Pages

Pages

Pages

Saturday 1 August 2015

ASKARI WA TANAPA ASHINDA TUZO YA ULINZI WA FARU AFRIKA


NA JOHN NGUNGE
Ushindi wa tuzo ya askari bora katika ulinzi wa faru barani Afrika, “2015 Rhino Conservation Awards” aliyoipata askari wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Malale Patrick Mwita, umeipaisha Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) kimataifa katika uhifadhi na ulinzi wa mnyama huyo adimu.
 
Meneja Mawasiliano wa Tanapa, Paschal Shelutete, alisema jijini hapa jana kwamba Malale alishinda tuzo hiyo Julai 27, mwaka huu, baada ya kuwashinda wenzake kutoka nchi mbali mbali Afrika.
 
Alisema Mwana wa Mfalme Albert wa Pili wa Monaco, ambaye ndiye mlezi wa tuzo hizo, alikabidhi tuzo hiyo kwa askari Malale katika hafla iliyofanyika jijini Johanesburg, Afrika Kusini.
 
Alisema Malale aliibuka mshindi miongoni mwa washindani wengine kutoka nchi zote za Afrika zenye miradi ya kuendeleza faru.
Tuzo hizo hutolewa kila mwaka baada ya taasisi hiyo kutambua matendo ya kijasiri yaliyofanywa na askari huyo alipokuwa akishiriki katika ulinzi wa wanyama aina ya faru katika hifadhi hiyo.
 
Alitaja baadhi ya vitendo vya kijasiri na kishujaa alivyowahi kufanya kuwa na uwezo wa kipekee wa kuwatambua faru asilimia zaidi ya 90 katika hifadhi hiyo kwa kutumia alama za asili.
 
Alisema mwaka 2007, Malale alizuia tukio la kuuawa kwa faru na mwaka 2008 alishiriki kikamilifu kukamata silaha tano za kivita toka kwa majangili waliokuwa kwenye mpango wa uwindaji haramu wa faru.
 
Alisema mwaka 2012 aliongoza askari wenzake kupambana na majangili wanne wenye silaha nzito za kivita wakiwa eneo la mradi wa faru.
 
Aidha alisema askari huyo ana uwezo wa kipekee awapo porini na hutumia muda wake mwingi katika kuwatafuta faru na kutambua maeneo yao mapya wapendayo kutembelea.
 
Alisema mradi wa faru wa Moru, Serengeti ndio mradi mkubwa kabisa wa faru wenye mafanikio barani Afrika unaongoza kwa kasi ya kuzaliana ambayo ni asilimia zaidi ya tano kwa mwaka.
 
Tuzo hizo huandaliwa kwa pamoja baina ya Wizara ya Mazingira ya Afrika Kusini ambayo husimamia pia masuala ya maliasili na Chama cha Askari Wanyamapori cha Afrika.
 
Akizungumzia tuzo aliyoipata, Malale alisema  ushindi wake unalifanya bara la Afrika kutambua Tanapa inafanya kazi na juhudi za kulinda faru.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment