Pages

Pages

Pages

Thursday 2 July 2015

SUMAYE ULISHINDWA VIPI KUPAMBANA NA RUSHWA ILIYOMALIZA MASHIRIKA YETU!?

Mawaziri Wakuu wa zamani, Frederick Sumaye (kulia) na Edward Lowassa wakifurahi pamoja mjini Dodoma wakati wa kurejesha fomu za kuwania kuteuliwa kugombea urais kupitia Chaa cha Mapinduzi (CCM).

Na Daniel Mbega
“Sumaye ahofia nchi kuongozwa na wauza dawa za kulevya”, “Sumaye: Rushwa ikizidi CCM nitajiondoa,” “Rushwa kuiweka CCM njiapanda,” “Sumaye: Epukeni wanaotoa fedha kwa kutumia mgongo wa zawadi,” “Sumaye kukimbia ufisadi CCM,” “Sumaye aanika mambo mazito,” “Sumaye-Wanaokerwa na maneno yangu waache kula rushwa,” “Sumaye awaonya urais 2015,” “Sumaye: Sijawahi kutoa, kupokea rushwa,” “Sumaye amshangaa Kikwete, ni kuhusu rushwa,” “Sumaye: Rushwa kwenye chaguzi, ufisadi vyanichukiza,” “Sumaye: Rushwa ikizidi CCM nitajiondoa.”
Hivi ni baadhi tu ya vichwa vya habari ambavyo nimekuwa nikivishuhudia kwenye vyombo vya habari kwa kipindi cha miaka mitatu sasa. Habari hizi zote zinamnukuu Waziri Mkuu mstaafu Frederick Tluway Sumaye, akisema kwa uchungu sana kuhusu masuala ya rushwa kwenye chaguzi mbalimbali pamoja na ufisadi.

Naam. Ni Sumaye yule yule, Mtanzania pekee kuwa Waziri Mkuu kwa kipindi cha miaka 10 mfululizo. Ni rekodi nzuri na ya kujivunia, kwani tangu tupate Uhuru mwaka 1961, hakuna waziri mkuu aliyepata kuongoza kwa kipindi chote hicho MFULULIZO.
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwanza alikuwa Waziri Kiongozi kwa miezi tisa tu (Septemba 2, 1960 hadi Mei Mosi, 1961) wakati wa utawala wa Mwingereza, halafu akawa Waziri Mkuu kwa miezi nane na siku 22 (Mei Mosi, 1961 hadi Januari 22, 1962) baada ya kupata Uhuru kabla ya kumpisha Rashid Mfaume Kawawa ambaye alidumu kwenye nafasi hiyo hadi Desemba 9, 1962 siku Tanganyika ilipokuwa Jamhuri na nafasi hiyo ikaondolewa.
Baada ya nafasi hiyo kurudishwa tena Februari 17, 1972, Kawawa akarudishwa na kushikilia hadi Februari 13, 1977 (takriban miaka saba) akampisha Edward Moringe Sokoine ambaye aliongoza kwa vipindi viwili -  Februari 13, 1977 – Novemba 7, 1980, na Februari 24, 1983 – Aprili 12, 1984 mauti yalipomkuta  - alikaa kwa miaka 4 na miezi 9 na siku 19!
Cleopa David Msuya naye alikaa kwa vipindi viwili – Novemba 7, 1980 – Februari 24, 1983, na Desemba 7, 1994 – Novemba 28, 1995 baada ya uchaguzi mkuu – miaka 3 miezi 3 na siku 8! Dk. Salim Ahmed Salim yeye alikaa kwa mwaka mmoja na miezi sita na siku 11 (Aprili 24, 1984 – Novemba 5, 1985 baada ya uchaguzi mkuu). Joseph Sinde Warioba alikaa kwa miaka mitano na siku nne (Novemba 5, 1985 – Novemba 9, 1990) akampisha Cigwiyemisi John Samuel Malecela aliyedumu kwa miaka minne na siku 28, yaani Novemba 9, 1990 hadi Desemba 7, 1994!
Edward Lowassa alikaa kwa miaka miwili na mwezi mmoja na siku 8 tu (Desemba 30, 2005 – Februari 7, 2008) kabla ya kulazimishwa kujiuzulu na kumpisha Mizengo Kayanza Peter Pinda, ambaye bado yuko madarakani!
Kwa hiyo ukitazama kwa makini utaona kwamba, Sumaye ndiye pekee ambaye amekaa pale Magogoni kwa miaka mingi zaidi, tuseme kwa kipindi chote cha awamu ya tatu ya Rais Benjamin Mkapa – waliingia wote wakatoka wote!
Katika masuala ya utawala, rekodi kama hii ni ya kujivunia kabisa japokuwa ina sura mbili: Kwanza, inawezekana utendaji wake ulikuwa mzuri, akatimiza wajibu wake ipasavyo. Lakini, Pili, yawezekana alikuwa ‘anaiva’ na kuaminiwa na Rais mwenyewe katika nafasi hiyo, vinginevyo angeweza hata akabadilishwa katika nafasi nyingine ya uwaziri kama tulivyoshuhudia kwa Mzee Kawawa na wengineo.
Nia yangu siyo kuandika sifa na historia ya mawaziri wakuu, la hasha. Bali nimesukumwa sana na matamko mengi yanayotolewa na Mzee Sumaye, ambaye Mei 29 2014 alisherehekea ‘happy birthday’ yake ya miaka 64.
Vita dhidi ya rushwa inapaswa kupiganwa na kila Mtanzania na binadamu wote kwa ujumla, maana hata kwenye Vitabu Vitakatifu tunaambiwa rushwa ni dhambi kubwa inayonyang’anya haki ya mwenye haki na kumpatia haki asiyestahili. Rushwa ndiyo inayozaa ufisadi, kwa sababu mtoaji au mpokeaji rushwa ya kawaida ndiye huyo huyo anayepata tamaa ya mali nyingi zaidi, hivyo kuingia kwenye kundi la ufisadi.
Kwa mukhtadha huo basi, ninaunga mkono ‘maneno’ ya Mzee Sumaye katika vita dhidi ya rushwa na ufisadi. Hii ndiyo inayowafanya Watanzania wengi wanakuwa mafukara wakati wachache wanakuwa na utajiri wa kufuru.
Hata hivyo, ninayo mashaka kwa Mzee Sumaye, hasa uamuzi wake wa kutoa matamko mfululizo tangu mwaka 2012. Vicha vya habari hapo juu vinadhihirisha kwamba agenda ya rushwa ndiyo kipaumbele chake, hakuna shida kabisa katika hili kwa sababu rushwa imekuwa kama kansa ndani ya serikali yetu.
Najiuliza tu, nini kilichomsukuma Sumaye kuyasema haya wakati huu? Hivi ni kweli anakerwa na rushwa kwa dhati ya moyo wake au ni kwa sababu pengine aliwahi kujeruhiwa – hasa katika chaguzi za ndani ya Chama cha Mapinduzi (Urais, Ubunge na Ujumbe wa Halmashauri Kuu)?
Sidhani kama amepata ndoto ya kuwania urais 2015 – japo kufanya hivyo ni haki yake ya kikatiba. Lakini nakumbuka Juni 2, 2008 alinukuliwa na gazeti la Tanzania Daima akisema “Urais basi”, kwamba hakuwa na nia ya kuwania tena nafasi ya urais hata itakapofika mwaka 2015, na badala yake anataka kuwa mtu wa msaada kwa nchi za Afrika, ili ziweze kujikwamua katika lindi la umaskini. Maneno haya aliyasema kwenye mkutano na waandishi wa habari pale kwenye Hoteli ya Protea, zamani Court Yard, jijini Dar es Salaam.
Nakumbuka pia siku hiyo alizungumzia kuhusu kesi aliyokuwa ameifungua dhidi ya gazeti la Tanzania Leo baada ya kuandika kwamba Sumaye alikuwa na akaunti nje ya nchi iliyokuwa na kiasi cha Dola za Marekani trilioni 10, na akataka kulipwa fidia ya Shs. 20 bilioni kwa kuchafuliwa jina. Hata hivyo, alisema pamoja na kulisamehe gazeti hilo, lakini lingemlipa kiasi cha Shs. 100 milioni, ambazo angezitumia kwa njia ya kuchangia Jukwaa la Wahariri ili kutoa semina kwa waandishi wa habari katika kusaidia kujenga maadili ya kazi hiyo, kuepuka kile alichokiita habari za kuingizwa mkenge. 
Namnukuu: “Kwa kweli hata kama ingetokea muujiza wakanilipa Shs. 20 bilioni, ningefungua kituo cha watoto yatima, baada ya kukata gharama zangu za uendeshaji wa kesi,” mwisho wa kunukuu.
Sumaye ni mwanachama na kada wa muda mrefu wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Ameshika nafasi nyingi nyeti ndani ya serikali ya chama hicho na pia amekuwa Mjumbe wa NEC kwa muda mrefu. Mawazo yake yanaheshimika ndani na nje ya chama.
Hata hivyo, taarifa za ndani ya chama zinaeleza kwamba, malalamiko mengi ambayo amekuwa akiyatoa kuhusu ufisadi na rushwa hajawahi kuyawasilisha kwenye vikao rasmi vya chama.
Ndiyo maana Oktoba 8, 2012 aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mkama, alibainisha kwamba kauli ya Sumaye kuhusu kuandamwa na rushwa ya kimtandao haikuwa imewasilishwa rasmi ndani ya chama. Hii ni baada ya Sumaye kulalamika wakati wa uchaguzi mkuu wa chama hicho uliokuwa ukiendelea.
Sumaye katika mkutano wake na waandishi wa habari Oktoba 7 aliouitisha mahususi kueleza yaliyojiri katika uchaguzi wa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) Wilaya ya Hanang’, mkoani Manyara, uliofanyika Septemba 29, 2012 alieleza kuwa sasa CCM inaandamwa na rushwa mpya aliyodai imetoka kwa mtu kuhonga ili achaguliwe katika eneo lake na sasa kuna rushwa za kimtandao.
Alisema rushwa za kimtandao ni zile, ambazo mtu hutoa fedha katika maeneo mbalimbali nchini ili watakaochaguliwa wawe wafuasi wake mbele ya safari atakapowahitaji katika safari za ndoto zake za kuwania uongozi ndani ya chama hicho.
Alisema rushwa hiyo ndiyo iliyotumika katika uchaguzi huo wa Nec Hanang', ambako aliyekuwa mpinzani wake mkubwa katika kinyang’anyiro hicho, Dk. Mary Nagu alimwangusha.
“Suala la rushwa katika nchi yetu na katika chama chetu siyo geni, lakini sasa nahisi tatizo hili sasa limeota mizizi na linazidi kuwa kubwa. Mimi binafsi nilizungumza tatizo hili mara kadhaa,” alisema Sumaye.
