Pages

Pages

Pages

Sunday 13 December 2015

MWANAMFALME WA SAUDIA AMSHUTUMU TRUMP KUZUIA WAISLAMU MAREKANI

Bin Talal amesema Donald Trump hawezi kushinda urais Marekani

Mwanamfalme Alwaleed bin Talal wa Saudi Arabia amemshutumu mgombea urais wa chama cha Republican Marekani Donald Trump kwa tamko lake kwamba Waislamu wazuiwe kuingia Marekani.
Mwanamfalme huyo, ambaye ndiye mtu tajiri zaidi katika ulimwengu wa Kiarabu, amesema Bw trumo anafaa kuacha azma yake ya kutaka kuwa rais kwa sababu hawezi kushinda.

"Unaletea aibu chama cha Republican na Marekani kwa jumla," ameandika Bin Talal kwenye Twitter.
Bw Trump, mfanyabiashara tajiri kutoka New York, alikuwa amependekeza Waislamu wazuiwe
Hii ni baada ya wanandoa wawili Waislamu kufyatua risasi na kuwaua watu 14 mjini San Bernardino, jimbo la California.
Amejibu matamshi hayo ya Bw Talal kwa kumuita mwanamfalme ”mjinga” na kumtuhumu kwa kutaka kufanya anachosema ni kutumia “pesa za baba” kudhibiti wanasiasa wa Marekani.
 
Trump amesisitiza kwamba hataacha kuwania urais Marekani
"Hutaweza kufanya hivyo nikichaguliwa," amemjibu Trump kupitia Twitter.
BBC

Zilizotangulia:

US: Maneno ya Trump ni hatari kwa usalama

9 Desemba, 2015

 Wizara ya ulinzi ya Marekani imesema matamshi ya Donald Trump kwamba Waislamu wanafaa kuzuiwa kuingia Marekani ni hatari kwa usalama.

Pentagon imesema matamshi hayo yatasaidia kundi linalojiita Islamic State (IS).
Trump, ambaye anaongoza katika kinyang’anyiro cha kumteua mgombea urais Marekani kwa tiketi ya chama cha Republican, alitoa matamshi hayo baada ya watu 14 kuuawa kwa kupigwa risasi mjini San Bernardino, California.
Afisa wa mawasiliano wa Pentagon Peter Cook amesema matamshi kama hayo yanaendeleza "mtazamo wa Isil”, akirejelea IS.
Pentagon alisema kufungia nje Waislamu kutaathiri sana juhudi za Marekani za kukabiliana na ueneaji wa itikadi kali.
Bila kumtaja Bw Trumo, Bw Cook alisema: “Jambo lolote linaloendeleza mtazamo wa Isil na kuifanya Marekani ionekana kana kwamba inapambana na dini ya Kiislamu ni kinyume na maadili yetu na ni hatari kwa usalama wa taifa.”
Bw Trump ameshutumiwa sana na viongozi mbalimbali duniani tangu atoe matamshi hayo.
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani John Kerry alijiunga na viongozi hao baadaye Jumanne na kusema maneno ya Trump hayasaidii kwa vyovyote katika vita dhidi ya IS.
Wapiganaji wa kundi hilo wamekuwa wakishambuliwa na majeshi ya muungano unaoongozwa na Marekani nchini Syria na Iraq.


Mambo 20 makuu anayoamini Donald Trump

 8 Desemba, 2015

Donald Trump anaongoza katika kinyang’anyiro cha kumtafuta mgombea urais atakayewakilisha chama cha Republican katika uchaguzi mkuu mwaka ujao. Wajua sera zake na mambo anayoyaamini?
1. Waarabu-Wamarekani jimbo la New Jersey walishangilia shambulio la Septemba 11, 2001 liliotekelezwa. Hakuna habari za kuthibitisha haya.
2. Kunafaa kuwa na mfumo wa kufuatilia misikiti Marekani kama njia ya kukabiliana na ugaidi.
3. Marekani inafaa kutumia njia kali za kuhoji washukiwa katika vita dhidi ya Islamic State.
4. Trump amesema akiwa rais anaweza kuwaangamiza Islamic State kwa mabomu na pia kuwazuia kupata mafuta.
5. Kuundwe mfumo rahisi wa ulipaji ushuru, watu wanaolipwa chini ya $25,000 (£16,524) wasiwe wakilipa ushuru wa mapato.
6. Watu wenye hazina za uwekezaji ng’ambo hawalipi ushuru wa kutosha. Lakini baadaye alibadilika na kusema watapunguziwa ushuru sawa na watu wa pato la wastani.
7. Anataka kujenga ukuta mpaka wa Marekani na Mexico kuzuia wahamiaji kutoka Mexico.
8. Anataka kuwafurusha wahamiaji wote 11 milioni ambao waliingia Marekani kwa njia haramu.
9. Yeye na Vladmir Putin wanaweza “kusikizana vyema”.
10. Ili kuzuia visa vya watu kupigwa risasi Marekani, nchi hiyo inafaa kuwekeza katika afya ya akili.
11. Uchina inafaa kuchukuliwa hatua kali katika masuala kadha ili kuhakikisha usawa wa kibiashara kati yake na Marekani.
12. Kundi la The Black Lives Matter ambalo hutetea haki za watu Weusi Marekani ni hatari.
13. Takwimu za sasa za Marekani ni za kupotosha. Anasema ukosefu wa ajira umefikia 20% kinyume na takwimu rasmi zinazoonyesha ni 5.1%.
14. Utajiri wake ni $10bn.
15. Mfumo wa kutoa huduma za afya kwa wanajeshi wa zamani unafaa kufanyiwa mabadiliko makubwa.
16. Mpango wa Obamacare ambao ulilenga kuongeza idadi ya Wamarekani wanaopata bima ya afya ni “mkasa”.
17. Mabadiliko ya tabia nchi ni hali ya kawaida tu ya hewa.
18. Ulimwengu ungekuwa pahala pema pa kuishi kama Saddam Hussein na Muammar Gaddhafi wangekuwa bado madalakani.
19. Angewarejesha makwao wahamiaji kutoka Syria wanaotafuta hifadhi Marekani.
harusi ya wapenzi wa jinsia moja, hakufaa kazi hiyo.
20. Yeye ni “mtu mzuri sana” na anataka sana kurejesha hadhi ya Marekani.


