Pages

Pages

Pages

Sunday 6 September 2015

MPAMBANO SASA WANOGA KWA MAGUFULI, LOWASSA

Mgombea urais kupitia CCM Dk.John Magufuli kulia na kushoto ni mgombea urais kupitia Chadema  Edward Lowassa ,wakifanya kampeni katika mikoa tofauti. 

Na Waandishi Wetu
Morogoro/Tabora. Wagombea urais wa CCM na Ukawa jana waliendelea kuchuana vikali kwenye maeneo tofauti, Dk John Magufuli akiahidi kutaifisha ardhi inayoshikiliwa na vigogo bila ya kutumika, na Edward Lowassa akiahidi kuondoa ushuru kwenye zao la tumbaku.

Dk Magufuli, anayewania urais kwa tiketi ya CCM, jana alikuwa mkoani Morogoro, ambako kumekuwa na migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji, wakati Lowassa alikuwa mkoani Tabora, ambako zao kuu la biashara ni tumbaku.

Mkoani Morogoro. Dk Magufuli aliahidi kuwanyang’anya ardhi vigogo wote waliohodhi ardhi bila kuiendeleza, akisema atawagawia wakulima na wafugaji.

Akihutubia wakazi wa Mtimbira wilayani Malinyi jana, Dk Magufuli alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza maeneo ya shughuli za kilimo na ufugaji na kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji iliyokithiri mkoani hapa.

Mgombea huyo alisema migogoro hiyo imechangiwa na kukosekana kwa eneo la kutosha kuziwezesha jamii hizo mbili kufanya shughuli zao. 

Alisema hali halisi inaonyesha kuna ongezeko  kubwa la matumizi ya ardhi inayohitajika na binadamu na mifugo huku eneo la ardhi likiwa ni lile lile.

Alisema wakati nchi inapata uhuru walikuwapo watu milioni 9 tu, lakini leo idadi hiyo inakaribia milioni 50 huku eneo likibaki kuwa kilomita 949,000 za mraba.

Dk Magufuli alisema wakati nchi inapata uhuru, kulikuwa na ng’ombe milioni 10, wakati hivi sasa wamefikia milioni 23.

Alisema mbuzi hawakufikia milioni moja, lakini sasa ni wamefika 14, kondoo ni milioni 6, na mbwa milioni 4, jamboambalo alisema linaloongeza mahitaji ya ardhi.

“Ila wapo watu wakubwa wengine wapo serikalini wana maelfu ya ekari ambazo hawazilimi, hawayafugii na wala hawaziendelezi, wameyahodhi tu. Nikipata urais nitawanyang’anya na kuwagawia wafugaji wanaohitaji kuchunga ng’ombe na wakulima wanaohitaji kulima,” alisema Dk Magufuli huku akishangiliwa.

Kauli hiyo aliirudia karibu mikutano yote aliyoifanya jana, ukiwamo wa Ifakara ambako aliwataka vigogo wanaomiliki hadi ekari 1,000 kwa mtu mmoja waanze kuzifanyia kazi mapema kwa kuwa serikali yake haitakuwa na wananchi wa daraja la kwanza wala la chini.

Dk Magufuli ambaye ameingia katika duru ya pili ya kampeni zake mikoani baada ya mapumziko ya kikazi ya siku mbili, alisema anatambua uwepo wa mgogoro wa mpaka wa pori na makazi ya wananchi wa bonde la Lamsa uliosababishwa na kutotenda haki na kwamba akiingia Magogoni atashughulikia haraka iwezekanavyo.

Akiwa Mahenge, mgombea huyo ambaye ni Waziri wa Ujenzi,  aliendelea kuahidi ujenzi wa barabara ya Kivukoni hadi Mahenge yenye kilomita 67 kwa kiwango cha lami na kubainisha kuwa Serikali ilishaanza kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya kuunganisha mkoa wa Morogoro na Ruvuma kupitia Wilaya ya Malinyi hadi Songea.

Alisema barabara hiyo ya lami itakayoanzia Mikumi kupitia Ifakara, Lupilo hadi Songea itajengwa na makandarasi wanne au watano ili waimalize kwa haraka.

Aliahidi pia kuwa Serikali yake itaendeleza ujenzi wa daraja la Mto Kilombero linalogharimu Sh53.6 bilioni na kwamba hadi mwakani litakuwa limeshakamilika. 

Dk Magufuli aliwaambia wananchi wa eneo hilo kuwa atawezesha kujenga viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vya mchele, nyama na maziwa.

“Tutaanzisha viwanda vya kuchambua mchele kwa sababu nimepita huku kila mahali ni mchele tu na hadi bei ipo chini kwa sababu mtu akija huku kununua anakulalia kwa sababu barabara ni mbaya,” alisema.

Katika mipango hiyo ya kukuza kilimo cha mpunga, alieleza kuwa ataanzisha soko la kimataifa la mchele litakalofanikisha uuzaji wa zao hilo hadi barani Ulaya.

Alirejea tena kauli yake kuwa anataka kuwa Rais wa Watanzania wote, Rais wa maendeleo, Rais wa kubadilisha nchi na kupiga vita rushwa.

CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment