Kikosi cha Mbeya City FC kimewasili salama mkoani Morogoro tayari kwa kambi ya muda kujindaa na mchezo wa ligi kuu ya Soka Tanzania bara dhidi ya Simba Sports Club uliopangwa kuchezwa Jumapili hii kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na mbeyacityfc.com mapema leo asubuhi kocha msaidizi wa City, Mohamed Kijuso amesema kikosi kimewasili salama na leo watafanya mazoezi ya jioni kwenye uwanja wa chuo cha Jordan kilichopo mkoani hapa yatakayofatiwaa na program maalumu ambazo zitakuwaa zikiongozwa na Mwalimu Kinnah Phiri kabla ya kuivaa Simba Siku ya jumapili jijini Dar.
“Tutakuwa uwanjani jumapili dhidi ya Simba kwenye uwanja wa Taifa,hilo ndiyo jambo kubwa naweza kusema, tumesafiri na kufika hapa Morogoro hali za wachezaji wote 18 zikiwa salama, kwa hilo tunamshukuru Mungu,jioni ya leo tutafanya mazoezi hapo chuoni Jordan na kesho tutakuwa na program maalumu amabazo mwalimu ameziandaa” alisema.
Kuhusu Simba, Kocha huyo kijana ameweka wazi kuwa timu hiyo kutoka mtaa wa msimbazi ni nzuri hivyo hawataibeza hata kidogo licha ya matatizo kadhaa yaliyopo kwenye kambi yake kwa sasa, na kusema kikosi chake kitaingia uwanjani kupambana kwa nguvu zote kuhakikisha City inaibuka na ushindi.
“Nafahamu Simba wana matatizo madogo kwenye kambi yao hivi sasa,jambo hilo halitufanyi kuwabeza, bado ni timu nzuri na iko kwenye nafasi ya juu kwenye msimamo wa ligi tofauti na sisi, tutaingia uwanjani kupambana kwa nguvu zote kuhakikisha tunaibuka na ushindi ili tuweze kujiimarisha zaidi, hivi sasa tunahitaji matokeo kwenye kila mchezo jambo ambalo pekee litatutoa tulipo na kutupeleka sehemu nyingine alisema”.
Akiendelea zaidi Kijuso alisema kuwa, anafahamu Simba ina wachezaji wengi vijana na wenye kasi pia inatumia nguvu nyingi kumiliki mpira kwenye eneo la kiungo hivyo ni wazi City itatumia kikosi tofauti na kile kilichozoeleka huku mbinu za kuhakikisha wanaziba nafasi zote kwenye eneo la katikati ya uwanja zikiwa tayari zimeshafanyia kazi.
No comments:
Post a Comment