Trump akemewa kwa matamshi kuhusu Waislamu

 8 Desemba, 2015

Vigogo wa chama cha Republican nchini Marekani wamemkemea mwenzao Donald Trump, anayetaka kuwania urais kupitia chama hicho, kwa kupendekeza Waislamu wazuiwe kuingia Marekani.
Mmoja wa wanaoshindani tiketi ya kuwania urais Jeb Bush amesema Bw Trump "mwenye kasoro akilini”. Makamu wa rais wa zamani Dick Cheney naye alisema pendekezo hilo "linaenda kinyume na yote ambayo huwa tunatetea”.
Ikulu ya White House, Umoja wa Mataifa na viongozi wa Kiislamu pia wamekosoa matamshi hayo ya Trump.
Bw Trump alikuwa amesema Waislamu wengi wana "chuki” dhidi ya Marekani.
Kwenye hotuba wakati wa kampeni, aliomba "Waislamu wote wazuiwe kuingia Marekani hadi wawakilishi wa nchi wajue ni nini kinachoendelea”
Meneja wake wa kampeni alisema marfuku hiyo ingeathiri "kila mmoja” bila kubagua kama ni mhamiaji au mtalii.
Lakini Bw Trump aliambia Fox News kwamba haingeathiri “watu wanaoishi humu nchini (Marekani), akiongeza kuwa Waislamu wanaohudumu katika jeshi la Marekani wangekaribishwa "nyumbani”.
Matamshi hayo ya Bw Trump yalitolewa Marekani ikiendelea kuomboleza kufuatia shambulio mbaya zaidi la kigaidi kutekelezwa tangu shambulio la Septemba 11, 2001.
Wiki iliyopita, wanandoa wawili Waislamu, ambao wanaaminika kukumbatia itikadi kali, walifyatua risasi na kuwaua watu 14 na kuwajeruhi wengine 21 katika kituo cha afya San Bernardino, jimbo la California.
Bw Trump alishangiliwa sana aliporudia ahadi yake katika mkutano wa kampeni jimbo la South Carolina saa chache baada ya kutoa matamshi hayo mara ya kwanza.


Trump ashutumiwa kwa kupanga kufurusha wahamiaji

 11 Novemba, 2015

Donald Trump, mmoja wa wanaowania kupeperusha benderea ya chama cha Republican uchaguzini Marekani, ameshutumiwa vikali kutokana na mpango wake wa kuwafurusha wahamiaji 11 milioni kutoka Marekani.
Kwenye mdahalo wa moja kwa moja kupitia runinga, wawaniaji wawili wanaoshindana naye, John Kasich na Jeb Bush, walikosoa vikali mpango huo wakisema hauwezi kutekelezeka.
Aidha, wamesema ni wa ubaguzi na wenye nia ya kuzua mgawanyiko kwenye jamii.
Bw Trump, ambaye ni bilionea kutoka New York, alizomewa alipojaribu kujitetea.
Wagombea wanane wanaoongoza kwenye chama hicho walikabiliana Milwaukee kwa mara ya nne.
Bw Trump alikariri mpango wake wa kujenga ua katika mpaka wa Marekani na Mezico kuzuia wahamiaji kuingia Marekani na pia kuhakikisha wahamiaji walioingia Marekani kinyume cha sheria wanafurushwa na kurejeshwa Mexico.
Lakini alikosolewa vikali na Bw Kasich, ambaye ni gavana wa Ohio.
"Tuseme ukweli, sote tunajua huwezi ukawashukua na kuwarejesha kwao vivi hivi tu. Hilo ni wazo la kijinga. Si wazo komavu.”
Bw Bush, aliyekuwa gavana wa Florida, pia alishutumu mpango huo akisema utatenganisha familia.
Lakini Trump alitetea msimamo wake na kusema wahamiaji hao wanadhuru uchumi wa Marekani.
Daktari wa upasuaji Ben Carson amekuwa akimfuata kwa karibu Donald Trump kwenye kinyang’anyiro hicho kwa mujibu wa kura za maoni.

No comments:

Post a Comment