Akasema mapambano dhidi ya rushwa ni agenda ya kudumu kwake na kwa hiyo ataendelea nayo popote atakapokuwapo.
“…Katika uchaguzi wa kidemokrasia wapiga kura humchagua mwakilishi wanayemtaka kwa sababu ya uwezo wake, yaani humchagua mwakilishi wao kwa ajili yao. Katika demokrasia iliyopondeka kwa rushwa, fedha huwachagulia watu mwakilishi kwa ajili ya waliotoa fedha. Wapiga kura ni wapiga mihuri tu,” alisema Sumaye na kuongeza:
“Zamani kulikuwa na rushwa ya mtu kuwahonga watu fedha wa eneo fulani ili achaguliwe, lakini leo hii kuna rushwa ya kimtandao.”
Alisema watu wanaochaguliwa kwa utaratibu huo, utumishi na uaminifu wao siyo kwa wale waliopiga muhuri kuidhinisha zile kura alizopata, bali ni kwa fedha zilizonunua zile kura na hasa kwa aliyetoa au waliotoa fedha, hivyo Watanzania kuwa na wawakilishi wa mtu au watu na siyo wa umma.
Nakubaliana naye kwa hoja ya CCM kukumbwa na wimbi la rushwa, lakini napingana naye anaposema kwamba kumbe zamani kulikuwa na rushwa ya mtu mmoja mmoja lakini sasa kuna rushwa ya kimtandao.
Hivi kumbe hata wakati wake alikuwa anaiona hiyo rushwa ya mtu mmoja mmoja lakini akaisamehe? Ameamua kupiga kelele kwa sababu alikosa ushindi kwa nguvu ya mtandao kama ule wa Urais 2005?
Sumaye ananishangaza sana: Hivi miaka yote ambayo amekuwa kada wa chama mpaka kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi serikalini hakuwahi kuiona rushwa hiyo? Nini hasa kinachomshtua sasa kiasi cha kuamua kutoa matamko mfululizo kuipinga rushwa hiyo?Sumaye alikuwa mtendaji mkuu wa shughuli za serikali kwa miaka 10 mfululizo. Katika kipindi chake tulishuhudia sheria nyingi za ajabu ajabu zilizoihalalisha rushwa kwa majina mbalimbali, ikiwemo ile Sheria ya Takrima. Aseme leo kama yeye mwenyewe hakuwahi kutoa takrima, tena aseme kama hakuwahi kupewa takrima!
Lakini ni Sumaye huyu huyu ambaye wakati inapitishwa sheria hiyo Bungeni mwaka 2000 chini ya Spika Pius Msekwa, yeye alikuwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni. Leo hii ndipo anakumbuka kwamba kumbe sheria ile haifai baada ya yeye mwenyewe ‘kuumia’ na sasa anaipiga vita rushwa.
Sina imani kama kweli Sumaye anaichukia rushwa kama anavyohubiri, kwa sababu kama ingekuwa kweli, basi chini ya uongozi wake tusingeshuhudia serikali ikifunga mikataba mibovu na kuyauza mashirika ya umma kwa watendaji wa serikali – tena kwa bei chee. Ujasiri huu ameupata baada ya kujeruhiwa?
Katika uongozi wake ndipo Tanzania ilipofunga mikataba mingi mibovu katika sekta ya madini, viwanda, mashamba na ranchi za taifa ikiwemo uuzwaji wa benki ya umma (NBC) iliyouzwa kwa bei ya kutupa ikiwa ni mikataba iliyofungwa kutokana na rushwa kubwa. Sema tu kipindi kile hakukuwa na uwazi kama ilivyo sasa.
Ni katika kipindi cha uongozi wake ndipo ufisadi mkubwa ulipoingia ambao ulizua kashfa za Ununuzi wa Radar, Ndege ya Rais, mikataba ya Meremeta, Songas, IPTL na hata wizi wa fedha za EPA. Ina maana wakati huo alivaa miwani ya mbao hakuona?
Najaribu kutoa ushauri – siyo kwamba naunga mkono vitendo vya rushwa, bali Mzee Sumaye angeweza kutulia kuliko kunyoosha kidole kwa wana-CCM wenzake kwa sababu ya mambo yanayoendelea. Kama kweli ni msafi, basi kauli zake hizi zinaweza kumchafua kwa sababu yawezekana wapo wanaojua wapi naye alikuwa na udhaifu.
Ni ushauri tu.

0656 331974

* Makala haya yaliyachapishwa pia na gazeti la WAJIBIKA la tarehe 08/06/2015

No comments:

Post a Comment