kwa wajumbe wa kikao cha Bodi ya Barabara mkoa wa Dar es salaam kuhusu miradi ya ujenzi wa Barabara inayosimamiwa na Wakala hiyo.
Na Aron Msigwa – Dar es salaam
Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam
Saidi Mecki Sadiki amepiga marufuku utoaji wa vibali vya malori ya mizigo na
magari yenye uzito wa zaidi ya tani 10 kuingia katika barabara zote
zinazosimamiwa na Manispaa za jiji la Dar es salaam zilizojengwa kwa kiwango
cha lami kufuatia barabara hizo kuharibika kwa kipindi kifupi kutokana uzito
jambo linaloisababishia Serikali hasara.
Aidha, ameziagiza manispaa za
jiji hilo kuweka alama za barabarani zinaonyesha zuio kwa magari yote yenye
uzito wa zaidi ya tani 10 kupita kwenye barabara hizo ili wamiliki na madereva
watakaokiuka agizo hilo wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Akizungumza na wajumbe wa Bodi
ya Barabara ya Mkoa wa Dar es salaam kwenye kikao cha kwanza kwa mwaka 2016 Mhe.
Sadiki Meck Sadiki amesema kuwa Manispaa za jiji hilo zinatenga fedha nyingi za
kujenga barabara mpya na kufanya matengenezo ya zile zilizopo ambazo nyingi
zinaharibiwa na malori ya mizigo.
Amefafanua kuwa matumizi hayo
mabaya ya barabara kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na ukiukwaji wa sheria za
barabarani ambapo malori makubwa ya mizigo huegesha na kuziba maeneo ya waenda
kwa miguu jambo linalowanyima haki wananchi kutumia maeneo yaiyotengwa kwa
ajili yao.
Amesema baadhi ya magari yenye
uzito wa tani 40 hudiriki kupita kwenye barabara za huduma (Service road),
madaraja na wakati mwingine maeneo ya waenda kwa miguu jambo linalosababisha
uvunjaji wa kingo za barabara na milingoti ya taa za barabarani na kuongeza kuwa
vitendo hivyo vinaisababishia Serikali hasara kutokana na gharama ya
matengenezo.
“Kuanzia leo katika mkoa wangu ni
marufuku kutoa vibali vya magari yenye uzito wa zaidi ya tani 10 kuingia kwenye
barabara zetu, tunataka barabara zetu zidumu, hatuwezi kuvumilia vitendo vya
watu wachache wanaokiuka sheria za barabarani kuharibu barabara zetu, lazima
tuchukue hatua Manispaa zinajitahidi kujenga bararaba lakini hazidumu” Amesisitiza
Mhe. Sadiki.
Amesema barabara zinazosimamiwa
na Manispaa za Dar es salaam zina uwezo wa kuhimili uzito wa tani 10 na
kubainisha kuwa kwa kipindi kirefu malori ya tani 40 yamekuwa yakipita kwenye
barabara hizo na kuzifanya manispaa kunajenga barabara hizo kila mwaka.
Mhe. Sadiki amesema kuwa ipo
haja ya mamlaka zinazohusika na miundombinu ya barabara katika jjiji la Dar es
salaam kwa kuwatumia wataalam wa sheria kuanza kuangalia uwezekano wa wamiliki
wa vyombo vinavyosababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara kulipa gharama
za uharibifu huo.
Kuhusu ulinzi na Usalama
watumiaji wa barabara za jiji amelitaka Jeshi la Polisi kuendelea kuchukua
hatua na kufanya Operesheni dhidi ya madereva wa pikipiki (Bodaboda) na Bajaji
wanaopitisha vyombo vyao vya usafiri kwenye njia za waenda kwa miguu na
kusababisha usumbufu na ajali za mara kwa mara kwa wananchi wanaotumia njia
hizo.
Pia amezitaka Manispaa za jiji
hilo kushirikiana na Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Dar es salaam
kusimamia maeneo yote yanayotakiwa kujengwa miundombinu ya Barabara ili yasivamiwe
na wananchi pamoja na kuwachukulia hatua wananchi wanaofanya biashara katika maeneo
yasiyoruhusiwa ya hifadhi za barabara na njia za waenda kwa miguu.
‘‘Ninaiagiza manispaa ya
Kinondoni kuondoa wafanyabishara wote walioko eneo la kituo cha kuzalishia umeme
Ubungo, eneo lile ni hatari kwa usalama na maisha yao, kukaa pale ni kinyume
cha sheria’’ Amesisitiza.
Aidha, amesema mwaka 2016 mkoa
wa Dar es salaam umetenga jumla ya Shilingi bilioni 343.5 ikilinganishwa na
shilingi Biliobi 266.6 zilizotengwa mwaka mwaka 2015/2016 kutekeleza miradi ya
ujenzi na matengenezo ya barabara katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo lengo
likiwa kupunguza msongamano wa magari.
Kuhusu Kikao hicho cha kwanza
cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Dar es salaam kwa mwaka 2016 amesema pamoja
mambo mengine kimepokea na kujadili taarifa ya utekelezwaji wa ujenzi wa miradi
ya barabara kwa mwaka 2015/2016 pamoja na kupokea Mpango wa matengenezo ya
barabara kwa mwaka 2016/2017.
Ametoa wito kwa wakazi wa jiji
la Dar es salaam kuzingatia usafi wa mazingira kwa kulinda miundombinu ya
barabara na kuepuka kutupa taka kwenye
mifereji ya kupitisha maji ili
kuzuia mlipuko wa magonjwa ukiwemo ugonjwa wa Kipindupindu.
No comments:
Post a Comment