Pages

Pages

Pages

Thursday 20 August 2015

MPAMBANO WA LOWASSA, MAGUFULI UMEIVA

Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli (CCM) na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa (Chadema).
Mpambano wa safari ya kuingia Ikulu umeiva baada ya wagombea wa vyama viwili vikubwa nchini, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kula kiapo kwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam jana.
Wagombea hao, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli (CCM) na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa (Chadema),  walifanya hivyo kama sharti la kutimiza sheria na kanuni kabla ya kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi hiyo.
Dk. Magufuli na Lowassa anayewania nafasi hiyo chini ya kivuli cha Umoja wa Katiba ya Wananchi kupitia Chadema, kwa nyakati tofauti, walifika mahakamani hapo jana wakiwa wameambatana na wafuasi wao wachache kwa ajili ya kula kiapo hicho.
DK. MAGUFULI
Kwa upande wake, Dk. Magufuli na mgombea mwenza wake wa urais, Samia Suluhu Hassan, walisaini fomu 40 za wadhamini waliowatafuta katika mikoa 10 ikiwamo minane ya Tanzania Bara na miwili ya Tanzania Visiwani.
Mgombea huyo wa CCM aliwasili katika viwanja vya mahakama hiyo saa 5:30 asubuhi akiwa ameongozana na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Tanzania Bara, Rajabu Luhwavi, maofisa wachache wa chama pamoja na maofisa usalama.
Baada ya kuingia ndani, Dk. Magufuli alikwenda moja kwa moja mbele ya Jaji Sekieti Kihio, kwa ajili ya kula kiapo na kusaini fomu zake pamoja na za mgombea mwenza wake.
ALICHOZUNGUMZA
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kusaini fomu hizo, Dk. Magufuli alisema kuna kanuni na sheria zinazotakiwa kufuatwa kwa mtu anapotaka kushika madaraka ya kuongoza nchi na lazima zifuatwe.
|"Mambo mengine tusubiri tutakapopitishwa tunaomba mtuombee ..." alisema Dk. Magufuli.
LOWASSA
Lowassa aliingia saa 7:00 mchana akitanguliwa muda mfupi na mgombea mwenza wake, Juma Duni Haji, Naibu Katibu Mkuu Chadema Bara, Salum Mwalimu, wanasheria wa Chadema, Mabere Marando na Peter Kibatala, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamisi Mgeja na aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga.
Mgombea huyo ambaye anapeperusha bendera ya Ukawa unaoundwa na Chadema, Cuf, NCCR-Mageuzi na NLD, baada ya kuingia ndani, alikwenda katika ofisi ya Jaji Kihio na kula kiapo pamoja na kusaini fomu za wadhamini za mikoa 10 kati yake minane ya Tanzania Bara na miwili ya Tanzania Visiwani.
ALICHOZUNGUMZA
Lowassa alisema hana kitu cha kuzungumza kwa kuwa bado wakati wake hadi pale atakapopitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
MSAJILI WA MAHAKAMA ANENA
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya wagombea hao wawili kumaliza kula kiapo, Msajili Mkuu wa Mahakama Kuu Tanzania, John Kahyoza, alisema Sheria ya Uchaguzi Namba 31, kifungu kidogo (1) cha Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Bunge ya mwaka 2015, inawataka wagombea urais kula kiapo mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania ama Mahakama ya Rufaa.
Alisema mgombea wa CCM alisaini fomu 40 za wadhamini aliopata katika mikoa 10 ikiwamo miwili ya Zanzibar, huku mgombea wa Chadema akisaini fomu sita za wadhamini kati ya 40 alizokwenda nazo.
Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu, Kibatala alisema mgombea wa Chadema alisaini fomu sita badala ya 40 kama alivyofanya mwenzake wa CCM, kwa kuwa sheria inatamka mgombea kusaini  fomu za wadhamini aliowapata mikoani kati ya nne hadi sita.
Alisema anashangaa kusikia mgombea wa CCM amesaini fomu 40 na kwamba hata marais waliopita walisaini idadi ya fomu nne za wadhamini.
KAMPENI ZA CCM
CCM imesema baada ya kesho kutwa kuzindua kampeni zake jijini Dar es Salaam, itafanya kampeni katika maeneo yote ya nchi, huku ikifanya mikutano 1,000 sawa na wastani wa mikutamo 15 kwa siku moja.
Kauli hiyo ya CCM ilitolewa na Luhwavi huku akiongeza kuwa maandalizi yote kwa ajili ya mgombea wa chama hicho kufanya kampeni yamekamilika.
Kuhusu namna chama kilivyojipanga kufanya kampeni katika mikoa ama maeneo yenye idadi ya wapigakura wengi, Luhwavi alisema watahakikisha wanawafikia watu wote ili wapate ujumbe wa kile wanachokisema.
KAMPENI ZA UKAWA
Wakati CCM wakitoa ratiba ya uzinduzi wa kampeni, Chadema chini ya mwamvuli wa Ukawa, bado hawajasema watazindulia wapi na lini kampeni zake.
Kampeni za uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani mwaka huu, zitaanza Agosti 22, mwaka huu na zifanyika kwa siku 63 na upigaji kura utafanyika Oktoba 25, mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment