Na Daniel Mbega
KILIO cha muda mrefu cha Watanzania ni
kudumaa kwa maendeleo na kukua kwa tabaka la maskini kunakochangiwa na mfumo
usio rasmi wa ufisadi uliotamalaki kiasi cha kuua maadili ya utumishi wa umma.
Misingi imara iliyowekwa na waasisi wa
taifa hili imevunjwa kwa makusudi na wale waliopewa dhamana ya uongozi, jambo
ambalo limefanya pengo kati ya walionacho na wasionacho liwe kubwa zaidi.
Japokuwa ufisadi umekuwepo kwa miaka mingi
nchini, lakini kashfa zimewekwa hadharani katika kipindi hiki cha awamu ya nne
ya uongozi wa Jakaya Kikwete, ambaye pamoja na kushindwa kutoa maamuzi magumu
katika baadhi ya mambo, lakini amethubutu kuweka uwazi na kuacha sheria ichukue
mkondo wake kwa baadhi ya watu waliotuhumiwa kwa kashfa mbalimbali.
Tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 25
mwaka huu kuna maswali mengi ya kuwauliza wanasiasa, hususan wa CCM na wale wa
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kwamba fedha wanazofanyia kampeni
wamezitoa wapi.
Pamoja na ukweli kwamba ipo Sheria ya
Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 na Sheria Namba 1 ya Uchaguzi ya mwaka 1985,
lakini kwa hali inavyoonekana sheria hizi hazifuatwi kwani dhahiri gharama
zinazotumiwa na vyama hivyo ni kubwa kuliko sheria inavyoelekeza.
Sheria ya Gharama za Uchaguzi inaagiza,
gharama za kampeni kwa Mbunge zinapaswa kuwa Shs. 30 milioni na zisizidi Shs.
80 milioni kulingana na ukubwa wa jimbo husika, na kwa upande wa kampeni za
urais, zinapaswa zisizidi Shs. 6 bilioni.
Sheria ya Gharama za Uchaguzi madhumuni
yake ni kujenga mazingira yatakayowezesha kuwapo kwa uwazi zaidi katika
matumizi ya fedha zitakazotengwa kwa ajili ya kampeni, pamoja na kudhibiti
vitendo vya rushwa ndani ya vyama vya siasa katika uteuzi wa mgombea na
uchaguzi wenyewe kwa ujumla.
Sheria hiyo inaelezea masharti kuhusu fedha
zitakazotumika kwa ajili ya uchaguzi, maana ya gharama za uchaguzi, uchaguzi
ndani ya Vyama vya Siasa, gharama ambazo vyama vya siasa vinapaswa kutumia
wakati wa uchaguzi, masharti kwa Vyama vya Siasa na wagombea kutoa taarifa
kuhusu gharama zitakazotumika wakati wa uchaguzi.
Aidha, sheria hiyo inazungumzia kuhusu michango
au misaada inayotolewa na kupokewa na vyama vya siasa, kuzuia fedha kutoka nje
ya nchi kwa ajili ya kampeni za uchaguzi, matumizi ya gharama kwa vyama na
taasisi za kiserikali wakati wa kutoa elimu ya Kampeni na chaguzi za kisiasa.
Tumeshuhudia jinsi chaguzi za ndani za kura
za maoni kwa CCM na Chadema zilivyogubikwa kwa rushwa na kuna baadhi ya
wagombea ambao walidakwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru), wengine wakaenguliwa na vyama vyao kwa matukio hayo.
Sehemu ya tano ya sheria hii inahusu
masharti yanayokataza baadhi ya matumizi ya fedha kama gharama za kampeni na
uchaguzi. Matumizi hayo ni yale yanayohusu gharama kwa vitendo vinavyozuiwa au
kuwa haramu wakati wa kampeni na uchaguzi.
Sheria inasema kila chama cha siasa kitagharamia
kampeni za uchaguzi kwa kutumia gharama za uchaguzi zinazotokana na vyanzo
vyake, kwa mujibu wa kifungu cha 8(1) cha sheria hii. Na kifungu cha 8(2)
kimezingatia kuwa mgombea anaweza kutumia gharama zake mwenyewe wakati wa
kampeni pale inapobidi kulingana na mahitaji ya kampeni zake.
Sheria hii inaweka sharti la uwazi katika
mapato na matumizi ya vyama na wagombea kwa ajili ya uchaguzi kabla, wakati wa
uchaguzi na baada ya uchaguzi na katika kifungu cha 9(1), inasema: “Mgombea
atatakiwa kutoa taarifa ya fedha alizonazo na anazotarajia kupata na anakusudia
kuzitumia kama gharama za uchaguzi ndani ya siku saba (7) baada ya siku ya
uteuzi. Taarifa hizo zitawasiliskwa kwa Katibu Mkuu wa chama kwa mgombea wa
nafasi ya Urais na kwa mgombea wa nafasi ya Ubunge na Udiwani taarifa zake
ataziwasilisha kwa Katibu wa Chama wilaya.”
Kila chama cha siasa kinachoshiriki katika
uchaguzi ni lazima ndani ya siku thelathini (30) baada ya siku ya uteuzi wa
wagombea kufanywa na Tume ya Uchaguzi kitoe taarifa kwa Msajili juu ya fedha
zote ambazo kinakusudia kutumia kama gharama za uchaguzi; na kutumia kwa
kuwadhamini wagombea wa chama hicho zikiwa ni kama gharama za uchaguzi.
Pamoja na maelekezo hayo ya Sheria, lakini
bado hakuna atakayekuwa na uhakika zilikotoka fedha hizo, zina masharti gani na
ni kiasi gani hasa, kwa sababu naamini hakuna anayeweza kueleza kiwango halisi
cha bajeti yake – si kwa wagombea wala vyama husika.
Inawezekana pia kwamba, hata kama fedha za
mgombea zimepatikana katika nia haramu, lakini kwa ‘kukinusuru chama na
kukisaidia kipate ushindi’ taarifa hizo zinaweza kufichwa kwa mamlaka husika na
kwa jamii.
Itakumbukwa kwamba, mwaka 2012 CCM iliwahi
kuituhumu Chadema kwamba ilikuwa inafanya harambee kwa wanachama wake kama
geresha tu ili kuhalalisha mabilioni ya chama hicho yaliyodaiwa kutolewa na
wafadhali kutoka mataifa tajiri duniani.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM,
Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye
alikaririwa akiyasema hayo Agosti 12, 2012, wakati akizungumza na waandishi wa
habari, kwenye Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, mtaa wa Lumumba jijijni Dar
es salaam.
Alisema: “Itakumbukwa mara kadhaa Chadema
wamekuwa wakiitisha harambee za kisanii kwa kujaribu kuwahadaa baadhi ya
Watanzania kwa kuwaomba wakichangie chama hicho huku viongozi wa chama hicho
wakijua kuwa tayari wameshapata mabilioni toka kwa wafadhili wao. Mfano mzuri
wa usanii huu ni juzi siku ya Jumamosi, Agosti 10, 2012, kwenye hoteli ya
Serena ambapo walifanyika kiini macho cha harambee na kurushwa moja kwa moja na
kituo kimoja cha televisheni."
Katika harambee hiyo, zilikusanywa jumla ya
Shs. 500 milioni (taslimu na ahadi) kwa ajili ya kuimarisha na kusaidia
shughuli za chama.
Pengine inaweza kusemwa kwamba CCM ilikuwa
imechanganyikiwa na zile kampeni za Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) ambazo
zilikuwa zinaendelea nchi nzima wakati huo, lakini hata Chadema nao walikuwa
wakiwanyooshea vidole viongozi wa serikali, wakiwemo mawaziri, ambao walikuwa
wakipita kwenye mataifa mbalimbali ‘kukusanya fedha za uchaguzi’.
Waziri ambaye aliandamwa na kashfa za
ukusanyaji wa fedha nje ya nchi ni Bernard Membe, ambaye gazeti la Rai liliwahi
kuandika kwamba alikuwa anaomba msaada wa fedha na magari kutoka Umoja wa Falme
za Kiarabu (UAE) kwa kilichoelezwa kwamba ‘ana Baraka za Rais Kikwete’, huku pia
akidaiwa kutumia kete ya kuipigania Mahakama ya Kadhi ambayo imeota mbawa.
Haikuishia hapo, akatuhumiwa kwamba
ametafuna Dola 20 milioni (takriban Shs. 40 bilioni) za Muamar Ghaddafi.
