Na Daniel Mbega
MABINGWA wa
soka Tanzania Bara, Yanga, watapambana na mabingwa wa Rwanda, Armée Patriotique Rwandaise (APR), katika raundi ya
kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufuzu raundi ya awali kwa ushindi
wa jumla ya mabao 3-0 dhidi ya Cercle de Joachim ya Mauritius.
APR yenyewe
imefuzu hatua ya awali kwa ushindi wa jumla ya mabao 4-2 dhidi ya mabingwa wa
Swaziland, Mbabane Swallows. Mechi ya kwanza walifungwa ugenini bao 1-0, lakini
Jumamosi, Februari 27, 2016 wakaichabanga timu hiyo mabao 4-1 kwenye Uwanja wa
Amahoro jijini Kigali.
Mechi ya
kwanza baina ya APR na Yanga itachezwa mbele ya mashabiki 30,000 kwenye Uwanja
wa Amohoro Machi 12, 2016 na inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na
rekodi nzuri ya APR ya kufanya vizuri nyumbani.
Kwamba hiyo
inaweza kuwa tiketi ya Yanga kubaki ama kuondoka mashindanoni ni suala la
kusubiri kutokana na rekodi baina ya timu hizo mbili zenye uzoefu tofauti wa
mashindano ya ndani na kimataifa.
Takwimu
ambazo Fikra Pevu inazo zinaonyesha kwamba, hii itakuwa mara ya pili kwa timu
hizo kupambana katika mashindano ya Afrika, hususan Ligi ya Mabingwa, lakini
itakuwa mechi ya nane kuzikutanisha timu hizo katika mashindano yote.
Katika mechi
saba zilizopita, timu zote zimeshinda mara tatu kila moja na kutoka sare mara
moja.
Zilipokutana
kwa mara ya kwanza kabisa kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na
Kati jijini Dar es Salaam mwaka 1996, APR ilishinda kwa penalty 4-2 katika
hatua ya nusu fainali baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 katika muda wa kawaida.
Wiki mbili
baadaye timu hizo zikapambana kwenye raundi ya awali ya Klabu Bingwa Afrika,
ambapo mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam Yanga ilishinda kwa bao 1-0, lakini
ziliporudiana mjini Kigali, APR ikashinda kwa mabao 3-0 na kusonga mbele.
Raundi ya kwanza ilikoing’oa AS Bantous ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa
jumla ya mabao 2-1 kabla ya kutolewa na Petro Atletico ya Angola kwa jumla ya
mabao 3-2.
Tangu wakati
huo timu hizo hazikubahatika kukutana tena hadi mwaka 2007 wakati wa mashindano
ya Kombe la Kagame mjini Kigali ambapo zilipangwa Kundi A.
Katika mechi
yao ya Januari 10, 2007, Yanga ilikubali kipigo cha bao 1-0 lililofungwa na
Mwemere Ngiricodu katika dakika ya 10 ya mchezo.
Aidha, Julai
13, 2008 timu hizo zilikutana tena kwenye Kundi C la michuano ya Kombe la
Kagame jijini Dar es Salaam ambapo safari hii zilitoka sare ya 2-2 huku mabao
ya Yanga yakifungwa na Mrisho Ngassa (65) na Jerry Tegete (68) wakati ya APR
yote yalifungwa na mlinzi Mbuyu Twite dakika za 15 na 77.
Mbuyu Twiye,
raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, hivi sasa ndiye beki tegemeo wa Yanga
baada ya kujiunga na timu hiyo msimu wa 2010/2011.
Mwaka 2012
APR na Yanga zikapambana tena kwenye Kombe la Kagame, zikiwa Kundi C mjini Dar
es Salaam, na safari hii Yanga ikashinda kwa mabao 2-0.
Timu hizo
zilifanikiwa kufuzu hadi nusu fainali ambapo zilikutana tena uso kwa uso na kwa
mara nyingine, Yanga ikashinda kwa bao 1-0 na kusonga mbele hadi kutwaa ubingwa
wake wa tano wa Kagame.
Uzoefu
Ukizungumzia
uzoefu na ukongwe, Yanga ndiyo kongwe zaidi na yenye mafanikio makubwa kwa ligi
ya ndani na mashindano ya kimataifa kulinganisha na APR, ingawa mpira
hauangalii umri.
Yanga
iliyoanzishwa mwaka 1935 imetwaa ubingwa wa Tanzania mara 20 na ndiyo
inayoongoza kwa kutwaa ubingwa huo mara nyingi zaidi kuliko klabu yoyote nchini
Tanzania.
Lakini pia
imetwaa Kombe la Nyerere (ndilo lililotumika kupata mwakilishi wa Kombe la CAF)
mara nne.
Katika
mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), vijana
hao wa Jangwani wametwaa mara tano katika miaka ya 1975, 1993, 1999, 2011 na
2012, na mara tatu imeishia fainali katika miaka ya 1976, 1986 na 1992.
Hii ni mara
ya 21 kuwania ubingwa wa klabu barani Afrika – mara 11 ilishiriki wakati
mashindano hayo yakiitwa Klabu Bingwa Afrika (kati yam waka 1969 na 1996) na
mara 10 tangu mashindano hayo yalipobadilishwa na kuitwa Ligi ya Mabingwa
Afrika kati yam waka 1997 na sasa.
Katika miaka
yote hiyo, hatua ya juu kabisa ambayo Yanga imefikia ni robo fainali mara tatu
katika miaka ya 1969, 1970 na 1998, mwaka ambao ilikuwa klabu ya kwanza ya
Tanzania kucheza hatua ya makundi kabla ya Simba kuifikia hatua hiyo mwaka
2003.
Ilishiriki
mara mbili Kombe la Washindi Afrika na hatua ya juu kabisa ilikuwa robo fainali
mwaka 1995 ambapo uzembe ulisababisha itolewe na Blackpool ya Zimbabwe kwa
kufungwa nyumbani mabao 2-0 licha ya kutoka sare ya 2-2 ugenini.
Aidha,
ilishiriki mara mbili Kombe la CAF na safari zote iliishia raundi ya kwanza.
Baada ya
Kombe la CAF kuunganishwa na Kombe la Washindi na kuitwa Kombe la Shirikisho ,
Yanga imeshiriki mara tatu na ikaishia hatua ya kati (Intermediate Round) mwaka
2007 ambapo kama ingeshinda ingeweza kushiriki hatua ya makundi (Robo Fainali)
ya Kombe la Shirikisho baada ya kuwa imetolewa kwenye raundi ya pili ya Ligi ya
Mabingwa ikiwa katika harakati za kutaka kucheza hatua ya makundi kwa mara ya
pili.
Kwa upande
wake, APR, timu ya Jeshi la Rwanda iliyoanzishwa mwaka 1993 (ina umri wa miaka
33 tu dhidi ya 81 ya Yanga) lakini imeweza kuzifunika timu kongwe kama Mukura
Victory Sports iliyoanzishwa mwaka 1963, Kiyovu na Rayon katika mashindano ya
ndani.
Maafande hao
wametwaa ubingwa wa Rwanda mara 14 tangu mwaka 1995, halafu imetwaa Kombe la
Rwanda mara 8.
Katika
mashindano ya Kombe la Kagame, imetwaa ubingwa mara tatu katika miaka ya 2004,
2007 na 2010.
Kwa upande
wa mashindano ya klabu za Afrika, APR inashiriki mara ya 13 na hatua ya juu
Zaidi iliyowahi kuifikia ni raundi ya tatu mwaka 2004 kabla ya kutolewa na
Enugu Rangers ya Nigeria kwa jumla ya mabao 3-1.
Mwaka 2003
ilifika nusu fainali ya Kombe la Washindi ambako ilitolewa na Julius Berger ya
Nigeria kwa jumla ya mabao 3-2. Ilifungwa 3-0 ugenini, lakini ushindi wake wa
mabao 2-0 nyumbani haukuweza kuivusha mbele ya Wanigeria hao ambao nao walishindwa
kutwaa ubingwa mbele ya Etoile du Sahel ya Tunisia iliyoshinda kwa jumla ya
mabao 3-2.
Katika
raundi ya kwanza, APR ilianza kuisambaratisha US Kenya ya Lubumbashi, Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Congo kwa jumla ya mabao 9-2, katika raundi ya pili ikaitoa
Etoile du Congo ya Brazzaville kwa jumla ya mabao 5-1 na kwenye robo fainali
ikaiondoa timu kongwe barani Afrika, Asante Kotoko ya Ghana, kwa faida ya bao
la ugenini. Ilifungwa 2-1 ugenini, halafu ikashinda bao 1-0 nyumbani.
APR imeishia
raundi ya kwanza mar azote mbili ilizoshiriki Kombe la CAF, na katika Kombe la
Shirikisho iliishia raundi ya kati (intermediate) mwaka 2004.
Mabenchi ya
ufundi
Linapikua
suala la benchi la ufundi, APR imekuwa na rekodi ya kusikitisha ya kuondokewa
na makocha, ambapo mwaka jana pekee iliondokewa na makocha wawili mfululizo,
huku mmoja wao akiondoka bila kuaga.
Kwanza
Ljubomir Ljupko Petrovic raia wa Bosnia aliondoka baada ya kukaa kwa miezi sita
tu na nafasi yake ikachukuliwa na raia mwenzake wa Bosnia Dusan Dule Suljagic,
ambaye licha ya kuisaidia kutwaa ubingwa, lakini aliondoka bila kuaga.
Lakini tangu
aliyekuwa kocha msaidizi wakati huo, Emmanuel Rubona, alipochukua mikoba mwezi
Septemba 2015 akisaidiwa na kipa mkongwe Jean Claude Ndoli, ameweza kuiongoza
timu hiyo hadi hatua hii iliyofikia.
Timu hiyo
inawategemea Zaidi wachezaji kama kipa Olivier Kwizera, walinzi Michael
Rusheshangoga, Albert Ngabo, Emery Bayisenge, Ismael Nshutinamagara na viungo
Migi Mugiraneza, Yannick, Hegman Ngomirakiza, Jean-Claude Iranzi na wengineo.
Kwa upande
wa Yanga, bado inanolewa na Mholanzi Hans van der Pluijm (67) anayesaidiwa na
Juma Mwambusi na Juma Pondamali.
Kikosi chake
kiko vizuri hata kwenye ligi kikiundwa na wachezaji kama makipa Deogratius
Munishi "Dida" na Ally Mustafa, walinzi Oscar Joshua Nkulula, Kelvin
Yondani, Mbuyu Twite, Vincent Bossou, Juma Abdul, nahodha Nadir Haroub, Salum
Telela, Simon Msuva, Issoufou Boubacar Garba, Haruna Niyonzima, Thabani
Kamusoko, Donald Ngoma, Amissi Tambwe, SHaji Mwinyi, Malimi Busungu, Deus Kaseke,
Paul Nonga na wengineo.
Kwa ujumla, mechi baina ya timu hizi ni
ngumu kutabiri, ingawa Yanga wanatakiwa kuwa makini Zaidi na APR ambayo huwa
haichagui uwanja wa kushinda. Ni kijeshijeshi tu!
No comments:
Post a Comment