Pages

Pages

Pages

Friday 21 August 2015

MTIHANI MGUMU WAIKABILI UKAWA

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene.

NA ELIZABETH ZAYA
Baada ya uamuzi wa serikali kuzuia Umoja  wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuutumia  Uwanja wa Taifa kuzindua kampeni zake, hatua hiyo imeupa mtihani mgumu umoja huo.
Viongozi wa Ukawa wamesema hatua hiyo imewaumiza vichwa kuhusu namna ya kupata eneo jingine lenye nafasi kubwa la kuwatosha kutokana na  idadi kubwa ya wafuasi wao.
Juzi serikali ilizuia Ukawa kutumia uwanja huo kwa madai kwamba hauruhusiwi kutumika kwa shughuli za mikutano ya kisiasa.
Serikali ilitangaza hatua hiyo  kupitia Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene, ambaye alisema serikali imechukua hatua hiyo ili uwanja huo utumike kwa shughuli za michezo pekee.
Alisema walipata barua ya  maombi  kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Agosti 12 , mwaka huu wakiomba uwanja huo kwa ajili ya uzinduzi wa kampeni zao.
Mwambene alisema baada ya kupata maombi hayo, waliwajibu kwamba hakuna chama cha siasa kitakachoruhusiwa kutumia uwanja huo kutokana na mihemuko ya kisiasa inayoweza kujitokeza miongoni mwa wafuasi wa vyama  na kusababisha uharibifu.
Alisema walichukua uamuzi huo kwa busara na unavihusu vyama vyote, ili kuufanya uwanja huo kubaki kuwa kwa shughuli za  michezo tu.
Kampeni za uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu, zinaanza rasmi Agosti 18, mwaka huu.
KAULI YA MBATIA
Jana Ukawa kupitia kwa mwenyekiti mwenza, James Mbatia Mbatia, aliwaambia waandishi wa habari kuwa kufuatia uamuzi huo wa serikali, viongozi wakuu wa umoja huo walilazimika kuitisha kikao cha kulijadili suala hilo.
Alisema kikao hicho ambacho kingewashirikisha viongozi wake wakuu kingefanyika jana jioni ili kujadiliana namna ya kupata eneo jingine ambalo litawafaa kwa ajili ya kuzindulia kampeni zao.
“Kwa kweli nikiri kwamba jambo hili limekuwa changamoto kubwa kwetu, tatizo lililopo Tanzania ambalo pia linatakiwa kuzungumzwa katika kipindi hiki cha kampeni ni ukosefu wa maeneo yenye nafasi ya kufanyia mikutano yenye uwezo wa kubeba idadi kubwa ya watu,” alisema na kuongeza:
“Hata hivyo, unaweza kuona ni namna gani serikali yetu imefika mwisho wa kufikiri,  inashindwa kuwasaidia wananchi kwenye rasilimali ambazo ni za kwao, wazitumie kwa mambo ambayo ni mustakabali wa nchi yao na pia  ni kwa ajili ya kuhakikisha wanaendesha mambo yao kwa amani na usalama, inasikitisha sana.”  
Kadhalika, Mbatia alisema baada ya kumalizika kwa majadiliano, watatoa taarifa kwa wananchi wapi watakuwa wamepanga kuzindulia kampeni hizo.
NCCR-MAGEUZI: BADO TUKO UKAWA 
Akijibu swali aliloulizwa kuhusu taarifa zilizochapishwa kwenye gazeti moja la kila siku (siyo Nipashe) za kuhusu chama chake kujitoa kwenye Ukawa, Mbatia alisema hazina ukweli wowote na yeye ndiye msemaji mkuu wa chama hicho.
Alisema Ukawa ni mtoto wa chama chake, hivyo suala la kujitoa haliwezekani na kwamba huo ni uzushi wa mitaani ambao hawawezi kuhangaika nao.
“Sisi tulikubaliana kwa maandishi Oktoba mwaka jana na tukasaini mkataba kwamba tutashirikiana kwa ajili ya maslahi mapana ya mama Tanzania kuondoa mfumo dhalimu uliopo Tanzania, hivyo chama changu hakiwezi kujiondoa kwa kuwa kinaheshimu makubaliano hayo kwa sababu yana mustakabali wa taifa,” alisema.
Kuhusiana na changamoto zinazotokea ndani ya vyama vinavyounda umoja huo katika  kutekeleza makubaliano ya kuachiana nafasi katika udiwani na ubunge katika uchaguzi huu, alisema hizo ni changamoto ndogo ambazo haziwezi kuwaumiza kichwa na kwamba zitapatiwa ufumbuzi.
Alisema kama ambavyo wamekubaliana kusimamisha mgombea mmoja katika nafasi hizo, vivyo hivyo hawatakuwa tayari kumpigia kampeni mgombea ambaye hakusimamishwa na umoja huo.
“Hakuna mtu aliye juu ya mwenzake katika Ukawa, si mali ya Mbatia, Mbowe, Makaidi wala mtu yeyote, hii ni sauti ya wananchi na ninaomba makubaliano hayo yazingatiwe na kuheshimiwa,  hivi  vitu vidogo vidogo vya umimi haviwezi kutupeleka mahali,” alisema na kuongeza:
“Natambua kwamba jambo la kuungana vyama vinne ambavyo kila moja kina misingi yake si jambo la kawaida kwa kuwa hata Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kiko peke yake tumeshuhudia wakigombana na kuvurugana wakati wa kufanya maamuzi mbalimbali, sembuse kwa hivi ambavyo vimeungana, kwangu mimi naona hizi changamoto zinazotokea kwetu ni ndogo sana.”
Ukawa unaundwa na Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment