Viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Na Daniel
Mbega
GUBU la
mawifi na kejeli ni mambo ya kawaida yanayompata mwanamke kutoka kwa ndugu wa
mumewe na jamii yetu kamwe haiwezi kuyakanusha.
Tumeshuhudia
mara nyingi ndani ya jamii pindi ndugu wa kiume anapoamua kuoa, hasa mwanamke
anapokuwa siyo chaguo la wanandugu – wazazi ama dada zake – kwamba mkamwana
huyo hupata shida sana kuelewana na ndugu wa mumewe.
Kama
hakuambiwa mvivu, basi ataambiwa mchoyo; na kama hakuambiwa ana maringo, ndugu
wa mume watamtoa kasoro yoyote kwamba ama ni mbaya, havutii na kadhalika,
ilimradi tu hawakosi cha kuongea.
Wanawake
wengi wanapoolewa hujiandaa kwa mazingira hayo, wakati mwingine hata waume zao
huwatahadharisha kuhusu tabia za ndugu zao.
Hata
hivyo, maandalizi hayo huwa hayasaidii kwa sababu kila siku ndugu wanaibuka na
mazengwe mapya, hawakosi cha kuongea na ukarimu wa mke huwa si kitu kwao.
Kinachofanywa
na wabunge wa upinzani – ambacho kimekuwa kikifanywa kwa muda mrefu sasa –
hakina tofauti na visa vya ndugu wa mume kwa mke wa ndugu yao.
Huko nyuma
hasa katika Bunge la 10 (maana ndipo mchezo huo ulipoanza) tulishuhudia jinsi
wawakilishi hao wa wananchi waliopewa dhamana kubwa ya kuwakilisha changamoto
za jamii husika walivyoanza na mchezo wa ‘kususa’ vikao kila walipozidiwa kwa
hoja. Wakazusha visa kama vya mwana wa kufikia kususa chakula kila mara
kinapowekwa mezani mpaka ‘baba arudi’ hata kama hakuna sababu.
Lakini
kila waliposusia vikao, kamwe hawakususa kwenda benki kuangalia kama mishahara
yao imeingia ama la! Walikomba kama kawaida huku akiendelea kukaa nje ya Bunge
na kuwanyima haki waajiri wao ambao ni wananchi.
Tunafahamu
wapinzani kazi yao kubwa ni kuisimamia serikali itekeleze majukumu yake
ipasavyo, lakini kususa kwao wala hakukuweza kuizuia serikali isiendelee na
majukumu yake – Bunge kwa maana hiyo likawa linaendelea na vikao kama kawaida
ilimradi tu akidi inatimia.
Wanasiasa
wetu wa upinzani wamekuwa na tabia mbaya ya ‘kujipiga wenyewe na kulia’ halafu
wanatoka nje wakitaka wahurumiwe na wananchi, wakati hakuna sababu yoyote kwao
kumwaga machozi.
Wengi
tulidhani tabia ile imeachwa hasa baada ya serikali ya sasa chini ya Dk. John
Magufuli kutekeleza kwa vitendo majukumu yake huku ikiwabana na kuwawajibisha
watendaji wazembe na kunyoosha mambo ambayo yamekuwa hayaendi sawa kwa muda
mrefu.
Kama
walivyo ndugu wa mume wasiokosa sababu, wapinzani hao walianza kwa kubeza,
kukejeli na kupinga uamuzi mbalimbali wa serikali tena katika mambo ambayo ni
ya msingi kabisa ambayo hata wenyewe walikuwa wakiyanadi kwa wananchi kwamba
wangeyatekeleza wakiingia madarakani.
Sasa kabla
ya Mkutano wa Pili wa Bunge la 11 haujaanza mjini Dodoma wiki hii, tumeshuhudia
walivyozua sababu nyingine na kususia uchaguzi wa wenyeviti wa Kamati za Kudumu
za Bunge kwa maelezo kwamba nao walitaka washirikishwe kwenye uteuzi wa wajumbe
wa kamati hizo.
Kambi ya
upinzani ikalalama kwamba Chama cha Mapinduzi (CCM) kilikuwa kinawapangia watu
wa kuongoza kamati zinazosimamia mapato ya serikali ambazo kikanuni zipo chini
ya wapinzani wenyewe hasa Kamati ya Hesabu za Serikali za (PAC) na ile ya
Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).
“Tumegundua
kwamba orodha ya majina yaliyotoka yana matatizo mengi na matatizo hayapo
kwenye kamati ya PAC na LAAC tu, kwenye kamati nyingi kuna matatizo kwa hiyo
kwa sasa viongozi wa kambi wanakutana kujadili na kuchambua taarifa iliyotolewa
baadaye tutakutana na wabunge wote kisha kesho tutatoa msimamo wetu,” alisema
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John
Mnyika Januari 21, 2016.
Kwa maana
nyingine, licha ya kamati hizo mbili kuundwa na wajumbe mbalimbali wakiwemo wa
upinzani, lakini bado wapinzani hawataki kwa madai kwamba wajumbe hao – ingawa
ni miongoni mwao wenyewe – ni ‘chaguo la CCM’.
Hili
linatia mashaka na kuzusha maswali mengi, kwa sababu wajumbe wa kamati hizo,
ambao kwa mujibu wa kanuni miongoni mwao ndimo wanamotoka wenyeviti, ni wabunge
wa upinzani, sasa kama leo hii hawawaamini kuingia kwenye kamati hizo, tuhoji
basi ni kwanini hata wakawateua kuwania ubunge kupitia vyama vyao kama walikuwa
hawastahili?
Kanuni za
Kudumu za Bunge Toleo la Aprili 2013,
inasema: “Wenyeviti wa Kamati za Bunge zinazosimamia matumizi ya fedha za Umma
ambazo ni Kamati ya Hesabu za Serikali, Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa,
watachaguliwa kutoka miongoni mwa wajumbe wa kamati hizo ambao wanatoka katika
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.”
Wapinzani
ambao wamo katika Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) yenye wajumbe 23 ni Mbunge
waSame Mashariki, Naghejwa Kaboyoka (Chadema), Mbunge wa Viti Maalumu, Rais
Abdallah Mussa (CUF), Mbunge wa Tanga Mjini, Mussa Mbarouk (CUF), Mbunge wa
Viti Maalumu, Yosefa Komba (Chadema), Mbunge wa Viti Maalumu, Tunza Issa Malapo
(Chadema) na Mbunge wa Mwanakwerekwe, Ali Salim Khamis (CUF).
Kwenye
Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) yenye wajumbe 22, wapinzani ni
Mbunge wa Mgogoni, Dk. Suleiman Ally Yusuf (CUF), Mbunge wa Viti Maalumu, Rose
Kamili (Chadema), Mbunge wa Viti Maalumu, Conchesta Rwamlaza (Chadema), Mbunge
wa Kilwa Kaskazini, Vedasto Ngombale (CUF), Mbunge wa Viti Maalumu, Grace
Kiwelu (Chadema) na Mbunge wa Ukerewe, Joseph Mkundi (Chadema).
Kwangu
mimi naamini kwamba, wabunge hawa – wa majimbo na viti maalum – wanafaa ndiyo
maana hata wananchi wamewachagua wawawakilishe, lakini kinachoendelezwa na viongozi
wa upinzani ni hoja zisizo na mashiko ambazo dhahiri zinaonyesha kwamba
walitaka ama walitaka wenyewe wawe kwenye kamati hizo au walitaka maswahiba wao
ndio wateuliwe.
Ninaamini
kwamba, wabunge wote ni sawa, wana haki sawa na hakuna mbunge aliye bora kuliko
mwingine.
Hapa pia
naungana na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) Zitto Zuberi Kabwe,
aliyesema kupitia ukurasa wake wa facebook, namnukuu; "Kamati zote za
Bunge zina hadhi sawa ndani ya Bunge. Kila mbunge ana haki ya kuwa kwenye
kamati yeyote ile na hakuna mbunge bora zaidi ya mwingine. Kanuni zimeweka
utaratibu wa uteuzi kwenye Kamati ikiwemo maombi ya mbunge, uzoefu na ujuzi wa
eneo husika.”
"Wanaolalamika
leo upangaji wa Kamati ndio usiku wa kuamkia jana walimshinikiza Spika
asiwapange mahasimu wao kisiasa kwenye Kamati wanazoona wao ni nyeti. Ni
unafiki uliopitiliza unapojenga hoja ya uzoefu, chaguo la Mbunge na ujuzi
wakati huo huo wenye vigezo vyote hivyo unawapiga vita kwa sababu za kisiasa.
"Ni
dhahiri kuwa mpangilio wa Kamati unajenga Bunge kibogoyo, Nilitahadharisha toka Bunge la 11 lilipoanza
kwamba, "kuna dalili za Serikali kutaka kulidhibiti Bunge ( kumbukeni
sarakasi za Tulia Ackson ambaye sasa ni Naibu Spika) ."
"Kiongozi
unapokwenda kwa Spika kusema 'fulani asipangwe Kamati fulani kwa sababu atapata
sifa' halafu ukataka 'nyumbu' wako ndio wapangwe huko ujue unaisadia Serikali
kudogosha Bunge. Spika anapoamua Nyote, huyo usiyemtaka na nyumbu wako wasiende
huko ujue amekudharau sana.
"Unapoona
Viongozi wa Serikali wanahangaika kupanga Kamati za Bunge watakavyo wao ujue
viongozi hao ni dhaifu, hawana nia njema na hawataki kuwajibishwa.
"Twendeni
kwenye hizi hizi Kamati tulizopangiwa kuwafanyia kazi Watanzania. Twendeni
tukaonyeshe kuwa Bunge litabaki Bunge tu na Wabunge tusikubali Bunge Kibogoyo.
Ni lazima Bunge lidhibiti Serikali hata Serikali hiyo ikiwa inaongozwa na
Malaika. Serikali ni chombo cha mabavu lazima idhibitiwe, na ndio kazi ya Bunge
kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 63."
Maneno
haya ya Zitto Kabwe yana changamoto kubwa kwa serikali, Bunge na wabunge wa
upinzani na hapa tunajifunza jambo jingine kwamba, kumbe siku moja kabla ya
kususia vikao, wapo viongozi wa upinzani waliojipenyeza hadi kwa Spika ili
kutaka ‘watu wao’ waingie kwenye kamati fulani na kuwazibia baadhi ya wabunge
eti watapata sifa wakipangwa huko.
Sasa Spika
akaamua ‘wote maziganyande’ – wamekosa wote – ndugu zangu wapinzani
wanaendeleza visa vya ndugu wa mume na kulalamika bila mpangilio.
Nawaomba
waheshimiwa wabunge wote wawe kitu kimoja, wajenge taifa hili si kwa kukomoana,
kukamiana au kuchukiana. Wote wanajenga nyumba moja hivyo hawana sababu ya
kugombea fito.
Kamati
hizi zinapaswa kuwajibika kwa kasi ile ile ya Serikali ya sasa, zijadili mambo
ya msingi yenye kuleta maendeleo kwa taifa na siyo ubabaishaji.
Suala la
kususa vikao kamwe halitaweza kuwafanya wabunge hawa wa upinzani wakaonekana ni
watetezi wa wananchi wao, zaidi vitendo hivyo vinawadhalilisha kwa sababu si
vya kiungwana.
No comments:
Post a Comment