Pages

Pages

Pages

Wednesday 22 July 2015

MBUNGE WA VITI MAALUM CCM AFARIKI

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mkoa wa Dodoma, Mariam Mfaki.

NA AUGUSTA NJOJI
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mkoa wa Dodoma, Mariam Mfaki (68), alifariki dunia jana katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
 
Mtoto wa marehemu, Mohamed Mfaki, akizungumza na waandishi wa habari Mjini Dodoma,  alisema mama yake alifariki majira ya saa sita mchana.
 
Alisema mama yake mpaka kufikwa na mauti hayo alikuwa anasumbuliwa na saratani ya utumbo.
 
“Alianza kuugua tangu mwaka 2012 vidonda vya tumbo, baadaye utumbo ulipata tatizo lililosababisha saratani ya mapafu na utumbo, baada ya kuendelea na matibabu hayo akapata pia ugonjwa wa moyo,” alisema.
 
Mohamed alisema marehemu alianza kutibiwa katika Hospitali ya Apollo nchini India mwaka 2012 mpaka mwaka 2014 huku akiwa anaendelea na shughuli zake ikiwamo kuhudhuria vikao vya Bunge.
 
“Marehemu alizidiwa usiku wa Julai 19 mwaka huu na kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya matibabu, ilipofika jana majira ya saa tano asubuhi hali ilibadilika hatimaye saa sita mchana akaaga dunia,” alisema.
 
Alisema taratibu za mazishi zinaendelea na kwamba wao kama familia wamepanga mazishi yafanyike leo saa 10 jioni shambani kwake maeneo ya Miyuji, Manispaa ya Dodoma.
 
Alipoulizwa kama ofisi ya Bunge ina taarifa za msiba huo, alisema taarifa wanazo na tayari baadhi ya maofisa walifika nyumbani kwa marehemu Area E.
 
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Ezekiel Mpuya, alithibitisha kutokea kifo hicho na kwamba kilitokea majira ya saa tano asubuhi.
 
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashillilah, alipotafutwa kwa njia ya simu kuelezea kifo hicho cha Mbunge, simu yake haikupokelewa.
 
Marehemu (pichani) alikuwa Mbunge wa Viti Maalum kwa vipindi vitatu kuanzia mwaka 2000 hadi Bunge lilipovunjwa Julai 9, mwaka huu.
 
Kabla ya kuwa mbunge, alikuwa Afisa Tarafa kwa zaidi ya miaka 20 katika wilaya mbalimbali za Mkoa wa Dodoma. Ameacha mume, watoto sita na wajukuu 10.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment