Pages

Pages

Pages

Thursday 10 December 2015

MAGUFULI AMREJESHA MUHONGO NISHATI NA MADINI



Profesa Muhongo siku alipotangaza kujiuzulu Januari 24, 2015

Na Daniel Mbega
RAIS Dk. John Magufuli amemrejesha Profesa Sospeter Muhongo katika Wizara ya Nishati na Madini huku akijaza sura ngeni nyingi katika Baraza lake jipya la Mawaziri lenye wizara 18 tu.
Profesa Muhongo alijiuzulu uwaziri Januari 24, 2015 kufuatia kashfa ya ufisadi wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow  na akasema siku hiyo kwamba uamuzi wake ulikuwa wa nia njema kabisa ili kupoza mvutano uliokuwepo baina ya serikali na Bunge.
Lakini waziri huyo atakumbukwa kutokana na mvutano uliowahi kutokea baina yake ya wawekezaji wazawa kuhusu ukodishaji wa vitatu vya mafuta na gesi Kusini mwa Tanzania, hivyo kurejea kwake kunaonyesha kutowafurahisha baadhi ya mahasimu wake ambao walisherehekea pindi alipojiuzulu.
Wakati Muhongo akireshwa Nishati na Madini, Dk. Magufuli amewachukua mawaziri 12 tu waliokuwa kwenye serikali iliyopita huku wengi akiwapandisha kutoka unaibu hadi uwaziri kamili.
Mawaziri waliorejea tena katika baraza jipya ambalo bado halijawapata mawaziri wanne ni George Simbachawene aliyekuwa Nishati na Madini, ambaye sasa atakuwa Ofisi ya Rais pamoja na Angela Kairuki wakishughulikia Utumishi na Utawala, Jenista Mhagama yeye amebaki Ofisi ya Waziri Mkuu akiwa ameongezewa majukumu ambapo sasa atashughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu na hana msaidizi.
January Makamba, ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, sasa ni waziri kamili wa Ofisi ya Makamu wa Rais akishughulikia Muungano na Mazingira ambapo atasaidiwa na Luhaga Mpina.
William Lukuvi amebaki kwenye Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi ambapo atasaidiwa na Angelina Mabula wakati ambapo Dk. Hussein Mwinyi amebaki kwenye Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Charles Kitwanga, Mbunge wa Misungwi, amepewa Wizara ya Mambo ya Ndani wakati Dk. Harrison Mwakyembe amekwenda Wizara ya Katiba na Sheria.
Mwigulu Nchemba, ambaye alikuwa naibu waziri wa fedha, sasa amepandishwa na kuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, ambapo naibu wake ni William Tate Ole Nashon, wakati Charles Mwijage, ambaye alikuwa naibu katika Wizara ya Nishati na Madini, amepandishwa na kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Ummy Mwalimu amerejeshwa katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto lakini sasa atashughulikia pia Afya na Wazee. Atasaidiwa na Mbunge wa Nzega Vijijini, Dk. Hamis Kigwangalla.
Wizara ya Sayansi, Teknolojia, Elimu na Ufundi bado haijapata waziri, lakini naibu wa wizara hiyo ni Injinia Stella Manyanya.
Wizara ya Maliasili na Utalii haijapata waziri, lakini naibu ni Injinia Ramo Makani. Wizara ya Fedha na Mipango nayo haina waziri bado, lakini naibu wake ni Dk. Ashantu Kijachi, wakati Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano iliyokuwa ikiongozwa na Magufuli mwenyewe bado nayo haina waziri ingawa naibu wake ni Edwin Ngonyani.
Mawaziri wapya walioingia ni Balozi Augustino Mahiga ambaye ataongoza Wizara ya Mambo ya Nje na EAC na Uhusiano wa Kimataifa huku naibu wake akiwa Dk. Suzan Kolimba.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa NEC ya CCM, Nape Nnauye, amepewa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ambapo anakabiliwa na changamoto kubwa ya kusimamia sekta hizo zinazoonekana kudorora kwa muda mrefu sasa.

Orodha kamili ya baraza hilo ni:

Wizara ya Mambo ya Nje na EAC/ Kimataifa
Waziri - Augustino Mahiga
Naibu Waziri - Dk. Suzan Kolimba

Wazara wa Utamaduni, Sanaa na michezo
Waziri-Nape Nnauye

Wizara ya Nishati na Madini
Waziri - Sospeter Muhongo
Naibu Waziri-Medard Kalemani

Wizara ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu
Waziri -Jenista Mhagama

Wizara ya ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala
Mawaziri wawili – George Simbachawene na Angela Kairuki

Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira)
Waziri - January Makamba
Naibu waziri - Luhaga Mpina.

Wizara ya Mambo ya Ndani
Waziri ni Charles Kitwanga

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi
Waziri - William Lukuvi
Naibu - Angelina Mabula

Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
Waziri – Dk. Hussein Mwinyi

Wizara ya Katiba na Sheria
Waziri - Harrison Mwakyembe

Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
Waziri- Mwigulu Nchemba
Naibu Waziri- William Tate Ole Nashon

Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
Waziri - Charles Mwijage

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Waziri - Ummy Mwalimu
Naibu - Dk Hamis Kigwangalla

Wizara ya Sayansi, Teknolojia, Elimu na Ufundi
Waziri - bado hajapatikana
Naibu Waziri - Stella Manyanya

Wizara ya Maliasili na Utalii
Waziri - bado hajapatikana
Naibu Waziri - Injinia Ramo Makani

Waziri wa Fedha na Mipango
Waziri - bado hajapatikana
Naibu Waziri - Dk. Ashantu Kijachi

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Waziri - bado hajapatikana
Naibu Waziri -Edwin Ngonyani

No comments:

Post a Comment