Wengine wakasema alikuwa anazitumia katika harakati zake za kusaka urais ndani
ya CCM, wengi wakasema alitaka kuanzisha Benard Membe Foundation na wengine
wakasema amezikimbizia Lindi kufungua kiwanda cha saruji.
Kuhusu fedha hizo za Libya ambazo zilikuwa
zimehifadhiwa katika akaunti ya Libya No.004-200-0002216-01 iliyokuwa Benki ya
Rasilimali Tanzania (TIB), Membe alisema Serikali ya Libya na Tanzania zilitia
sahihi mkataba wa nyongeza (Addendum to the Dept Swap Agreement) ambao
ulizungumzia, pamoja na mambo mengine, matumizi ya fedha hizo na akasema
walikubaliana zikopeshwe kwa mwekezaji aliyeteuliwa na Libya, ambaye ni kampuni
ya Meis Industries Limited kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa kiwanda cha Saruji
mkoani Lindi.
Lakini CCM kwa upande mwingine imekuwa
ikituhumiwa kufadhiliwa na wafanyabiashara wa ndani na nje ambao biashara zao
‘hazieleweki’ na wengine ni wakwepa kodi wakubwa, huku pia kashfa mbalimbali
kama za usafirishaji wa meno ya tembo pamoja na zile za uchotaji wa mamilioni
ya fedha kama Escrow zikiwa miongoni mwazo.
Inafahamika kwamba, kampeni zozote za
uchaguzi kote duniani zinahitaji fedha za kutosha ili kuwafikia wapiga kura.
Hii maana yake ni kwamba vyama vinajipanga kuangalia ni namna gani wanatunisha
mifuko yao.
Siyo vibaya kupokea fedha za wafadhili
isipokuwa zisiwe na masharti ya kuliangamiza taifa letu wala taswira yake.
Ufadhili si jambo geni na hata Chama cha
TANU wakati ule wa kupigania uhuru kilikuwa kikifadhili vyama vya siasa vya
nchi mbalimbali barani Afrika na vingine vilianzishwa hapa hapa nchini, mfano
mmoja wapo ni Frelimo cha Msumbiji.
Katika nchi hizo za Magharibi, wenzetu
huwasilisha bajeti zao za kampeni zikiwa na makisio na baada ya uchaguzi
ukaguzi hufanyika kuona kama fedha zilizotumika zimezidi, zimepungua ama ziki
sawa sawa. Kama zimezidi, zilizoongezeka zimetoka wapi na sababu gani zilizofanya
zizidi, zikiwa pungufu ni afadhali.
Ni hivi karibuni tu Rais Barack Obama wa
Marekani alieleza namna anavyokusanya fedha kwa ajili ya kampeni ambapo
anatumia mtandao wa intaneti.
Hapa Tanzania ukithubutu kuhoji
utashambuliwa kwa maneno kwamba ‘umetumwa na nani’? Watu hawaki kuzungumza
hoja, hata kama hoja ni za msingi. Na katika kipindi hiki ambapo Ukawa wamepata
nguvu kubwa kutokana na ujio wa Edward Lowassa, ukihoji watasema umetumwa na
CCM, lakini CCM nao watasema umetumwa na wapinzani!
Hoja yangu ni kwamba tunapaswa kuelewa bila
kificho kwamba mabilioni haya ya kampeni yametokana na michango ya aina hii au
msaada kutoka taasisi fulani iwe ya ndani au ya nje ya nchi.
Kama ni fedha za wafadhili pia tuelezwe ni
wa aina gani na zimetolewa kwa masharti gani. Kama ni mfadhili, katoa kwa
madhumuni gani, maana Waingereza wanasema: “There
is no free lunch” (Hakuna mlo wa bure).
Kukaa kimya hakuna maana nyingine zaidi ya
kuendelea kuzua minong’ono ambayo ingeweza kufutwa kama kila kitu kingewekwa
hadharani, kinyume chake ipo siku tutashuhudia wafadhili wa siri wakidai
kulipwa fadhila kwa mtindo wa kuliangamiza taifa. Naogopa wanasiasa wasije wakaliweka taifa letu
rehani kwa tamaa yao ya madaraka.
Nawasilisha.
0656-331974
CREDIT: Makala haya yalichapwa kwa mara ya
kwanza na gazeti la WAJIBIKA la Septemba 7, 2015.
No comments:
Post a Comment