Pages

Pages

Pages

Wednesday 30 September 2015

MAAFISA AFYA TABORA WALAUMIWA KWA UCHAFU



Na Hastin Liumba, Tabora

WANACHAMA na viongozi wa umoja wa katiba ya wananchi UKAWA Manispaa Tabora wameamua kujitolea kufanya usafi katika mji huo kwa lengo la kupunguza mlundikano wa uchafu hali inayoonyesha wahusika wameelewa na kazi za kuweka mji huo safi.

Zoezi hilo lililoongozwa na mgombea ubunge wa jimbo la Tabora mjini kwa tiketi ya UKAWA Peter Mkufya ambapo zoezi hilo lifanyika katika dampo lililopo eneo la shule ya msingi Town School.

Akizungumza na gazeti hili mara baada ya kumalizika kwa zoezi hilo mgombea huyo alisema wamefikia uamuzi wa kujitolea kufanya usafi baada ya kutoridhishwa na usafi wa mazingira ya mji wa Tabora kwani hali sio nzuri, uchafu umekithiri katika maeneo mbalimbali.

Mkufya aliwalaumu Maafisa afya wa Manispaa hiyo kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo hali iliyopelekea kuongezeka kwa malundo ya uchafu katika mitaa hiyo pasipo kuchukuliwa hatua wahusika wa maeneo hayo.

‘Inashangaza kuona mkoa wenye historia nzuri ya ukombozi wa nchi ukishindwa kuendelezwa na badala yake unageuzwa kama mji wa makumbusho, jambo hili halikubaliki, hii ni ishara tu kwamba viongozi tulionao hawatoshi, tunahitaji mabadiliko ya haraka’, aliongeza.

Aidha mgombea huyo alieleza kuwa ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha mazingira yanayomzunguka yanakuwa safi lakini hapa kuna kila dalili za kulipuka kwa kipindupindu.

‘Ndugu zangu mji ukiwa safi unavutia na hata wageni wanapowatembelea wanafurahishwa zaidi, wengine wanaguswa kuja kuwekeza biashara zao na hasa ikizingatiwa kuwa mkoa huu una historia ya kipekee hapa nchini’, alisema.

Alibainisha kuwa zoezi la ukusanyaji taka katika maeneo yote ya mji huo linaweza kusaidia upatikanaji ajira kwa vijana wengi kama litawekewa utaratibu mzuri na litachochea suala la usafi katika mji huo kuwa endelevu.

‘Tatizo la mji wetu kuwa mchafu tunaliendekeza wenyewe kwani kama tungeweka mkakati madhubuti tungeweza kuondokana na hali hiyo, hii inaashiria kuwa na viongozi wenye dhamana hiyo hawatambui wajibu wao’,alisema Peter.

Mgombea udiwani kata ya Gongoni wa CUF Hamis Mwami aliahidi kufanya zoezi hilo kuwa endelevu kwa kuyashirikisha makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo akina mama na vijana sanjari na kutumia fursa hiyo kutengeneza ajira ya kudumu makundi hayo.

Aidha alitoa wito kwa vyama vyote vya siasa kujiwekea mikakati ya kusimamia suala la usafi katika mitaa yao ili kuufanya mji wa Tabora uwe kivutio kuliko kuendekeza vijembe tu kwenye majukwaa ya siasa badala ya kutanguliza maendeleo ya mkoa huo mbele.

No comments:

Post a Comment