Pages

Pages

Pages

Sunday 5 July 2015

KOMBE LA KAGAME: YANGA YAKUTANA NA SIMBA FAINALI MARA 3, TIMU ZA NCHI MOJA ZIMEKUTANA MARA 9!


Na Daniel Mbega wa www.brotherdanny.com

RATIBA ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame, imekwishatolewa ambapo imepangwa kuanza Julai 18 na kufikia tamati Agosti 2, 2015 jijini Dar es Salaam.
Timu ambazo zimethibitisha kushiriki michuano hiyo inayofanyika nchini kwa mara ya 12 tangu mwaka 1974 ni mabingwa wa Tanzania Yanga na washindi wa pili Azam (Tanzania), APR (Rwanda), Gor Mahia (Kenya), Telecom (Djibout), KMKM (Zanzibar), Khartoum-N (Sudan), Al Ahli Shandy (Sudan) LLB AFC (Burundi), Heegan FC (Somalia), Malakia (Sudani Kusini), Adama City (Ethipia) na KCCA (Uganda).
Sudan na Tanzania zimeingiza timu mbili kila moja na kuna uwezekano kwamba huenda timu za nchi moja zikaingia fainali na hivyo kuongeza rekodi katika mashindano hayo.
Mtandao wa www.brotherdanny.com utakuletea uchambuzi na dondoo mbalimbali za mashindano hayo tangu yalipoanzishwa mwaka 1974.
Rekodi zilizopo zinaonyesha kwamba, tangu mwaka 1974 mashindano hayo yalipoanzishwa rasmi, timu za nchi moja zimekutana mara tisa kwenye fainali huku Yanga ikiongoza kwa kucheza fainali nne na timu za nyumbani, ikishinda tatu na kufungwa moja.
Gor Mahia ya Kenya, ambayo safari hii ipo kwenye kinyang’anyiro, yenyewe imecheza fainali tatu na timu za nyumbani kwao ikishinda mbili na kupoteza moja.
Hata hivyo, kwa nchi, Kenya ndiyo inayoongoza kwa timu zake kucheza fainali tano wakati Tanzania timu zake zimekumbana fainali mara nne. Kwa maana nyingine, timu pekee ‘ndugu’ ambazo zimewahi kukumbana fainali ni kutoka Kenya na Tanzania.
Yanga wakiwa bandarini kuelekea Zanzibar Januari 3, 1975 ambako waliivua ubingwa Simba.

Fainali ya kwanza kabisa kuzikutanisha timu za nchi moja ilikuwa mwaka 1975 kwenye Uwanja wa Amani, Zanzibar ambapo Yanga iliivua ubingwa Simba kwa ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Sunday Manara na Gibson Sembuli.
Simba na Yanga zilikutana kwa mara ya pili kwenye fainali ya kihistoria mwaka 1992 huko Zanzibar ambapo baada ya dakika 120 na matokeo kuwa 1-1, ilibidi mikwaju ya penati ipigwe na ndipo Simba wakashinda kwa matuta 5-4.
Yanga walipotwaa ubingwa wa Cecafa mwaka 2011 miguuni kwa Simba.

Safari nyingine ilikuwa mwaka 2011 jijini Dar es Salaam ambapo Simba ilikubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Yanga, ambao mwaka 2012 waliingia tena fainali, safari hii wakikumbana na Azam FC na kuichapa mabao 2-0.
Kikosi cha AFC Leopards cha mwaka 1984 kilichotwa ubingwa.

Gor Mahia na mahasimu wao AFC Leopards (zamani ikijulikana kama Abaluhya FC) wamekutana fainali mara tatu: Mwaka 1980 Gor iliifunga AFC Lepards 3-2 nchini Malawi; mwaka 1984 AFC Leopards ikaifunga Gor 2-1 jijini Nairobi; na mwaka 1985 Gor Ikainyuka AFC Leopards 2-0 nchini Sudan.
Leopards iliingia fainali 1997 jijini Nairobi na kukutana na ‘ndugu’ zao Kenya Breweries (sasa Tusker FC), ambapo ‘chui’ hao walishinda bao 1-0.
Lakini mwaka 2001 Tusker ikakutana na Wakenya wenzao, Oserian Fastac na kushinda kwa mikwaju ya penati 3-0 kufuatia matokeo ya dakika 120 kuwa suluhu.

Mechi nyinginezo
Ukiacha kukutana huko mara tisa kwenye fainali, lakini timu za nchi moja zmepata kukutana tena mara 13 katika hatua mbalimbali ikiwemo ya makundi hadi kutafuta mshindi wa tatu.
Rekodi zinaonyesha kwamba, mwaka 1976 nchini Uganda, Yanga ilipangwa Kundi B pamoja na mabingwa wa Tanzania, Mseto Sports ya Morogoro na katika mchezo wao, Yanga ikashinda kwa mabao 2-1.
Mwaka 1977 kule Tanga lilikokuwepo Kundi A, Luo Union ilikabiliana na Gor Mahia na ikashinda 4-2.
Mwaka 1979 mjini Mogadishu, Somalia, Kampala City Council ilikumbana na ndugu zao ‘wanajeshi’ wa Simba FC ambapo KCC ililala kwa bao 1-0.
Mwaka 1980 kule Blantyre, Malawi, kabla ya kukutana kwenye fainali, AFC Leopards ilikutana na Gor Mahia kwenye Kundi B na ikashinda 1-0, lakini kwenye fainali ikalala 3-2.
Mwaka 1982 AFC Leopards ilipambana na mahasimu wao Gor kwenye nusu fainali jijini Nairobi, ambapo ilishinda 2-0 ushindi wa mezani baada ya Gor kugomea sheria ya penati kufuatia matokeo kuwa suluhu.
Mwaka 1983 tena AFC Leopards iliifunga Gor kwenye mchezo wa Kundi B mjini Zanzibar.
Katika hatua ya nusu fainali mwaka 1988, Al Hilal ilicheza na mahasimu wao El Merreikh mjini Kahrtoum, ambapo Merreikh ilishinda kwa mikwaju ya penati 5-4. Tmu hizo zilikuwa zipambane kwenye nusu fainali mwaka 1994 mjini Khartoum pia, lakini Al Hilal ikagoma kwa maelezo kwamba kulikuwana njama zilizopangwa kuitoa Simba ya Tanzania kwenye hatua ya makundi ili Merreikh itwae ubingwa.
Mchezo mmojawapo wa robo fainali mwaka 2006 mjini Dar es Salaam ulizikutanisha Simba SC na Moro United ambapo Moro ilishinda kwa mabao 2-1 yaliyofungwa na Moses Odhiambo katika dakika ya 26 na Nsa Job dakika ya 46, kulifuta la Simba lililofungwa na Sadiq Muhimbo katika dakika ya 12.
Nusu fainali ya mwaka 2007 ilizikutanisha APR na Atraco, ambapo wanajeshi hao walishinda 2-0 kwa mabao ya Robert Laurent Kabanda dakika ya 15 na Twite Mbuyu dakika ya 84.
Mwaka 2008 Simba ilipewa ushindi wa chee baada ya Yanga kugomea mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu. Ikafungiwa miaka mitatu kutoshiriki mashindano hayo na kutozwa faini ya Dola za Marekani 50,000.
Mmojawapo wa michezo ya robo fainali mwaka 2009 ulizikutanisha Tusker FC na Mathare United za Kenya Julai 8, ambapo matokeo ya dakika 90 yalikuwa 1-1 lakini Mathare wakashinda kwa mikwaju ya penati 3-2. Hakukuwa na muda wa nyongeza.
Mwaka 2012 ulishuhudia mechi mbili za nchi moja; kwanza Azam ilikumbana na Simba kwenye robo fainali na kushinda 3-1, halafu walipokwenda fainali Azama wakalala kwa mabao 2-0 mbele ya Yanga.
Mwaka 2013 timu za Sudan zilikutana mara mbili katika mashindano yaliyofanyika Darfur Kaskazini na Gordofan Kusini nchini Sudan. Kwanza Al Hilal ya Kadugli ilipambana na Al Ahli kutoka Shandy na kutoka sare ya 1-1 kwenye Kundi C. halafu katika robo fainali El Merreikh kutoka mjini Al-Fasher ikaifunga Al Ahli Shandy kwa mabao 2-1.
Mwaka 2014 huko Rwanda, APR iliifunga kwa mikwaju ya penati 4-3 Rayon Sports baada ya kutoka sare ya 2-2 kwenye mchezo war obo fainali.
Kwa hiyo, ukiangalia rekodi hizi, lolote linaweza kutokea kwenye soka.

Ubingwa kwa penati
Ukiachana hizo, karibu mara nne bingwa wa Afrika Mashariki na Kati amepatikana kwa mikwaju ya penati.
Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1978 kule Uganda wakati Kampala City Council ilipoitoa Simba SC ya Tanzania kwa mikwaju 3-2 baada ya kutoka suluhu katika mchezo uliochezeshwa na Nelson Chirwa wa Malawi. Wafungaji wa penati hizo kwa upande wa KCC walikuwa Moses Ssentamu, Philip Omondi na Tom Lwanga; waliokosa ni Jamil Kasirye na Tim Ayieko ambaye penati yake ilizuiliwa na kipa Omar Mahadhi bin Jabir. Waliofunga kwa upande wa Simba walikuwa Abdallah 'King' Kibaden na Mohammed Bakari 'Tall' wakati penati ya Saad Hamid Ally ‘Watakiona’ ilipanguliwa na penati ya kipa Omar Mahadhi iligonga mwamba na kutoka nje.
Mwaka 1986 jijini Dar es Salaam Yanga baada ya kulazimisha sare ya bao 1-1 na El Merreikh hatimaye ilikubali kipigo cha penati 4-2 kwenye mchezo huo wa fainali.
Yanga ikatolewa tena kwa jumla ya mabao 6-5 kwenye fainali ya mwaka 1992 kule Zanzibar, safari hii na mahasimu wao Simba. Yanga walipata penati 4 na Simba wakapata 5, na matokeo ya dakika 120 yalikuwa bao 1-1.
Mara ya mwisho kwa bingwa kupatikana kwa penati ni mwaka 2001 wakati Tusker FC ilipowafunga ‘ndugu’ zao Oserian kwa penati 3-0 nchini Kenya.

KUMBUKUMBU HIZI ZIMEANDALIWA NA MTANDAO WA www.brotherdanny.com. Ukirejea weka chanzo tafadhali cha habari.

No comments:

Post a Comment