Pages

Pages

Pages

Saturday 5 March 2016

AZAM VS YANGA HAKUNA MBABE, ZAFUNGANA 2-2 NA KUACHA KAZI KUBWA KUTABIRI BINGWA!

Wachezaji wa Yanga wakipiga jalamba kabla ya pambano

Na brotherdanny.com
BAO la John Bocco la kusawazisha kwa Azam FC katika dakika ya 72 dhidi ya Yanga leo hii limekifanya kitendawili cha nani bingwa msimu wa 2015/16 kuwa kigumu kuteguliwa.
Hali hiyo imezifanya timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2 na kuzidi kufukuzana kileleni zikiwa na pointi 47 kila moja, lakini Azam ikizidiwa na wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa, huku zote zikiwa zimeshuka dimbani mara 20.
Mtandao wa brotherdanny.com unaripoti bila shaka yoyote kwamba, kwa sasa ubingwa unaweza kutwaliwa na timu yoyote kati ya Yanga, Azam ama Simba, ambayo kuna kila dalili kwamba inaweza kuukalia usukani wa Ligi Kuu ya Vodacom kesho ikiwa itaifunga Mbeya City wakati timu hizo zitakapocheza kwenye Uwanja wa Taifa ambako ndiko mtanange wa Azam na Yanga umefanyika leo hii.
Mechi ya Azam na Yanga ilikuwa na ushindani mkubwa ndani na nje ya uwanja, ambapo kila timu ilikuwa inahitaji kushinda ili iweke mazingira bora ya kunyakua ubingwa huo.
Azam ndio walioanza mashambulizi kwa kasi kubwa na presha yao ikasababisha Juma Abdul atumbukize mpira kwenye lango lake la Yanga katika dakika ya 11 ya mchezo wakati akiwa katika harakati za kuokoa shuti la Kipre Tchetche na hivyo kuipa Azam bao la kuongoza.
Hata hivyo, Juma Abdul alisawazisha makosa yake kwa kuisawazishia Yanga bao dakika ya 29 baada ya Yanga kufanya mashambulizi mfululizo katika harakati za kusawazisha na kutafuta ushindi.
Awali Yanga walikuwa wapate bao katika dakika ya 19, lakini kipa Aishi Manula na Shomari Kapombe walifanya kazi ya ziada kuondosha hatari hiyo.
Katika dakika ya 35 Shomari Kapombe alifunga bao, lakini likakatiliwa na mwamuzi kwa maelezo kwamba mfungaji alikuwa amejenga kibanda kinyume na sheria za mazingira.
Dakika ya 41 Amissi Tambwe aliwainua vitini mashabiki wa Yanga baada ya kufunga bao la pili kwa timu yake, huku wachezaji wa Azam wakidhani alikuwa ameotea, kelele ambazo mwamuzi alizipuuza.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa timu zote ambazo zilikuwa zikishambilia kwa zamu, lakini walikuwa ni Azam ambao walifanikiwa kupata bao katika dakika ya 72 wakati Bocco alipomalizia kazi nzuri ya Kipre Tchetche.
Jitihada za Yanga kuimarisha safu yake ya ushambuliaji kwa kumtoa Tambwe katika dakika ya 82 na kumwingiza Pato Ngonyani hazikuweza kubadili matokeo.
Katika dakika ya 88 Simon Msuva alikosa bao baada ya shuti lake kupanguliwa na kipa Aishi Manula na kuwa kona tasa.
Yanga na Azam bado zina mechi moja mkononi hata kama itatokea Simba ikashinda kesho, hivyo kuufanya mchuano wa ubingwa kuwa mgumu zaidi.
Matokeo mengi ya mechi za Ligi Kuu leo hii ni kwamba, Kagera imeshindwa kuipiku Mgambo JKT kwenye msimamo baada ya timu hizo kufungana bao 1-1. Mgambo ina pointi 19 wakati Kagera imefikisha 18.
Prisons imechupa hadi nafasi ya sita na kuipiku Stand United baada ya kuifunga timu hiyo ya Shinyanga bao 1-0 jijini Mbeya na kufikisha pointi 32. Stand imeshuka hadi nafasi ya saba iliyokuwa inashikiliwa na Prisons.
Licha ya kushinda bao 1-0 dhidi ya Mwadui, JKT Ruvu bado inaendelea kuburuza mkia kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 15, wakati Mwadui imebaki katika nafasi yake ya tano kwa kuwa na pointi 32 ikiizidi Prisons mabao ya kufunga.
Kwa upande mwingine, Mtibwa Sugar imebaki nafasi ya nne licha ya ushindi wake wa mabao 3-0 dhidi ya Wagosi wa Kaya Coastal Union. Wakata miwa hao wamefikisha pointi 36, tisa nyuma ya Simba inayoshika nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 45.
African Sports inaweza kurudi daraja la kwanza, kwani imebanwa mbavu na Maji Maji jijini Tanga na kutoka sare tasa huku Toto African nayo ikipata matokeo kama hayo nyumbani dhidi ya Ndanda FC.

No comments:

Post a Comment