Pages

Pages

Pages

Friday 11 December 2015

MAGUFULI KAWAPA UWAZIRI WAPINZANI WAKE!


 Dk. Hamisi Kigwangalla
 Balozi Augustino Mahiga
 Profesa Sospeter Muhongo

 Dk. Harrison Mwakyembe
 Komredi Mwigulu Nchemba

January Makamba


Na Daniel Mbega

RAIS Dk. John Magufuli amewapa uwaziri makada 6 kati ya 37 ambao walishindana naye mpaka hatua ya mwisho kuwania uteuzi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Ndani ya makada hao sita, pia wamo wawili kati ya nane ambao walikuwamo kwenye Kamati ya Kampeni ya CCM iliyoundwa na wajumbe 32.
Waliokumbukwa na Dk. Magufuli kwa utendaji wao makini ni Profesa Sospeter Muhongo, Balozi Augustino Mahiga, Dk. Harrison Mwakyembe, Mwigulu Nchemba, January Makamba na Dk. Hamisi Kigwangalla.
Mwigulu na Dk. Mwakyembe walikuwemo kwenye Kamati ya Kampeni iliyoundwa Agosti 17, 2015 ikiwahusisha makada wengine sita ambao pia waliwania kuteuliwa kugombea urais.
Makada hao ni Dk. Asha-Rose Migiro, Bernard Membe, Samuel Sitta, Makongoro Nyerere, Steven Wasira na Lazaro Nyalandu. Hata hivyo, Migiro, Membe, Sitta na Makongoro hawakugombea ubunge safari hii, lakini Wasira alibwagwa vibaya na Ester Bulaya wa Chadema katika Jimbo la Bunda Mjini, wakati ambapo Nyalandu, licha ya kushinda ubunge Singida Kaskazini, ameshindwa kurejeshwa kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii, ambayo bado haijapata waziri kamili.
Wajumbe wengine wawili wa kamati hiyo – Nape Nnauye na Ummy Mwalimu – nao wamekumbukwa kwenye uwaziri.
Wajumbe wengine kwenye kamati hiyo walikuwa Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana (ambaye ndiye alikuwa Mwenyekiti), Rajab Luhwavi (Makamu Mwenyekiti – Bara), Vuai Ali Vuai (Makamu Mwenyekiti - Z’bar), Sophia Simba, Mohamed Seif Khatib, Amina Makillagi, Christopher Ole Sendeka, Abdallah Majura Bulembo, Hadija Aboud, Mohamed Aboud, Issa Haji Ussi, Waride Bakari Jabu, Mahmoud Thabit Kombo, Shamsi Vuai Nahodha, Dk. Maua Daftari, Stephen Masele, Pindi Chana, Shaka Shaka, Sadifa Juma Khamis, Antony Diallo na Livingston Lusinde.
Wajumbe watatu katika kundi hilo - Shamsi Vuai Nahodha (Kijitoupele), Livingstone Lusinde (Mtera) na Stephen Masele (Shinyanga Mjini) – wamerejea bungeni, lakini Masele na Nahodha ‘hawakukumbukwa’ licha ya kuwemo kwenye baraza lililopita.
Profesa Sospeter Muhongo amerejeshwa kwenye Wizara ya Nishati na Madini ambako Januari 24, 2015 alijiuzulu kufuatia kashfa ya uchotaji wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow, lakini Balozi Augustino Mahiga amekabidhiwa Wizara ya Mambo ya Nje, EAC na Ushirikiano wa Kimataifa.
Dk. Mwakyembe amerejea lakini akikabidhiwa Wizara ya Katiba na Sheria, wakati Mwigulu Nchemba amekuwa waziri kamili na kukabidhiwa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Katika baraza lililopita alikuwa naibu waziri wa Fedha akishughulikia uchumi.
January Makamba amepandishwa na sasa ni Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira wakati Dk. Kigwangalla ameingia kwa mara ya kwanza na kuwa naibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Magufuli kweli kiboko. Kati ya mawaziri 38 waliokuwemo kwenye serikali iliyopita kwa nyakati tofauti amewachukua 12 tu na kuwatosa 26 katika baraza lake lenye wizara 18.
