Pages

Pages

Pages

Monday 1 June 2015

SERIKALI IONGEZE BAJETI YA DAWA MUHIMU NA VIFAA TIBA KWA 2015/16

Displaying Picha.JPG
Mkurugenzi wa Sikika Bw. Irenei Kiria akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya Serikali kuongeza bajeti ya dawa muhimu na vifaa tiba kwa mwaka wa fedha 2015/16.


Utangulizi

Uwepo na upatikanaji wa dawa muhimu na vifaa tiba katika vituo vya huduma za afya vya umma ni moja ya viashiria vya huduma bora za afya  katika nchi yoyote ile. Nchini Tanzania, kumekuwa na uhaba wa mara kwa mara wa dawa muhimu na vifaa tiba katika vituo vya huduma za afya vya umma ambao umekuwa ukizorotesha utoaji wa huduma za afya na hatimaye kuzorotesha afya za wananchi walio wengi.

Tunatambua jitihada za Serikali katika kuboresha upatikanaji wa dawa muhimu na vifaa tiba nchini kama vile kutengeneza mipango mbalimbali ya kuboresha huduma hii. Mathalani, Mpango Mkakakati wa tatu wa sekta ya afya una lengo la kuboresha  upatikanaji wa dawa muhimu na vifaa tiba katika vituo vyote vya huduma za afya vya umma  nchini. Pia, Mpango wa matokeo makubwa sasa  (BRN) uliozinduliwa mapema mwaka huu unalenga kuhakikiksha uwepo na upatikanajii wa dawa na vifaa tiba kwa asilimia 100 ifikapo mwaka 2019. Mbali na mipango na jitihada zote hizi, bado kumekuwa na uhaba mkubwa wa dawa muhimu na vifaa tiba nchini

Uhaba wa dawa  muhimu na vifaa tiba

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Ifakara nchini, (Ifakara Health Institute) ilibainika kuwa, dawa muhimu zilikuwepo katika vituo vya huduma za afya kwa asilimia 41 tu katika mwaka 2012 (MOHSW, 2013)[1].  Hii inamaanisha kuwa kwa takribani asilimia 60 ya dawa muhimu hazikuweza kupatikana katika vituo vya huduma za afya.  Katika utafiti huohuo, ilibainika kuwa dawa za antibiotks zilipatikanna kwa asilimia 57 tu kitu ambacho ni hatari sana kwa magonjwa ya milipuko ambayo yamekuwa yakisababisha vifo kwa watoto na watu wazima. Kwa upande wa vifaa tiba, utafiti uliofanywa na Sikika mwaka 2011[2], ulionesha kuwa, asilimia 42 ya waganga wakuu wa wilaya waliohojiwa (N=71) walikiri kutokuwa na akiba ya gozi kwa muda kati ya miezi mitatu hadi sita.

Moja ya sababu zinazochangia uhaba wa mara kwa mara wa dawa na vifaa tiba ni ufinyu wa bajeti inayotengwa kwa ajili ya dawa muhimu  na vifaa tiba. Ufinyu huu wa bajeti umekuwa ukiendelea siku hadi siku.


Hali halisi ya mwenendo wa bajeti ya Afya
Kwa takribani miaka minne iliyopita, bajeti ya dawa muhimu na vifaa tiba imekuwa ikishuka na kusababisha ongezeko kubwa la uhaba wa dawa muhimu huku waathirika wakuu wakiwa ni wananchi wa hali ya chini kabisa. Kiuhalisia, bajeti inayopangwa imekuwa haiendani na mahitaji halisi ya dawa muhimu na vifaa tiba nchini. Makidirio ya dawa muhimu na vifaa tiba nchini yamekuwa yakiongezeka wakati bajeti inayopangwa imekuwa ikishuka siku hadi siku. Mathalani, mahitaji ya dawa muhimu na vifaa tiba yameongezeka   kutoka shilingi Bilioni 188 (2011/12) hadi  shilingi Bilioni 577 ( 2014/15) huku bajeti inayopangwa ikiwa ni shilingi Bilioni 123.6 (2011/12) na  makadirio ya shilingi Bilioni 36.2 kwa mwaka wa fedha 2015/16.

