Pages

Pages

Pages

Friday 18 September 2015

JUBILEE NA RUTO, UKAWA NA LOWASSA!

Ndege aina ya Hustlers Jet ambayo Ruto aliitumia. 

Na Daniel Mbega
JUMANNE ya Agosti 4, 2015 wabunge wa Jubilee nchini Kenya waliamua kwa ‘nia moja’ kumsafisha na kumtakasa Makamu wa Rais William Kipchirchir Samoei arap Ruto baada ya kuitupilia mbali ripoti ya uchunguzi kuhusu ubadhirifu wa fedha za umma kuhusiana na ndege aliyotumia kiongozi huyo kutembelea mataifa kadhaa mnamo 2013.
Uchunguzi huo ulikuwa unafanywa dhidi ya kashfa ya ukodishaji wa ndege hiyo maarufu kama “Hustler’s Jet” ambapo  mamilioni ya fedha za umma yalitumika.
Uamuzi wa kuitupilia mbali ripoti hiyo ukawaacha midomo wazi wabunge wa upinzani na baadhi ya wanachama wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ambayo kwa mujibu wa ratiba ya Bunge, ripoti hiyo ilikuwa miongoni mwa miswada kadhaa ambayo ilipaswa kupigiwa kura baada ya mjadala kuihusu kukamilika Julai 30, 2015.
Lakini kwa mshangao mkubwa, ripoti hiyo ilijadiliwa haraka haraka kabla ya kutupiliwa mbali, licha ya kuwasilishwa bungeni tangu Aprili 2014. Ripoti hiyo ilikuwa ikimlaumu Rais Uhuru Kenyatta kwa kumwagiza Ruto kusafiri katika mataifa manne, mwezi mmoja tu baada ya serikali yake kuingia madarakani.
Mbunge wa Suba John Mbadi, ambaye pia ni mwenyekiti wa ODM alisema kulikuwa na njama za siri kuhusu jinsi ripoti hiyo ilivyojadiliwa. “Haiwezekani ripoti iliyokaa katika Bunge kwa karibu mwaka mmoja kutupiliwa mbali huku mjadala wake ukionekana kutotiliwa maanani. Ni kana kwamba kuna mtu anayelengwa kulindwa na ripoti hii.”
Ruto alisafiri katika mataifa ya Congo Brazaville, Ghana, Nigeria na Gabon kati ya Mei 16 na 19, 2013. Uchunguzi wa ripoti hiyo ulionyesha kuwa jumla ya Shilingi za Kenya 18.9 milioni (takriban TShs. 369.6 milioni) zilitumika katika ziara hiyo, wakati ambapo stakabadhi zilionyesha kuwa zilizotumika ni KShs. 100 milioni (TShs. 1.9 bilioni).
Wanasiasa wa Kenya wanasema, hatua hiyo ni njama za kumsafisha Ruto katika kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 nchini Kenya.
Ruto amekuwa na kashfa nyingi huko Kenya. Mwaka 2009 akiwa Waziri wa Kilimo alikumbwa na kashfa ya ubadhirifu wa mahindi kiasi cha maguni milioni moja kati ya milioni 2.6 ambayo yalipaswa kutolewa kama msaada kutokana na baa la njaa. Yeye akasema alikuwa anachafuliwa kisiasa.
Agosti 24, 2011 ‘alitimuliwa’ kazi akiwa Waziri wa Elimu ya Juu, katika kipindi ambacho alikuwa amejiuzulu kupisha uchunguzi kuhusu kashfa iliyokuwa inamkabili ya kununua jengo la ubalozi wa Kenya mjini Tokyo.
Oktoba 2012 alitajwa katika kashfa ya kuuza sehemu ya Msitu wa Ngong kwa kampuni ya Kenya Pipelines Limited (KPC) kwa kiasi cha KShs. 272 milioni (takriban TShs. 5.3 bilioni) na kwamba alikuwa akipokea kiasi cha KShs. 96 milioni (TShs. 1.9 bilioni) kwa vipindi tofauti.
Lakini pamoja na yote hayo, alichaguliwa kuwa makamu wa rais katika uchaguzi wa mwaka 2013! Kweli Wabantu wanaugua ugonjwa wa Epodomia kama Mchungaji Christopher Mtikila anavyosema.
Nilikuwa natafakari namna wabunge wa Jubilee walivyomtakasa Ruto na jinsi ilivyotokea kwa viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) walivyofanya kwa Edward Lowassa wakati wanampokea akitokea Chama cha Mapinduzi (CCM) alikoenguliwa kuwania urais.
Ni wapinzani hao hao ambao tangu Septemba 15, 2007 walimtangaza Lowassa kuwa fisadi miongoni mwa mafisadi 11 wanaoliangamiza taifa. Wakapita kila kona ya Tanzania kwa kutumia ‘Operesheni Sangara’ na baadaye ‘Vuguvugu la Mabadiliko’ (Movement for Change) kunadi sera yao ya mapambano dhidi ya ufisadi.
Hao hao wapinzani walikuwa wakiisubiria tu CCM kwenye kona kama ingemsimamisha Lowassa kugombea, ili wafumue ufisadi wake ulivyo.
Lakini ghafla bin vuu, kwa kutegemea kwamba mwanasiasa huyo atairahisisha safari yao ya kuingia Magogoni Oktoba mwaka huu, wakasema Lowassa ni msafi na anafaa kuliongoza taifa hili.
Wamewalisha watu sifongo inayoonekana tamu mdomoni lakini chungu tumboni, kwa kuwafanya hivi sasa wavae miwani ya mbao na kuziba masikio kwa gundi wasione wala kusikia kila baya linalotajwa kumhusu Lowassa.
Kila ninapoandika makala kuzungumzia hoja mbalimbali za uadilifu wa Lowassa, nimekuwa nikipokea simu za vitisho na matusi mengi. Sijali, kwa sababu ninaongozwa na uzalendo kwa nchi yangu pamoja na maadili ya taaluma yangu.
Nikiwahoji hao wanaoshabikia, hawana hoja yoyote zaidi ya kusema wanataka mabadiliko tu. Hawaitaki CCM kwa sababu imekaa madarakani kwa miaka mingi.
Huwa napenda kuwaambia watu kwamba, Hakuna anayemwacha mke kwa sababu ya mwanamke mwingine, isipokuwa tu ni kwamba hajaweza kuelewana na mkewe ndiyo maana anamwacha. Huwezi kusema mkeo kwa sababu amekuwa mzee, basi umwache ukaoe mwingine eti tu kwa sababu huyu umeishi naye miaka mingi, amezeeka. Nasikitika kusema kwamba huo ni upumbavu na uendawazimu. Hakuna imani ya dini inayoelekeza hivyo.
Wapinzani wanamtakasa Lowassa kwa wimbo ule ule usio na kiitikio “CCM imeshindwa kuleta unafuu wa maisha kwa Watanzania.”
Kila mmoja anapenda mabadiliko yenye neema, lakini lazima kuwe na sababu. Hawa mashabiki wanaofuata mkumbo kama panzi kwenye safari ya nzige ni lazima wakae chini watafakari, lakini siyo kila wanapoona maandiko yanayomgusa Lowassa kwa mtazamo hasi wanaanza kung’aka.
Tafsiri ya neno ‘Mpinzani’ iko wazi kabisa. Ni mtu anayepinga, anakwenda kinyume na kile kilichopo, kwa nia na madhumuni ya kutaka afanikishe mambo yake – yawe ya heri au shari!
Siasa za upinzani ni nzuri zikifanywa kwa kuzingatia ukweli wa mambo. Chadema ilipata nguvu zaidi kutokana na sera ya kupiga vita ufisadi kwa vitendo, kwa kufichua kashfa nyingi ambazo zimeiyumbisha serikali mpaka ikafanya mabadiliko ya baraza la mawaziri. Haya ni mafanikio.
Lakini Chadema ninayoiona sasa siyo ile ya mwaka 2007 hadi 2010, ni chama kingine tofauti kabisa.
Kumtakasa Lowassa kwa kashfa moja tu ya Richmond, ambayo hata hivyo inayo maswali mengi ya kujiuliza, kunawaharibia, kwa sababu zipo kashfa nyingine kadha wa kadha ambazo anastahili kuzijibu, achilia mbali maelezo yake ya ‘utetezi’ wa Richmond kutotosheleza.
Tanzania ni nchi yetu sote. Uamuzi wa leo ndio unaoweza kuwa msingi wa taifa la kesho. Tukijenga msingi mbovu tusijilaumu nyumba itakapoporomoka.

0656-331974

No comments:

Post a Comment