Mbali ya Dk. Mwakyembe, Profesa Muhongo, Makamba na Mwigulu, wengine waliobahatika kuingia kwenye serikali ya awamu ya tano ni Dk. Hussein Ali Mwinyi (Kwahani) aliyerejeshwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Jenista Mhagama (Peramiho) ambaye amerudishwa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, George Simbachawene (Kibakwe) aliyekuwa Nishati na Madini, ambaye sasa atakuwa Ofisi ya Rais pamoja na Angela Kairuki wakishughulikia Utumishi na Utawala.
Wengine ni William Lukuvi (Isimani) amebaki kwenye Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi, Charles Kitwanga ‘Mawe Matatu’ (Misungwi) amepandishwa na kupewa Wizara ya Mambo ya Ndani, Charles Mwijage (Muleba Kaskazini), ambaye alikuwa naibu katika Wizara ya Nishati na Madini, amepandishwa na kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, na Ummy Mwalimu aliyerejeshwa katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto lakini sasa atashughulikia pia Afya na Wazee.
Waliotemwa ni Juma Nkamia, Mahmoud Mgimwa, Prof. Anna Tibaijuka (ambaye alifukuzwa kufuatia kashfa ya Escrow), Diodorius Kamala, Daniel Nsazugwako, Prof. Jumanne Maghembe, Dk. Mathayo David, Dk. Mary Nagu, Janet Mbene, Dk. Hadji Mponda, Dk. Charles Tizeba, Dk. Seif Rashid, Lazaro Nyalandu, Andrew Chenge, Dk. Raphael Chegeni na Ezekiel Maige.
Wengine ni William Ngeleja, Sophia Simba, Hawa Ghasia, Kapteni George Mkuchika, Gerson Lwenge, Dk. Shukuru Kawambwa, Margret Sitta, Shamsi Vuai Nahodha na Saada Mkuya Salum aliyekuwa Waziri wa Fedha.
Lakini Magufuli amehakikisha mrithi wake katika Jimbo la Chato, Dk. Medard Matogolo Kalemani anaingia kwenye baraza hilo ambapo atamsaidia Profesa Muhongo katika Wizara ya Nishati na Madini kama ilivyo kwa Angelina Mabula wa Jimbo la Ilemela ambaye naye ni naibu katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi akimsaidia Lukuvi.
Injinia Stella Manyanya (Nyasa) naye ameingia kwenye baraza hilo akiwa naibu waziri wa Wizara ya Sayansi, Teknolojia, Elimu na Ufundi huku waziri akiwa haijapatikana kama ilivyo kwa Injinia Ramo Matala Makani (Tunduru Kaskazini), ambaye ni naibu katika Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo haijapata waziri.
Edwin Amandus Ngonyani (Namtumbo) amekuwa naibu waziri katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano iliyokuwa ikiongozwa na Magufuli mwenyewe ambayo nayo bado haina waziri, wakati Luhaga Mpina (Kisesa) atamsaidia Makamba katika Wizara ya Muungano na Mazingira.
Mbunge pekee wa CCM mkoani Arusha, William Tate ole Nasha (Ngorongoro) ameteuliwa kuwa naibu waziri katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi akimsaidia Mwigulu, wakati Mbunge wa Kondoa Vijijini, Dk. Ashantu Kijaji, amekuwa naibu waziri wa fedha, wizara ambayo bado haijapata waziri.
Kwa upande mwingine, Balozi Mahiga atasaidiwa na Dk. Suzan Kolimba katika Wizara ya Mambo ya Nje na EAC na Uhusiano wa Kimataifa.

0656-331974
www.brotherdanny.com

No comments:

Post a Comment