Kwa miaka ya fedha 2011/12 na 2012/13 kulikuwa na ongezeko kubwa kidogo la bajeti ya dawa muhimu na vifaa tiba ambazo ni shilingi Bilioni 123.4 na shilingi Bilioni 80.5 ingawa hakukuwa na matokeo chanya ya upatikanaji wa dawa muhimu na vifaa tiba katika vituo vya huduma za afya vya umma kwani takwimu zinaonesha uhaba wa dawa hizo kwa takribani asilimia 60. Kama uhaba ulionekana kwa zaidi ya asilimia 50 katika vipindi ambavyo bajeti angalau ilikuwa juu, hivyo ni dhahili kuwa  hali itakuwa mbaya mara dufu kwa mwaka wa fedha 2015/16 ambao makadirio ya bajeti ya dawa muhimu na vifaa tiba yameshuka hadi kufikia shilingi Bilioni 36.2 huku mahitaji yakiongezeka  kwa zaidi ya mara tatu ya mwaka 2011/12. Makadirio ya bajeti ya mwaka 2015/16 yameshuka kwa zaidi ya asilimia 48 kutoka katika bajeti ya mwaka uliopita(Jedwali 1) ,  cha kujiuliza hapa ni je hii bajeti inaendana na malengo ya BRN ya kuhakikisha upatikanaji wa dawa muhimu kwa zaidi ya asilimia 80 ifikapo mwaka 2016? Je bajeti hii imeangalia pia masuala ya ongezeko la watu, ongezeko la vituo vipya vya huduma za afya ,ongezeko la magonjwa na mahitaji halisi ya nchi?. Ni dhahili kuwa bajeti hii ni ndogo ambayo sio tu itaathiri utoaji wa huduma za afya nchini bali pia itakuwa ni mzigo mkubwa kwa wananchi hususani wa hali ya chini.
Jedwali 1 : Mwenendo wa bajeti ya dawa muhimu na vifaa tiba
Chanzo
2010/11
2011/12
2012/13
2013/14
2014/15
2015/16
Fedda za Ndani (bn.)
30.3
49.8
34
34
60
36.2
Fedha za Nje (bn.)
33.6
73.6
46.5
30
10.5
  0
Jumla (bn.)
63.9
123.4
80.5
64
70.5
 36.2
Mahitaji
-
188
198
549*
577*
577+
Pengo (bn.)

64.6
117.5
485
506.5
540.8+
* Makadirio ya mahitaji kwa mujibu wa hotuba ya Waziri wa Aya na Ustawi wa Jamii 2014/15 Bungeni

Kuchelewa kutolewa na kutotolewa kwa Fedha yote Inayoidhinishwa
Pamoja na bajeti ya dawa muhimu na vifaa tiba kuwa ndogo, kuna changamoto nyingine kama vile kuchelewa kutolewa kwa fedha zilizo idhinishwa na kutotolewa kwa fedha zote. Kuchelewa kutolewa kwa fedha kuna athiri mfumo mzima wa ununuzi na usambazaji wa dawa hiyo hivyo kuchangia tatizo la upungufu wa dawa muhimu na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma. Kwa mfano, kipindi cha miaka minne iliyopita (ukiondoa mwaka wa fedha 2012/13 ambapo fedha yote iliyoidhinishwa ilitolewa,) ni asilimia 78 tu ya wastani wa fedha zinazoidhinishwa  ndizo zimekuwa zilizokuwa, (jedwali 2 ). Kuchelewa kutolewa kwa fedha na kutolewa kasi kisicho kamili kumeendelea kuongeza tatizo la uhaba wa dawa nchini ambao tayari umesababishwa na bajeti ndogo inayotengwa.

Jedwali 2: Fedha Iliyoidhinishwa vs. Fedha iliyotolewa kwa ajili ya Dawa Muhimu na Vifaa Tiba
Mwaka
2010/11
2011/12
2012/13
2013/14
2014/15
Iliyoidhinishwa
63,900,000
123,400,000
80,500,000
64,000,000
70,500,000
Iliyotolewa
48,300,000
98,000,000
80,500,000
50,000,000
23,500,000*
% Iliyotolewa

75.6

79.4

100

78.9

33.3
*Kiasi cha fedha kilichotolewa  mpaka Aprili 2015

Fedha za uchangiaji (Cost Sharing) zilizoko Halmashauri
Tunaelewa kwamba Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapanga kutumia mapato  mbadala kutoka fedha za uchangiaji ili kusaidia bajeti ya dawa muhimu na vifaa tiba katika mwaka wa fedha 2015/16. Hata hivyo kutumia fedha hizi ili kuziba pengo ni kitu kisichowezekana kwa sasa. Kwa sababu zipo changamoto nyingi zinazokabili matumizi ya mapato haya kama vile mwongozo uliopitwa na wakati. Lakini pia, bima hizi za afya yaani NHIF na CHF/TIKA imewafikia asilimia 20 tu ya wananchi wote nchini hivyo ni dhahiri kabisa mapato yake hayawezi kuziba pengo la bajeti ya dawa katika mwaka wa fedha unaokuja. Vilevile, makusanyo na matumizi ya fedha hizi katika baadhi ya wilaya yamekuwa hayako wazi na kuibua maswali kama kuna uweledi katika matumizi yake. Kwa sasa ni vigumu kujua ni kwa kiasi gani haya mapato ya halmashauri yanachangia katika upatikanaji wa dawa muhimu na vifaa tiba, hivyo mapato haya kutumika kwa sasa kuziba pengo ni kuweka maisha ya wananchi rehani. Ni sahihi kabisa kwamba mapato haya yakiwa na mwongozo mzuri pamoja na mfumo wa uwazi na uwajibikaji yanaweza kusaidia katika kuboresha upatikanaji wa dawa kama mkakati wa muda mrefu na sio suluhisho la haraka kama ambavyo linavyochukuliwa kwa sasa.  Kuhamisha wajibu huu mkubwa wa serikali wa kuwezesha upatikanaji wa dawa kwenda kwa serikali za mitaa ni kukwepa wajibu na pia kuwanyima wananchi haki zao za msingi za afya.


Mapendekezo

  1. Serikali iongeze fedha za kutosha kwa ajili ya dawa muhimu na vifaa tiba kwa mwaka wa fedha 2015/16 ili kuhakikisha upatikanaji wa dawa nchini unaongezeka kufikia asilimia 80 mwaka 2016 kama inavyotarajiwa na mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
  2. Serikali kupitia wizara za Fedha na Afya zinapaswa kuhakikisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya dawa muhimi na vifaa tiba zinatolewa kwa wakati ili kupunguza uhaba wa dawa nchini
  3. Wizara ya Afya itoe mwongozo na mikakati inayoeleweka na kuwezekana katika kutumia mapato ya afya ya halmashauri kwa ajili ya ununuzi wa dawa muhimu na vifaa tiba. Pia ni vyema miongozo hii ikaweka wazi mifumo ya uwazi na uwajibikaji .


Mr. Irenei Kiria, Mkurugenzi wa Sikika, S.L.P 12183 Dar es Salaam,
Simu: +255 222 666355/57, Nukushi: 2668015, Barua pepe: info@sikika.or.tz,
Twitter: @sikika1, Facebook: Sikika Tanzania, Tovuti: www.sikika.or.tz




[1] MOHSW  (2013)  “Tanzania Service Availability and Readiness Assessment (SARA) 2012”
Ifakara Health Institute, Dar es Salaam

[2] Sikika (2011) medicine and Medical Supplies Availability Report: Using absorbent gauze availability survey as an entry point: A case of 71 Districts and 30 health Facilities across mainland Tanzania, May 2011

No comments:

Post a Comment