Pages

Pages

Pages

Sunday 6 September 2015

LOWASSA AITEKA NGOME YA CCM

Mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi(Ukawa), Edward Lowassa akihutubia wananchi kwenye uwanja Town School mjini Tabora jana.

Harakati za mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa za kuchanja mbuga mikoani kusaka kura kwa wananchi kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mwaka huu, jana zimefungua ukurasa mpya baada ya kuvunja rekodi ya mahudhurio katika mikutano yake kwa kuiteka ngome ya CCM Tabora.
Lowassa ambaye baada ya uzinduzi wa kampeni jijini Dar es Salaam Agosti 29, mwaka huu alianza kufanya mikutano ya kampeni katika mikoa ya Iringa, Njombe, Rukwa, Katavi na baadaye Kigoma, jana aliendelea kuwaomba ridhaa wananchi Mkoa wa Tabora kumpigia kura Oktoba 25.

Katika mkutano huo wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Town Primary School, ulikuwa wa kihistoria hasa kutokana na maelfu ya wananchi kuhudhuria ukilinganisha na mikutano mingine iliyofanywa katika mikoa ya Iringa, Njombe, Rukwa, Katavi na Kigoma

Baadhi ya wafanyabiashara walilazimika kufunga maduka yao kwa zaidi ya saa sita kumsubiri Lowassa awasili huku waendesha bodaboda na mama lishe nao wakiungana kusitisha kazi zao kumsubiria waziri mkuu huyo wa zamani.

Baadhi ya wananchi walisikika wakisema mahudhurio ya wananchi wa Mji wa Tabora katika mkutano huo yametia fora na kuvunja ngome ya CCM ambayo kwa miaka mingi Jimbo la Tabora Mjini limekuwa likiongozwa na wabunge kutoka CCM.

Akihutubia katika mkutano huo wa kampeni, Lowassa alisema amepata malalamiko kutoka kwa wakulima wa Tumbaku wa Mkoa wa Tabora kuwa hawajalipwa pesa zao walizokopwa na baadhi ya wafanyabiashara na kuahidi kuwa kama wananchi watampa ridhaa ya kuingia madarakani watu hao watalazimika kulipa deni hilo mara mbili.

Alisema amelazimika kugombea urais kwa kuwa amejipima na kuona anatosha katika nafasi hiyo na wananchi wanamatumaini makubwa naye kwa ajili ya kuwaletea maendeleo.

Lowassa ambaye alitumia takriban dakika tano kuzungumza na wananchi, aliwaomba kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ili kura ziwe nyingi ambazo hata wapinzani wake ambao ni CCM wakiiba washindwe.

“Natafuta urais ili nibadilishe nchi. Nataka nibadili mfumo wa elimu. Sitaki michango ya penseli wala chaki,” alisema huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi.

Aliongeza kuwa suala la ajira kwa vijana litakuwa agenda muhimu kwake endapo akichaguliwa na kwamba cha msingi ni kuunganisha nguvu kuchagua Ukawa ili mabadiliko yaweze kupatikana haraka.

SUMAYE ASHINDWA KUHUTUBIA
Waziri Mkuu mstaafu wa awamu ya tatu, Frederick Sumaye, ambaye jana aliungana na Lowassa kwa ajili ya kuendelea na kampeni, alishindwa kuendelea kuhutubia wananchi waliofurika kwenye uwanja huo baada ya wananchi kuona helikopta iliyokuwa angani imembeba mgombea huyo, na kuanza kushangilia mfululizo kwa kupiga kelele.

Sumaye ambaye alikuwa ametangulia katika mkutano huo wa kampeni, alianza kuwahutubia wananchi kwa kuwaeleza mambo mbalimbali wakati Lowassa akisubiriwa, lakini hali ya upepo ilibadilika na kumkatisha baada ya wananchi kuanza kupiga kelele kushangilia helikopta iliyokuwa angani.

Lowassa alitua katika uwanja huo saa 11.45 jioni akitokea Jimbo la Urambo ambalo mbunge wake wa sasa ni Waziri wa Uchukuzi, Samweli Sitta ambako alifanya mkutano mkubwa wa kampeni.

Awali Sumaye alisema CCM ndio watakaoleta machafuko kama watakataa kukubali mabadiliko kwa sababu wananchi kwa upande wao wameshayakubali.

Alisema kumekuwa na propaganda zinazoenezwa na viongozi wa CCM kwamba wananchi wakichagua upinzani nchi itaingia katika machafuko jambo ambalo siyo la kweli kwani zipo nchi ambazo vyama vikongwe vimeondolewa madarakani na amani imeendelea kutamalaki katika nchi hizo.

MBOWE ATAKA UMOJA KITAIFA
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, alisema umoja wa taifa unahitajika kutoka kwa wanachama wa vyama vyote kwa kushiriki kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

“Tunataka ushirikiano wa vyama vyote ikiwamo CCM kutupigia kura Oktoba 25 ili mabadiliko ambayo yamekuwa kiu ya Watanzania yaweze kupatikana."

Leo Lowassa ataendelea na ziara yake katika majimbo ya Nzega na Igunga yaliyopo mkoani Tabora kabla ya kwenda mkoani Dar es Salaam Jumatatu wiki ijayo kuendelea na ziara hiyo.

No comments:

Post a Comment