Pages

Pages

Pages

Saturday 20 June 2015

41% BARAZA LA MAWAZIRI WAJITOSA KUMRITHI KIKWETE

Rais Jakaya Kikwete

NA GODFREY MUSHI
Hadi sasa, asilimia 41 ya mawaziri, Baraza la Mawaziri la Rais Jakaya Kikwete, wamejitosa kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kuwania kiti hicho cha urais, katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Kiwango hicho cha asilimia kimefikiwa, kufuatia kada mwingine wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Waziri wa Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe  kuwa waziri wa 13 wa serikali ya Rais Kikwete kuchukua fomu jana mjini hapa. Wapo mawaziri 32 katika baraza hilo. 
Dk. Mwakyembe, amesema endapo CCM kitampitisha na Watanzania kumpa ridhaa kuwania Urais, wanaojihusisha na vitendo vya rushwa, inabidi wabadili tabia.
 Dk. Mwakyembe amekuwa Waziri wa 13 katika Baraza la Mawaziri la Rais Jakaya Kikwete na kada wa 38 kuchukua fomu ya kutangaza nia ya kuomba kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM. 
Akisisitiza alisema, “Nitaendeleza kwa spidi kali, juhudi zinazofanywa na serikali katika kupambana na rushwa; niwahakikishie Watanzania kwamba nikipata dhamana, wanojihusisha na rushwa, inabidi wawe wamebadili tabia kwa sababu nitapambana nao bila kunyong’onyea,”.
Dk. Mwakyembe alikuwa akizungumza na waandishi wa habari jana, Makao Makuu ya CCM mjini Dodoma ikiwa ni muda mfupi baada ya kuchukua fomu na kutangaza nia, akitokea Bujumbura nchini Burundi. Akiwa ameongozana na Mbunge wa zamani wa jimbo la Lupa, mkoani Mbeya,Victor Mwambalaswa na nduguye Izack Mwamanga, Dk. Mwakyembe alikabidhiwa fomu hiyo na Katibu wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Anaamringi  Macha, saa 4:15 asubuhi.
Alisema jitihada zake zote katika vita dhidi ya rushwa huwa zina baraka za viongozi wa chama chake ambacho alikielezea kimekuwa kikijipambanua kwamba ni chama cha wafanyakazi na wakulima.
Dk. Mwakyembe anakuwa kada wa 38 kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama chake kuwania kiti hicho.
AKITEULIWA
Waziri Mwakyembe alisema iwapo atateuliwa na chama chake kugombea urais, kazi kubwa atakayoifanya ni kuendeleza mambo yote makubwa na mazuri yaliyofanywa na serikali ya awamu ya nne, chini ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete.
“Hata wagombea wakifika 100, hiyo ni afya kwa chama cha Mapinduzi; kwanza nina uelewa wa kina kuhusu serikali na mafanikio yake yaliyopatikana…Mimi ni mgombea nitakayetembea kifua mbele kuliko wote,” alisema Dk. Mwakyembe. Hata hivyo, kuhusu madai ya kuwapo kwa uhasama wa kisiasa, Dk. Mwakyembe, alisema anamuomba Mungu aingilie kati na kumuepusha na yeyote mwenye chuki na uhasama dhidi yake.
MADAI YA KUCHAFUANA
“Tatizo ni watu ku-personalize mambo (kuchukulia mambo binafsi) kuhusu Richmond. Suala lile halikuwa langu, lilikuwa la Bunge na lilisababisha kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge; na kati yao wabunge waliotokana na CCM tulikuwa wanne. 
Mimi nilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati; na uzuri ni kwamba yale hayakuwa maazimio ya Mwakyembe…Naapa kwa jina la Mungu, sina chuki na mtu na ninamuomba Mungu aingilie kati kama kuna mtu mwenye chuki na mimi,” alisema.
Hata hivyo, kuhusu madai ya baadhi ya watu kutumika kumchafua mitandaoni, Dk. Mwakyembe alisema, “Tumewakamata baadhi ya watu na mimi nimesema piga ua, lazima wapelekwe mahakamani. Kwa bahati mbaya  mmoja wa waliokamatwa ni mpambe wa mmoja wa wagombea urais, alisema. "Katika mahojiano kijana huyo amekiri kuhusika kusambaza ujumbe maalum ukinihusisha na kumshambulia mmoja wa wagombea wa urais.
Amenieleza kwamba wamepewa kazi ya kuikarabati ripoti ya Richmond na kuisambaza upya mitandaoni…Nimemwambia atafungwa,”alisema Dk. Mwakyembe.
DK. MWAKYEMBE NI NANI?
Kitaaluma ni Mwanahabari na Mwanasheria ambaye alijiingiza kwenye siasa na kujiwekea historia ya makada wa CCM waliojipambanua kwa kuichukia rushwa.
Ana Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Sheria, aliyoipata kati ya mwaka 1992-1995, Chuo Kikuu cha Hamburg (FRG); kabla ya hapo, alikuwa na Shahada ya Pili ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Alisoma uandishi wa habari katika Chuo cha Uandishi wa habari Tanzania-TSJ, (Sasa, Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Mwaka 1975 hadi 1977 alitunikiwa Stashahada ya taaluma hiyo.
Dk. Mwakyembe amewahi kutumikia umma kupitia taaluma hiyo, katika Shirika la Habari Tanzania (Shihata), kati ya mwaka 1977 hadi 1978. Miaka ya 80, aliwahi kufanya kazi na Idara ya Habari-Maelezo, iliyopo chini ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
Aliingia rasmi kwenye siasa mwaka 2005 akiwakilisha jimbo la Kyela, mkoani Mbeya. Kabla ya kuingia katika Bunge, Dk. Mwakyembe alikuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki; kati ya mwaka 2001 hadi 2005.
Wakati wa Bunge la tisa, Dk. Mwakyembe aliteuliwa kuongoza Kamati Teule ya Bunge hilo iliyochunguza na kutoa mapendekezo kuhusu kashfa ya Kampuni ya Kufua Umeme wa Dharua (Richmond LCC).
Aidha, amewahi kushika nyadhifa mbali mbali katika serikali ya awamu ya nne, ikiwamo Waziri wa Ujenzi, Waziri wa Uchukuzi na sasa Waziri wa Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment