07/03/2016
BASATA YAWAPONGEZA WASANII LULU NA
RICH RICH KUSHINDA TUZO ZA AMVCA 2016
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kama msimamizi
na mratibu wa sekta ya Sanaa nchini linapenda kutoa pongezi za dhati kwa Wasanii
Singo Mtambalike (Rich Rich) na Elizabeth Michael (Lulu) kwa kushinda tuzo za
African Magic Viewers’ Choice Awards (AMVCA2016) zilizotolewa mwishoni mwa wiki
nchini Nigeria na kushuhudiwa na Dunia kupitia luninga na mitandao ya kijamii.
Katika tuzo hizo Msanii Singo Mtambalike ameshinda
tuzo ya Filamu Bora ya Lugha ya Asili (Best Local Language - Swahili) kupitia
filamu ya ‘Kitendawali’ huku Msanii Elizabeth Michael (Lulu) akishinda tuzo ya
Filamu Bora ya Afrika Mashariki (Best Movie -Eastern Africa) kupitia filamu
yake ya ‘Mapenzi’
Kuteuliwa na kushinda kwa Wasanii wa Tanzania
katika tuzo hizi zilizoshirikisha wasanii na filamu nyingi za Afrika ni ishara
kwamba wasanii wetu wanakubalika, kutambuliwa na kuthaminiwa ndani na nje ya
Tanzania.
Aidha, ushindi huu unazidi kulipa heshima na
kulitangaza taifa letu katika nyanja mbalimbali hivyo kuzidi kulifanya ling’ae
na kuwa kinara katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.
Baraza linatoa wito kwa wasanii na wadau wote
kuzidisha ubunifu, bidii na weledi katika kazi wanazozifanya ili wasanii wengi
zaidi waweze kuchomoza katika tuzo na majukwaa mbalimbali ya kimataifa kwa
lengo la kulitangaza taifa na kukuza soko la kazi zao kimataifa.
Ni matumaini ya Baraza kwamba wasanii wataendelea
kutambua umuhimu wa kufuata sheria, kanuni na taratibu za kutambuliwa na
Serikali.
Sanaa ni kazi, tuipende na
kuithamini
Godfrey Mngereza
KAIMU KATIBU MTENDAJI

No comments:
Post a Comment